Waasisi wa TANU 1954 Kulia waliosimama wa tano ni Dossa Aziz wa nne Abdul Sykes Waliokaa wa katikati ni Julius Nyerere na wa pili kushoto ni John Rupia |
Ilikuwa
katika miaka ya 1980 mwishoni siku mimi na Ally Sykes tulipokwenda kumtembelea
Dossa Aziz. Wakati ule nilikuwa nafanya utafiti kuandika kitabu cha maisha ya
Abdul Sykes kaka yake Ally Sykes. Tulikuwa tuko mbali katika kazi ile na siku
moja nikamuomba Ally Sykes anipeleke kwa Dossa Aziz nikamfanyie mahojiano.
Ilikuwa
siku ya Jumapili na nilimsubiri Ally Sykes Mbuyuni katika kituo cha basi mimi
nikitokea Masaki. Hapa ni barabara ya Ali Hassan Mwinyi zamani ikiitwa (Upanga
Road). Huu Mbuyu ulikuwa unaitwa Mbuyu wa Kigwe lakini si wengi walikuwa
wanajua jina hili. Jina hili mimi alinipa Mzee Jimpota ambae yeye na baba yangu
walikuwa pamoja katika Dar es Salaam ya 1950 na akaniambia kuwa hilo jina la
Kigwe ni Mzee Mwinyikhamis Kigwe wa Msasani ambao wote wakijuana toka utoto
wao. Mwinyikhamisi Kigwe akitoka kwao ni Msasani kuja kusoma shule ya Kitchwele
Government School pamoja na baba yangu, Ally Sykes kaka yake Abdul na vijana
wengine wa Dar es Salaam.
Jimpota yeye alikuwa fundi cherehani, siku
moja katika mazungumzo ndipo akaniambia kuwa ule Mbuyu waliupa jina wao wakauita,
‘’Mbuyu wa Kigwe.’’
Ally
Sykes ainipitia pale na Mercedes Benz yake mpya, nyeusi inang’ara kama kioo.
Alikuwa na mama mmoja Mmarekani Mweusi akanitambulisha kuwa ni mwandishi wa ‘’Washington
Post,’’ Ally Sykes akipenda muziki na safari kwenda Mlandizi ilikuwa ya raha sana
muziki uliokuwa ukitoka katika spika za lile dude haukuwa wa kawaida. Unasikia
kila chombo. Tulipofika Mlandizi tukasimama ofisi ya CCM kuuliza nyumbani kwa
Dossa Aziz. Nilipata mshtuko mkubwa pale tulipojibiwa kuwa hawamjui Dossa Aziz.
Tuliondoka na tukauliza mbele watu wawili, watatu hivi mwisho bwana mmoja
akatuelekeza akatuambia tuifuate njia ya majani iliyokuwa pembeni yetu
itatufikisha hadi nyumbani kwa Dossa.
Tulimkuta
Dossa amekaa barazani kwake ilikuwa kiasi cha saa tatu asubuhi hivi mkononi
ameshika radio ya kizamani kidogo na amefungua BBC anasikiliza. Alipomwona Ally
Sykes, Dossa aliweka radio yake chini akapiga ukelele, ‘’Ally ndugu yangu
karibu karibu…’’ Kwa jinsi walivyosalimiana na mazungumzo yao yalivyokuwa nilijua
kuwa wawili hawa hawajaonana kwa miaka mingi. Pale pale Dossa akamuita mkewe
akaja pale barazani. Dossa akamwambia, ‘’Huyu ni Ally kaka yake Bwana Mzuri.’’
Nikajakujua kuwa huyu, ‘’Bwana Mzuri,’’ ni Abbas Sykes ambae yeye alikuwa kila
akija Dar es Salaam kutoka Ulaya alipokuwa balozi alikuwa lazima aende Mlandizi
kumjulia hali Dossa. Baadae Dossa atanieleza mapenzi yake na Abbas yalianzaje
na lini.
Ally
Sykes akanijulisha kwa Dossa, ‘’Huyu Mohamed, mtoto wa Said,’’ Dossa akauliza, ‘’Said
yupi?’’ Jibu likatoka, ‘’Said Popo.’’ Dossa akanipokea kwa tabasamu kubwa
kabisa, ‘’Namjua baba yako alikuwa mpole sana…’’ Dossa akaagiza tuchinjiwe
mbuzi lakini Ally Sykes akamwambia Dossa hatukuwa na muda. Ally Sykes
akamweleza sababu ya mimi kumfuata.
Dossa
alizungumza kwa kama saa moja hivi akianza mapinduzi waliyofanya Abdul Sykes na
Hamza Mwapachu kuchukua uongozi wa TAA 1950 na vipi walijuana na Nyerere
alipofika Dar es Salaam mwaka wa 1952 na vipi walimchagua kuwa rais wa TAA 1953
chama kikafa. Dossa akanieleza kwa kirefu sababu ya TAA kufifia na nini
walifanya kukirudishia chama nguvu yake. Dossa akanieleza maisha ya utoto wake
na jinsi alivozuiwa na baba yake kuanza shule hadi awe amehitimu Qur’an kwanza hivyo
ikawa yeye kaanza darasa la kwanza akiwa na miaka 14 na ndiyo sababu ya kuanza
darasa la kwanza na Abbas ingawa Abbas ni mdogo sana kwake.
Mbele
ya nyumba yake kulikuwa na mabaki ya Land Rover. Dossa akanyoosha kidole chake
cha shahada akasema, ‘’Unaona gari hiyo hapo. Nimetembea na Nyerere Tanganyika
nzima na gari hii tukiwaamsha wananchi waingie TANU tumtoe Mwingereza nchini
kwetu. Tulikuwa tunakwama kwenye barabara mbovu na inabidi tushuke tusukume
gari na Nyerere na yeye akipiga kibega kusukuma. Usimuone mwembamba vile ana
nguvu yule…’’
Hili
neno ‘’kupiga kibega,’’ lilinidhihirishia kuwa kweli Dossa ni mtoto wa Gerezani
kabisa kwani ni lugha ambayo mimi nimeizoea kuisikia kwa wazee wengi wakati
ule. Ally Sykes alikuwa kimya, mimi niko kimya sote tunamsikiliza Dossa
akizungumza kwa taratibu tena bila ghadhabu. Nimefanya mahojiano na wazalendo
wengi na huwa itafika mahali katika maelezo yake utaona ameghadhibika kwa yale
ambayo yeye anaona hakustahili kutendewa. Dossa hakuwa hivyo alikuwa ametulia
tuli akizungumza kwa upole.
Dossa
alikuwa kachoka ufukara umempiga pasi na kiasi. Sifa za utajiri wa baba yake
Aziz Ali na sifa zake mwenyewe Dossa zilikuwa zinafahamika. Rafiki zake
wanasema walikuwa wakimuona Dossa ameingia kila mtu anapumua kwani watakula na
kunywa kwa furaha. Dossa alikuwa mtu karimu sana. Rafiki zake wa karibu sana walimpa
jina la utani, ‘’The Bank.’’
Mimi
nilikuwa namwangalia huku nikishusha pumzi kwa huzuni. Katika miaka ya 1920
babu yangu alikuwa na nyumba Mtaa wa Mbaruku jirani na nyumba ya Aziz Ali. Sifa
zao zikijulikana na wote. Mwisho Dossa akanieleza safari yake ya Nairobi
alipokwenda kufanya usaili wa kozi ya urubani na jinsi Wazungu wakakataa
kumfanyia usaili juu ya kuwa walimwita wenyewe yeye na mtoto wa Ali Mmanga aliyekuwa
kati ya matajiri wakubwa wa Dar es Salaam miaka ile. Jumba lake la fahari bado
lipo hadi leo pale Kisutu.
Dossa
akanieleza alivyomkuta Ally Sykes Nairobi mwaka wa 1947 tayari keshajiingiza
katika siasa za akina Kenyatta. Dossa akanieleza kuwa baada ya kukataliwa
alipiga simu Dar es Salaam kwa baba yake huku analia. Baba yake kwa huruma siku
ya pili akampelekea fedha akamwambia basi anunue gari kama kifuta machozi.
Dossa akanyanyua uso akaniangalia akasema, ‘’Nilikwenda Nairobi na basi
nikarudi Dar es Salaam naendesha gari yangu mwenyewe tena mpya. Gari hii ndiyo
ikajakuwa gari ya kwanza ya TANU…’’
Mwalimu
Nyerere alipokuwa anastaafu alitoa medali 3979 kwa Watanzania walioitumikia
nchi hii. Jina la Dossa halikuwapo katika orodha ile…
No comments:
Post a Comment