Shajara ya Mwana Mzizima:
KUVUNJIKA KWA JUMUIYA EAC NA ATHARI ZAKE—1
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Abdallah Tambaza akiwa Nairobi 1972 |
ASALAMAALEKUM
mpendwa msomaji wa Shajara ya Mwana Mzizima. Juma lilopita tulimwangalia shujaa
wa ukombozi wa taifa letu, hayati Dossa Azizi, ambaye ametufanyia makubwa
kwelikweli, ili leo sisi tuwe tumejitawala wenyewe namna hivi tulivyo.
Leo, shajara
inataka kuwapa wasomaji mapumziko kidogo, au kama wanavyosema wacheza Mpira wa
Kikapu (Basketball), ‘time out’, ili tuone inatwambia nini kuhusu kuvunjika kwa
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na athari zake.
Katika uhai
wote wa taifa hili, bado sijapata kuliona tukio baya lililoleta athari kubwa sana
kama pale kijingajinga tutulipokubali kushirikiana na wanajumuiya wengine
(Kenya na Uganda), tukachukua mikuki, mishale, miundu na shoka tukaishambulia
Jumuiya yetu mpaka ikakatika vipande vipande, ikaaga dunia—Inna Lillah Waina
Illayhi Rajuun!
Najua tutakimbilia
kusingizia sisi hatumo, eti ni Charles Njonjo wa Kenya; tutasema hatumo, eti ni
Nduli Iddi Amin wa Uganda aliyehusika, lakini ukweli utabakia palepale kwamba na
sisi tumo— tena kwa asilimia zote— maana damu tulikutwa nayo mikononi na nguoni
mwetu!
Jumuiya ile
kongwe pengine kuliko zote zilizopata kuwepo duniani, ilikuwa ndiyo chachu ya
maendeleo katika nchi zote wanachama katika ukanda huu wa Afrika. Kwa wale
wasiofahamu, kwa hapa kwetu ilikuwa ndiyo mwajiri namba moja halafu ndio
inafuata Serikali.
Nyenzo zote
kuu za uchumi, kijamii, kielimu zilikuwa zikihudumiwa na mashirika makubwa
makubwa yaliokuwa mali ya pamoja miongoni mwa nchi wanachama. Kuvunjika kwa
mashirika yale ‘manene’ na kuanzishwa vishirika vidogo mahala pake au
kutokuwepo mbadala kabisa, kumerudisha nyuma maendeleo takriban ya nchi zote
hizo. Hapa kwetu ndio usiseme.
East African Airways VC 10 |
Miongoni mwa
mashirika makubwa ambayo yalikuwa ni milki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni
pamoja na Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAAC), ambalo lilikuwa moja ya
mashirika ya ndege makubwa kidunia, likiwa na ‘madege’ mengi sana makubwa
makubwa (VC10s, DC9s, FK27s na Twin Otters) na hivyo kuweza kushindana na
mashirika makubwa ya nchi za Magharibi.
EAAC lilitoa
ajira kwa watu wengi sana wa nchi hizi
na pia kuweza kutoa wataalamu wengi wa uendeshaji ndege (marubani), mainjinia
(flight & maintenance engineers), wahudumu wa kuuza tiketi (tickets and
reservations), wahudumu wa ndani ya ndege (cabin attendants) na wengineo wengi
sana, wote kwa viwango vya kimataifa.
Safari za nje
za EAAC ziliokoa muda na rasilimali nyingi sana kwa nchi wanachama kwani ndege
zake zilikuwa zikienda duniani kote na kutoa ushindani mkubwa. Kwa safari
zozote za nje usafiri ulikuwa ni wa kwetu wenyewe!
Kwa safari za
ndani, nchi yote hii kubwa ya Tanganyika unavyoiona, basi ndege zake za F27 na
Twin3 zilikuwa zinaifika. Iwe Masasi, iwe Njombe; iwe Mafia, iwe Nachingwea
kote huko ndege zilikuwa zikienda na kurudi, wakati huo wa zamani yapata karibu
miaka 70 sasa. Mishahara ya wafanyakazi ilikuwa juu sana ya kupigiwa mfano.
Kulikuwapo na
shirika kubwa sana la Bandari la Kupakia na Kusafirisha Mizigo ndani na nje ya
nchi (East African Cargo Handling Services), lililokuwa na jukumu la pamoja la
kushughulikia mizigo inayotoka na kuingia kwenye nchi, si tu zile wanachama,
bali na zile za jirani za Afrika Mashariki na Kati. Uchumi na mzunguko wa fedha
kwa miji ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Mombasa, Zanzibar ulikuwa mkubwa sana
kiasi cha kuwafanya wakazi wa miji hiyo kuishi maisha ya raha mno. Ajira za
bandarini siku hizo zilikuwa hazikauki bali zinatafuta watu wako wapi waje
kuzijaza!
Mishahara ile
minono pamoja na ‘overtime’ zisizokwisha, iliwapa jeuri hata watu wa kawaida tu
wanaofanya kazi bandarini; kwani waliweza kujenga nyumba zao bila mikopo na
kuweza kununua nguo za fahari kwelikweli kutoka maduka makubwa ya B. Choitram,
J.R. Stephens, Afi na Teekay ya pale
Independence (sasa Samora) kwa hapa jijini.
Amini au
usiamini, hiyo ni shauri yako; lakini ikutoshe tu kwamba wakati ule wa uhai wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, hakukuwa na haja ya mtu kwenda kutafuta mitumba ‘iliyonajisiwa’
na wazungu wa Ulaya, na viatu – eti raba mtoni— vinavyotoa harufu mbaya ya
fangasi za Wazungu miguuni kule Manzese, Tandika na Machinga Complex Ilala.
Kulikuwa na
Shirika la Reli la Afrika Mashariki pia. Nchi yote hii kubwa, lakini ilikuwa
inafikiwa na treni kirahisi kabisa. Abiria waliweza kusafiri wao na kusafirisha
mizigo pamoja na mazao kutoka nchi nzima kila siku. Pale ambapo treni haikuweza
kufika, basi safari hiyo ilifanywa na mabasi makubwa na imara ya EARC. Barua na
vifurushi viliweza kuwafikia walengwa kwa wakati popote pale katika Afrika
Mashariki na dunia kwa kutumia Shirika la Reli la Afrika Mashariki.
Ajira kwa
watu wa Afrika Mashariki zilikuwa za kumwaga tu katika shirika hili la Reli.
Mijini na vijijini watu waliajiriwa kwenye shirika mama na kampuni tanzu za Shirika
la Reli kila kukicha na kuwafanya watu waneemeke.
Mimi
nilizaliwa mwaka 1949 hapa Dar es Salaam; na watu wa kwanza niliowaona
nilipofungua macho walikuwa ni babangu na kakake mkubwa waliokuwa wakiishi
nyumba moja pale Kisutu Dar es Salaam. Mzee Yahya na Mzee Mohammed wote hao walikuwa
waajiriwa wa Shirika la Reli Afrika Mashariki; mkubwa akiendesha treni na mdogo
wake akiwa fundi kwenye karakana ya vyuma (locomotive workshop).
Mabehewa ya
treni yalikuwa safi na maridadi kwelikweli na watu wakisafiri kwa madaraja (I,
II, III) na treni zilikuwa zikifika vituoni kwa wakati na sio kwa kubahatisha
tu. Kila safari ilikuwa na mabehewa yanayotoa huduma ya chakula (Buffet Car).
Huduma zilikuwa za hali ya juu sana kiasi kwamba mimi mwandishi sikupatapo
kujua kula chakula kwa vijiko, visu na uma mpaka pale (mwaka 1967),niliposafiri
na babangu mkubwa kutoka Dar kwenda Dodoma katika treni ya Abiria na yeye ndiye
aliyenionyesha kisu kinashikwa hivi na uma unashikwa vile.
Msomaji,
Shirika hili la Reli Afrika Mashariki lilikuwa na hoteli kubwa kwenye kila mji unaoujua
wewe katika Afrika Mashariki. Kwa mfano ukisikia Musoma Hotel, Mwanza Hotel,
Dodoma Hotel, Tabora Hotel, Mbeya Hotel n.k, zote hizo zilikuwa mali ya Shirika
la Reli Afrika Mashariki. Meli zote kwenye maziwa makuu zilimilikiwa na shirika
hilo pia.
Huko miaka ya
nyuma, nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zikitumia sarafu moja ya fedha
zilizotolewa na Benki Kuu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board).
Nguvu ya fedha kwa nchi zote wanachama ilikuwa moja; siyo kama ilivyo sasa
Kenya wakitupita kwa mbali wenyewe tukichechemea kama mtu aliyepata ajali.
Tukiwa sasa
tumeachwa nyuma na kila nchi duniani kielimu, kiwango cha elimu Afrika
Mashariki wakati wa EAC kilikuwa kimoja na mitaala ikitolewa na Board ya Elimu
ya Afrika Mashariki na mitihani yote ya A na O level ikisahihishwa Chuo Kikuu
cha Cambridge, Uingereza, chini ya East African Examination Council. Hapakuwa
na wasiwasi wa upendeleo au kuonyeshwa mtihani mapema kama tufanyavyo sasa.
Yalikuwa ni maendeleo makubwa mno; sijui sasa tumetumbukia shimo gani hatuwezi
tena kuja juu!
Ushuru wa
Forodha (Customes and Excises) ulikuwa na shirika lake lenye Makao Makuu, kule
Mombasa Kenya. Utabiri wa Hali ya Hewa ilikuwa ni jukumu la Idara ya Hali ya
Hewa Afrika Mashariki, lenye Makao Makuu kule Dagoreti Kenya. Kwa huduma za usafiri
wa angani (air navigation) huduma Afrika Mashariki yote hii zilikuwa zikitolewa
viwanjani na Idara ya Usalama wa Anga (Directorate of Civil Aviation East
Africa)—sasa TCAA.
Katika safari
ndefu ya maisha, mwandishi huyu aliajiriwa kazi kwa mara kwanza na Kurugenzi ya
Usalama wa Anga ya Afrika Mashariki mwaka 1970 na kupata mafunzo ya kuwa
Aeronautical Communications Officer pale School of Aviation, Wilson Airport, Nairobi.
Baadaye nilipata
mafunzo mengine ya juu pale kwenye Chuo cha
Ecole Nationale de la Aviation Civil— L’ENAC, pale Toulouse, Ufaransa.
Kule Ufaransa nilitembelea maonyesho makubwa ya ‘madege’ duniani yanayojulikana
kama Le Bourget Air Show, pale jijini Le Bouget. Nilitembelea pia kiwanda
kikubwa kinachotengeneza matumbo (fuselage) ya ndege za Airbus, Airbus
Industry. Injini za ndege hizo hutengenezwa nchini Marekani na Kampuni ya
General Electric.
SARCAT—CORPUS
ni mahala pengine nilipofika. Ni kituo kikubwa cha Satelaiti duniani ambacho
nchi hasimu Marekani na Urusi (bila kujali tofauti zao za kiitikadi na kisiasa)
zinashirikiana kutoa huduma pamoja kwa usalama wa safari za ndege duniani
(safety of air navigation). Ndege itakapoanguka kokote duniani, hata iwe maporini
labda Mpwapwa, Tanzania, basi kituo hicho kitaweza kuonyesha mahala
ilipoangukia na hivyo kufanya uokoaji kuwa mwepesi.
Inaniuma roho
sana kuwa leo EAC haipo, ila kuna ‘mfufuko’ wake tu uliojaa matatizo lukuki
kabla hata haijawa rasmi! Mh! Sijui; lakini naona ni porojo tu za siasa
(political rhetorics), hakuna kitakachozuka pale.
Jumba lile
kubwa la AICC pale Arusha ndipo ilipokuwa Makao Makuu ya Afrika Mashariki na
likiitwa EAC—HQs. Ukilipiga picha kwa juu plani yake inaashiria herufi ‘H’ kwa
maana ya Headquarters. Jumba lile
halikuwa mali yetu Watanzania hata siku moja, bali tulilirithi baada ya kuuawa
mwenye nyumba.
Jiji la
Arusha, pamoja na vivutio vyake vya utalii, lakini lisingekuwa na hadhi ile
kama si uwepo wa EAC, Makao Makuu na nyumba za watumishi zilizotapakaa mji
mzima. Hata siku moja sikuwahi kuisikia Serikali ya Tanzania ikieleza wapi
ililipata jengo lile zuri la AICC. Mzee Malecela anajua hilo; Alnoor Kassam
anajua hilo; na Cleopa Msuya anajua hilo kwani hawa wote walipata kuwa mawaziri
wa Afrika Mashariki wenye ofisi zao pale EAC—HQs.
Jumba lile ‘ng’areng’are’
tulilirithi kama vile tulivyorithi ile ATC House pale Ohio; Bandari House pale
Bendera Tatu; Customs House (sasa TRA) pale Samora; Jumba la Wizara ya Nishati na
Madini (pale Sokoine); jumba la Extelecoms pale Samora; Jumba la Posta House
pale Ohio; pamoja na majengo yote unayoyasikia yanaitwa ya Posta hapa Dar es
Salaam yalikuwa mali ya Afrika Mashariki.
Pamoja na
utajiri mkubwa kama huo wa rasilimali ambazo tumezirithi kutokana na kuvunjika
kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bado tumeshindwa kuziendeleza wakati wenzetu
wa Kenya wamepiga hatua kutoka walipochukua mpaka kufikia leo. Shirika la Ndege
la KQ ni moja ya mashirika makubwa duniani. Kenya leo kwenye Shirika lake la
Reli inatoa huduma ya treni kwa jiji la Nairobi kwa watu wapatao 30,000 kwa
siku pamoja na stesheni kubwa kubwa za kisasa jijini humo (tembelea google
Kenya Railways). Sijui katuroga nani, lakini ni msiba mkubwa sana unapoona
bandari moja tu ya Mombasa, ikizipiku bandari ya Dar, Mtwara, Tanga na ile ya
Zanzibar hapa kwetu.
Kwenye Posta
na Simu hali ndio hivyo hivyo. Majumba ya kilichokuwa Chuo cha Posta pale
Kijitonyama yameuzwa kitambo. Sijui kwa nini kwa maana, “utaukataaje ukunga na
uzazi ungalipo!” kaimba mwimbaji Bi Kidude.
Sehemu ya pili ya makala haya ya
Afrika Mashariki itaendelea wiki ijayo.
Simu
0715808864
No comments:
Post a Comment