Monday, 12 March 2018

DOSSA AZIZ YEYE NA TANU TANU NA YEYE - ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA


Mbele aliyesimama kushoto ni Abbas Sykes, waliokaa mbele kushoto ni Doosa
Aziz na Julius Nyerere ni wa sita waliokaa

Kushoto Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona




Shajara ya Mwana Mzizima
WAZIRI DOSSA AZIZ: YEYE NA TANU, TANU NA YEYE
Na Alhaji Abdallah Tambaza
WILAYANI Temeke, jijini Dar es Salaam, kuna eneo linaitwa Mtoni. Mtoni yenyewe nayo ina mitaa mingi ikiwamo Mtoni Kijichi, Mtoni Mtongani, Mtoni kwa Chaurembo, Mtoni kwa Mwenye—Kuuchimba na Mtoni kwa Aziz Ali.

Hapa Mtoni kwa Aziz Ali, siku nyingi nyuma alipata kuishi bwana mmoja aliyekuwa mmoja wa Waafrika matajiri sana kupata kutokea wakati huo wa ukoloni nchini Tanganyika. Aliitwa Azizi Ali Dossa; na kwa hiyo kutokana na umaarufu wake, mahala hapo pakaitwa Mtoni Kwa Aziz Ali.

Aziz Ali, alikuwa Mdigo aliyetokea sehemu za Tanga na kuja kuweka kambi mjini Mzizima, ambako alijitengenezea umaarufu kutokana na kwamba aliweza kumiliki ‘majumba’ mengi, ‘magari’ ya biashara (yaani malori ya mchanga) pamoja na ya kutembelea, na vitu vingine kadhaa, kutokana na kazi yake ya kuwa mtaalamu wa kujenga nyumba (building contractor).

Mzee Aziz Ali, katika uhai wake alijaaliwa kupata watoto kadhaa ambao kutokana na nguvu yake ya fedha aliweza kuwapatia elimu bora ambayo ilikuwa adimu wakati huo wa utawala wa kikoloni wa Kiingereza, ambao walitoa elimu hapa ilimradi kukidhi mahitaji yao wao tu.

Miongoni mwa watoto hao, ambao pia walikuja kuwa maarufu hapa kwetu Mzizima, ni pamoja na Juma Aziz; Ramadhani Aziz, aliyekuwa afisa mkubwa bandarini Dsm; Mwanakombo Azizi, Afisa Mwandamizi wa Jeshi la Polisi kabla na baada ya uhuru; Ali Aziz, kachero wa Jeshi la Polisi pia; Hamza Azizi, kachero Jeshi la Polisi la kikoloni na baadaye akawa IGP wakati nchi ya Tanganyika ilipopata uhuru wake.

Waziri Dossa Azizi, ndiye aliyekuwa mtoto mkubwa wa Mzee Aziz Ali. Huyu alikuja kuungana na wapigania uhuru wengine  mashuhuri hapa nchini (akina Mwalimu Nyerere hao), akaja kutoa mchango mkubwa sana kwa nchi yake, lakini leo jina lake limesahauliwa miongoni mwa vizazi vya leo. Katika harakati za kupigania uhuru, hayati Mzee Dossa, unaweza kusema alikuwa yeye ni TANU; na TANU ni yeye! Usingeweza kumtenganisha hapo.

Dossa Aziz, alikuwamo katika kuasisi vyombo vyote vya mwanzo vinavyonasibishwa na harakati za kumng’oa Mkoloni, kama vile TAA na TANU akiwa Afisa na Mjumbe mwanadamizi aliye na sauti - hili  sawa; hili fanya; hili wacha na mambo yakawa hivyo asemavyo.

Dossa, kwa kushirikiana na mwanachama mwengine Alexander Tobias, walichaguliwa na wenzao wakati fulani wawe makatibu wa pamoja wa muhtasari. Harakati ziliposuasua alikuwa hachoki kuwapitia wenzake na kuwakumbusha majukumu waliyopeana akienda kwa mmoja mmoja nyumbani kwake kwa kutumia gari lake na kutaka kujua kulikoni mambo hayendi ipasavyo.

Habari zinasema, ilikuwa ni Dossa Aziz aliyemwomba Nyerere kuacha tena kuvaa kaptura mbele ya wazee, kwani sasa ameshakuwa kiongozi ambaye atakuwa akikutana na watu wazima na hivyo si vizuri kuonekana na kaptura na stockings (zile soksi ndefu mpaka magotini). Mzee Dossa alifanikiwa katika  hilo kwani alimnunulia pia Nyerere suti kadhaa maridadi katika safari yake ya kule UNO -Umoja wa Mataifa, kupeleka kilio cha Watanganyika kudai nchi yao.

Katika siku za mwanzo za harakati, chama cha TAA na baadaye TANU havikuwa na uwezo wa kifedha wa kujiendeshea mambo yake hata kidogo. Tegemeo lao kubwa lilikuwa ni kwa watu kama akina Dossa Azizi, aliyekuwa mkurugenzi na msimamizi mkuu wa biashara na mali za babake. Wengine ni Mzee John Rupia na wale akina Sykes watatu (Abdul, Ally na Abbas), ambao baba zao walikuwa na uwezo wa fedha, ‘wawapige jeki’ (wachangie pakubwa).  

Katika hilo, Dossa Azizi alikuwa mstari wa mbele sana kwa nguvu zake na mali yake, kwani katika vita ile, si tu aliizunguka nchi hii yote na wenzake kuhamasisha na kufanya mikutano mbalimbali na wadau walioko mikoani, lakini pia alitoa gari la mwanzo kabisa aina ya Land Rover kwa chama cha TANU litumike kwa shughuli za siasa ili nchi yetu iwe huru.

Kutoa gari siku hizo si jambo la mchezo hata kidogo. Kwanza gari zenyewe zilikuwa chache mno. Hata hiyo serikali yenyewe ya kikoloni haikuwa na magari mengi. Land Rover ile iliyokuwa ikiendeshwa na dereva wa mwanzo kabisa wa TANU aliyeitwa Saidi Tano, nadhani ipo imehifadhiwa kama kumbukumbu muhimu za mapambano ya uhuru.

Dossa hakuishia hapo, lakini pia alikuwa akizitumia nyumba za kwao kufanyia vikao muhimu vya chama na baadaye kuwarudisha wajumbe majumbani kwao kwa gari lake jengine alilomiliki binafsi. Mwalimu Nyerere ilimbidi awe anampeleka mpaka Pugu alikokuwa akifanya kazi ya ualimu.

Msomaji, Pugu ile ya zamani si ya leo. Si barabara kuwa mbaya tu, lakini vilevile huwa ni majanga kama gari itakuharibikia wakati wa kurudi ukiwa peke yako, huku wanyama wakali kama Simba na Chui, wakirandaranda kutafuta mawindo.

Mwanahahistoria Rejea, wa harakati za kupigania Uhuru, ndugu yangu Mohammed Said, katika kuelezea mchango wa Dossa kwa kutoa gari lake, kwenye kitabu chake mashuhuri cha Maisha na Nyakati cha Abdulwahid Sykes, ameandika hivi:

“Dossa Azizi alikuwa amekwenda Nairobi kufanya usaili wa urubani akiongozana na mtoto wa tajiri mmoja wa kiarabu Ali Mmanga… Dossa alikataliwa kufanyiwa usaili kwa sababu alikuwa ni Mwafrika na wakati huo Waingereza walidai kuwa Waafrika hawakuwa tayari kufundishwa urubani. Alifadhaika sana akampigia simu babake huku akilia na kumpasha habari ile…

“…Babake alimtumia pesa anunue gari iwe kama kifuta machozi …gari hilo ndilo lilokuja kuwa chombo cha kwanza cha usafiri kwa TAA, TANU na Julius Nyerere mwenyewe,” anaandika Said ukurasa 166.

Wakati fulani nchi baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa akiumiza kichwa akitafuta mtu wa kumpa uongozi wa Jeshi la Polisi. Alipomshauri Dossa, haraka sana akamwambia ampe kazi hiyo nduguye Hamza Aziz. Nyerere alisita kidogo akihofia kwamba Hamza alikuwa bado kijana mdogo pengine kazi ile asingeiweza. Dossa akamwambia, ‘mpe ataiweza tuu’.

Hamza Aziz akawa IGP na akaifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa mpaka pale alipokuja kupata mkasa wa kumgonga na gari, maeneo ya Oysterbay, raia aliyekuwa  akitembea kwa miguu.

Hamza hakusimama kama sheria ilivyomtaka. Alikutwa na hatia na hivyo kutakiwa kujiuzulu wadhifa huo. Mwalimu alimpeleka Washington DC kuwa mwambata katika Ubalozi wa Tanzania Marekani.

Mtu mwengine mashuhuri aliyotokea katika ukoo wa Aziz Ali, ni Luteni Kanali Abdallah Juma Azizi. Kabla ya kujiunga na Jeshi, Abdallah Aziz alikuwa mchezaji mpira wa hali ya juu akichezea timu ya Dar es Salaam Kombaini na ile ya Taifa. Kwenye miaka ile ya 60, huyu ndiye aliyekuwa nyota mkubwa wa Timu ya Taifa la Tanganyika, akiwa mpachika mabao hatari kupitia winga ya kushoto. Alikuwa na chenga za maudhi, mbio za kasi na bila shaka yeyote ile kwa sasa ungeweza kumfananisha na Messi au Diego Maradona wa Argentina.

Alikuwa ni mchezaji muhimu na tegemeo kwa kweli na kama sio babake mkubwa Mzee Dossa Azizi kupinga hilo wazo la kumrudisha, basi pengine angekuwa mchezaji wa kwanza kurudishwa nyumbani kwa ajili ya mpira tu.

Sasa wakati bado tukimtafakari na kuungalia mchango na harakati za Dossa Aziz katika kuikomboa nchi yetu na madhila ya Waingereza wale ‘makatili na wakandamizaji’; habari za mchango wa Dossa Aziz hazitimii kama hutasimulia safari ya Nyerere kwenda na kurudi Umoja wa Mataifa (UNO).

Mwezi Februari 1955, uongozi wa TANU ulipanga ndiyo iwe safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuhutubia na kuueleza utayari wa Watanganyika kushika wenyewe hatamu za uongozi wa nchi yao, ambayo Mwingereza alikuwa hataki kuiachia kabisa baada ya kuwa inamtajirisha kwelikweli. Sisi sisi tukilima, madini yakichimbwa, kodi zikikusanywa, vyote hivyo vilikuwa mali yake na huingia katika utajiri wa mtawala nyang’au, Malkia Elizabeth wa Uingereza.

Safari ile ilikuwa na mafanikio, kwa maana ya kwamba Mwenyezi Mungu alimpa Nyerere kauli thabiti—nzuri iliyonyooka - na ujumbe wake alioutoa ukaeleweka vizuri na baraza lile la kidunia.

Mipango ikaandaliwa sasa ya kumpokea kishujaa Nyerere atakapokanyaga kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Siku hiyo watu walijaa chekwa, wakafurika nje na ndani ya uwanja. Ulinzi ukawa una mashaka na hivyo kukaamuliwa kwamba, Dossa, ambaye kama kawaida yake alikuwapo na gari yake kumpokea rafiki yake yule, aruhusiwe aende mpaka inapoegesha ndege (apron) na kumchukua Nyerere kutoka hapo.

Kelele, vifijo, nderemo, hoihoi na nyimbo, hasa ule wa ‘baba kabwela UNO’, uliokuwa ukiimbwa na wapiga ngoma wa Kizaramo wa ngoma ya Gombe sugu ukatawala uwanjani hapo. Neno ‘baba kabwela UNO’, kwa lugha ya Kizaramo, maana yake ni, baba karudi UNO (Umoja wa Mataifa).

Gari lile ambalo Nyerere alikuwa amepanda lilikuwa mali ya Dossa, na yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa dereva; lakini katika siku ile kuu kwenye historia ya nchi yetu, lilisukumwa njia nzima kutoka uwanjani pale huku maelfu ya watu wakilifuata nyuma na wengine kusimama kando ya barabara mwote lilimopita, wakiimba na kushangilia; ‘baba kabwela Uno, baba kabwela Uno’. Msafara ule uliishia Makao Makuu ya TANU pale New Street (sasa Lumumba).

Msomaji, sasa hebu tafakari kidogo kwa nini watu wazungumzie jambo dogo tu hili la kutoa gari lake Dossa Azizi. Hili halikuwa jambo dogo kwa wakati huo ambao sisi watu weusi (daraja la tatu) hatukumiliki vitu vya namna hiyo. Na hata kama ingekodiwa Teksi ambazo zilikuwepo chache, basi gharama yake isingewezekana kwa namna ya umasikini wetu ulivyokuwa; ukizingatia na ile kuchukua muda mrefu kuusukuma msafara ule yangekuwa ‘mapesa’ mengi sana.

Kitendo kile cha kupokewa namna ile kilimuathiri sana Nyerere wakati huo na kuanzia hapo akazidi kuwapenda watu wa chini na kuanza kuwaita ‘makabwela’ kuanzia siku hiyo. Nafikiri kwa sasa neno kabwela ni neno rasmi kwenye Kamusi na TUKI za Kiswahili.

Sasa, mheshimiwa mpendwa msomaji wa makala haya, mwandishi nashindwa kuelewa ni kwa nini Taifa staarabu kama hili lishindwe kuzifahamu sifa na michango ya watu wetu kama Mzee Dossa, Mzee Haidar, Mzee Kiyate na wengineo na hivyo kuwapa heshima stahili?

Wako wapi leo watu kama akina Dossa, waliotoa vyao badala ya wao kudai nchi iwape chao kutoka hazina; eti tu wao ni waheshimiwa sana wabunge wanaofanya kazi nyingi sana. Kila kikao cha Bunge Dodoma hakimaliziki bila kusikia wabunge wanalamika kwa kukosa posho hii, posho ile; stahili hii, stahili ile; marupurupu haya, marupurupu yale. Akina Dossa wale walitoa vyao kwa nchi yao. Hebu na nyie waigeni basi kidogo tu!

Huyo ndiye Waziri Dossa Aziz, aliyejitolea bila kuchoka kutoa vyake na vya babake mpaka leo tunaringa hivi. Taifa halimjui kwani alikufa na kuzikwa kikawaida sana kule shambani kwake Mlandizi, ambako alihamia baada ya kuondoka mjini kichwa chini!

simu: 0715808864

No comments: