Thursday, 15 March 2018

NAKUMBUKA: AVALON CINEMA

Avalon Cinema
Siku moja nilimtembelea Balozi Abbas Sykes nyumbani kwake Sea -View. Kwangu mimi saa moja au mbili  za mazungumzo na Balozi Sykes huwa zinanirudisha nyuma sana katika maisha yangu ya utoto, Balozi siku nyingine akinihadithia yale yaliyopita wakati mimi bado mdogo akitaja majina ya watu ambao wengi wao wameshatangulia mbele ya haki lakini ninawafahamu.

Siku hiyo niliona video cassette kwenye meza yake na nilipoangalia nikaona ni – ‘’High Society.’’

Hii ilikuwa filamu maarufu katika miaka ya 1950 ambayo ndani walicheza wanamuziki nyota wa nyakati zile – Louis Armstrong, Bing Crosby, Frank Sinatra na wengineo. Niliingalia sana ‘’cover’’ ya ile video cassette. Wakati ule ni zile cassette za VHS madude makubwa ya mikanda.

Bwana Abbas kumbe na yeye alikuwa akiniangalia jinsi nilivyochukuliwa na video ile. Sauti yake ndiyo iliyonitoa katika fikra zangu wakati nilipokuwa nimehama dunia hii ghafla nimerudi kwenye dunia ambayo hakuna ajiuaye ila mimi.

‘’Mohamed mimi na baba yako tulitembea kutoka Kipata hadi Avalon Cinema kuangalia filamu hiyo.’’

Balozi Sykes alikuwa kanitoa nilikokua.

Bing Crosby jina hili nililisikia kwa mara ya kwanza mwaka wa 1964 asubuhi siku ya Eid Pili nikinywa chai na baba yangu. Jana yake ilikua Eid Mosi baada ya Mfungo wa Ramadhani na nilikwenda kuona filamu ya Elvis Presley, ‘’Blue Hawaii, Empire Cinema.

Siku ya Eid ilikuwa siku kubwa sana kwetu watoto kwani tulinunuliwa nguo mpya na kupewa fedha kwenda Mnazi Mmoja kusheherekea. Sisi wengine ambao tulijiona, ‘’sophisticated,’’ tulipita njia tu pale Mnazi Mmoja. Tuliliogopa vumbi la pale Sisi starehe yetu ilikuwa kwenye kuangalia senema na kwena kula ''fish and chips,'' baada ya kutoka.senema.

Siku ile Empire Cinema walikuwa wanaonyesha filamu ya Elvis Presley ‘’Blue Hawaii.’’

Hii ilikuwa filamu yangu ya kwanza ya Elvis. Nilimpenda sana Elvis na akawa ‘’hero,’’ wangu katika udogo wangu wote. Hakuna nyimbo yake ambayo nilikuwa siwezi kuimba na nilikuwa na maktaba yangu ndogo nyumbani ya rekodi zake.

Fedha niliyokuwa nikipewa kwa ajili ya shule zilikwenda kwenye vitabu, comics na rekodi za Elvis na nyingine nilitumia Snow Cream Parlour ambayo bado ipo hadi leo na haikuwa mbali na Avalon Cinema.

Miaka ile haikunipitika hata kwa mbali kuwa hili duka la Ice Cream iko siku atalinunua rafiki yangu marehemu Yusuph Zialor na litakuwa mali yetu.

Wakati nikinywa chai nikawa namuhadithia baba filamu niliyoona jana na sifa kem kem za Elvis.
Baba alipozungumza akanambia kuwa wao walipokuwa vijana wakimpenda Bing Crosby.

Sasa pale nilipokuwa naangalia ile ‘’cover,’’ ya High Society nilikuwa nimerudi kote huko nilikoeleza hapo juu na ni kwa hakika ni nyuma sana wakati ule nikiwa mtoto mdogo wa  miaka 12.

Nilimkumbuka baba yangu ambae alikuwa keshatangulia mbele ya haki na nikaikumbuka maktaba yake ya muziki ambayo kwa mara ya kwanza nilisikiliza ‘’trumpet,’’ ya Louis Armstrong na yeye mwenyewe akiimba kwa sauti yake nene na kavu na nikakumbuka pia habari za Bing Crosby.


Louis Armstrong alikuja Dar es Salaam mwaka wa 1960 na akafanya onyesho Ilala Stadium. 
Hii picha inamuonyesha Armstrong katikati akiwa nje ya duka la muziki la Mzee Mahmoud 
wa pili kushoto Lucille mke wa Armstrong ni huyo wa kwanza kulia
Acacia Avenue (sasa Samora Avenue)

Nilikuwa New York na nikamwambia mwenyeji wangu Abdillah Rijal anipeleke kwenye Louis Armstrong Museum ambayo niliona inatangazwa katika ‘’brochure,’’ bahati mbaya sikupata muda wa kufika kule.

Kumbukumbu yangu ya Avalon Cinema ina mengi. Sikumbuki jina la filamu lakini nakumbuka kumuona Loius Armstrong katika filamu moja hapo Avalon Cinema. Filamu hii ilikuwa ndani yake na wanamuziki wengi na nakumbuka walikuwapo Herman’s Hermits.

Leo hapa ninapoandika inanijia picha ya Dar es Salaam ilivyokuwa katika miaka ya 1960 na nasikia nyimbo za nyakati zile kama ‘’Something Good’’ ya Herman’s Hermits, ‘’Hello Dolly,'' ya Louis Armstrong…

Ilikuwa Avalon Cinema nilipoangalia moja ya filamu zangu nizipendazo sana – Lawrence of Arabia (Peter O’ Toole, Omar Shariff na Anthony Quinn), The Sound of Music (Julie Andrews), Kissin’ Cousins (Elvis Presley), Concert for Bangladesh (George Harrison na  Ravi Shankar) The Godfather (Marlon Brando) kuzitaja chache.

Miaka imepita na Dar es Salaam imebadilika sana.

Jengo la Avalon bado lipo lakini sasa si jumba la senema tena. Historia ya Avalon Cinema itabaki katika kumbukumbu yangu ikinikumbusha siku za utoto wangu.

No comments: