ALHUDA, Februari 15, 2018
Taazia
Buriani Mwalimu Iddi
Kikong’ona akiwa shule ya msingi alijitahidi kusoma vitabu vya Maududi
Na Mussa Ally Bwakila
Mwanaharakati wa Uislamu na Mwalimu wa somo la dini ya Kiislamu
Iddi Suleiman Kikong’ona amefariki dunia.
Kiko(45) alifariki siku ya Ijumaa usiku na kuzikwa Jumamosi
iliyopita jioni katika makaburi ya Kola Mjini Morogoro, baada ya kuswaliwa
katika Msikiti wa Al-Fiqihiya chini ya Sheikh Ayub Salum Muwinge.
Mmoja wa walimu wake aliyehusika pakubwa katika kumjenga
mwanaharakati huyo ambaye ni sehemu ya watendaji wa Al-Huda anamuelezea
marehemu kuwa ni kijana aliyekua akiwa na mapenzi ya dini yake.
“Nilimfahamu Iddi akiwa darasa la tano shule ya msingi
Kikundi mjini Morogoro wakati huo nikihudhuria kufundisha elimu ya dini ya Kiislamu,
nikiwa chini ya taasisi ya Munadhamat al Daawa al Islamiya ambayo ilikuwa chini
ya Ukurugenzi wa Sheikh Abdulkarimu baadaye AbdulRahman Khalil wakisaidiwa na
marehemu ustaadh Mtengwa Burhan, tangu siku ya kwanza ya vipindi vyangu Iddy
alipenda kusikiliza mafunzo ya dini ya Kiislamu akiwa katika umri mdogo sana”,
anaeleza Mwalimu wake huyo.
Ustaadh huyo anataja program hiyo ya ufundishaji elimu ya
dini ya Kiislamu iliendeshwa na Munadhamat katika mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani, Tanga na Tabora.
“Wakati Munadhamat daawa al islamiya ikianza shughuli zake
rasmi Tanzania mwaka 1988 Ofisi yetu ikiwa shule ya Alharamain baadaye tukahamia
mtaa wa Agrrey upande wa Mishen Kota, Mimi nilikuwa mmoja wa waanzilishi wa
shughuli hizo nikiwa mmoja wanaohudumu chini ya taasisi hiyo, wengine walikuwa
ni pamoja na Mwalimu Said Nsigarila, Mwalimu Mohammed Kassim Rulengelule na
Mwalimu Adam Salim Kaoneka”, ameeleza Mtendaji huyo wa gazeti hili la ALHUDA.
“Wengine ni Mwalimu Subira Nzole, baadaye waliongezeka
Mwalimu Hashim Kassim, Mwalimu Zainab Mweche na Marehemu Mwalimu Iddy Juma” na
Sekretary wetu akiwa mmoja wa waanzilishi wa TAMWA, Asmah Basafari, tukiongozwa
na Ustaadh Mtengwa Burhan, timu yetu hii ndiyo iliyotafuta vile viwanja
vilivyojengwa shule za sekondari za Ununio na Kunduchi”, ameongeza.
Akimzungumzia Marehemu Kikong’ona ameongeza kuwa kutokana na
shauku aliyoonesha kutaka kuijua dini yake, alikuwa akifika mara kwa mara
nyumbani kuangalia na kujaribu kusoma vitabu kadhaa vya Kiislamu katika maktaba
yake, viliyokuwa katika lugha ya kiingereza akiwa hajaijua hiyo, wakati huo huo
akihudhuria Madrasa iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu wake Ustaadh dady Ramadhani
Kambi maeneo ya mtaa wa Mtoni mjini humo.
“Mimi na Bwana Mussa Nzige tuliiboresha Madrasa
hii(Alfiqhiya) wakati huo ikiwa katika nyumba ya aliyekuwa mfanyabiashara wa
kiarabu Mzee Swalah ambaye hivi anaishi Temeke jijini Dar es Salaam, tulinunua
bati tukapaua, awali watoto walikuwa wakisoma huku jua likiwachoma, tukaweka
utaratibu mzuri wa masomo, asubuhi na mchana walikuwa wakisoma Qur’an, jioni
nilikuwa nikifika pale kuwafundisha tabia za Kiislamu(Akhlaq) na tawhiid(Kumjua
Muumba vilivyo)”, Iddy aliweza kuhifadhi majina yote ya Muumba katika umri ule
mdogo”, ameeleza.
Mwalimu huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini
amesema aliendelea kuwa na Iddy akimpa kila aina ya usaidizi vikiwemo vitabu
vya masomo yake ya msingi hadi alipomaliza shule ya msingi na kufaulu kuingia
shule ya sekondari ya Morogoro ambako pia alikutana naye wakati wa somo hilo
ambalo pia Mwalimu huyo alikuwa akifundisha katika shule hiyo na shule nyingine
za sekondari mjini humo.
“Nilikutana tena na Iddy pale nilipowakusanya wanafunzi wa Kiislamu
wa shule za sekondari kidato cha pili katika kituo cha Jabal Hira ambako
niliandaa masomo ya ziada kwao pamoja na kuwafundisha elimu ya dini yao, Iddy
akiwa kidato cha pili alikuwa mmoja wa wanafunzi hao”, ameeleza.
Aidha anasema Iddy alikuwa mtoto pekee aliyekuwa akihudhuria
semina za Kiislamu za watu wazima maalumu ambazo ziliandaliwa na ama MSAUD,
WARSHA, Munadhamat au IPC.
“Ni kutokana na shauku yake ya Uislamu aliamua kutokwenda
shule ya Sekondari ya Pugu kusoma mchepuo wa sayansi PCB badala yake akajiunga
na Ubungo Islamic High School kusoma EGM akiwa ni miongoni mwa wanafunzi
walioanzisha A Level kwa shule hiyo ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Mohmmed
Kassim kwa kushirikiana na Mwalimu Said Nsigarila na Sheikh Omar Msangi,
iliyopo jijini Dar es Salaam,” ameeleza.
Akikariri maneno yake ya mwisho akiwa katika Zahanati ya
Wakorea Magomeni siku ya jumamosi mwishoni mwa mwezi uliopita, Mwalimu huyo
anasema Iddy alieleza mambo kadhaa yakiashiria kuiaga dunia muda si mrefu.
“Brother umenitoa mbali, nilikuwa nacheza Disco toto, ni wewe
uliyenitoa huko, umenifunza dini yangu, Brother umenitoa mbali, nimekumbwa na
Kadari kubwa”, Mwalimu huyo alimkariri marehemu Iddy akimsikia kutamka hayo
akimuashiria yeye baada ya kufika kumjulia hali hospitalini hapo.
Kiongozi mwingine wa Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda
amehimiza kumuomba Allah (S.W) Amrehemu, na kuwapa uwezo waliobakia nyuma
kuendeleza pale alipoishia.
Prof. Hamza Njozi aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha waislamu
Morogoro (MUM), na Mwenyekiti wa bodi ya Islamic Propagation Center (IPC),
ambayo marehemu aliwahi kufanya kazi kama mwalimu wa moja ya shule za taasisi
hiyo, na msanifu kurasa katika vitabu vya maarifa ya Kiislamu, amemsifu kuwa
hakuchoka kutumikia Dini yake.
Dkt. Khalid aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi ya Daa’wa ya
Munadhamat ambayo marehemu Iddi Kikong’ona alikuwa mfanyakazi wake hadi umauti
unamkuta, naye amesifu utumishi wake wa kupigiwa mfano.
Ust. Sadiki Gogo na Ust. Ramadhan Sanze wanamuelezea Marehemu
Iddi Kikong’ona kuwa katika uhai wake amewahi kushiriki harakati nyingi za
maendeleo ya jamii yake ikiwa ni pamoja na programu ya kutoa elimu ya ziada
katika ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Kiislamu, harakati za kuendeleza
taasisi za Kiislamu, na harakati za kuandika na kusanifu tovuti, magazeti, na
vitabu vya Kiislamu, na nyinginezo kadhaa.
Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu walioongea na mwandishi
wa habari hizi wamesema, ulingo wa harakati za kupigania haki na maendeleo ya
Uislamu na waislamu utakuwa umemtendea haki marehemu Idi Kikong’ona si tu kwa
kundeleza mema aliyoyaacha, bali pia kutazama namna ya kukiendeleza kizazi
chake (watoto wake) kitaaluma, ili wasihisi pengo la kihuduma baada ya
kuondokewa na mzazi wao.
Mwalimu Iddi Suleiman Kikong’ona atakumbukwa na wengi
aliofanya nao kazi kama mwanaharakati aliyejitenga na majukwaa ya hadhara, bali
alikuwa mpiganaji wa chini kwa chini aliyefanya Daa’wa kikamilifu hadi Muumba
wake alipomchukua.
Tunamuomba Allah (S.W) Amrehemu. Sote ni wa Mwenyezi Mungu
(S.W) na sote kwake tutarejea.
No comments:
Post a Comment