Friday, 9 March 2018

BI. CHIKU KISUSA (MAMA SAKINA)

Kulia Bi. Chiku Kisusa (Mama Sakina), Bi. Titi Mohamed, wa kwanza kushoto
Bi. Tatu bint Mzee wakiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam safari ya kwanza UNO 1955

Picha hii inamuonyesha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na akina mama watano ambao walimsindikiza Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam safari ya kwanza UNO mwaka wa 1955.



Hii picha alinipatia marehemu Jim Bailey mmiliki wa gazeti la Drum lililokuwa likichapwa Johannesburg sasa zaidi ya miaka 30. Bailey alinipatia picha hii pamoja na nyingine wakati nilipokuwa nafanya uhariri wa kitabu chake cha picha, ‘’The Story of Julius Nyerere.'' Nilimfahamu Bailey kupitia rafiki yake Ally Sykes.

Katika  picha hii kwa miaka mingi sana niliweza kupata majina mawili tu ya akina mama hawa. Kulia wa kwanza Bi. Tatu bint Mzee wa tano Bi. Titi Mohamed.

Jana tarehe 8 March nimeletewa jina la huyo Bi. Mkubwa wa kwanza kulia. Huyo ni Bi. Chiku Kisusa mama yake Maalim Sakina binti Arab, mwanamama maarufu sana katika mji wa Dar es Salaam ya 1950s na mmoja wa wanawake wa mwanzo kabisa kujuana na Mwalimu Nyerere alipofika Dar es Salaam mwaka wa 1952 na kuingia katika siasa za TAA kisha TANU.

Juhudi za kuitembeza hii picha kutafuta majina alifanya rafiki yangu wa miaka mingi Juma Bilal Khamis ambae yeye Maalim Sakina ni shangazi yake. Mama Sakina yaani Bi. Chiku Kisusa nyumba yake ilikuwa Mtaa wa New Street na Mchikichi na ni moja ya nyumba ambazo Mwalimu Nyerere alikuwa akipokewa kwa mikono miwili wakati wa harakati za kudai uhuru akiongozana na mwenyeji wake Abdulwahid Sykes.

Mama Maria Nyerere katika siku hizi za mwanzo za harakati aliishi kwa karibu sana na watoto wa Bi. Chiku - Maalim Fatna na Maalim Sakina kiasi kuwa Mama Maria alipata kufungua kijiduka cha mafuta ya taa hapo mtaani. Hii ‘’Maalim,’’ hawa ndugu wote wawili walikuwa waalimu katika Al Jamiatul Ismaiyya fi Tanganyika Muslim School, shule iliyokuwa Mtaa wa New Street na Stanley.

Utambuzi huu wa sura ya Bi. Chiku kaufanya Bi. Sauda mjukuu wa Bi Chiku. Kwangu mimi Bi. Sauda ni dada yangu na kanipita umri si haba. Wadogo zake marehemu Tahiyya na Jamila ndiyo makamu yangu.

Hivi sasa nyumba hii ya Bi. Chiku Kisusa iliyokuwa Mtaa wa Mchikichi haipo tena na badala yake kuna nyumba ya ghorofa kumi.

Sasa katika kuhangaika huku ndipo nikapata kisa kingine ambacho sikuwa nakijua.

Mwalimu Nyerere aliporudi kutoka UNO 1955 mtoto aliyemvisha skafu Baba wa Taifa alikuwa Jamila, mjukuu wa Bi. Chiku Kisusa.

No comments: