Friday, 2 March 2018

UGAIDI: SHEIKH MOHAMED ISSA ALIPOZUNGUMZA NA GAZETI LA HABARI LEO

Sheikh Mohamed Issa
Sala ya Eid Mnazi Mmoja Dar es Salaam


DUNIA imeingia tena katika simanzi baada ya kudhihirika kwamba wasichana 110 ambao ni watoto wa shule, wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria.

Wasichana hao walitekwa nyara Februari 19 mwaka huu, baada ya wanamgambo wa kundi hilo kuvamia shule yao katika mji wa Dapchi ulioko kaskazini-mashariki mwa Jimbo la Yobe.

Kutokana na hali hiyo, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari anasema hilo ni “janga la kitaifa”, ameomba radhi kwa familia za wasichana hao na kuahidi vikosi vya serikali kuwasaka watekaji hao.
Tukio hilo limekumbusha yale yaliyotokea katika shule ya wasichana ya Chibok mwaka 2014 na kusababisha huzuni na hasira kwa wazazi wa wasichana hao.

Dapchi, ambayo iko umbali wa kilometa 275 kaskazini-magharibi mwa Chibok, ilivamiwa na Boko Haram na kusababisha wanafunzi na walimu wa Shule ya Sayansi na Ufundi ya Wasichana inayomilikiwa na serikali kukimbilia katika vichaka vinavyozunguka shule hiyo.

Wakazi wa Dapchi wanasema baadaye vikosi vya serikali ya Nigeria vilianza kupambana na waasi hao ambao baadaye walikimbia.

Mamlaka awali zilikana madai kwamba kulikuwa na wasichana waliotekwa nyara, zikisema kuwa walikuwa wamejificha dhidi ya wanamgambo hao. Hata hivyo, baadaye walikiri kwamba wasichana 110 walikuwa hawajulikani walipo baada ya uvamizi huo.

Wanagambo wa Boko Haram wamekuwa wakipambana katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo yenye Waislamu wengi, wakidai kwamba wanataka eneo hilo liendeshwe kwa sharia za Kiislamu.
Ni takribani miaka minne sasa imepita tangu kundi hilo liteke nyara wasichana 276 wa Chibok na kupeleka kilio dunia nzima na hivyo kuanza kwa kampeni iliyoitwa’BringBackOurGirls (rejesheni wasichana wetu)’.

Hadi leo serikali ya Nigeria imeshindwa kutambua wasichana zaidi 100 waliotekwa walipo.
Tangu kundi hilo la Boko Haram liibuke kupitia mgongo wa dini limesababisha mauaji ya maelfu ya Wanigeria.

Boko Haram wanapigania dini?

Je, ni kweli wanachopigania Boko Haram ni dini? Je, Uislamu unaruhusu yanayofanywa na kundi hilo?

Mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, Shehe Mohamed Issa, aliulizwa maswali hayo na mwandishi wa makala haya na kujibu kama ifuatavyo:

“Boko Haram na makundi mengine yanayojitambulisha kwamba yanapigania Uislamu kama Al-qaeda, Islamic State (IS) na Al Shababu, wanatumia Uislamu kama ngazi tu ya kufanikisha mambo yao, lakini ukweli ni kwamba wanachokifanya kinapingana kabisa na mafundisho sahihi ya Uislamu.”

Shehe Issa anasema hayo ni makundi ya waasi kama waasi wengine na Uislamu unatumiwa tu kama ngazi kwa ajili ya kupata wafuasi au kuungwa na mkono na Waislamu ambao hawajui vyema misingi ya dini yao.

“Heri hata makundi mengine yanapambana na maadui zao, lakini hawa wanateka waislamu wenzao… Wanateka wasichana ambao pia ni Waislamu wenzao… Hakuna Uislamu wa aina hiyo,” anasema.

Anasema alisikia pia wanawaoa wasichana hawa, jambo ambalo ni la ajabu kwa sababu ndoa ya Kiislamu inakuwa halali pale kunapokuwa na ruhusa ya mzazi wa msichana.

Anasema Uislamu unakataza kuua nafsi isiyo na hatia bila kujali mhusika ana dini gani na hivyo huwezi kupiga bomu sokoni na kisha ukadai kwamba unapigana vita kwa njia ya Mwenyezi Mungu, maarufu kama jihadi.

Anazidi kufafanua kwamba, Uislamu pia unasema: “Hakuna kulazimishana katika dini…” (Al-Qur’an 2:256).

Shehe Abdulqadir al-Ahdal, Rais wa Taasisi ya al-Hikma ya Dar es Salaam, amekuwa akisema kwamba mapambano mengi yanayofanywa na makundi ya kigaidi kama IS hayana sifa ya kupigana kwa njia ya Mwenyezi Mungu (jihadi).

Anasema Waislamu kupigana jihadi ni mpaka kwanza wachokozwe na wawe katika mazingira ambayo wanazuiwa kutekeleza ibada zao, jambo ambalo halipo kwenye makundi yanayodai kwamba yapigana jihadi.

Kadhalika, anasema hata pale Waislamu wanapolazimika kupigana vita, ni marufuku kuwapiga watu wasio vitani, watoto, wanawake, kupiga nyumba za ibada kama makanisa, kuua wanyama na hata kukata miti holela.

Nini kifanyike kukomesha makundi haya?

Shehe Mohamed Issa anasema ili dunia iepukane na makundi hatari kama haya ni Waislamu kujifunza dini yao na wale wasio Waislamu kuacha kuyaita makundi haya kuwa ya ‘Kiislamu’ au mujahidina (wanaopigana kwa njia ya Mwenyezi Mungu).

“Baadhi ya vijana wa Kiislamu hukutana na mafundisho yaliyokwishapotoshwa. Ni vyema vijana wasomeshwe kwa mashehe wenye itikadi na mafundisho sahihi ya dini yao,” anasema Shehe Issa.
Lingine la kufanya anasema ni vijana wa Kiislamu kusoma pia elimu ya dunia ili kuijua kwa uhakika dunia yao.

“Ipo shida kwa baadhi ya vijana wa Kiislamu kutokuwa na elimu sahihi kuhusu mazingira yao na hivyo huwa na upeo mdogo kuhusu dunia,” anasema.

Anashauri pia serikali mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania kuwa na sera zitakazowanyanyua wananchi, hususani vijana kiuchumi.

“Vijana wengi wanadanganywa kwamba wakijiunga na hawa magaidi watapata manufaa ya kiuchumi; watapata pesa, watapatawake, watahudumiwa vyema na mambo kama hayo,” anasema.

Nafasi ya taasisi za dini

Kwa mujibu wa Shehe Issa, mbali na madhara yanayosababishwa na makundi haya, lakini pia yanaupaka Uislamu picha mbaya.

“Katika muktadha huo, ninashauri taasisi za Kiislamu kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kufanya kampeni maalumu ili umma ufahamu kwamba kinachofanywa na makundi haya hakina asili katika dini ya Kiislamu,” anasema.

Anasema kwa vile Tanzania haiku kisiwani, kama haifanyi kampeni za nguvu za kupeleka elimu sahihi kwa wananchi, siku moja vijana wa Kitanzania wanaweza kurubuniwa kujiunga na makundi haya hatari kwa mgongo wa dini.

Anasema kampeni ya kuufumbua macho umma inaweza pia kufanywa kupitia hotuba mbalimbali zinazotolewa misikitini na kwenye majukwaa mengine au kwenye makongamano na warsha.

Anasema nchi zinazosumbuliwa na magaidi zinaweza pia kuwa na kampeni kama iliyofanyika hivi karibuni nchini Uingereza iliyopewa jina la “Ujue Msikiti Wangu” (Know my Mosque).

Anasema katika kampeni hiyo, mtu yeyote alikuwa anakaribishwa kuuliza swali lolote kuhusu Uislamu na kwamba imesaidia sana kuwafanya watu kuijua vyema dini hiyo dhidi ya mambo yasiyohusu Uislamu, baadhi yakienezwa kipropaganda na watu wanaouchukia Uislamu.

Dk Zakir Naik katika kitabu chake ‘Maswali Yanayoulizwa kuhusu Uislamu na Wasio Waislamu’, anasema kwamba kutokana na propaganda au mitazamo isiyo sahihi juu ya Uislamu kujirudiarudia, imefikia hatua ya watu kudhani kwamba Uislamu ndivyo ulivyo.

Anasema wale wanaoziamini propaganda hizi kutokana na kutopata usahihi wa mambo, huwafanya wauangalie pia Uislamu vibaya na hivyo anahimiza Waislamu kuwa na kampeni kama hiyo ya ''Ujue Msikiti Wangu.''

Dk Naik anasema propaganda zinazotokana na mtazamo kwamba Waislamu ni watu wa siasa kali au magaidi, zimesababisha wakati mwingine Waislamu kubaguliwa, kutengwa au hata kufanyiwa fujo.

Chanzo Habari Leo, Febuari 28, 2018.
Hamisi Kibari

No comments: