Sheikh Hamisi Mataka |
Shule ya Msingi Mchikichini sikupata
kushika zaidi ya nafasi tatu za juu muda wote wa miaka saba hapo shuleni. Kwa
kuwa nilianza darasa la kwanza nikiwa na umri wa miaka 11 ule moja wa miaka mine
ambayo ningekuwa shule ya msingi iliniwezesha kumiliki chuo changu mwenyewe
yaani madrasa, nikiwa mwalimu mkuu katika umri mdogo wa miaka 15. Nilipoanza
shule darasa la kwanza katika huo umri wa miaka 11 ambao ni mkubwa kwa kuanza
darasa la kwanza pale Shule ya Mchikichini nilikuwa pia mwalimu wa dini kwa wenzangu.
Kwa ajili ya makuzi yangu ya Kiislam nilikuwa nikilitoka eneo la shule tu nilivaa
kanzu yangu juu ya sare kwa kuwa sikujisikia kuvaa kaptula mitaani kwani uchi
wa mwanmme unaanza juu ya magoti yake.
Mwalimu wangu wa Historia Mzee
Kasunsumo alipata kuniambia: '’Sheikh Khamis, pamoja na uwezo wako wa kielimu
hutochaguliwa kwenda sekondari na kinachokuponza ni huu ualimu wako wa Dini ya
Kiislamu.'’ Hakika na kweli ikawa hivyo badala ya kuchaguliwa kwenda sekondari
nikapelekwa Chuo Cha Ufundi Chang'ombe kusomea Usukaji Mota. Uhodari wangu wa
masomo na tabia yangu nzuri hazikutazamwa. Kilichoangaliwa ni ule Uislam wangu.
Sikukaa sana pale Chuo Cha Ufundi na kwa hakika moyo wangu ulikuwa ukiniuma
nikiwaona wale ambao mimi nikiwapita katika masomo wako sekondari wanasoma na
mimi nimepelekwa Chuo Cha Ufundi nikiwa muhitimu wa darasa la saba.
Kilichofuatia ni kuwa nikaacha katikati na kujiunga na Chuo Cha Biashara ambapo
nilichukua Basic Book-Keeping Certificate (BBC) na kufanya vizuri sana. Katika
mitihani ya ndani, '’’I was first out of 67 candidates,’’ yaani nilikuwa
mwanafunzi wa kwanza nikiongoza katika wanafunzi 67. Huu ndiyo ulikuwa uwezo
wangu mimi mwanafunzi niliyotokea shule ya msingi Mchikichini na maalim wa
madras mtoto.
Nilipokabidhiwa cheti cha BBC taarifa ya ufaulu ilinizuia kuendelea na
NABOCE kwa ibara hii: '’If you are Standard Seven you will be eligible to sit
for NABOCE Exams after you have completed formal Form Four Education.’’ Bahati
mbaya ilikuwa inazidi kuniandama. Wakati huo umaskini wa familia ulinilazimisha
kufanya kazi za kutafuta riziki halali mbali ya kuendelea kufundisha dini
katika chuo change. Baba yangu Sheikh Saidi Mnuta Mataka akinilazimisha kuoa
mapema ili amuone mjukuu wa jina lake kabla hajafa.
Nilioa.
Sasa kwa ajili ya kizingiti kile cha
kuwa na cheti cha kidato cha nne nililazimika kuitafuta elimu ya sekondari
kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (National Correspondence Institute) na nikafaulu
QT (NECTA) Mtihani wa Kidato cha Nne na nikaweza kurudi chuoni CBE
kuendelea na masomo ya NABOCE huku
nikipata ajira ya kudumu ya Mfasiri wa Lugha za Kiarabu, Kiingereza na
Kiswahili katika moja ya balozi nchini.
Laahawla! chuoni sikuikuta tena NABOCE bali mtaala mpya wa ATEC I na II
nami nikazisoma kozi husika nikafaulu na nikaweka cheti kibindoni. Lakini ajira
mpya ya Ubalozi haikuendana na mambo ya uhasibu nikalazimika kubadili upepo na nikasoma
Lugha ya Kiingereza na kufanikiwa kutunukiwa Diploma ya Lugha (Kiingereza).
Muhimu leo nikuandikiapo haya
nimeweza kupata vyeti hivi vifuatavyo hapo chini:
1. B.A. (Philosophy, Religious Studies
& Kiswahili) - OUT.
2. Post Graduate Diploma (Education) -
UDSM.
3. M.A. (Education) - UDSM.
4. Post Graduate Diploma (Management) -
IGNOU/UDSM under Pan African E-Network (African Union/Government of India)
through Tele-Conference facility.
5. Post Graduate Diploma (Human Resource
Management)- IGNOU/UDSM.
Hapa nilipo sasa In Shaa Allah nasubiri MBA (HRM)
baada ya kuwasilisha tasnifu yangu juu ya Time Management kupitia utafiti
nilioufanya IFM, Dar es Salaam chini ya Dr. Adam Jamal kwa anuani hii: ‘’Managing
Time Effectively: A Case of Lecturers in the Higher Learning Institutions.’’
Sasa hivi ni mwanafunzi wa LLB
anayefikiria kuja kufanya Comperative Study kati ya Islamic Law na Conventional
Law (Common Law and Others).
Kinachofurahisha siku ya Graduation
wale walioungaunga elimu na waliounganisha husimama mstari mmoja kutuzwa.
HM
HM
No comments:
Post a Comment