MKASA WA ABDUL NONDO
Abdul Nondo |
Wiki kadhaa zilizopita niliandika ya
kwamba sakata la Abdul Nondo litawavua nguo serikali na jeshi la polisi na
hakika inaenda kutimia. Leo mwandishi mzoefu Luqman Maloto ameandika machache
kuhusu sakata hilo.
Idara ya Uhamiaji ilimtaka Abdul
Nondo athibitishe uraia wake kwa kuwasilisha cheti chake cha kuzaliwa, vyeti
vya wazazi wake, babu zake na bibi zake. Lilikuwa agizo la hovyo mno.
Hata hivyo, historia ipo na inaishi.
Mpaka sasa maofisa hao wameshachapwa KO (Knock Out) na Abdul.
UNONDO WA ABDUL UBABANI
Unondo wa Abdul upande wa baba yake
unaelezwa vizuri na Sheikh Khamis Hababi wa Kigoma Ujiji. Sheikh huyu anaijua
vizuri familia ya Abdul Nondo.
Sheikh Hababi anasema: "Huyu
Kijana (Abdul Nondo) ni Mjukuu Wa mzee Omar Athuman Kagobe. Mzee Kagobe ni
mwanajeshi wa zamani (veteran) aliyepigana vita kuu ya pili ya dunia, na ndiye
aliyeileta TANU Kigoma. Wakati wa kudai uhuru Nyerere alipofika Kigoma amewahi
kufikia kwa mzee Kagobe mara mbili akiwa na Bibi Titi na Sheikh Suleiman
Taqadir. Nyerere alikula, kunywa na kusaidiwa nauli na familia ya kina Abdul
Nondo.
"Nyumbani kwa Sheikh Kagobe
ndipo alipofikia pia Sheikh Abdallah Saleh Al Farsy mara mbili na Sheikh Hassan
bin Ameir.
"Bibi yake mdogo Nondo ndiye
Mama yake Sherry Taki, aliyekuwa mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, na mama huyu
ndiye aliyemuuliza Nyerere kama atawanyang'anya Wahindi, waarabu na Wazungu
majumba na Mashamba, baada ya Uhuru. Nyerere akasema hapana, Utawala wa TANU
hautofanya hivyo (ingawa alifanya hivyo baada ya uhuru)."
TAFAKURI
Kwahiyo Uhamiaji wanaposema Nondo si
raia wanamaanisha Babu yake (mzee Kagobe) si raia. Mtu aliyepigana vita kuu ya
dunia hakua raia? Mtu aliyeintroduce TANU Kigoma (ambayo ndio CCM leo) hakuwa
raia. Mtu aliyemlisha na kumlaza Nyerere mara mbili nyumbani kwake hakua raia?
Kwamba Nyerere alikuwa akipewa msaada na mtu asiye raia.
Bibi yake mdogo Abdul, mama Sherry
Taki nae hakuwa raia, licha ya kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM? Yani CCM
iliruhusu mtu asiye raia kuwa mjumbe wa kamati kuu?
Ni wazi alama ya uraia wa kijana huyu
haiwezi kufutika kamwe katika historia. Familia ya kijana huyu imechangia uhuru
wa nchi hii, imechangia kuzaliwa kwa taifa hili, imechangia kuzaliwa kwa TANU
na hatimaye CCM.
UNONDO WA ABDUL UMAMANI
Unondo wa Abdul upande wa mama yake
unaelezwa kinagaubaga na Maalim Razaq Seleman.
Anasema: "Huyu kijana (Nondo)
mama yake ni wa ukoo Mzee Haruna Taratibu aliyesisi TANU Dodoma. Mzee Taratibu
alisaidia kuanzishwa kwa TANU kipindi ambacho watu wengi hasa wafanyakazi
walikua wanaogopa kujihusisha na siasa. Kati ya mwaka 1954 hadi 1958 kilikua
kipindi kigumu mno katika harakati za kudai uhuru.
"Mwalimu Nyerere mwenyewe
aliwahi kusema 'Hicho kilikuwa kipindi kigumu sana katika historia ya Chama
chetu na ni watu wachache sana walikuwa na ujasiri wa kujiunga na chama na
kukifanyia kazi.'
"Mmojawapo wa watu waliokua na
ujasiri huo ni mzee Taratibu (babu yake mdogo Nondo upande wa mama). Mwaka
1953, Haruna Taratibu, alikuwa na umri wa miaka 23 tu, akifanya kazi Public
Works Department (PWD) Dodoma kama fundi mwashi (mason). Pamoja na umri wake
mdogo alijaribu kuunda chama cha wafanyakazi kwa kuwahamasisha na kuwakusanya
vibarua walioajiriwa katika kazi za ujenzi (wengi wakitokea Kigoma).
"Kwa sababu ya harakati hizo za
kutaka kuanzisha chama cha wafanyakazi, Taratibu alionekana na wakoloni kama
mtu mkorofi na mzusha vurugu. Hata hivyo Taratibu hakufanikiwa kuanzisha chama
hicho na matokeo yake akapewa uhamisho kwenda Singida kama adhabu.
"Mwandishi Nguli wa Historia,
Mohamed Said katika kitabu ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 -
1968)...: (Phoenix Publishers, Nairobi, 2002) ukurasa wa 216, anaeleza kuwa
mzee Taratibu alivutiwa sana na harakati za MAUMAU nchini Kenya na alizoea
kufuatilia matukio yake katika gazeti lake alilokuwa akilipenda sana,
''Baraza', gazeti la Kiswahili la kila wiki kutoka Kenya.
"Ilikuwa katika Novemba 1954
wakati Taratibu alipokuwa akipekuapekua gazeti hilo ndipo alioposoma habari
kuhusu TANU. Taratibu aliuliza pale Singida mjini kama kuna tawi la TANU.
Taratibu alifahamishwa kuwepo kwa tawi la TANU pale mjini na katibu wake
alikuwa mzee mmoja kwa jina la Mzee Kinyozi.
"Taratibu alikata kadi yake toka
kwa huyo mzee na akawa mwanachama wa TANU. Asubuhi iliyofuata Taratibu aliingia
ofisini kwake na akaiweka kadi yake ya uanachama wa TANU yenye rangi nyeusi na
kijani juu ya meza yake, kila mtu aione. Ofisa Mzungu wa PWD Singida hakuweza
kuvumila ufedhuli kama ule, alishauri Taratibu apewe uhamisho kurudi Dodoma
alikotoka, kabla hajaeneza sumu yake kwa Waafrika wengine.
"Kwa kifupi mzee Taratibu
alijitoa kwa hali na mali kuianzisha TANU bila hofu ya kushughulikiwa na serikali
ya kikoloni, licha ya kwamba alikuwa mfanyakazi. Hatimaye alichaguliwa kuwa
mjumbe wa sejretarieti na kamati ya siri ya TANU (kwa pendekezo la Oscar
Kambona), na baadae alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TANU kanda ya kati,
Rais akiwa Alexander Kanyamara, Katibu Abdu Mohamed Mwamba, Mweka Hazina Omari
Suleiman, huku Binti Maftah Karenga, Bakari Yenga, Maalim Khalfan, Idd Waziri
na Said Suleiman wakichaguliwa wajumbe."
TAFAKURI
Leo mjukuu wa mzee huyu aliyepigania
uhuru anaambiwa si raia.
Mimi kama kawaida yangu nacheka. Ona
nacheka tena. Yaani nacheka mno. Nacheka zaidi dogo anavyowagonga KO watu
wakubwa wasiotumia 'hikma' na weledi kwenye kazi zao. Eti vyeti vya kuzaliwa
vya babu na bibi zako wa upande wa mama na baba. Nina siku nyingi sijasonya!!!!!
MAELEZO YA PICHA
Kutoka kushoto ni Idd Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramiya, Mwalimu Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu wakiwa stesheni ya reli Dodoma mwaka 1955. |
Kutoka kushoto ni Idd Faiz Mafungo,
Sheikh Mohamed Ramiya, Mwalimu Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna
Taratibu wakiwa stesheni ya reli Dodoma mwaka 1955.
Ndimi Luqman MALOTO
No comments:
Post a Comment