Monday, 5 March 2018

MWAMVUA MRISHO: MWANAHARAKATI ALIYEKUWA ANASUBIRIA ‘U—FIRST LADY’ NA ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA

Raia Mwema Jumatatu Machi 5-6, 2018

Kushoto Bi. Mwamvua bint Mashu, wa tatu
Bi. Titi Mohamed akifuatiwa na Bi. Zainab mke
wa Tewa Said Tewa



Shajara ya Mwana Mzizima

MWAMVUA MRISHO: MWANAHARAKATI ALIYEKUWA ANASUBIRIA ‘U—FIRST LADY’

Na Alhaji Abdallah Tambaza

JUMA lililopita, Shajara ilimwangazia aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa chama hicho wakati wa harakati za kupambana na Wakoloni; Mzee Haidar Mwinyimvua.

Leo, tutamwangalia mwanaharakati mwengine mwanamama aliyetokea hapa kwetu Mzizima; na ambaye amefanya mambo mengi makubwa ya kukumbukwa, kwenye mapambano ya kuutokomeza utawala dhalimu wa Malkia Elizabeth wa Kiingereza. Huyo ni mama yetu Bi Mwamvua Mrisho Mashu; maarufu mama Daisy.

Mwamvua Mrisho Mashu, alikuwa ni mke wa hayati ‘Bwana Mkubwa wetu’,  Abdulwahid Kleist Sykes, aliyekuwa kiongozi wa kwanza kabisa kuasisi harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika kabla ya ujio wa Mwalimu Nyerere wa Butiama.

Bila shaka yeyote, Mama Mwamvua alishuhudia na wakati mwengine kushiriki kwenye vikao vile vya siri na dhahiri, vya kujadili mustakabali wa mapambano dhidi ya mkoloni vilivyokuwa vikifanyika kutwa na kucha ndani ya nyumba yao; kwani wadau wakubwa walikuwa ni wale kina Sykes watatu – Abdulwahid (mumewe), Ali na Abbas (shemeji zake) na yeye akiwa mhudumu mkubwa kwa wageni kwa kuwapatia chakula na vinywaji pale vilipohitajika. 

Mazungumzo ya aina ile yalikuwa yakichukua muda mrefu kumalizika kwani watu kama Mwalimu Nyerere, walikuwa wakija mwishoni mwa juma tu, akitokea Pugu ambako kwa mazingira ya zamani ni mbali kwelikweli. Dossa Azizi, aliyekuja kuwa rafiki wa karibu wa Mwalimu ndiye aliyekuwa na jukumu la kumrejesha Pugu usiku usiku, ili awahi kazini asubuhi.

Waswahili wana msemo kwamba; unapokaa chini ya muwaridi lazima unukie! Akiwa mke wa kaka mkubwa na ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa iliyokuwa AA, TAA na baadaye TANU, alikuwa na nafasi kubwa ya kujua hili ama lile, lilokuwa likitayarishwa kupeleka mbele mapambano. Ni dhahiri basi, kama kusingekuja kutokea mabadiliko mbeleni katika mapambano kwa kubadilishana uongozi wa juu, mama huyu ndiye angekuwa ‘First Lady’ wetu kabla ya Mama Maria Nyerere (mke wa Mwalimu).

Nilimfahamu Mama Daissy, kwenye miaka yangu ya utoto nilipokuwa nikiongozana na rafiki yangu kipenzi wa utotoni hayati Kliest Abdulwahid Sykes, ambaye alifariki dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Marehemu Kliest Sykes, alikuwa mtoto wa pili wa Bi Mwamvua kuzaliwa. Wa kwanza alikuwa ni Halima Mselem Mlangwa (mke wa aliyewahi kuwa kada mashuhuri wa CCM hayati David Mlangwa), akafuatia Daisy Sykes Buruku ambaye kwa sasa anaishi na mumewe raia wa Uganda kule Kampala. Dada Daisy amekuwa mwalimu mkuu kule Uganda kwenye vyuo mbalimbali kwa muda mrefu, kabla hajajiunga na Shirika la UNHCR la kuhudumia wakimbizi, kule Geneva, Switzerland.  Watoto wengine wa Mama Daissy ambao  walikuwa mashuhuri hapa Dsm, ni Omar na Adam Sykes ambao tayari wameshatangulia mbele za haki. Inna Lillah Wainna Illayhi Rajuun.

Mama Daissy, anatajwa kwamba ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na watu wengine kama Bibi Titi, Hawa Bint Maftah, Sakina Arab, Asha Ngoma, katika kuanzisha chama cha TAPA (Tanganyika Parents Association) na UWT (Umoja wa Wanawake Tanganyika). Vikao vilivyokuwa vya mwanzo vya kuanzisha vyama hivyo inasemekana aliviitisha yeye na kufanyika uwani nyumbani kwao Aggrey Street.  

Hakuna asiyejua umuhimu wa UWT na mchango wake katika maendeleo ya wanawake hapa nchini. Chini ya mwenyekiti wake wa mwanzo Bibi Titi Mohammed, UWT kiliweza kuwaunganisha wanawake wa taifa hili kutoka makabila na dini mbalimbali wakawa kitu kimoja kabla na baada ya uhuru kupatikana. Baada ya kuanzishwa kwake, nimemshuhudia Bi Mwamvua Mrisho akidumu kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo muhimu kwa Mkoa wa Pwani na baadaye Dar es Salaam kwa muda mrefu sana. 

UWT ilianzisha udugu na vyama vya wanawake kutoka nchi jirani, Afrika na Dunia nzima kwa ujumla kikihudhuria kwa kupeleka wajumbe kwenye mikutano mingi ya kimataifa na hivyo kujenga uhusiano wa kubadilishana mawazo na fikra kutoka watu wa mataifa mbalimbali ulimwenguni kote.
Viongozi waandamizi wa UWT wakati huo, akina Bibi Titi, Sophia Kawawa, Lucy Lameck, Getrude Mongella akiwamo na mama yetu Mama Daisy, walikuwa wakipigana vikumbo tu na ‘maguo’ yao ya vitenge na batick walivyonunua kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika, hasa zile za Afrika Magharibi na Zaire, walikohudhuria mikutano mbalimbali.

Mchango wa chama cha TAPA katika kuleta maendeleo kabla na baada ya uhuru ni mkubwa sana. Kabla ya uhuru, TAPA kilitumika kama chombo kilichokuwa kikitetea maslahi ya watoto wa Kiafrika kwenye shule za kibaguzi za serikali ya Kiingereza. Chini ya mwenyekiti wake wa mwanzo Mzee Waziri Simba Waziri (babake Brigedia mstaafu wa JWTZ, Simba Waziri), chama cha TAPA kiliweza kujipenyeza na kuwamo kwenye kamati za wazazi za mashuleni ambako walimudu kupunguza madhila na manyanyaso miongoni mwa wanafunzi wa Kiafrika.

TAPA pia, katika kipindi hicho cha ukoloni kuelekea kujitawala kiliweza kuanzisha na kuziendesha shule zake wenyewe na kwa hiyo kutoa mchango mkubwa sana katika kuwasomesha watoto wa masikini ambao walikuwa wakitengewa shule chache sana bila kujali kwamba wao ndio waliokuwa wengi. Miaka kadhaa baada ya uhuru kupatikana, wanafunzi waliweza kuchaguliwa kwa wingi kutoka katika shule za TAPA na kujiunga na zile za serikali na hivyo kukawa na ongezeko kubwa la watoto wa Kitanganyika kupata elimu ya juu kutokana na juhudi  za wazee wao na siyo serikali. Kulikuwapo na kampeni kwamba kila palipokuwapo na tawi (branch) la TANU, basi pia ianzishwe na shule ya TAPA.   

Mwaka 1965, mwandishi huyu alijiunga na Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph pale Forodhani, Dar es Salaam, kwa mafunzo ya Sekondari. Miongoni mwa wanafunzi wapya walikuwamo pia waliopitia shule za TAPA.  Mmoja wao ni marehemu Iddi Omari Machuppa ambaye alipata kuwa kocha wa Mpira wa Miguu na kufikia kuwa mmoja wa wakufunzi wa makocha wa mchezo huo hapa nchini wakati wa TFF ya Leodegar Chilla Tenga. Mwengine alikuwa ni Shaaban Mohammed Manda, ambaye alikuja kuwa mwalimu mzuri na kufikia kuwa Mwalimu Mkuu wa shule mbalimbali hapa nchini. Hali ilikuwa hivyo takriban kwa nchi nzima; na popote kwenye shule ya TAPA, uniform (sare za shule) yake ikawa ni bendera ya TANU, kijani, njano na nyeusi.

Wakati watoto kwenye shule nyingine wakiimba nyimbo za kishuleshule zile zenye mahadhi ya ‘kipambiopambio’ na za ‘Happy Birthday to you’, kwenye shule za TAPA watoto waliimbishwa nyimbo za kimapinduzi na za kuwasifu viongozi wakuu wanaopigania uhuru; au za kuwaponda wale walioko kwenye vyama vya upinzani kama Kassanga Tumbo, Zuberi Mtemvu na Sheikh Hussein Juma. Hebu basi angalia mashairi haya ya wimbo huu wa shule ya TAPA wa Kizaramo:
“Tumbo kibaraka, Kambona jenga kambi  Ukonga, Mtemvu inno, kolonda kukomaisi;
Tumbo mmbozi haa! Kolonda kukomaisi”

Sasa utaona ni kwa namna gani watoto waliaminishwa kwamba wapinzani hao,  hawakuwa wapigania uhuru, bali walikuwa ni vibaraka wa wakoloni tu; na hivyo kumtaka aliyekuwa Katibu Mkuu wa TANU wakati huo, akajenge jela Ukonga na vibaraka hao ‘wajinga’ wakafungwe na kufia humo. 

Kazi nyingine kubwa aliyoifanya Bi Mwamvua Mrisho Mashu, katika uongozi wake kwenye harakati ni kuanzisha tawi la TANU la Kata ya Miburani, Wailes, kule Temeke mwisho, nyumba ya tatu tu kutoka ilipo nyumba yake (The Blue House), mtaa wa Mjimwema. Alidumu hapo wengine wakimfanya mwenyekiti wao moja kwa moja, akichaguliwa kwa kura nyingi kila mara.

Wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere, Mama Mwamvua alichaguliwa na rais kuwa kwenye Tume ya Rais ya Kukadiria Kodi za Majumba na kusuluhisha migogoro baina ya wenye nyumba na wapangaji (Tanzania Rent Tribunal Board), pamoja na Kamati ya Ugawaji wa Nyumba za Msajili wa Majumba na NHC. 

Katika watoto wa Mama Daisy aliowapata kutokana na ndoa yake na hayati Abdulwahid Sykes, ni mmoja tu, Kliest Sykes aliyependa kujishughulisha na siasa. Mama Daisy alikuwa ndiye mwalimu na mshauri mkuu kwa mwanawe huyo kila mara alipokuwa anataka kufanya hili ama lile katika kusaidia jamii. Kila mara alikuwa akielekeza nani wa kuendewa; nani wa kufuatwa; nani wa kumsikiliza katika hali ilipofikia na nini zaidi kifanyike kuweka hali tulivu. Mafanikio yote aliyokuwa akiyapata hayati Kleist Sykes wakati akiwa Meya wa Jiji na pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, yalitokana na mama yake kuwa nyuma ya pazia.  

Kuna wakati fulani, marehemu Kliest Sykes, alikuwa akiwania nafasi ya kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwenye Chama Cha Mapinduzi. Kwenye mkutano wa kuchuja majina ya kupendekezwa kwenye Kamati Kuu, jina lake likakatwa kimizengwe kutokana na ‘makambikambi’ na ile tabia iliyozoeleka katika CCM ya ‘huyu si mwenzetu.’ 

Sasa, akiwa pale Dodoma kufuatilia matokeo ya uteuzi, Kleist Sykes alikutana na mjumbe mmoja kutoka Zanzibar ambaye aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Muungano, Mzee Abdisalam Khatib, aliyempasha habari mbaya kwamba jina lake limekatwa miongoni mwa wagombea. 

Kleist anasema, pamoja na mambo mengine, alimweleza Khatib kwamba inakuwaje mtu kama yeye, ambaye mbali na mchango wa babake katika ukombozi wa taifa hili, lakini mamake pia ndiye aliyeanzisha chama cha TAPA katika mkutano uliofanyika uwani kwao na yeye Kleist akishuhudia. Kusikia hivyo, Kleist anasema, Khatib hakukubali na siku ya pili alipoingia kikaoni alichachamaa mpaka jina la Kleist likapitishwa na hatimaye kuwa mjumbe wa NEC.  

Hayati  Bi Mwamvua Mrisho Mashu, ambaye alifia kwenye hospitali moja kule Afrika Kusini, kama miaka 10 iliyopita baada ya kuugua Saratani ya Kinywa, bado namkumbuka kama vile amekufa jana. 
Bado nakumbuka simulizi za namna alivyokuwa akiwapokea watu mashuhuri nyumbani kwake kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu, kama kina Chifu Kidaha Makwaia wa Wasukuma; Chifu Abdallah Fundikira wa Unyanyembe; Chifu Kunambi wa Waluguru; akina Chifu Marealle wa Wachagga pamoja na Balozi Abdallah Swedi Kagasheki wa Bukoba.

Alikuwa akieleza pia namna ambavyo alikuwa akiwaza na kuwazua kama ingetokea akawa First Lady wa kwanza nchini, na namna ndoto ile ilivyoyayuka mapema. 

Kutokana na urafiki kati ya mwandishi huyu na mwanawe, mama Daisy alikuwa akipenda sana niwepo wakati nyumbani kwake kunapokaribishwa wageni au akiwa ameandaa chakula kwa ajili ya wanawe wote. 

Alikuwa ni mpishi mzuri wa kukata na shoka wa mahanjumati ya kimrima; hasa kuku wa kupaka, samaki wa kupaka na tambi za sawia. Kutokana na malezi na mafunzo ya nyumbani kwetu ya namna ya kula na wageni, sikuwa napata tabu pale aliponitaka mimi niwe mbelembele na wageni nikiwasogezea hiki ama kile, huku kelele za mgongano wa vijiko na sahani zikihanikiza moja kwa moja!

Huyo ndiye Mama Mwamvua Mrisho, na mchango wake katika kufanikisha nchi yetu kuwa huru na yale aliyokuwa akiyafanya kwa Nyerere akitokea Pugu, kwa kumlisha, kumnywesha na kumwandalia pa kulala anapoamua kutorudi Pugu, kwa siku zile za mapambano na uamsho ule mkuu wa kumtoa mkoloni! Sasa wewe msomaji amua kama hafai kushukuriwa na sisi tuliopo sasa hivi.
atambaza@yahoo.com
simu: 0715808864     


No comments: