Monday, 16 April 2018

KUTOKA MAKTABA YA JUMA MWAPACHU: BARUA YA BABA YAKE KWA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS NYERERE 1949


Barua ya Hamza Mwapachu kwa Julius Nyerere 1949

Hamza Kibwana Mwapachu


Balozi Hamza Mwapachu ameiweka hadharani barua ya baba yake Hamza Kibwana Mwapachu (1913 – 1962) aliyomwandikia Julius Nyerere mwaka wa 1949.

Barua hii sasa karibu itafikia miaka 70.

Sababu ya kuiweka barua hii nadhani ni kutaka kulizindua taifa kuhusu kupotoshwa kwa historia ya wananchi wa Tanganyika katika kujikomboa kutoka makucha ya ukoloni wa Waingereza.

Kumekuwa na tatizo kubwa sana katika kutafiti na kuiandika kwa sawa historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.

Takriban yote yaliyoandikwa kuhusu historia hii yamemtaja Julius Nyerere peke yake kiasi cha kufanya iaminike kuwa kabla yake hapakuwa na wanasiasa wala hapakuwapo na juhudi zozote za kutaka kuikomboa Tanganyika kutoka katika ukoloni.

Mwelekeo huu uneifanya nchi ikose mashujaa wake.

Jambo la kusikitisha ni kuwa na pale inapojaribiwa ingawa kwa kuchelewa kuwaenzi mashujaa waliopambana na ukoloni maswali mengi hujitokeza ambayo hakuna awezaye kuyajibu kwa uhakika na kwa ithibati ya kuaminika.

Mathalan inawezekanaje ikatolewa Medali ya Mwenge wa Uhuru kwa Abdulwahid na Ally Sykes, ndugu wawili waliokuwa kati ya waasisi 17 wa TANU ukawaacha waasisi wengine kama Saadan Abdul Kandoro na Japhet Kirilo kwa kuwataja wachache.

Itoshe tu kueleza kuwa medali hizi zimetolewa kwa kuchelewa miaka 50.

Ally Sykes kapokea medali yake akiwa katika miaka yake ya mwisho wa maisha yake, akiwa mgonjwa, miaka miwili kabla ya kifo chake mwaka 2013.

Lakini swali linakuja vipi utawapa medali mashujaa hawa wa uhuru usimpe medali Hamza Mwapachu ambae ushahidi wa historia unaonyesha kuwa ndiyo alikuwa, ‘’mentor,’’ wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Abdul Sykes na mwalimu wao hawa wote waliokuja kudai uhuru katika nafasi zao tofauti na baada ya uhuru kupatikana wakaja kuwa viongozi wa Tanganyika huru?

Dr. Vedasto Kyaruzi alipatapo kumwambia Juma Mwapachu kuwa kama si mpango walioweka Hamza Mwapachu na Abdul Sykes Tanganyika isingepata uhuru mwaka wa 1961.

Dr. Kyaruzi akaongeza kwa kumwambia Juma kuwa kule Nansio kisiwani alikopelekwa baba yake na Waingereza ile ilikuwa jela kumtia kizuizini kumzuia asishiriki katika siasa.

Wazalendo hawa ndiyo waliochora ramani ya njia ipi ichukuliwe kuidai Tanganyika na kuitoa katika mikono ya Wiangereza kwa salama.

Kwa wale waliokuwapo katika ‘’circle,’’ ile ya kupambana na Waingereza hakuna ambae hakuwa anajua kuwa Hamza Mwapachu ndiye aliyekuwa akisukuma mambo nyuma ya pazia iwe yuko Nansio au Rungwe sehemu za mbali alizotupwa na wakoloni ili asiwasumbue kwa kumtoa karibu na miji mikuu ambako ndiko yalipokuwa mashina ya kupinga ukoloni.

Mtafiti yeyote katika historia ya uhuru wa Tanganyika kama atakuwa makini hatoweza kumuepuka Hamza Mwapachu kwani ni vigumu kumtaja Julius Nyerere usimtaje Hamza Mwapachu.

Barua hii ya iliyoandikwa na Hamza Mwapachu kwa Julius Nyerere kwanza imedhihirisha ule ukweli kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika ipo katika vichwa vya watu na wengi wao wameshatangulia mbele ya haki,

Halikadhalika nyaraka nyingi za kipindi kile zipo mikononi kwa watu binafsi.

Barua hii ya Hamza Mwapachu kwa Nyerere imethibitisha ukweli huu na pia imefungua mlango kuwawezesha watafiti kuchungulia ndani kusoma na kufahamu nini Hamza alikuwa anasema kumwambia Nyerere.

Barua hiyo ni matokeo ya barua ambayo Nyerere alimwandikia Mwapachu kuhusu mambo muhimu waliyozungumza siku za nyuma.

Mwapachu anaandika na anasema kuwa hakutia katika maandishi kwa ajili ya kumbukumbu yale mazungumzo yao.

Baada ya kuandika haya Mwapachu anaorodhesha moja baada ya jingine katika yale waliyozungumza kama ifuatavyo:

1.       Trusteeship as compared to Protectorate and Mandate
2.      White Paper 191
3.      White Settlement in Tanganyika

Ukurasa wa kwanza wa barua hiyo ya kurasa tatu unaonyesha mambo manane lakini nimeweka kwa leo hayo matatu hapo juu nayo ni Udhamini wa Tanganyika chini ya Waingereza, Mjadala wa East African High Commission na Ukazi wa Wazungu Tanganyika.

Haya yalikuwa mambo mazito, makubwa na ya kuzungumzwa kwa siri sana baina ya Waafrika.
Inawezekana vipi historia kama hii ikaachiwa ipotee hivi hivi tu?

Barua hii ni muhimu sana na kwa haraka ikawekwa katika Makumbusho ya Taifa kwa faida ya vizazi vijavyo na naamini katika Maktaba ya Juma Mwapachu yapo mengi sana achilia hayo aliyohifadhi kichwani kwake.

MS


***
Mwisho wa barua hiyo utaona amemwomba Nyerere atoe salaams kwa Andrea and Catherine. Huyo Andrea ni Mwalimu Andrew Tibandebage na Catherine ni mkewe. Barua hii Nyerere aliiacha kwa Tibandebage mwalimu hapo St Mary's School in Tabora pamoja na vifaa vyake wakati akiondoka kwenda Edinburgh. Richard Tibandebage, mtoto wa marehemu Tibandebage  alinitumia baada ya kusoma makala yangu ya kumbukumbu ya marehemu Baba ya miaka 50 tangu afariki.
JVM

No comments: