UJUMBE KWA
MAADHIMISHO YA KUMKUMBUKA SHUJAA KARIMI NDUTHU
Abdilatif Abdalla
Professional Centre
Nairobi, 24 Machi, 2018
Ndugu zangu na wanaharakati wenzangu.
Ni fahari kubwa kwangu kushirikishwa katika maadhimisho haya ya kumkumbuka Karimi Nduthu,
mmojawapo miongoni mwa mashujaa wetu wa Kenya waliojitolea maisha yao ili
kuendeleza harakati za mapambano ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa sehemu kubwa
ya Wakenya – hasa wale walioko katika matabaka ya chini. Shujaa ambaye bado naendelea kumheshimu.
Kushoto Abdilatif Abdalla, Karimi Nduthu |
Ninavyoamini ni kwamba tumejumuika hivi leo ili
kuadhimisha na kusherehekea maisha ya mzalendo huyu; wala si kuadhimisha kifo
chake. Kwa sababu Karimi hakufa. Dhati yake bado inaendelea kuishi. Kama dhati
yake ingekuwa imekufa, tusingekuwa tunaendelea kumtaja na kumkumbuka. Na kwa
kuwakumbuka mashujaa wetu kama yeye huwa ndiyo tunaipa uhai historia yetu ya
mapambano dhidi ya dhuluma za kila aina; na pia tunaendeleza mbele ule moyo wa
kizalendo wa kujitolea nafsi zetu kwa ajili ya nchi yetu.
Nashukuru kwamba nilikuwa ni miongoni mwa Wakenya
waliopata bahati ya kufanya kazi na mzalendo Karimi Nduthu wakati wa kile
kipindi kigumu cha historia ya Kenya, ambapo nchi yetu ilikuwa imetandwa na
giza la ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na serikali dhalimu iliyokuwa ikiongozwa
na Daniel arap Moi na KANU.
Nakumbuka kukutana naye Karimi kwa mara ya kwanza
mwaka 1994, mjini Nairobi.
Mwaka huo wa 1994 ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kurudi nchini Kenya baada ya kulazimika kuishi uhamishoni (mwanzo Tanzania na baadaye Uingereza) kwa miaka 22 – baada ya kufunguliwa gerezani mwaka 1972. Mwaka 1994 Karimi alishakuwa Mratibu wa Kitaifa wa MWAKENYA. Mwaka huo nilifika Nairobi kutoka London nilikokuwa nikiishi, na ambako nilikuwa nikishirikiana na Wakenya wenzangu katika harakati dhidi ya serikali ya Moi-KANU. Nilikuwa nimetumwa na chama chetu hicho cha MWAKENYA kuja kukutana na kushauriana na Karimi pamoja na mzalendo mwenzake, Tirop arap Kitur, kuhusu mipango ya mikakati ya kuendeleza harakati zetu ndani ya nchi. (Ni matumaini yangu kwamba Tirop naye yuko hapo ukumbini kwenye maadhimisho haya). Kutokana na hali mbaya ya ukandamizaji iliyokuwako nchini wakati huo, ilibidi sisi watatu tukutane kwenye msitu wa Ngong ili tuweze kuzungumza bila ya kuhofia kwamba tunasikilizwa na serikali. Siku chache baadaye Karimi akanialika kwake, Riruta Satellite, alikokuwa anaishi. Lakini hapo nyumbani kwake hatukuzungumza jambo lolote la kisiasa. Baada ya hapo, tulikutana tena nje ya Kenya, pamoja na wanaharakati wenzetu kutoka ndani na nje ya Kenya, ili kufanya shughuli za MWAKENYA.
Mwaka huo wa 1994 ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kurudi nchini Kenya baada ya kulazimika kuishi uhamishoni (mwanzo Tanzania na baadaye Uingereza) kwa miaka 22 – baada ya kufunguliwa gerezani mwaka 1972. Mwaka 1994 Karimi alishakuwa Mratibu wa Kitaifa wa MWAKENYA. Mwaka huo nilifika Nairobi kutoka London nilikokuwa nikiishi, na ambako nilikuwa nikishirikiana na Wakenya wenzangu katika harakati dhidi ya serikali ya Moi-KANU. Nilikuwa nimetumwa na chama chetu hicho cha MWAKENYA kuja kukutana na kushauriana na Karimi pamoja na mzalendo mwenzake, Tirop arap Kitur, kuhusu mipango ya mikakati ya kuendeleza harakati zetu ndani ya nchi. (Ni matumaini yangu kwamba Tirop naye yuko hapo ukumbini kwenye maadhimisho haya). Kutokana na hali mbaya ya ukandamizaji iliyokuwako nchini wakati huo, ilibidi sisi watatu tukutane kwenye msitu wa Ngong ili tuweze kuzungumza bila ya kuhofia kwamba tunasikilizwa na serikali. Siku chache baadaye Karimi akanialika kwake, Riruta Satellite, alikokuwa anaishi. Lakini hapo nyumbani kwake hatukuzungumza jambo lolote la kisiasa. Baada ya hapo, tulikutana tena nje ya Kenya, pamoja na wanaharakati wenzetu kutoka ndani na nje ya Kenya, ili kufanya shughuli za MWAKENYA.
Kwa hivyo, nilifanya kazi naye Karimi kwa jumla ya
miaka miwili tu, kabla ya kuuliwa. Lakini katika muda huo mfupi niliobahatika
kufanya kazi naye, niligundua kwamba Karimi alikuwa na vitu vine, au sifa nne,
ambazo ni muhimu sana kwa kila mwanaharakati wa kisiasa kuwa nazo:
Sifa ya kwanza ni kwamba Karimi alikuwa akiipenda
nchi yake bila ya kiasi! Lau kama mtu angekifunua kifua chake, angeuona moyo
wake umetandwa na umbo la Kenya.
Sifa ya pili aliyokuwa nayo ni kujitolea kwake
mhanga ili kuitumikia nchi yake kwa moyo wake wote - bila ya kuchoka wala
kunung’unika. Hakuna kazi ambayo aliiona kuwa ni nzito au ni ngumu, au ni chini
ya hadhi yake kuitekeleza.
Sifa ya tatu aliyokuwa nayo ilikuwa ni unyenyekevu
na kutopenda makuu. Kwa wale waliowahi kufanya naye kazi, watakubaliana nami
nisemapo kwamba licha ya nyadhifa na vyeo alivyokuwa navyo katika shughuli
mbalimbali za harakati, Karimi hakuwa ni
mtu wa majivuno na mbwembwe.
Sifa ya nne – ambayo ndiyo muhimu zaidi na ndio
msingi mkuu wa harakati – ni imani thabiti aliyokuwa nayo kuhusu aliyokuwa
akiyatenda. Hata mara moja hakuteteleka
(hakutetereka) au kuyumbayumba. Alikuwa ni mwamba madhubuti usioweza
kutingishika! Na hakukata tamaa!
Huyo ndiye Karimi Nduthu, mwanaharakati, mzalendo
na shujaa, ambaye serikali ya Moi-KANU ilitishika naye. Huyo ndiye Karimi
Nduthu ambaye usiku wa tarehe 23 Machi, mwaka 1996, serikali hiyo dhalimu
ilifikiri kwamba kwa kumuua itaifuta kumbukumbu yake. Lakini kumbukumbu za
mashujaa hazifutiki! Kwa sababu kumbukumbu hizo huwa zimegubikwa ndani kabisa
ya nyoyo za wale wanaoendelea kuishi, na ambao wanaijua thamani ya wazalendo
wao; wale ambao wanapokezana kumbukumbu hizo kwa kizazi hadi kizazi; wale ambao
kamwe hawausahau – wala kamwe hawatausahau – mchango wa mashujaa kama Karimi
Nduthu, Dedan Kimaathi, Pio Gama Pinto, Bildad Kaggia, JM Kariuki, na wengineo
wengi, katika kuifanya Kenya kuwa ni nchi ya usawa na uadilifu kwa kila
Mkenya.
Ni matumaini yangu kwamba wanaharakati watajifunza
na kuyapatia faida maisha ya Karimi Nduthu; na kwamba yatawahamasisha na
kuwaongoza katika utendaji kazi wao. Hiyo ni miongoni mwa heshima kubwa
tunayoweza kumpa Karimi Nduthu.
Nilitangulia kusema kwamba tumekusanyika hivi leo
ili kuadhimisha na kusherehekea maisha ya mzalendo huyu; wala si kuadhimisha
kifo chake. Kwa sababu dhati ya Karimi haikufa. Kwani shujaa aliyemo katika
mapambano ya kupigania haki na kuleta mabadiliko katika jamii, ili jamii hiyo
iweze kuishi maisha ya kibinadamu yaliyo huru na yenye heshima, huwa hafi!
Kama nilivyopata kusema mahali kwengine, kila
pumzi moja ya shujaa inayomtoka wakati anapokuwa anakata roho, pumzi hiyo
haipotei bure bali huingia katika nafsi za wale waliobakia, na kuwazidishia
uhai na nguvu za kuiendeleza mbele kazi hiyo. Kila tone la damu linalomwagika
kutoka katika mwili wa mwanaharakati kama huyo, damu hiyo huwa ni maji matukufu
na yenye rutuba yanayouimarisha mti wa kupigania haki. Mti ambao una matawi
mingi sana. Matawi ambayo hakuna mtu yoyote, au nguvu yoyote ya kilimwengu,
inayoweza kuyakata na kuyamaliza. Wala mti huo haufi. Kama ungekuwa unakufa,
ungekuwa umeshakufa kitambo sana katika nchi yetu hii baada ya wanaharakati na
wapiganiaji haki wengi kuuliwa. Lakini mti huo bado unaendelea kuishi. Na utaendelea
kukua. Hautakufa!!
Katika
ukurasa wa 26 wa kitabu, Karimi
Nduthu: A Life in the Struggle kumeandikwa kwamba Karimi alikuwa akipenda
kusoma mashairi; na kwamba shairi mojawapo alilokuwa akilisoma mara kwa mara ni
shairi langu liitwalo “Siwati”, lililomo katika kitabu changu cha mashairi
niliyoyatunga nilipokuwa gerezani baina ya mwaka 1969 na 1972, kiitwacho Sauti ya Dhiki. Kwa hivyo, nataka
niumalize ujumbe wangu huu kwa kumsomea Karimi shairi hilo, ikiwa ni njia ya
kumhakikishia huko aliko kwamba vizazi na vizazi vya Wakenya havitaacha
kuendelea na mapambano ya kujikomboa kutokana na mfumo dhalimu unaowakandamiza
walio wengi:
Siwati nshishiyelo, siwati; kwani niwate
Siwati ni lilo hilo, ‘talishika kwa vyovyote
Siwati ni mimi nalo, hapano au popote
Hadi kaburini sote, mimi nalo tufukiwe
Siwati ngaadhibiwa, adhabu kila mifano
Siwati ningaambiwa, ‘tapawa kila kinono
Siwati lililo sawa, silibanduwi mkono
Hata ningaumwa meno, mkono siubanduwi!
Siwati si ushindani, mukasema nashindana
Siwati ifahamuni, sababuye waungwana
Siwati ndangu imani, niithaminiyo sana
Na kuiwata naona, itakuwa ni muhali
Siwati nimeradhiwa, kufikwa na kila mawi
Siwati ningaambiwa, niaminiyo hayawi
Siwati kisha nikawaa, kama nzi; hivyo siwi
Thamma nakariri siwi, na Mngu nisaidiya
Ahsanteni sana kwa
kunisikiliza.
Abdilatif Abdalla
Hamburg, Ujerumani
24 Machi, 2018
No comments:
Post a Comment