TANGULIA LUKUGA DKT. AMANI WALID KABOUROU - KINARA WA MAGEUZI YA VYAMA
VINGI NCHINI - MWAMI KABUYUKI MWAMBA WA KIGOMA
Dkt. Aman Walid Kabourou |
Asubuhi ya jana,
nimeamshwa na simu ya Baba yangu Mzee Kabwe. Sio kawaida yake kunipigia simu
asubuhi namna hii, nami nilikuwa nimelala nimejichokea kufuatia kazi za siku ya
juzi za kumtembelea diwani wa Chama chetu cha ACT Wazalendo, hapa Kasulu. Licha
ya uchovu mkubwa, pia nilichelewa kulala kwa sababu ya Mpira, timu
ninayoishabikia nchini Uingereza ya Liverpool ilikuwa inacheza na timu ya FC
Porto ya Ureno.
Naitazama simu
naiogopa! Simu inakatika! Nikampigia simu baba, ambaye kwa majonzi makubwa akanijulisha
kwamba mwamba wa Kigoma hatunao tena! Dkt. Aman Walid Kabourou, mbunge wa
kwanza wa jimbo la Kigoma Mjini mara baada ya vyama vingi ametutoka,
ametangulia mbele ya haki. Inna lillah waina ilaih raajiun.
Kwa umri wake
Dkt. Kabourou ni mjomba wangu, na kwenye siasa yeye ni mlezi wangu. Hivyo
wajibu wangu wa kwanza kama mtoto awali ya yote ni kumsitiri mzazi wangu. Baada
kupata taarifa hizi za majonzi, nilizungumza na Diwani wetu kule Ujiji, ndugu
Fuad Seif wa Kata ya Kasimbu, ambaye ni mkwe wa Dkt. Kabourou, kuhusu mipango
ya mazishi. Baadaye nilizungumza na ndugu wa marehemu waliopo Dar es Salaam.
Wote walinithibitishia kwamba wosia wa marehemu ni mauti yakimkuta, basi azikwe
Ujiji, Kigoma.
Hivyo baada ya
kuwa sasa tumeshaandaa taratibu za mazishi yake hapo kesho, nami nimepata wasaa
wa kuandika machache juu yake, na hii ni ada kwangu, kuandika tanzia ya kila
marehemu anayenigusa binafsi au kuligusa Taifa. Dkt Kabourou ana sifa zote
mbili, ananigusa binafsi, na anao mchango mzito kwa Taifa letu, zaidi msiba
wake ni jambo zito hapa Kigoma Mjini, mahali ambapo mimi ni mwakilishi wa
wananchi.
Hii ni kutokana
na mchango mkubwa wa Dkt. Kabourou kwenye ujenzi wa siasa za vyama vingi nchini
Tanzania. Yeye ndiye Mbunge wa kwanza nchini kuchaguliwa na wananchi baada ya
mfumo wa vyama vingi kurejeshwa nchini 1992!
Yeye ndiye
aliyepandikiza mbegu nzuri ya Watanzania kukataa kuburuzwa na kusimamia haki
zao, ambapo kupitia kwake mwanga wa ukombozi katika siasa za vyama vingi
ulienea kote nchini. Jambo hili alilifanya zaidi hapa Kigoma, kwa maana
nyingine, Kigoma ndio mkoa wa kwanza kuonesha kwa vitendo utayari wa kupokea
vyama vingi nchini, yote ni kwa sababu ya kazi ya ‘Uamsho’ ya Dkt. Kabourou. Ni
mbegu hii ya mageuzi aliyoipanda ndiyo iliyofanya wakati flani Mkoa wote wa
Kigoma ukawa na idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama vya upinzani.
Dkt. Kabourou
ana historia ndefu, tangu zama za usomi wao na rafikiye Manju Salum Msambya,
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini. Ujio wa Dkt. Kabourou kwenye siasa haukuwa
wa hiari, ulitokana na wito wa wazee wa Kigoma, baada ya habari mbaya ambayo
Mkoa wa Kigoma uliipata Oktoba, 1993, ya msiba mzito wa marehemu Rajab Omar
Mbano Kakolwa, aliyekuwa mbunge wetu wa hapa Kigoma Mjini, aliyefariki dunia
ghafla huko Dar es Salaam.
Kifo cha mzee
Mbano kilitustua sana wana Kigoma. Kwa kuwa Nchi ilikwishaamua kurejea kwenye
mfumo wa vyama vingi, uchaguzi mdogo
ilibidi ushirikishe vyama vingi. Hapo ndipo jina la Dkt. Aman Walid Kabourou
likaibuka kwenye siasa za Kigoma na Tanzania kwa ujumla. Akiwa Profesa wa
Historia huko Marekani, aliombwa na kuridhia
kurudi nyumbani na kuendeleza kazi ya marehemu Mbano, ambaye alikuwa
akishirikiana kwa karibu sana na mzee
Manju Msambya. Aidha, katika kipindi hicho Mzee Msambya alikutwa na
ajali mbaya ya gari, iliyomfanya alazwe hospitalini kwa kipindi mrefu. Hakika zilikuwa ni nyakati za
majaribu kwetu.
Dkt. Kabourou
aligombea dhidi ya Azim Premji wa CCM, Hussein Beji NCCR na Kashugu Anzaruni wa
TADEA, na kampeni zilikuwa moto sana. Yalipotangazwa matokeo pale ukumbi wa
Magereza Bangwe, Premji wa CCM alitangazwa mshindi. Dkt. Kabourou alifungua
shauri Mahakamani kupinga ushindi wa Premji, na kesi husika ikatumika kuonyesha
namna rasilimali na miundombinu ya Serikali, ilivyotumika kumfaidisha mgombea
wa CCM.
Kesi hii ina
maana kubwa sana kwa mageuzi, majina ya mawakili wa Dkt. Kabourou, ndugu Boaz
na mzee Bob Makani yakawa gumzo mjini Kigoma na nchi nzima. Watu walikuwa
wanashinda Mahakama ya Kigoma kusikiliza kesi hii, na watoto wengi Kigoma
waliozaliwa wakati huo walipewa majina Makani, Boaz na Vema, kumaanisha kura ya
ndiyo (V). Dkt. Kabourou mwenyewe mtoto wake mmoja anaitwa Vema. Rafiki na
ndugu yangu wa karibu, Boaz Chuma pia alibadili jina lake alilopewa na Mzee
Ndaha na sasa kila mtu anamjua kwa jina la Boaz kwa sababu ya kesi ile. Utaona
athari za kesi husika kwetu.
Kesi ilikwenda
mpaka Mahakama ya rufaa ambapo Azim Premji alivuliwa Ubunge. Katika Kipindi
ambapo kesi husika ilikuwa inaendelea, kazi kubwa ya ujenzi wa chama chake,
Chadema ilifanyika mkoani Kigoma, kuelekea Uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.
Kazi hiyo ya
Ujenzi wa Chama, uliiwezesha Chadema kupata Madiwani wa kwanza nchini katika
Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 1994, madiwani hawa ndio wa kwanza kwa
chama hicho kabla ya Mkoa mwengine wowote nchini. Shaaban Mambo, Makamu
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, ambaye baadaye alikuwa Naibu Meya na
Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, miongoni mwa madiwani hao wa mwanzo kabisa.
Kazi ya
mafanikio hayo ya Kimageuzi yaliyoletwa naye Dkt. Kabourou haikuwa lelemama,
ilikuja na machungu makubwa sana. Katika kata ya Mwandiga, Vijana kama kina
Nyembo Mustafa wanaweza kuelezea kwa undani simulizi nzuri na za kusisimua
kuhusu namna Dkt. Kabourou alivyokuwa anatembea usiku kucha kwenye mifereji ya
maji kujificha kukamatwa na polisi wakati wa ujenzi wa Chama na kuwezesha
Diwani Sempa kushinda udiwani kata ya Mwandiga.
Kipindi hiki
kilishuhudia Vijana wengi wakifungwa jela kwa sababu za kisiasa. Matukio
yanayotokea sasa ya wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani kukamatwa na
kuswekwa jela si mapya, sisi Kigoma, chini ya Dkt. Kabourou tumeyaishi, inaudhi
tu kuwa sasa tunarudishwa tulikotoka.
Vijana wa
Mwandiga wakati mwengine walilala juu ya dari za nyumba zao ili kukwepa polisi.
Hakika mazingira ya sasa ya siasa za nchi yetu yanawakumbusha watu wa Kigoma
miaka 23 iliyopita. Pia Demokrasia tuliyonayo sasa kwa kiwango kikubwa
ilichangiwa na kujitoa muhanga kwa Vijana hawa wa Kigoma chini ya Uongozi wa
Dkt. Kabourou na wenzake, kina Mzee Menge (marehemu), Mzee Kasisiko, pamoja na
wengine wengi.
Mwaka 1995
ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa
tena. Uchaguzi huo ulikuwa wa kihistoria, na Dkt. Kabourou akaendelea
kuimarisha historia yake na heshima kwa mkoa wa Kigoma, akawa Mbunge wa kwanza
wa Kigoma Mjini kutoka Upinzani kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza. Kipindi hicho
chama kikuu cha upinzani kilikuwa NCCR - Mageuzi.
Kwenye uchaguzi
huo CHADEMA ilipata majimbo matatu tu ya Kigoma Mjini, Rombo kwa Justine
Salakana, na Karatu kwa Dkt. Wilbroad Slaa. Hata hivyo Dkt. Kabourou alipoteza
nafasi ya Ubunge kufuatia Mahakama kutengua ushindi wake. Uchaguzi wa marudio
ulipofanyika mwaka 1999 vurugu kubwa zilitokea na kupelekea Viongozi zaidi ya
40, akiwemo Mzee Jaffary Kasisiko kuwekwa ndani kwa miezi miwili na zaidi.
Hali ya siasa
ilikuwa mbaya sana Kigoma mjini, uhasama dhidi ya wakazi ulikuwa mkubwa sana.
Kuna simulizi kwamba aliletwa ngamia Kigoma ili kufanya dua kuondoa uhasama
uliokuwepo baada ya uchaguzi huo mdogo uliacha ufa mkubwa kwa watu. Katika
kipindi hicho jitihada za kufanya siasa na kusambaza Chama Mkoa wa Kigoma
ziliendelea, jambo lililomuwezesha Dkt. Kabourou kushinda Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2000.
Mwaka 2000 Dkt.
Kabourou aliongoza kampeni zilizofanikiwa kupata Uongozi wa Halmashauri ya Mji
wa Kigoma Ujiji ambapo Chadema ilipata madiwani wengi zaidi. Kipindi hiki
alifanikiwa pia kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kabla ya kumpisha
Dkt. Slaa kwenye nafasi hiyo mwaka 2004, ambapo pia Dkt. Kabourou alichaguliwa
kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama chake na Dkt. Slaa akawa Katibu Mkuu.
Kwenye jimbo
Dkt. Kabourou alifanikiwa kumaliza muda wake wa Uongozi. Hata hivyo, kwenye
Chama chake ukaibuka mgogoro mkubwa kati yake na viongozi wenzake, kutokana na
sababu mbalimbali, ikiwemo kugombania madaraka na chuki binafsi. Ilipofika
Mwaka 2005 Dkt. Kabourou aligombea Ubunge bila kuungwa mkono na Chama chake ngazi
ya Taifa, jambo lililofanya apoteze nafasi ya Ubunge kwa mwanasiasa mpya
kabisa, Peter Serukamba.
Ilikuwa mshtuko
mkubwa kwetu, kwani pia ndio mwaka mimi niligombea Ubunge kwa mara ya kwanza,
jimbo la Kigoma Kaskazini, Dkt. Kabourou ndiye aliyezindua kampeni zangu Katika
kijiji cha Bitale na kunipa baraka zote. Nilitarajia kuwa yeye ndiye
angeniongoza Bungeni, lakini hakuweza. Nilifanya Mkutano pale Sign Atlas Ujiji
mara baada ya uchaguzi wa 2005, baada ya mkutano watu wengi walitokwa na
machozi pale nilipowaeleza namna naenda Bungeni nikiwa mkiwa bila kwenda na
Mwalimu wetu wa Siasa, Dkt. Walid Amani Kabourou.
Kuanguka kwa
Kabourou mwaka 2005 na hulka ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani
kushindwa kutatua migogoro ya ndani ya vyama vyao, kulimfanya aamue kubadili
siasa na kuhamia CCM, akiondoka Chadema, chama ambacho alinunua Ofisi za Makao
Makuu yake, pale Kinondoni, mtaa wa Ufipa, wakati akiwa Kiongozi. Baada ya
kuhamia CCM aligombea Ubunge wa Afrika Mashariki mwaka 2007 na kushinda. Mwaka 2012
akawa pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, kwa muda wa miaka mitano.
Uamuzi huo wa
Dkt. Kabourou wa kuondoka upinzani ulitakiwa kuwa na funzo kwetu sisi wanasiasa
wa vyama vya upinzani, kwamba hakuna tofauti ambazo haziwezi kuzungumzwa na
kutatuliwa, maana ni uamuzi uanaoathiri imani ya wananchi juu ya uwezo wetu wa
kiuongozi. Bahati mbaya sana tunajifunza taratibu na kuendelea kufanya makosa
yaleyale. Jambo hili halina afya kwa mustakbali wa siasa za nchi yetu, ni
lazima upinzani tujifunze kutazama picha kubwa ili kuepuka kupoteza miamba ya
aina ya Dkt. Kabourou.
Dkt. Kabourou
alifanya kazi moja kubwa kwa watu wa Kigoma, alitufungua macho kuhusu haki
zetu. Alikuwa mtetezi mkubwa wa haki za watu wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
Alifungwa jela mara kwa mara kwa kusimamia haki za watu wa Kigoma. Alifanya
mikutano mingi na Wananchi kuelimisha watu Kuhusu haki zao kipindi ambacho watu
wengi walikuwa kwenye giza nene, katika kipindi ambacho wasomi wengi walikuwa
wanajiweka karibu na watawala. Dkt. Kabourou alikwenda katika kila kijiji, mkoa
mzima wa Kigoma kufanya kazi ya kutoa elimu ya siasa na kuamsha Wananchi.
Wananchi
walikuwa wanakusanya pesa kumchangia mafuta ili aweze kufika kwenye vijiji vyao
kuwaeleza masuala mbalimbali ya nchi yetu. Alitujengea ujasiri mkubwa. Aliitwa
majina mbalimbali kama vile Lukuga, jina la mto mkubwa unaotoa maji Ziwa
Tanganyika kupeleka mto Kongo. Pia Lukuga ni upepo mkali ziwani ambapo ukivuma
huwa ni hatihati kwa wenye maboti. Alikuwa ni upepo mkali wa kufukuza udhalimu,
alikuwa ni Mwalimu wa Haki, Utu, Demokrasia na Usawa.
Dkt. Kabourou
amefariki dunia tukiwa kwenye kazi moja kubwa. Mwaka jana (mara baada ya kuwa
ameshindwa Uchaguzi wa Uenyekiti wa CCM Mkoa) nilimnasihi mambo mawili. Mosi
ilikuwa ni aanze kuandika historia ya maisha yake ili vizazi visome harakati
zake za siasa na kuhudumia Wananchi, mchango wake kwenye Demokrasia ya nchi nk,
na pili kuanza mradi wa kuandika Historia ya kwetu mirumbani, Ujiji. Dkt.
Kabourou alikuwa mwanahistoria kitaaluma na nilitaka atumie muda wake wa
ustaafu kuandika Historia ya Mji wa Ujiji ambao ulianza miaka mingi sana, karne
ya 17.
Tayari tulikuwa
tumepata andiko la shahada ya uzamivu (PhD) lililoandikwa na mwanahistoria
mmoja huko Marekani, mwaka 1973, juu ya historia ya mji wetu wa Ujiji ambalo
lilipaswa liwe kianzio cha kazi hii ya kuandika historia ya Ujiji. Sina hakika
kama Dkt. Kabourou alianza kuandika kuhusu historia yamaisha yake, kifo chake
kinaongeza orodha ya wazee wetu wanaondoka bila kuacha mafunzo ya maisha yao kwa
kizazi cha sasa cha taifa letu.
Sisi viongozi vijana
wa Kigoma hatukuacha kumtumia Dkt. Kabourou, tukichota busara na hekima zake
kila pale inapobidi. Katika kazi zake za mwisho mwisho ilikuwa ni kuhudhuria
kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Kigoma, ambapo moja ya ajenda ilikuwa ni
kutoa majina kwa baadhi ya mitaa ya Manispaa ya Kigoma Ujiji. Katika Kikao kile
tulipanga kutoa majina ya mitaa na barabara kwa kwa wabunge wote wa Mkoa wa
Kigoma waliopita. Yeye ndiye aliyenipa orodha ya wabunge wote waliopita.
Mjadala ule wa
kuipa majina mitaa yetu ulitugawa, ulipokuwa mkali sana, Dkt. Kabourou
alisimama na kuniunga mkono kuhusu suala la kumpa heshima anayostahili
mwanaharakati wa Haki ulimwenguni Ernesto Che Guevara wa Cuba, ambaye aliishi
hapa Kigoma Ujiji wakati akisaidia mapambano ya msituni ya kumng’oa Dikteta
Mobutu Seseseko wa Zaire. Dkt. Kabourou akijenga hoja kuwa si tu kuupa mtaa
jina la Che Guevara tunalinda historia yake, bali pia tunalinda historia ya
Zaire (sasa DRC Congo) mkoa wetu wa Kigoma, na Taifa kwa ujumla.
Jambo
lililoungwa mkono na wajumbe wote, ikionyesha uwezo wake wa ushawishi, busara
na hekima zake hata sasa ambapo alikuwa mstaafu. Ernesto Che Guevara tumempa
jina la barabara ya kwenda Bangwe kutokea stesheni ya reli, mtaa ambao aliishi
wakati wa harakati zake. Kuenzi kazi na mchango wa Dkt. Kabourou kwa mkoa wa
Kigoma na Tanzania kwa ujumla, nitawashauri viongozi na wananchi wenzangu kuipa
jina la Dkt. Kabourou barabara ya kutoka
Uwanja wa Ndege wa Kigoma (Gombe Mahale Airport) ili kila anayeingia Kigoma kwa
njia hiyo ajue kuwa tumewahi kuwa na Mwamba, Rukuga Dkt. Amani Walid Kabourou.
Hakika Kabourou
amefariki na Kigoma yake moyoni. Kesho, Mola akitujaalia, tutampumzisha kwa
heshima zote anazostahili, kama mzazi na kiongozi wetu. Huyu ni shujaa wa
Kigoma na Taifa kwa ujumla. Tumepoteza Jabali la siasa za mageuzi, tumepoteza
upepo (Lukuga) wa kufukuza udhalimu, tumepoteza mwalimu wa Haki, Utu na
Demokrasia, tumepoteza Mwanahistoria, na binafsi nimepoteza Mlezi.
Allah ampe
pumziko la amani.
Kabwe Z.
Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa
Chama, ACT Wazalendo
Kata ya
Muhinda
Buhigwe
Kigoma
Machi 8, 2018
No comments:
Post a Comment