Tuesday, 17 April 2018

DAR ES SALAAM DOCKWORKERS’ UNION (CHAMA CHA MAKULI WA DAR ES SALAM) 1947 – 1950

DAR ES SALAAM DOCKWORKERS’ UNION
(CHAMA CHA MAKULI WA DAR ES SALAM)
1947 – 1950

Utangulizi
Historia ya Dar es Salaam Dockworkers’ Union, yaani Chama Cha Makuli wa Bandari ya Dar es Salam niliisoma mahali kama ilivyoandikwa na mtafiti na mwandishi mmoja Mwingereza lakini kwa kuwa nilishasoma kazi zake nyingi kuhusu historia ya Tanganyika na kwa kuwa sikuridhika na jinsi alivyokuwa anakwepa kueleza mengi yaliyofanywa na Waswahili wa pwani nikamtilia shaka katika maelezo yake ya historia ya chama hiki. Kwa ajili hii basi nami nikaamua kufanya utafiti wangu niangalie kama na huku nako kafanya kama ilivyo kawaida yake. Naam na huku nako kafanya yale yale aliyozoea. Haya hakufanya yeye peke yake. Hata watafiti wengine waliokuja kuandika baada yake mtindo ulikuwa hivyo. Watafiti hawa walipokuja kuandika historia ya vyama vya wafanyakazi, historia hii ilipuuzwa. Baada ya kumaliza utafiti na kuandika historia ya makuli wa Dar es Salaam ya miaka ya 1940 sikujuta na nilishukuru kuwa nimepata nafasi ya kuinusuru historia hii iliyotukuka ya wazee wangu wenyeji wa Dar es Salaam. Hii ndiyo historia ya makuli, wazee wetu naeleza hapo chini vipi walikabiliana na dhulma za wakoloni wakati palikuwa hakuna hata chama kimoja cha wafanyakazi Tanganyika. Prof. Mohamed Bakari amepata kusema kuwa ikiwa kama sisi hatutaandika historia yetu na tukawaachia watu wengine waiandike basi wataandika mambo ambayo sisi hayatatupendeza. Namshukuru marehemu Mzee Islam Barakat kwa kunisomesha historia hii na mke wa Abdulwahid Sykes, Bi. Mwamvua bint Mashu kwa kuniongezea taatifa nyingine.

Bandari ya Dar es Salaam, 1947
Waajiri wakuu katika bandari ya Dar es Salaam yalikuwa makampuni matatu ya kupakua na kupakia shehena melini: African Wharfage Company, East African Lighterage and Stevedoring Company (Dar es Salaam) Ltd; na Tanganyika Boating Company Ltd. Zaidi ya makampuni hayo, Tanganyika Landing and Shipping ilifanya kazi za gati kwa mkataba na Tanganyika Railways.  Wafanyakazi wengi wa bandarini walikuwa kutoka sehemu za mbwambao wa pwani ya Tanganyika - Wangindo, Wazaramo, Warufiji, Wamashomvi na Wamatumbi, takriban wote wakiwa Waislam. Katika miaka ya 1940 Dar es Salaam ilikuwa mji mdogo ambako karibu watu wote mjini hapo walikuwa wakifahamiana. Kwa ajili hii wafanyakazi wa bandarini walikuwa ni kama jamii ndogo iliyounganishwa pamoja kwa kila hali kuanzia mila na utamaduni wao hadi Mungu muumba wao. In Shaa Allah tutakuja kuona huko mbele vipi mambo haya yalikuha kutumika kama silaha dhidi ya wakoloni. Wengi wa wafanyakazi bandarini waliishi si mbali sana na bandari yenyewe: - Gerezani, Kisutu, Msasani, Kariakoo, Ilala, Temeke, Mbagala na Buguruni.

Mbali na Tanganyika Railways na utumishi serikalini, bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ya tatu kama mwajiri mkuu. Lakini kazi nyingi za Waafrika pale pwani zilikuwa za mkataba wa kulipwa kwa siku, kukiwa na wafanyakazi wachache sana waliokuwa wakilipwa kwa mwezi. Utaratibu huu uliojulikana kama kile kilichojulikana kama, ‘’daily pay,’’ yaani kufanya kazi kama kibarua kwa lugha ya Kiswahili, mfanyakazi analipwa bada ya kumaliza kazi yake ya siku. Mpango huu uliwekwa kwa makusudi ili kuweka ushindani katika kupata kazi na hivyo makampuni yapate kupanga mishahara, hasa ya vibarua ili iwe ya kiwango cha chini. Zaidi ya hayo, kukosekana kwa mikataba ya kudumu, kulisaidia kumweka mwajiri katika hali ya kutowajibika na yale ambayo angewajibika amtimizie mfanyakazi chini ya sheria za mikataba ya kazi. Ili kupata faida kubwa kwa kutumia upenyo huu, makampuni haya ya kupakua na kupakia shehena melini yalikuwa yakibadilisha wafanyakazi wao karibu kila baada ya miezi kumi na miwili ili kutumia udhaifu huu kwa ukamilifu. Vilevile hili liliwezekana kwa kuwa kazi ya bandari ni ya msimu, kuna wakati meli zinakuwa nyingi bandarini na kuna wakati zinaadimika.

Katika miaka ile kazi ya bandarini ilikuwa ya hatari, ikishindana na kazi ya migodi. Kiwango cha vifo na ulemavu kutokana na ajali na ilikuwa juu sana. Wafanyakazi wengi waliathirika kwa kutokuwepo kwa mikataba ya kudumu ambayo ingewafunga waajiri kutoa fidia kwa ajili ya vifo na vilema kazini. Wafanyakazi wengi walipata vilema vilivyowatia umaskini na hawakulipwa fidia yoyote. Masharti haya ambayo dhahiri yalikuwa ni ya kukandamiza na ya uonevu yalizusha migogoro mingi sehemu za kazi. Hali hii ya migogoro ilijidhihirisha zaidi kwa wafanyakazi kutoroka kazini, kufanya hujuma na migomo isiyokwisha. Lakini bado serikali ya kikoloni ilijifanya kutoelewa ukweli kwamba Mwafrika alikuwa mwanadamu kama alivyo Mzungu, Muasia au Mwarabu. Serikali ilikuwa na dhana ya ajabu na wakati mwingine ya kusikitisha juu ya hisia ya Waafrika kama binadamu. Taarifa ya kila mwaka ya Idara ya Kazi ya mwaka wa 1945 ilisema hivi:

Mwafrika ni muhafidhina kuhusu kula na inamhitaji mwajiri awe shababi sana kuweza kumzuia aache tabia yake ya kufanyia kazi mchana kutwa akiwa hana kitu tumboni mwake, kisha kila siku jioni alivimbishe tumbo lake kwa ratili mbili za ugali uliopikwa vibaya.[1]

Taarifa hiyo inatoa dhana kwamba Waafrika wamezoea maisha magumu kwa kupenda kwao wenyewe si kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi iliyokuwa ikiwakabili. Shida zilipozidi kumuelemea huyu Mwafrika kutokana na sheria za kazi zilizojaa dhulma na kwa kupewa mishahara midogo, watu walikigeukia chama cha African Association ili kupata msaada na uongozi.

Hapa ndipo tunakutana na Abdulwahid Sykes na African Association na hii ilkikuwa mwaka wa 1947 miaka miwili imepita baada ya yeye na mdogo wake Ally kurudi kutoka Burma walipokwenda kupigana katika Vita Kuu ya Pili. Abdulwahid alikuwa mtoto wa Kleist Sykes mmoja wa waasisi wa African Association mwaka wa 1929. Dhiki ilitawala mji mzima hasa kwa kuwa ndiyo kwanza Tanganyika ilikuwa inatoka katika kishindo na mkiki mkiki wa vita. Hali hii ndiyo iliyomsukuma Abdulwahid katika siasa na ikamfanya aelewe maana ya harakati za wananchi dhidi ya utawala wa kigeni akiwa bado kijana mdogo sana. Kidogo kidogo baba alianza kumkabidhi Abdulwahid kazi za African Association na mara akawa msaidizi wa baba yake katika siasa za Dar es Salaam. Ilikuwa katika kutimiza haya ndipo Abdulwahid akajikuta anahusika na ule mgogoro wa makuli ulioibuka bandarini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukichemka pole pole chini kwa chini kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili. Hatimaye, Abdulwahid alihusika na harakati za siri za wafanyakazi bandarini ambao, wakiwa wamechoshwa na sheria za kazi za ukandamizaji na wakiwa wamechoka kunyonywa na makampuni ya meli, walikuwa wanapanga kuitisha mgomo. Kleist mwenyewe alikuwa hakuwa mbali na siasa za wafanyakazi yeye akiwa mwajiriwa wa Tanganyika Railways alijaribu kuwakusanya wafanyakazi wa Railway kuasisi chama chao.

Chama cha African Association ndicho kiliwakilisha maslahi ya wananchi wa Tanganyika na kimya kimya kiliunga mkono zile harakati za chini kwa chini za wafanyakazi katika kutafuta haki zao. Abdulwahid, kijana mdogo mwenye elimu na akiwa karibu zaidi na uongozi wa African Association kuliko Mwafrika yoyote pale mjini, alichaguliwa kuongoza harakati za tabaka la wafanyakazi zilizokuwa zinaibuka. Ili kuifanya serikali iwasikilize mahali ambapo hapakuwa na sheria za kazi, ilibidi iwekwe mikakati ambayo ingeifanya serikali ipitishe sheria hizo. Kamati ndogo ya siri iliundwa na Abdulwahid akatiwa ndani ya kamati hiyo ili kuongoza mgomo uliokusudiwa. Kazi ya kamati hiyo ilikuwa kupanga na kuratibu mikakati ya kuitisha mgomo ambao ungelisaidia katika kuondoa ile dhulma iliyokuwepo. Makuli waliitisha mkutano pembeni kidogo mwa mji, mahali palipokuwa pakijulikana kama ‘’Shamba kwa Mohamed Abeid,’’ katika bonde la Msimbazi. Mohamed Abeid mwenye shamba hili alikuwa Muarabu mwenye asili ya Yemen na shamba lake lilianzia Msimbazi kuelekea Mchikichini. Sehemu hii ilichaguliwa makhususi mbali na macho ya watu ili ipatikane faragha waweze kufanya shughuli yao waliyokusudia kwa utulivu. Makuli walikula kiapo na kusoma Ahilil Badr ili kujikinga na unafiki, usaliti pamoja na shari ya vizabizabina wangeokataa kugoma. Ubani ulifukizwa na Qur’an ilisomwa. Wakijikinga na kiapo hicho cha mashahidi wa vita vya Badr na huku wakichochewa na ushujaa wa mashahidi waliokufa katika katika vita vya Badr wakipigana na makafiri wa Makka wakiwa pamoja na Mtume Muhammad (Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu Yake), makuli walichagua tarehe 6 Septemba, 1947 kuwa ndiyo siku ya kuanza  mgomo wao.

Siri ya mgomo huu ilihifadhika hakuna nje yao aliyejua nini kitatokea. Mapema asubuhi moja kile kilichoanza kama mipango ya siri dhidi ya makampuni ya Wazungu bandarini, kililipuka na kuwa mapambano ya dhahiri. Watu katika mitaa jirani ya Mtaa wa Kipata, alipoishi Abdulwahid mitaa wa New Street, Kirk na Livingstone walikuwa hawajatoka vitandani mwao alifanjiri moja wakasikia vishindo na makelele vimetanda mtaani. Makuli, baadhi yao wakiwa vidari wazi, walikuwa wameizingira nyumba ya Kleist, wakipiga makelele wakimtaka Abdulwahid atoke nje. Makuli wale walipiga kwata njia nzima kutoka bandarini huku wakitoa maneno ya kupinga ukoloni na wakiimba kupandisha morali zao. Tukio hili halikuwa na kifani. Ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Tanganyika kwa wananchi kushuhudia katika mitaa ya Dar es Salaam uasi wa dhahiri kama huo dhidi ya serikali ya kikoloni. Abdulwahid, wakati ule kijana mdogo kabisa wa umri wa miaka 23, akichungulia kupitia dirisha la chumba chake alichokuwa amelala, alishangazwa kuona umati mkubwa wa watu nje ya nyumba yao. Aliweza kuwatambua baadhi ya wenzake katika kamati ile ya siri iliyokuwa inapanga mipango ya mgomo. Alipotoka nje kuonana nao makuli wenye hasira walimfahamisha kuwa mgomo ulikuwa umeanza na wasingerudi kazini hadi madai yao yote yamekubaliwa.

Mgomo huu ulienea kama moto wa makumbi ulikumba nchi nzima kwa kasi ya ajabu. Ilikuwa kama vile wafanyakazi wa nchi nzima wametaarifiana. Wafanyakazi wa Tanganyika Railways huko Tabora wakiongozwa na Salum Abdallah Popo waliingia kwenye mgomo tarehe 11 Septemba, siku tano baada ya mgomo wa makuli kuanza Dar es Salam. Chama cha African Association mjini Tabora kilimteua Mwalimu Pinda, aliyekuwa akifundisha shule ya St Mary, kuwa 'mshauri' wa wafanyakazi waliogoma. Kama ilivyokuwa Dar es Salaam, African Association, Tabora ilijiingiza katika mgomo huu kutoa ujongozi na mwelekeo wa madai ya Waafrika, Asubuhi ile ya siku ya mgomo wafanyakazi wa Tanganyika Railways walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira cha Town School, wakakaa chini ya miembe kujikinga jua. Tabora ni maarufu kwa miti hiyo. Tangu siku hiyo kiwanja hiki kikawa ndicho uwanja maalum kwa mikutano yote ya siasa.

Serikali ilimtuma kijana mmoja kutoka Masasi aliyesoma katika shule za misheni, Frederick Mchauru kuwahutubia wafanyakazi na kuwaomba wasimamishe mgomo na warudi kazini. Mchauru alikuwa Mmakonde kutoka Newala. Alielimishwa St. Josephís College, Chidya na St. Andrewís College, Minaki. Mwaka 1946, Mchauru alikuwa amerudi kutoka London University akiwa amehitimu masomo yake na kuanza kazi mjini Tabora kama Assistant Social Development Officer. Wafanyakazi waliokuwa kwenye mgomo walimpigia kelele wakimtaka anyamaze huku wakimwita msaliti. Inashangaza namna shule za misheni zilivyowatengeneza watumishi wa serikali walio wasomi wawe watiifu na waaminifu kwa dola. Wasomi hawa mara nyingi walijikuta wanasigana na wale waliokuwa wakipinga ukoloni na udhalimu. [2]

Mchauru alishindwa kutambua hali halisi iliyokuwapo pale sike ile. Mchauru alipuuza zile kelele akaendelea kuzungumza akijaribu kuwasihi wafanyakazi warudi kazini kwao. Ghafla hali iligeuka. Watu walipandwa na hasira na kusikia wakisema ashikishwe adabu. Watu waliokuwa wamehamaki wakaanza kumsogelea. Salum Abdallah, akiwa kiongozi wa watu wale, alihisi kuwa endapo hatachukua hatua ya kumnusuru Mchauru huenda watu wakamuadhibu. Alienda pale aliposimama Mchauru. Aliinua mikono yake juu akawataka watu watulie. Salum Abdallah alikuwa mtu wa miraba minne na alikuwa na sauti kubwa. Wanachama wengi wa Tanganyika Railways African Union (TRAU) wanamkumbuka kwa sauti yake, hasira zake na kwa umbo lake kubwa. Salum Abdallah alikuwa anafanyakazi katika karakana ya kufua vyuma. Wafanyakazi walipomuona Salum Abdallah walitulia na Mchauru akaondoka pale kimya kimya kupeleka taarifa kwa hao waliomtuma kuwa watu wamegoma, hawasikii la muadhini wala la mnadi sala. Salum Abdallah alikuwa kahamia Tabora mwaka ule ule wa 1947 akitokea Dar es Salaam. Alihamia Tabora baada ya karakana ya Railways kuhamishwa kutoka Dar es Salaam na kupekekwa Tabora.

Mgomo ulienea nchi nzima na wananchi katika sekta zote kote waliweka chini zana zao za kazi. Mfumo mzima wa uchumi ulisimama. Mgomo ulidumu mwezi mzima. Wanazuoni wengi wamechambua kipindi hiki cha kuibuka kwa tabaka la wafanyakazi katika Tanganyika. Wote wamekubali kuwa ule mgomo wa mwaka 1947 ndio uliofungua ukurasa mpya katika  historia ya vyama vya wafanyakazi Tanganyika. Friedland, akitathmini aina ya uongozi ulioongoza mgomo, yeye anasema:

Mgomo uliandaliwa na kamati ya siri ya makuli wasiojua kusoma; hawakujua lolote kuhusu vyama na walidhani kama wangetambulikana wangekamatwa.  Baada ya kutoa madai kwa waajiri bila kufichua utambulisho wao, madai ambayo yalipuuzwa, mgomo mkubwa ulitokea. [3]

Mgomo ule ulisababisha serikali ya kikoloni kupitisha sheria ambayo iliruhusu kuundwa na hatimae kusajiliwa kwa Dar es Salaam Dockworkers’ Union. Bienefield, akifafanua mapatano yaliyofuata mara baada ya mgomo baina ya makuli na mwakilishi wa waajiri wao, anasema: Vili mwakilishi kama huyo atakavyokuja yaangalia mambo, au kutekeleza maamuzi, bila ya kuwepo chama cha wafanyakazi kinachofahamika, ilikuwa ni kitendawili.

Mafanikio ya mgomo huo hayakutegemea kiwango cha elimu ya makuli kama kujua kusoma na kuandika au kuwako kwa chama cha wafanyakazi ambacho kingeratibu. Mafanikio ya harakati hizo yalitegemea ule udugu uliokuwapo baina ya wafanyakazi ndani na nje ya ile kamati ya siri. Kinyume cha madai ya Friedland makuli bandarini hawakuwa hawajui kusoma katika maana halisi hasa ya neno lenyewe. Wengi wao walipata elimu ya madras ambako maarifa ya Kiislam yalifundishwa. Hii ni elimu, na kuhusu kusoma na kuandika wengi wao walijua kusoma na kuandika kwa irabu za Kiarabu. Haiwi mtu hajui kusoma pale anapokuwa hajui herufi za Kirumi.

Wafanyakazi bandarini walikuwa wamejifungamanisha na kiapo kimoja kikubwa sana cha Waislam, kukumbuka ule moyo wa jihad zile siku za Mtume (Rehema na Amani Ziwe Juu Yake). Makuli walifungua na kufunga mikutano yao yote ya kupanga mikakati ya mgomo kwa kusoma Quran na kuomba msaada wa Allah. Kwa kufanya hivi walikuwa wakijinyanyua hadi kufikia daraja ya masahaba wa Mtume (Rehema na Amani Ziwe Juu Yake) waliopigana katika vita vya Badr, ambako jeshi dogo la Waislam mia tatu kumi na tatu wenye silaha duni walipata ushindi mkubwa dhidi ya jeshi lenye nguvu la makafiri 1000 wa Makka. Hii ni hali ambayo Friedland na Bienefied wameshindwa kuitambua na kuifahamu. Vivyo hivyo wanavyuoni wengi kabla na baada yao, kwa makosa au kwa makusudi, wamepuuza suala la Uislam katika siasa za Tanganyika wakati wa ukoloni. Kuanzia Vita Vya Maji Maji mwaka wa 1905 wakati wa kipindi cha Wajerumani, hadi harakati za vyama vya wafanyakazi mwishoni mwa miaka ya 1930 na harakati dhidi ya utawala wa Waingereza mwaka wa 1954, Uislamu ulitumika kama itikadi ya ukombozi. Tutafafanua ukweli huu hapo baadaye tutakapofikia kueleza jinsi Wakristo walivyokuja kufuta mchango wa Uislam katika historia ya Tanganyika baada ya uhuru kupatikana.

Mgomo wa mwaka 1947 ni mfano mzuri jinsi wa nguvu za Waislamu ziliyoungana kupambana na ukoloni. Vilevile unathibitisha vile kwa kutumia dini yao na mafundisho yake Waislam waliweza kutumia fursa hiyo kuilazimisha serikali ya kikoloni kubadilika na kukubali kuzungumza na wananchi. Katika mazungumzo hayo baina ya makuli na serikali, makuli waliweza kuwapenyeza wawakilishi wao wenyewe kwenye nafasi za uongozi zilizokuwa muhimu kwa kulinda maslahi ya wananchi. Serikali ya kikoloni ilitambua kuwa tabaka la wafanyakazi Waafrika hawalingewezi tena kupuuzwa, na ilianza juhudi kuruhusu kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi ili kuepuka migogoro siku za usoni.

Ukweli ni kuwa migomo haikukoma. Tutakutana na Salum Abdallah mara nyigine katika mgomo mwingine mwaka wa 1949 na mwingine tena mwaka wa 1960 lakini kabla ya kufika huko tutasoma historia yake mwanzo wa miaka ya 1950 wakati wazalendo walipoanza kufanya mipango ya kuunda chama cha siasa kudai uhuru wa Tanganyika. Kama vile haikutosha, baada ya kuunda TANU Salum Abdallah tajitokeza na kuunda TRAU kiwa mwenyekiti muasisi katibu akiwa Kassanga Tumbo. TRAU itampandisha hadi kwenye kilele cha juu kabisa katika maisha yake kama mpigania haki ya Waafrika wa Tanganyika na uwezo wake wa uongozi utadhihirika mwaka wa 1960 katika mgomo wa Railways uliodumu siku 82 na kuvunja rekodi iliyowekwa na Makhan Singh Kenya katika mgomo uliodumu siki 62. Kwa miezi mitatu wafanyakazi wa Railways waligoma na hivyo kusimamisha huduma zote za treni, meli na mabasi. Ingawa mgomo huu ulikuwa ushindi mkubwa kwa wafanyakazi wa Railways lakini kwa viongozi wa TRAU huu ulikuwa mwanzo wa mapambano kati yao na utawala mpya wa wananchi uliokuwa unasuburi kuchukua madaraka ya nchi.

Erika Fiah
Naibu Kamishina wa Kazi, M. J. Molohan alikuwa pandikizi la mtu na alikuwa na desturi ya kutumia baiskeli kwendea kazini, jambo geni katika siku zile kwa afisa wa Kiingereza. Molohan alianza kutafuta watu wangeoweza kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Dockworkers’ Union, chama ambacho kilikuwa kiundwe mwaka uliofuatia. Aliyekuwa akimsaidia katika kazi hii ya kumtafuta katibu alikuwa Islam Barakat, askari katika Vita Kuu vya Pili. Barakat alikuwa na damu ya Kiafrika na Kiarabu. Yeye ndiye alikuwa Labour Inspector wa kwanza Mwafrika. Barakat alipendekeza majina mawili kwa Molohan. Moja lilikuwa lile la Abdulwahid Sykes, kijana wa mjini, mtoto wa Kleist Sykes, mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu. Jina lingine lilikuwa la Erika Fiah, mwanasiasa mpevu na mtu wa makamo. Wakati huo Fiah alikuwa na umri wa miaka 53. Erika Fiah alikuja Tanganyika pamoja na majeshi ya Waingereza kutoka Uganda wakati wa Vita Kuu vya Kwanza. Fiah alikuwa Mwafrika wa kwanza kuanzisha na kumiliki gazeti lake mwenyewe katika Tanganyika. Baada ya vita alilowea Tanganyika na kuishi Mission Quarters ambako alihariri gazeti lake, Kwetu.

Fiah kama wanasiasa wote wa zama zake, alikuwa Mwafrika kwanza na uzalendo ukafuatia. Vilevile alikuwa mmoja wa wafuasi wa mwanzo wa Karl Marx nchini Tanganyika na gazeti lake Kwetu, lilikuwa maarufu kwa sababu ya ukali na vijembe vyake dhidi ya ukoloni. Fiah alikuwa mwanasiasa aliyekuwa amepea sana katika wakati wake. Katika miaka ya 1930 aliwahi kujaribu kuhamasisha tabaka la wafanyakazi na wakulima kuwaunganisha dhidi ya ukoloni, lakini alishindwa kwa kuwa wananchi walikuwa bado hawajaamka kiasi cha kutosha kuweza kuitikia mwito wa kuuhamasisha umma kama tabaka. Kwa wakati ule Fiah alikuwa na upeo mkubwa wa siasa na alikuwa na uwezo wa kuhamasisha zaidi kuliko Abdulwahid. Vilevile Fiah alikuwa mtu mzima na uzee ni dawa. Haiwezekani kumlinganisha Fiah na Abdulwahid aliyekuwa kijana mdogo ambaye Fiah angeweza kumzaa. Kati ya kipindi kile kati ya vita vya kwanza na vya pili ya dunia, Fiah alitumia kalamu yake kudhihirisha bila ya woga matatizo yanayowakabili Waafrika. Mara kwa mara mawazo yake kama ilivyotegemewa hayakupokelewa vizuri na serikali.

Lakini Fiah hakuwa tu adui wa serikali alikuwa pia adui wa Kleist na Waafrika wengine mashuhuri, wengi wa hao wakiwa katika utumishi wa serikali. Huko nyuma katika mwaka wa 1933 kulikuwako na mgongano baina ya Kleist na Fiah kuhusu uongozi wa African Association. Kupitia gazeti lake Fiah alimshambulia Kleist akimshutumu kwa kile Fiah alichokiona kuwa tabia yake isiyokuwa ya kizalendo iliyotokana na asili yake ya Kizulu. Fiah alidai kuwa mambo yanapokuwa mazuri kwa Watanganyika Kleist atajinasibisha na Utanganyika, lakini upepo unapobadilika na kuvuma upande wa Wazulu, mara Kleist anakuwa Mzulu. Ili kuepuka mgongano Kleist alijiuzulu kama katibu wa African Association na Fiah alichaguliwa kushika nafasi hiyo. Kalamu ya Fiah ilikuwa haina muhali. Katika rambirambi alizotoa za kijeuri na za dharau juu ya kifo cha Martin Kayamba, Fiah aliomboleza kwa kusema kwamba Waafrika hawakunufaika kwa elimu ya Kayamba wala kwa wadhifa wake kama karani wa kaimu Katibu Mkuu katika serikali ya Waingereza. Fiah alipingana na Wazungu vilevile. Mwaka wa 1940 aliandika tahariri iliyowalenga Wazungu waliokuwa wakimpinga kwa kueleza wazi wazi fikra zake na kwa kuchapisha gazetini makala juu ya haki za Waafrika. Fiah alikuwa mwanaume kweli kweli hata ingawa wakati wa zile harakati za bandarini makuli wakiwa wanakwenda nyumbani kwa Abdulwahid kwa maandamano na hivyo kumpa hadhi ya uongozi wa harakati zile, kwa hakika Abdulwahid hakuwa anafikia hadhi wala kiwango cha Fiah ktika siasa za nyakati zile. Kumfananisha Abdulwahid na Fiah ilikuwa sawa na kufananisha mlima na kichuguu.

Molohan alikataa jina la Fiah kwa sababu ya msimamo wake mkali na vilevile kwa kuwa Fiah alikuwa si Mtanganyika. Serikali ya kikoloni ilimhitaji Mtanganyika mzaliwa kushika nafasi hiyo. Barakat alisaidia sana katika kuteuliwa kwa Abdulwahid kwa sababu alikuwa askari mwenzake waliyepigana pamoja Vita vya Pili na alitoka katika ukoo mashuhuri. Zaidi ya hayo Abdulwahid tayari alikuwa ni sehemu ya harakati za makuli. Halikadhalika kulikuwako na dalili kuwa makuli walimtegemea Abdulwahid awe kiongozi wao kuliko Mzee Fiah. Februari, 1948, Erika Fiah aliwekwa pembeni na Abdulwahid, kijana mdogo asiye na uzoefu wa siasa, akachukua nafasi ya uongozi wa Dar es Salaam Dockworkers’ Union na kuanza kazi ya kubadili vuguvugu lile kuwa chama cha wafanyakazi halisi kama vyama vinavyotambulika ulimwenguni kote. Hivi ndivyo Abdulwahid alivyochaguliwa kuwa katibu wa Dar es Salaam Dockworkers’ Union. Kuanzia kipindi hiki katika mwaka 1948 ndiyo maisha ya Abdulwahid  yanaanza hasa katika siasa, miaka mitatu baada ya kurudi kutoka vitani.

Kleist lazima alikuwa amefurahishwa sana na uteuzi wa mwanae. Siyo kwa kuwa mwanae alikuwa amechukua uongozi wa harakati za wananchi, lakini hasa kwa kuwa alikuwa amemshinda adui yake Fiah. Kuchaguliwa Abdulwahid kwenye nafasi hiyo kulikuwa kitu kilichotarajiwa kwa sababu tayari alikuwa anaongoza vuguvugu hilo tangu zile siku za ile kamati ya siri ambayo ilipanga mgomo wa makuli katika shamba la Mohamed Abeid mwaka wa 1947.

Hivi ndivyo wale makuli, ‘’wasiojua kusoma,’’ ambao hawakujua lolote kuhusu vyama vya wafanyakazi, kama alivyoeleza Friedland, walivyoweza kuandaa na kupenyeza uongozi wao wenyewe ndani ya mfumo wa utawala wa kikoloni. Abdulwahid kupitia nafasi yake mpya, alikuwa sasa ni msemaji wa tabaka la wafanyakazi lililokuwa likiibuka Tanganyika. Kuzuka kwa uongozi wa wananchi kutoka kwa makuli ilikuwa ni ishara kwa serikali ya kikoloni kuwa upepo wa mageuzi ulikuwa ukivuma. Waafrika walikuwa wanaanza kusimamisha uwakilishi wa kidemokrasia katika vyama vyao wenyewe. Kwa kumchagua Abdulwahid makuli walikuwa wameanza utaratibu wa kuchagua uongozi wa wananchi kuwakilisha maslahi ya Waafrika, na huu ulikuwa ndio mwanzo tu. Abdulwahid alihamia ofisi mpya ya katibu wa Dockworkers’ Union kama mjumbe wa chama cha African Association akiwakilisha maslahi ya wafanyakazi Waafrika.

Dockworkers’ Union, (Chama Cha Makuli), 1948
Mwaka wa 1948 serikali ilimleta kutoka Uingereza bingwa wa vyama vya wafanyakazi, G. Hamilton. Hamilton aliletwa kufanya kazi maalum katika Idara ya Kazi kukishauri Chama cha Makuli kuhusu kanuni za kufanya mapatano ya pamoja baina ya wafanyakazi na muajiri wao, hususan namna ya kuendesha chama cha wafanyakazi. Hamilton akiwa na Barakat kama msaidizi wake walitumia ofisi moja na wakisaidiana kuanzisha na kusimamisha chama hicho cha makuli. Hamilton mwenyewe aliwahi kufanya kazi bandari ya London na alikuwa na uzoefu mkubwa katika migogoro ya makuli. Ofisi za Dockworkers’ Union zilikuwa katika banda la mbao na paa la mabati. Banda hili lilikuwa mbele ya Avalon Cinema ambapo sasa ipo Ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Mikutano yote ilifanyika humo ikihudhuriwa na Hamilton na Barakat kutoka Idara ya Kazi na Abdulwahid na kamati yake ya utendaji wakiwakilisha Dockworkers’ Union. Hamilton alikuwa akiishi Gerezani, European Quarters ambako, sasa zipo nyumba za wafanyakazi wa Reli. Abdulwahid alikuwa anaishi Mtaa wa Kipata si mbali kutoka nyumba ya Hamilton. Ilimchukua Hamilton, kwa mwendo wa kawaida, kama dakika kumi tu kwa gari kufika nyumbani kwa Abdulwahid. Siku za mwanzo Hamilton alifanya kazi karibu sana na Abdulwahid wakati mwingine akimtembelea nyumbani kwake kusawazisha matatizo. Wakati ule ilikuwa kioja kumwona Mzungu akimtembelea Mwafrika nyumbani kwake. Watu walimwangalia Abdulwahid kwa heshima na maya kwa jinsi alivyokuwa na uwezo wa kuingiliana hata na Wazungu.

Kuundwa kwa Dockworkers’ Union, pamoja na urasimu uliozuka, kitu cha kawaida kwa chama chochote, kulizusha tatizo jipya kabisa kwa Abdulwahid kama mtendaji mkuu na kwa chama chenyewe kama taasisi. Maafikiano ya pamoja huhitaji ushirikiano wa pande zote zenye kuhusika katika mgogoro wa kazi. Madai ya makuli yalikuwa yanajadiliwa kwanza na kamati ya utendaji ya Dockworkers’ Union, kisha Abdulwahid anayawakilisha kwa wawakilishi wa makampuni ya meli. Halafu madai haya yatajadiliwa na pande zote, wakiwepo Hamilton na Barakat toka Idara ya Kazi, ili kutafuta msimamo wa pamoja. Kipaji cha Abdulwahid cha kuandika, ujuzi wake wa hati mkato pamoja na fasaha yake ya lugha ya Kiingereza vilisaidia sana katika kusukuma mbele haraka kazi nyingi za Dockworkers’ Union.

Kwa bahati mbaya maamuzi machache sana yalifanyika na majadiliano yalionekana kama kwamba yanalegalega mara nyingi. Hakuna maamuzi ya maana au makubaliano yaliyofikiwa. Kwa makuli huu mfumo mpya ulikuwa unachosha, unasumbua na unapoteza wakati bila kuonekana tija yoyote. Kufanya majadiliano ilikuwa ni jambo geni kwao ambalo hawakulitazamia hata kidodgo. Hili lilizusha mgogoro ndani ya Dockworkers’ Union yenyewe.  Abdulwahid alikabiliana na tatizo jipya kabisa, hali nyeti ambayo ilitishia kuvunja Dockworkers’ Union na kudhoofisha uongozi wake.  Hakuweza kufanya majadiliano moja kwa moja na makampuni ya meli, wala hakuweza kufanya majadiliano kwa kasi waliyotaka wanachama wake wala kwa mtindo ambao yeye ungemridhisha. Aliwajulisha wanachama juu ya hali hii ngumu inayomkabili. Aliwawekea wazi kwamba masharti ya kazi yaliyokuwepo yalikuwa hayakupendelea hatua za kishupavu dhidi ya makampuni ya meli au mawakala wao.          
      
Wafanyakazi bandarini walipoona hakuna chochote cha maana kinafanyika katika malalamiko yao walianza kumshinikiza Abdulwahid aharakishe majadiliano au sivyo wangeitisha mgomo wao wenyewe bila hata ya kutaka idhini ya chama. Utaratibu wa majadiliano na mwelekeo wa kutafuta ufumbuzi kwa migogoro ya kazi ulikuja kuwa chanzo cha mapambano ndani ya chama chenyewe. Wanachama waliendelea kumshinikiza Abdulwahid akatae majadiliano na aitishe mgomo mara moja. Mgogoro ndani ya uongozi wa chama ulifuata na makuli wakarudia mtindo wao wa kuandamana kati ya ofisi ya Chama cha Makuli na nyumbani kwa Abdulwahid wakimshinikiza Abdulwahid kuitisha mgomo haraka dhidi ya makampuni ya meli. Wakati wa mgogoro huu wa ndani ambao ulikuwa ukitishia kukigawa chama, Abdulwahid, Barakat na Hamilton walikuwa wakikutana mara kwa mara kujaribu kutumia ushirikiano wao binafsi pamoja na nyadhifa zao na mamlaka waliyopewa na serikali kuepusha mgawanyiko ndani ya uongozi wa chama. 

Abdulwahid alitaka kumaliza mgogoro huo uliokuwa unachemka pole pole kwa utulivu na kwa namna ya kiungwana kwa kadri iwezekanavyo. Lakini makuli hawakuwa na subira, walidai mgomo uitishwe kutatua tatizo lao mara moja na bila ya kuchelewa. Wakati Abdulwahid anahangaika kujaribu kutatua tatizo hilo na kuondoa mvutano baina ya uongozi wake na wanachama, mgomo wa pole pole ulianzishwa na wakorofi dhidi ya makampuni bila amri wala idhini yake.  Baada ya kutambua kwamba makuli hawakuwa tayari kwa maelewano yoyote zaidi ya hatua ya mgomo, Kleist alimshauri Abdulwahid ajiuzulu nafasi yake ili kuepusha mgongano na serikali. Ilikuwa dhahiri kwa Kleist kuwa harakati za wafanyakazi bandarini zilikuwa zikitoka nje ya udhibiti na mwanae alikuwa hawezi kuzirudisha tena kwenye njia ya kuridhiana. Kleist alikuwa na uzoefu wa siasa za wafanyakazi. Kati ya miaka 1939-1947 alishuhudia migomo mitatu na kama kiongozi wa chama cha wafanyakazi na katibu wa TAA aliwahi kuitwa mbele ya tume iliyoteuliwa na serikali kuchunguza migogoro kazini.

Kleist kama mwanasiasa mzoefu na kiongozi wa chama cha wafanyakazi alimwomba mwanae azuie harakati hizo. Alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa Abdulwahid na yale ambayo yangeliweza kutokea baada ya mgomo huo. Kleist alifahamu kwamba si chama cha African Association wala zile cheche za harakati za bandarini zilizokuwa zikiongozwa na mwanae zilikuwa na nguvu ya kuhimili kishindo na kisasi cha serikali endapo dola itaamua kuwashughulikia. Ilikuwa dhahiri kwake kuwa mabavu ya serikali pamoja na nguvu zake zisizo na kikomo hapana budi zingemwangukia mwanae, hao makuli na Dockworkers’ Union yenyewe. Kipindi hiki afya ya Kleist haikuwa nzuri kifua kilikuwa kikimtaabisha maradhi ambayo si muda mrefu yalichukua maisha yake ulipofika mwaka wa 1949.

Wakati huo Barakat alikuwa anapanga chumba Kariakoo miongoni mwa baadhi ya makuli. Barakat alipata fununu kutoka kwa makuli kuwa yule Mzungu, yaani Hamilton, alikuwa akiwachochea makuli kutomtii Abdulwahid na uongozi wake na waitishe mgomo. Wakati huo huo tetesi zilivuja kwa Abdulwahid kuwa Hamilton vilevile alikuwa akiwachochea makuli kumuondoa yeye kwenye uongozi. Wanachama walisikika wakilalamika kuwa Abdulwahid alikuwa akiwasaliti serikalini kwa kuwa hakuwa mgumu kiasi cha kutosha na kwa hiyo lazima afukuzwe au afanywe ajiuzulu cheo chake mara moja. Sasa Hamilton akawa tatizo na kikwazo kikubwa kwa Abdulwahid na Barakat. Abdulwahid na Barakat walishangazwa na zile tetesi ambazo ilikuwa vigumu kuzipa tafsiri. Inawezekanaje afisa Mzungu aliyeletwa kufanya kazi ya serikali ya kikoloni awaunge mkono makuli ambao machoni mwa serikali walionekana ni wakorofi?

Lakini kulikuwepo na dalili kwamba Hamilton hakuwa Mzungu wa kawaida. Mwenendo wake ulikuwa si wa kawaida kwa afisa wa Kiingereza.  Alikuwa na msimamo mkali kuhusu mambo ya dunia ambayo Waafrika waliokuwa chini yake hawangeelewa.  Siku moja Barakat alipokea jarida la Kikomunisti miongoni mwa barua zake.  Hakujua nani alimtumia makaratasi yale kwa kuwa hakukuwepo na anwani yoyote. Hamilton ambae walikuwa wakichangia naye ofisi alilinyakua jarida lile kutoka kwake bila kutamka hata neno moja la kumuasa. Siku nyingine Barakat alimwona Hamilton akisoma jarida la Kikomunisti ofisini na hakulificha hata alipojua kuwa Barakat alikuwa akimwangalia. Siku zile vitabu na majarida ya Kikomunisti yalikuwa yakichukuliwa sawasawa na maandishi yoyote ya kihaini yaliyokuwa yanawachochea watu dhidi ya serikali. Siku iliyofuata baada ya tukio lile Hamilton alimualika Barakat nyumbani kwake kuja kunywa chai.  Huku wakinywa chai Hamilton alimuuliza kama yeye anaamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu. Hamilton kusadikisha kuwa Mungu hayupo alimueleza Barakat habari za Charles Darwin na ile dhana ya Evolution. Ili kumaliza kufru ile, Barakat alimwambia Hamilton kuwa yeye kama Muislamu hakuwa na shaka yoyote kuhusu kuwako kwa Mwenyezi Mungu na uwezo wake mkubwa usio kifani.

Mwanzoni Barakat alidhani Hamilton alikuwa akiwapeleleza yeye na Abdulwahid ili apate kufahamu muelekeo wao wa kisiasa.  Barakat alimjulisha Abdulwahid kuhusu jambo hili. Lakini jinsi siku zilivyokuwa zinapita, ilimdhihirikia kuwa mambo hayakuwa hivyo. Iliwaingia moyoni kuwa Hamilton alikuwa mtu muovu sana na mwenye msimamo mkali wa siasa. Siku zile Ukomunisti na falsafa yake vilidhaniwa na nchi za magharibi kuwa ni usaliti kwa uhuru na ubinadamu. Waafrika waliokuwa na msimamo mkali kama huo hawakuvumiliwa hata kidogo. Gazeti la Kikatoliki Kiongozi lilipata kutoa onyo:  ‘’Upumbavu wa mwanadamu unathibitisha kuwa hauna kikomo. Urusi na utawala wake wa kikomunisti bila tone lolote la shaka ni adui wa mwanadamu asiyeweza kusuluhishwa naye.’’ Huu ndio ulikuwa msimamo wa Kanisa na serikali kuhusu Ukomunisti. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo lisiloweza kufikirika kwa afisa wa kikoloni kuukumbatia Ukomunisti. Lakini hakukuwa na lolote Abdulwahid na Barakat wangeweza kufanya kuhusu jambo hilo. Haikuwa rahisi kwa Waafrika kutoa shutuma dhidi ya afisa Mzungu. Jambo pekee lililowezekana ilikuwa kwa wao kuwa macho na kuchukua tahadhari. Akumulikae mchana usiku atakuchoma.

Hali kadhalika, Abdulwahid alikuja kupata habari kuwa mpinzani wake katika kile kinyang’anyiro cha nafasi ya katibu na adui wa baba yake wa miaka mingi, Erika Fiah, alikuwa akiuchochea uongozi wa chama kumpindua akisema, ‘’Muondoeni yule mtoto wa Kleist Mzulu.’’ Baadhi ya wale makuli walikuwa wanataka hasa Abdulwahid ajiuzulu na ampishe Fiah achukue uongozi wa Dockworkers’ Union. Jambo hili liligawa chama pande mbili. Upande mmoja ulimtaka Abdulwahid aendelee kukiongoza chama na mwingine ulimtaka ajiuzulu mara moja. Fiah alitakiwa kwa sababu baadhi ya wanachama walidhani Abdulwahid alikuwa na msimamo wa wastani mno na wakaunga mkono mwelekeo mkali wa Fiah.  Mgogoro ulipoendelea na bila na dalili zozote za kutatulika, Abdulwahid aliitikia wito wa baba yake na akajiuzulu cheo chake Julai 1948. Abdulwahid aliiongoza Chama cha Makuli kwa miezi sita tu.

Lakini ilipodhihiri kuwa kweli Abdulwahid sasa anajiuzulu na itawabidi wanachama wachague katibu mpya, kikundi cha wanachama kilimzuia na kumuomba abakie. Abdulwahid hakutaka kubadili uamuzi wake. Alikuwa ana matatizo mengine nyumbani. Baba yake alikuwa mgonjwa kitandani taabani kwa maradhi na alikuwa akikisisitiza kuwa Abdulwahid lazima ajiuzulu nafasi yake mara moja. Katika kuonyesha mshikamano makuli walimbeba kijana wao Abdulwahid juu juu mabegani toka ofisi za Chama cha Makuli Acacia Avenue (Samora Avenue) hadi viwanja vya Mnazi Mmoja mahali ambapo wanachama wa Dockworkers’ Union walikuwa wakifanya mikutano yao. Kujiuzulu kwa Abdulwahid hakumaanisha kuwa alikuwa hana maelewano na chama. Kujiuzulu kwake kulisababishwa na sababu nyingi zikiwemo fitina na hila zilizomhusisha Hamilton, Fiah na baadhi ya wanachama wa Dockworkers’ Union.

Mara baada ya Abdulwahid kujiuzulu, Fiah, adui mkubwa wa Kleist, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Dockworkers’ Union badala ya Abdulwahid. Lakini Fiah hakudumu kwenye nafasi hiyo mara aliondolewa na wanachama na bwana mmoja kwa jina Salum Mohamed akachukua uongozi kutoka kwake.

Tarehe 1 Februari, 1950, makuli walifanya mgomo mkali sana ambapo walipambana vilivyo na askari wa kuzuia fujo. Serikali ilichukulia kuwa migogoro ya mara kwa mara ya makuli ni siasa za vurugu na fujo dhidi ya serikali. Serikali iliwatuma askari wa kuzuia fujo (Kavirondo kama walivyokuwa wakiitwa na watu wa pwani) wakakomeshe mgomo. Hawa Kavirondo walikuwa askari toka bara waliojulikana kwa upofu na ukatili wao katika kutekeleza amri za kikoloni. Aghalabu walikuwa, kama kanuni, wakipelekwa kufanya kazi mbali na makwao ili wasipambane na watu wa kwao, endapo itabidi kuamriwa hivyo. Waislam wa mijini katika mapambano dhidi ya utawala wa Waingereza waliwaona Kavirondo kama vibaraka wa wakoloni na watu washenzi. Katika mapigano baina ya Kavirondo na makuli, Kavirondo kumi na tisa waliuawa.

Hali iliporudi kuwa shwari, Hamilton aliwekwa kizuizini nyumbani kwake na kimya kimya aliondolewa na kurudishwa Uingereza. Makuli wengi walikamatwa, wakatupwa rumande na mashitaka ya jinai yalifunguliwa dhidi yao. Serikali ilikuja kutambua kuwa Hamilton, mtaalamu wao wa vyama vya wafanyakazi waliyemleta Tanganyika, alikuwa mwanachama wa British Communist Party (Chama cha Kikomunisiti cha Uingereza. Wakati wote alipokuwa akifanya kazi Idara ya Kazi, Hamilton alikuwa mara kwa mara akiwachochea makuli wazushe migogoro pale bandarini.  Kama mfuasi wa kweli wa Marx alikuwa akiamini kuwa wafanyakazi wanastahili washike hatamu za juu za rasilimali. Aliamini kwamba mgogoro ule ungesambaa hadi kwenye sekta nyingine muhimu za uchumi kama ilivyokuwa katika mgomo wa mwaka 1947. Jambo hili linaeleza kwa kiasi fulani kwa nini Abdulwahid alijiuzulu wadhifa wake baada ya miezi sita tu na kwa nini kulikuwa na mabadiliko ya uongozi katika Dockworkers’ Union mara tatu katika kipindi cha miaka miwili. Katika mwezi wa Juni, 1950, Dockworkers’ Union ilivunjwa kwa amri ya mahakama na shughuli za vyama vya wafanyakazi hazikuibuka tena hadi mwaka 1955 baada ya kuasisiwa kwa TANU.

Sasa turejee kwa kifupi tu kwa Salum Abdallah aliyeongoza mgomo wa Railways wa mwaka wa 1947 na 1949. Serikali ilipo ruhusu vyama vya wafanyakaz mwaka 1955, haraka sana Salum Abdallah akishirikiana na Kassanga Tumbo wakaasisi Tanganyika Railways African Union (TRAU).

Harakati za makuli bandarini dhidi ya unyonyaji zilikuwa ndizo kichocheo kwa wafanyakazi wengi waliokuwa wakitumika chini ya hali ngumu za kazi. Mara baada ya mgomo wa mwaka 1947 vyama vitano vya wafanyakazi vilianzishwa: African Cooks, Washermen and House Servants’ Association, African Tailors Association, Morogoro Personal Servants Association na Dar es Salaam African Motor Drivers’ Association. Alipochukua ukatibu wa TAA mwaka 1950 Abdulwahid alitumia uzoefu alioupata Dockworkers’ Union kuwahamasisha watu kuingia TAA.  Ni uzoefu huo huo wa bandarini ndiyo alioutumia katika kuibadili TAA na kuunda TANU mwaka wa 1954.  Mapolu anasema kuwa harakati za vyama vya wafanyakazi vilienda pamoja na harakati za kudai uhuru:

Tanganyika African National Union iliundwa mwaka 1954. Siyo tu viongozi wake waliokuwa wale wale wa harakati za vyama vya wafanyakazi, lakini mara nyingi uongozi wa harakati mbili hizi zilifanana. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kwa harakati za kudai uhuru kukita mizizi miongoni mwa wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi ambavyo vilikitumika kwa malengo yake ya siasa.[4]

Vyama vilivyoonekana kama kwamba viliundwa kulinda maslahi ya wafanyakazi vilikuweko tangu miaka ya 1930. Serikali ya kikoloni, pamoja na kuanzisha sheria ya Trade Union Ordinance ya mwaka 1932, ilikuwa bado inapinga umoja wowote wa wafanyakazi ulioundwa kudai haki zao. Lakini jambo hili halikuwazuia wafanyakazi wasipiganie haki zao bila ya kujali kitisho cha wakoloni. Hakuna chama au jumuiya iliyoundwa iliyoamsha hamasa ya tabaka la wafanyakazi wa Tanganyika kama harakati zile za makuli wa mji wa Dar es Salaam.  Kuna tofauti kubwa sana kati ya Tanganyika Territory Civil Servants Association (TTACA) iliyoundwa mwaka 1922 na Martin Kayamba na Dockworkers’ Union katika uongozi na mwelekeo. TTACA kilikuwa chama halisi cha ustawi wa jamii ambacho hakikuwa na taathira yoyote dhidi ya ukoloni; TTACA ilikuwa kilabu ya makarani na waalimu, ikiwa na magazeti na timu ya kandanda, ikisaidiwa na kuungwa mkono na serikali.[5] Chama hiki na vingine vya namna hii vilivyoundwa na kuongozwa na wasomi havikufanikiwa chochote.

Kama vile wanahistoria walivyowapuuza waanzilishi wa harakati za kudai uhuru kabla ya mwaka 1954, vivyo hivyo historia rasmi ya vyama vya wafanyakazi Tanganyika inaanza baada ya mwaka 1955. Iliffe ameuona tena upungufu huu:

Fikra iliyozoeleka ya historia ya vyama vya wafanyakazi Tanzania ni kuwa vyama havikuanzishwa hadi miaka ya 1950.  Bwana Tandau anasema kuwa chama cha wafanyakazi kiliundwa na vijana ambao mwaka 1955 waliunda Tanganyika Federation of Labour, ambacho baadaye kilisababisha wafanyakazi kujiunga pamoja. Harakati za vyama vya wafanyakazi Tanzania, zinaonekana kama zinavyoonekana harakati za kudai uhuru - kama kitu kilichoundwa kutoka juu kwa juhudi ya kundi dogo la wanaharakati wasomi.






[1] LDAR, 1945, p.5.
[2] Mwaka wa 1955 Mwafrika mwingine kutoka sehemu hiyo hiyo, kusini mwa Tanganyika na mwanafunzi wa shule ile ile aliyosomea Mchauru, Yustino Mponda, alisimama pamoja na serikali ya kikoloni kuipinga TANU majimbo ya kusini wakati Masudi Suleiman Mnonji, Yusuf Chembera na Salum Mpunga walipokuwa wanawahamasisha wananchi kujiunga na chama ili kudai uhuru.

[3] M.A. Bienefield, ‘Trade Unions, The Labour Process,’ JMAS Vol. 17 No. 4 December, 1979, pp. 557-558.
[4] Henry Mapolu, Workers and Management, TPH, Dar es Salaam, 1976, p. 139.

[5] Iliffe, ‘Tanzania Under British Rule’ in B.A. Ogot and J. Kieran (Eds) Zamani: A Survey of East African History, East African Publishing House, 1968 p. 22 ikinukuliwa katika African Studies Working Paper No. 8, April, 1979, by G.W. Reeves.


No comments: