Sunday, 8 April 2018

ABDULRRAHMAN AHMED: MWALIMU MTOTO WA HISTORIA YA TANU NA UHURU WA TANGANYIKA


Abdulrahman Yahya

Leo nyumbani kwangu nimepata bahati kubwa ya kutembelewa na kijna mdogo anaesoma kidato cha pili.

Kijana huyu amesoma kitabu cha Abdul Sykes na baada ya kukimaliza alipata hamu ya kukutana na mwandishi na ndiyo hii leo asubuhi akabisha hodi nyumbani kwangu.

Kijana huyu jina lake ni Abdulrahman Yahya.

Baada ya mamkuzi mgeni wangu kwa muhtasari tu akaniambia kuwa kaipenda sana historia ya uhuru jinsi watu walivyojitolea kwa hali na mali kuikomboa Tanganyika kutoka katika mikono ya ukoloni wa Waingereza.

Baada ya kumaliza haya Abdulrahmani akanichukua katika safari ambayo ingawa njia naijua na nchi tunayokwenda naifamu lakini kwa mara ya kwanza nikajiona na kuhisi kama vile njia ile tunayosafiri na nchi ambayo tayari tushavuka mpaka na kuingia, nikajiona nchi hii ambayo mimi ni mwenyeji sijapatapo kufika wala njia tuliyopita sijapatapo kutia mguu wangu.

Kijana alianza kunieleza historia ya uhuru kutoka kichwani kwake akianza sura ya kwanza ya kitabu akinihadithia kwa ufasaha wa hali ya juu huku uso una tabasamu kubwa.

Alinihadithia nini kimeandikwa mwanzo wa kitabu.

Hakika nilipigwa na butwaa kama kweli nasikia hiki kitabu kikisomwa na mtu mwingine tena ghibu asiyekuwa mimi, kijana akiyataja majina ya wazalendo waliopigania uhuru na yale waliyofanya tena kwa mpangilio uliokuwa sawia.

Katika ya maelezo nilimkatiza nikamuuliza, ‘’Abdulrahman wewe ushahifadhi juzuu ngapi?’’
Akanijibu kuwa kahifadhi juzuu tatu na anaendelea.

Jibu nikawa nimelipata.
Ikiwa kijana keshakunywa juzuu tatu zipo kichwani unategemea nini?

Nilimsikiliza kwa kiasi cha saa nzima kijana akimwagika na kutiririka kwa ufasaha alinihadithia mwanzo wa African Association 1929 hadi kufika Al Jamiatul Islamiyya 1933 akiwataja wahusika wakuu na yale waliyoyafanya.

Abdulrahamani kanishika mkono tuko na Kleist Sykes anapigana na Waingereza akiwa askari katika jeshi la Wajerumani mwaka wa 1914.

Hapo keshanitoa Pangani na Kalenga jeshi la Wazulu mamluki wameshinda vita dhidi ya Bushiri bin Salim na Mtwa Mkwawa.

Jeshi hili si miaka mingi kupita sasa linapambana na Waingereza na Kleist Sykes akiwa askari katika jeshi la Wajerumani katika Vita Kuu ya Kwanza (1914 – 1918).

Abdulrahman ananihadithia vipi Abdulwahid Sykes na mdogo wake Ally na wao kama ilivyokuwa kwa babu yao Sykes Mbuwane na baba yao Kleist na wao wakingia kupigana katika Vita Kuu ya Pili (1938 – 1942) Burma safari hii wao wakiwa askari katika jeshi la Waingereza, King’s African Rifles (KAR).

Mwalimu wangu Abdulrahman ananieleza yalitotokea Dar es Salaam katika miaka ya 1930 magomvi katika ya Wazulu, Wanubi na Wamanyema, ''watu wa kuja,'' dhidi ya wenyeji wenye nchi yao na mji wao, Wamashomvi na Wandengereko.

Abdulrahman akanieleza vita iliyokuwapo 1930s katika Kleist, Mzulu na Erika Fiah Mganda, aliyekuwa na gazeti lake, ''Kwetu,'' lililokuwa sauti ya Waafrika.

Sauti ya Maalim Abdulrahman imetanda ukumbini chumba kizima.
Utake usitake lazima utamsikiliza...Mashaallah.

Abdulrahman ananifikisha shule ya St. Francis, 1952 Julius Nyerere alikokuwa anafundisha ananifahamisha vipi Nyerere alifika nyumbani kwa Abdul Sykes kitendo kilichokuja kubadilisha maisha yake yote.

Ilikuwa kama niko katika ukumbi wa senema taa zimezimwa giza limetanda ukumbi wote na mbele kwenye ‘’screen,’’ inaonyeshwa filamu nzima ya uhuru wa Tanganyika.

Ilikuwa kwangu mimi ni burudani ya aina yake kwani kitabu hiki kwa lugha ya Kiingereza kilipotoka mwaka wa 1998 Abdulrahmani alikuwa bado hajazaliwa na hata ilipotoka nakala ya Kiswahili 2002 yeye bado alikuwa bado hajaja duniani.

Tulipokuwa tunaagana nilimwambia, ‘’Sheikh Abdulrahman leo nimekupa ijaza In Shaa Allah nenda kakisomeshe kitabu hiki popote kwani wewe unajua.’’

Allah amuhifadhi na amzidishie ilm kijana huyu.
Amin.

Abdulrahman Yahya akieleza historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika




No comments: