Utangulizi
Francis Daudi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Ulaya ambae akimaliza masomo yake atakuja kuwa mwalimu wa historia. Tumejuana na tunabadilisha mawazo katika historia ya Tanzania. Ameniletea hii hotuba hapo chini nami nimempa fikra zangu.
HOTUBA YA MWALIMU NYERERE YA KUAGA TAIFA TAREHE 5 NOVEMBA, 1985 KABLA
HAJASTAAFU URAIS ALIYOITOA MBELE YA WAZEE WA DAR ES SALAAM
Baraza la Wazee wa TANU 1955 (Picha kwa hisani ya Msakala Mohamed Tambaza) |
[9:10 AM, 3/20/2018] Francis Daud:
‘"Mimi nimeanza siasa na wazee
wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli.
Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo
nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.
MS
MS
Niliporudi nikakubaliana na
wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa
shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya
siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali
inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.
Niliporejea nchini hapo Oktoba,
nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua
habari za African Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia
habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa
Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.
Pale, mimi na wanafunzi wenzangu
tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association
(TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo
yanakwenda vizuri kidogo.
Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi
peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu
Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi
ya chama hicho?
Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo.
Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia – nikiwa Makerere –
akasema: wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha
TAA (Tanganyika African Association).
Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha
matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama
chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.
KUVUNJWA KWA TAWA
Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo
mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza
kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa
katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika
mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.
Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika
African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa
nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache,
nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA?Nikaambiwa kuna jamaa
mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati
huo.
Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye
naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa
mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam,
nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela
Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.
Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia
kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika
Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu
wakanichagua…''
UCHAMBUZI WA HOTUBA YA MUAGO YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE
NYERERE
Francis,
Hotuba
hii mimi inanishangaza kwa jinsi Mwalimu Nyerere alivyoacha kutaja majina ya
hao wazee anaowashukuru. Huwezi kuwaadhimisha watu wasio na majina, maana yake na
tafsiri yake ni kuwa huwajui au umesahau majina yao. Hawa wazee wanafahamika na
kila mtu alichangia kwa namna yake kiasi Mwalimu Nyerere hawezi hata kidogo
kuwasahau. Wapo aliojuananao kwa shughuli za TANU na siasa tu na kuna wale aliojuananao
zaidi katika udugu kwa kuwa wao ndiyo waliompokea kama mgeni wao na akawa
sehemu ya ndugu katika ukoo. Hapa sitawataja akina Sykes kwa kuwa historia yao
na Baba wa Taifa sasa ni mashuhuri inafahamika. Lakini kuna watu kama Shariff
Abdallah Attas na mkewe Bi. Chiku
Kikusa, mama yake Maalim Sakina na Maalim Fatna Baba wa Taifa alionekana zaidi kama ndugu. Maalim Sakina na Maalim Fatna ndugu hawa wawili wote
walikuwa walimu katika shule ya Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika. Shariff Attas alijuana na Nyerere si zaidi
katika siasa bali kama mgeni wa Abdul Sykes.
Shariff Abdallah Attas |
Shariff
Attas alikuwa akifanya kazi Soko la Kariakoo ambako Nyerere alianza kufika pale
1952 kila akija mjini kutoka Pugu mwisho wa juma. Abdul Sykes alikuwa ndiye
Market Master na Shariff Attas akiwa Dalali Mkuu wa Soko. Kupitia kwa Abdul
Sykes ndipo Nyerere akajuana na Shariff Attas na watu wa nyumbani kwa Shariff
na jamaa zake wote kama Maalim Fatna, Bi. Chiku Kisusa mama yao mzazi Maalim
Sakina na Maalim Fatna. Lakini hawa wote niliowataja ndiyo wakajakuwa wanachama
wa kwanza wa TANU mjini Dar es Salaam. Hata ukiangalia picha hiyo hapo chini
huyu mama utamuona yuko na Baba wa Taifa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam
akimsindikiza Mwalimu Nyerere safari yake ya kwanza UNO, 1955.
Kulia ni Bi, Tatu bint Mzee, Bi, Titi Mohamed, wa nne Julius Nyerere na wa mwisho ni Bi. Chiku Kisusa |
Hapo
sokoni Karikakoo ndipo Mwalimu Nyerere akajuana na Mzee Mshume Kiyate. Sasa huyu
Mzee Mshume Kiyate wakajuana zaidi katika siasa na udugu ukaja baadae. Mzee
Mshume alikuwa mmoja wa wajumbe katika Baraza la Wazee wa TANU na alikuwa mmoja
wa wafadhili wakubwa wa chama hadi uhuru ulipopatikana na hili hakuna
asiyelijua. Haiyumkini ikawa mtu kama Mzee Mshume KIyate akatajwa kwa ujumla wa
‘’wazee,’’ pasi na kulitaja jina lake. Katika hotuba hii Mwalimu Nyerere
kamtaja Sheikh Mohamed Ramiyya lakini hakueleza alimjua vipi Sheikh Ramiyya
kwani yeye hakuwa mkazi wa Dar es Salaam. Sheikh Ramiyya alikuwa akiishi
Bagamoyo na waliomchukua Baba wa Taifa kumpeleka Bagamoyo kumjulisha kwa Sheikh
Ramiyya walikuwa Mzee Idd Tosiri na Mzee Idd Faiz Mafungo na wote hawa watatu,
Sheikh Ramiyya, Tosiri na Faiz ni ndugu Wamanyema na wazee wao walitokea
Belgian Congo. Hawa walitoa mchango mkubwa katika TANU. Ilistahili siku ile
Baba wa Taifa awataje kwa majina yao. Hii
mosi.
Pili, tuje
kwa Abdul Sykes.
Kulia Idd Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere na Haruna Taratibu |
Abdul
alikuwa wakati ule Nyerere alipopelekwa kwake kukutananae, Abdul alikuwa Kaimu
Rais na Katibu wa TAA. Rais alikuwa Dr. Vedasto Kyaruzi lakini kwa sababu ya
uongozi huu wa Abdul na Dr. Kyauzi kuiingiza TAA katika masula mazito ya siasa walipoingia
madarakani 1950, Dr. Kyaruzi akapewa uhamisho akapelekwa Kingolwira Prison
akawe daktari wa wafungwa na ilipoonekana kuwa uhamisho ule haukumzuia kuja Dar
es Salaam mwisho wa juma kuja kuonana na Abdul Sykes kendeleza harakati za TAA,
Dr. Kyaruzi akahamishiwa Nzega. Hii ndiyo ikafanya sasa nafasi ya rais iwe wazi
haina mtendaji na Abdul akakaimu nafasi ile kwa miaka takriban mitatu bila ya
kuitisha uchaguzi. Ulipofika mwaka wa 1953 ulipofanyika uchaguzi wa mwaka
Nyerere na Abdul wakagombea nafasi ya urais. Hili si Nyerere wala wanahistoria
wetu wamelieleza popote.
Nyerere
katika hotuba yake hii kwa Wazee wa Dar es Salaam anasema,’’ Tukafanya mkutano hapo
Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua…’’ Katika hotuba hii Mwalimu
Nyerere kamtaja Abdul Sykes kuwa ni mmoja wa vijana wenzake waliokuwa katika
siasa mwingine akisa Dossa Aziz lakini hakusema kuwa aligombea na Abdul Sykes nafasi
ya urais wa TAA katika uchaguzi wa mwaka wa taehe 17 April 1953 pale Ukumbi wa Arnautoglo.
Wala hakusema kuwa alishinda uchaguzi ule kwa kura chache sana. Hii ni muhimu
sana kwani In Shaa Allah nitaeleza huko mbele kuwa hii ilikuja kuwa ndiyo
sababu TAA ilikufa baada ya yeye kuchukua
uongozi.
Kushoto Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona, Ukumbi wa Arnautoglo katika tafrija ya kumaga Nyerere safari ya pili UNO 1957 |
Tatu,
si kweli kuwa TAA ilikuwa imesinzia kwa sababu 1950 ilikuwa imeunda TAA
Political Subcommittee ikiwa na wajumbe hawa wafuatao: Mufti Sheikh Hassan bin
Ameir, Sheikh Said Chaurembo, Hamza Mwapachu, Stephen Mhando, John Rupia, Dr.
Vedasto Kyaruzi na Abdul Sykes. Kamati hii ilitengeneza mapendekezo ya katiba
kwa Gavana Edward Twinning. Haya mapendelezo ndiyo Mwalimu Nyerere aliyasoma
katika hotuba yake UNO mwaka wa 1955. Haiwi chama kilichosinzia kikaja na
mapendelezo mazito kama haya ambayo yalifika hadi UNO. Licha ya hili
mapendekezo haya ndiyo yalijadiliwa katika mkutano uliounda TANU na wanakamati
wake wawili Abdul Sykes na John Rupia wakiwa kati ya wajumbe 17 wa mkutano ulioasisi
TANU mwaka wa 1954.
Kulia Sheikh Said Chaurembo na Liwali Ahmed Saleh, 1956 |
Lakini
ukweli ni kuwa chama kilisinzia Mwalimu Nyerere alipochaguliwa kuwa Rais wa TAA
na ikabidi zifanyike jitihada ili kukihuisha upya chama. Muhimu ieleweke kuwa
TAA haikudorora kwa kuwa kiongozi alikuwa hana uwezo, la hasha, TAA ilidorora
kwa kuwa Nyerere alikuwa hafahamiki hili la kwanza la pili ni kuwa kwa wakati
ule Nyerere hakuweza kutia katika chama kile ambacho Abdul alikuwa akifanya kwa
muda wote alipokuwa kiongozi wa juu. Ukweli ni kuwa ikiwa halmashari ya TAA
itakutana nyumbani kwake basi kikao kitamalizika vizuri kwa pengine kula na
kunywa pale nyumbani au Princess Hotel. Hulka hii iliendelea hadi wakati wa
TANU. Mwalimu Nyerere alikuwa mgeni Dar es Salaam na hakuwa na fedha wala na
nyumba ambayo angeliweza kufanya haya. Nyumba ya Abdul ambayo kabla yake
ilikuwa nyumba ya baba yake, Kleist Sykes, ilikuwa kituo cha harakati dhidi ya
ukoloni. Toka miaka ya 1920.
Nne,
mwaka wa 1952 TAA ikishirikiana na Meru Citizens Union ilifanikisha kumpeleka
Japhet Kirilo na Earle Seaton UNO katika "petition" ya Mgogoro wa
Ardhi ya Wameru na ilikuwa Abdul Sykes akiwa Katibu na Kaimu Rais wa TAA ndiye
aliyemwomba Earle Seaton asaidie kutoa ushauri kwa Meru Citizens Union katika
mgogoro ule kwani Seaton alisaidia sana TAA Political Subcommittee katika kuandika mapendekezo ya katiba yaliyokwenda
kwa Gavana Twinning 1950, mapendekezo ambayo kama ilivyoelezwa huko juu, ndiyo
yaliyotengeneza hotuba ya Mwalimu Nyerere UNO 1955.
Kushoto Earle Seaton na Julius Nyerere baada ya uhuru Seaton akiwa mfanyakazi wa serikali |
Tano,
si kweli kuwa hawa wazee walikuwa hawajui nafasi ya Waingereza katika
Tanganyika kwani Visiting Mission za UNO zilikuwa zikipita Tanganyika na TAA
ikishiriki katika mazungumzo na taarifa zao zikiandikwa katika gazeti la Zuhra
lililokuwa likiendeshwa na Ramadhani Mashado Plantan kama mhariri. Hii ndiyo ilikuwa
sauti ya Waafrika wa Tanganyika. Nyerere mwenyewe kaandikwa kwa mara ya kwanza
jina lake na habari zake ndani ya gazeti
hili mwaka wa 1953. Haiwezekani katika hali ya siasa kama hii ikawa kuwa wazee
hawakujua waanzie wapi kudai uhuru. Ukiachia TAA Political Subcommittee 1950
ambamo walikuwa watu wazima kama Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Said
Chaurembo na John Rupia, zipo pia barua za 1933 walizoandikiana Rais wa African
Association Mzee bin Sudi na Katibu, Kleist Sykes zikizungumza kuhusu uhuru wa
Tanganyika.
Kwa
ajili hii basi si kweli kuwa watu hawakujua namna ya kutaka kujitawala. Abdul
Sykes alianza harakati za kuunda TANU akiwa Burma katika Vita Vya Pili Vya
Dunia (1938 -1945) na msingi wa kuasisi TANU aliujenga kupitia 6th Battalion ya
King African Rifles (KAR) Burma Infantry. Shajara ya Abdul Sykes inaonyesha
kuwa mazungumzo ya mwisho ya azma ya kuunda chama cha siasa yaliyafanywa
Kalieni Camp India tarehe 25 Desemba 1945 mkesha wa Xmas wakisubiri meli
kurejeshwa Tanganyika baada ya kumalizika vita.
Mimi
naamini hotuba ya Baba wa Taifa ilitolewa akiwa yeye mwenyewe hajui mengi kabla
ya wakati wake. Naamini kabisa kuwa yawezekana pia Mwalimu Nyerere hakuwa
anamjua Abdul Sykes vizuri na historia ya baba yake Kleist, katika siasa za
ukombozi wa Tanganyika na kuundwa kwa African Association 1929 lau kama aliishi
na watoto wake, Abdul, Ally na Abbas kwa karibu sana hadi uhuru ulipopatikana mwaka
wa 1961. Lakini vilevile utafiti umeonyesha pia kuwa baada ya uhuru ziliingia
sababu nyingine zilizofanya historia ya TANU ielezwe kwa namna alivyoieleza
Baba wa Taifa ikiwaweka pembeni baadhi ya wazalendo. Itoshe tu kwa kuhitimisha
kusema kuwa hata hao wazee ambao Mwalimu Nyerere hakuwataja kwa majina, alijulishwa
kwao na Abdul Sykes na Dossa Aziz. Iwe iwavyo si rahisi kusahau kuwa Msajili wa
Vyama Vya Siasa alikataa kuiandikisha TANU kwa kuwa chama hakikuwa na wanachama
Nyerere alipofikisha maombi ya TANU kwake. Si wengi wanajua hili lakini Ilikuwa
Mzee Said Chamwenyewe ndiye aliyetumwa Rufiji na Abdul Sykes akaandikishe
wanachama wa mwanzo wa TANU ambao Baba wa Taifa alifikisha orodha yao ile kwa
Msajili wa Vyama Vya Siasa na TANU ikaandikishwa.
Hatujachelewa
lau kama miaka mingi imepita bado iko nafasi ya kuwaadhimisha Wazee wa Dar es
Salaam na kwengineko waliomuunga mkono katika kuijenBaba wa Taifa katika kuijenga
TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
No comments:
Post a Comment