KUANZISHWA KWA AFRICAN FIESTA
Na Mohamed Bakari – Churchill – Simu: 0713361719
1963 - 1965
African Jazz |
Wingu zito lililohanikishwa na ngurumo
lilitanda siku ya harusi ya Kabasele, lakini siku hii ya Jumamosi angavu ya
mwezi Mei, 1963 hawakujishughulisha na hali ya hewa. Mvua nzito zinyeshazo
mapema kila mwaka katika nchi za joto za kusini zilianza kupungua na kuiacha
Leopoldville na hali safi ya mandhari ya kijani ikijitokeza. Wageni waalikwa
walikusanyika kushuhudia ndoa rasmi baina ya Kabasele na Antoinette France
Cedas aliyechukua nafasi ya Catherine ambaye alikuwa na nafasi muhimu katika
moyo wa Le Grand Kalle japo hakuwa mke rasmi. Joseph Malula, mjomba wake
Kabasele, kwa wadhifa aliokuwa nao katika kanisa Katoliki ndiye aliyeendesha
shughuli nzima ambayo kwake ilikuwa ni sherehe ya kutimiza wajibu wake binafsi
na ule wa kazi yake.
Ni miezi mitatu tu (kabla ya ndoa)
Kabasele na wanamuziki wake walikuwa wamerudi safari iliyofanikiwa kwa kishindo
katika nchi za Afrika Magharibi. Walianzia Mali walikomstarehesha Raisi Modibo
Keita na wananchi waliojazana uwanja wa Bamako. African Jazz iliendelea
kuyatumbuiza makundi ya wapenzi waliojaa shauku huko Upper Volta (Burkina
Faso), Senegal, Liberia, Cote d’Ivoire na Nigeria. Mwandishi mmoja alihitimisha
kuhusu safari hiyo, alidai kuwa African Jazz walipopamba moto, wachezaji
walikuwa wakishambulia sakafu.
Waliporudi Kongo, mapema mwezi wa
Februari, walijiunga na washabiki wao katika usiku wa Jumamosi uliochangamka
katika ukumbi wa Petit Bois Club. Baadaye katika mwezi huo huo wa pili, African
Jazz iliung’arisha mji wa Brazzaville kwa onesho la usiku lililofanyika pale
Tam Tam Bantou. Onesho hilo lilifana na kusifiwa sana.
Mbele ya hadhara ya ndugu na marafiki
wapatao 1500 katika kanisa la Eglise St. Pierre la Leopoldville, Monsignor
Malula aliwaongoza Joseph Kabasele na Antoinette katika kiapo chao cha ndoa.
Sherehe ya kiapo cha ndoa ilifuatiwa na sala na baadaye tafrija iliyofanyika
katika hoteli ya karibu. Jioni wageni waalikwa walikusanyika katika ukumbi wa
mgahawa wa Zoo kwa ajili ya sherehe kabambe ya harusi; Lakini katika jukwaa la
wanamuziki kulitokea jambo ambalo si la kawaida. Sura za watu waliokuwa wanajulikana
waliochukua nafasi zao jukwaani walikuwa ni wanamuziki wa Orchestre Bantou ya
Brazzaville. Nico, Roger na Rochereau hawakutokea. African Jazz ilikuwa wapi?
African Jazz walikuwa wanajiandaa
kwenda Brussels. Jumanne iliyofuata walirejea kwenye studio ya Fonior kurekodi
nyimbo mpya kwa jina la kiongozi wao bila ya yeye kuwepo na bila idhini yake;
kitendo kilichomaanisha wanamuziki hao walikuwa wamemtosa kiongozi wao.
Ukiachia kadhia ya kutengwa kwa Nico na Dechaud iliyotokea siku za nyuma, safari
hii wanamuziki wote walisimama pamoja. Wachambuzi walimuoneshea kidole Roger
Izeidi kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa maasi hayo kutokana na uhusiano wake na
Fonior. Inasemekana Izeidi aliwahi kusikika akisema kuwa “Tulikuwa tunazozana
na Kabasele mara kwa mara kuhusu fedha”.
Kabasele alimwambia mwandishi wa
habari wa ‘Presence Congalaise’ kuwa,
kundi liliamua kila mwanamuziki alipwe mshahara kila mwezi. Kabla ya azimio
hili yeye (Kabasele) alikuwa akiwalipa malipo ya awali kwa kutumia mfuko wake
mwenyewe; Lakini Nico na Rochereau hawakuridhika na utaratibu huo. Alikuwa
akiwalipa wanamuziki kila mwezi kwa kuzingatia mikataba yao; kwa hiyo, hawakuwa
na sababu ya kulalamika. Hivyo ndivyo ilivyotokea ndani ya bendi kubwa katika
historia fupi ya muziki wa Kongo, jinsi wanamuziki walivyomtosa na
kumfedhehesha kiongozi wao wakati wa sherehe za harusi yake.
Joseph Kabasele alikuwa nyota maarufu
sana katika wakati wake. Amekuwepo katika tasnia ya muzki kwa muda mrefu kiasi
kwamba baadhi ya wapenzi wa muziki humuita baba wa muziki wa kisasa wa Kongo.
Wakati huu hapakuwepo fursa
kupatanisha tena. Wanamuziki wake walimfedhehesha na kumpuuza wakati wa harusi
yake wakaenda zao Brussels. Kabasele ndiye aliyekuwa na jina la kundi na alama
ya biashara ya kundi. Isingewezekana awaachie waendelee kutumia jina la kundi
lake na alama yake ya biashara bila ya yeye kuwemo ndani ya kundi hilo. Hayo
ndio machungu yaliyosababisha kuzaliwa kwa Orchestre African Fiesta.
Tungo za Nico, “Bilombe ya Africa”
(Bingwa wa Afrika), iliyotolewa Brussels, kwa uaminifu kabisa ilitumia jina la
African Jazz katika mashairi yake kana kwamba Kabasele angelikubali mapinduzi
bila kupambana nao. Izeidi alisema, “Tulitengeneza santuri, lakini bado
zilikuwa katika jina la biashara la “Surboum African Jazz”.
Kabasele alipopata habari
aliwafikisha kina Izeidi mahakamani. Kwa mtazamo wao kina Izeidi waliona kuwa
walikuwa wakifanya hivyo kwa niaba yake (Kabasele). Kwa kuwa aliwapeleka
mahakamani wakaamua kubadili jina. Hivyo ndivyo lilivyopatikana jina la AFRICAN
FIESTA. Kibiashara Izeidi alianzisha matumizi ya jina la biashara la Vita (Vita
Label) kutoa santuri mpya za African Fiesta.
Pamoja na ‘Bilombe ya Africa’
wanamuziki walitoa nyimbo zingine zenye vionjo vya African Jazz kama vile
“Mwasi Abandaka” (Ni mwanamke ndiye anayeanza), “Pesa La Tout” (Gawa kila
kitu), “Ngonga Abeti” (Kengele inalia) nyimbo ambazo magitaa ya Nico na Dechaud
yalisindikiza sauti laini zilizotiririka kwa nguvu kama mto Kongo. Katika wimbo
wa Izeidi, “Mobembo Eleki Tata” (Safari ni ndefu Baba), Nico alicheza gitaa
lake kwa kubadilisha badilisha mapigo huku akionekana kufurahia wakati wote.
African Fiesta na muziki wake
ulisababisha kuibuka kwa vita ya maneno mitaani na katika vyombo vya habari.
Gazeti la ‘Actualities Africaines’ la Leopoldville, kwa maneno mazuri lilitoa
tamko zito la kuikubali African Fiesta:
“Nyimbo za African Fiesta zinaendeleza mfungamano na Nyanja za hisia zinazoonekana wazi katika mifumo ya muziki
iliyoanzishwa kwa misingi mbali mbali ya muziki unaohusika”
‘Presence Congolaise’ kwa kuchukizwa
na kitendo cha kumtusi Kabasele, lilizikanusha, kwa uchambuzi mkali, sifa za
majigambo zilizotolewa kwa African Fiesta:
“Kila mtu anajua kuwa African Fiesta kwa hakika inaelekea kutoweka katika
uwanja wa muziki. Nyimbo zake mpya hazina mashiko. Gita la Nico halina kipya,
limeanza kuchosha na kuchukiza”
Lakini katika maduka ya santuri na
vilabu vya usiku nyimbo za African Fiesta zilikubalika sana. Nyimbo za Brussels
zilivuma kila juma; na mpya zilizoinua jina la African Fiesta zilizorekodiwa na
‘Leo’ katika safari ya pili ya Brussels mwaka 1964. Izeidi, Nico na Rochereau
walifikia makubaliano ya uwajibikaji kwa pamoja; jambo lililoonekana, walau kwa
muda, lingedhibiti tamaa, ubinafsi na kutokuaminiana. Wanamuziki hawa,
waliokuwa wamechafuka sana mbele ya watu kutokana na jinsi walivyomtendea
Kabasele, walilazimika kufanya kazi ya ziada kurejesha heshima yao hadi kufikia
kuonekana kuwa katika nafasi sawa na OK Jazz.
Utulivu katika uendeshaji, haja ya
kurejesha hadhi yao na hali ya ukomavu ilimuinua mmoja mmoja na kundi lao kwa
ujumla. Rochereau akiwa nje kidogo ya kivuli kikubwa cha Kabasele alikubali
kuchukua nafasi sawa na ile ya mlezi wake. Rochereau aliteka hisia kwa kiwango
cha hali ya juu karibu katika kila neno aliloimba. Mmoja wa wafuatiliaji
aliandika katika miaka ya 1970 kuwa:
“Ni furaha inayoendelea na iliyojaa moyo wa kizalendo … Sauti yake ni
kijito cha maji halisi … ni sauti halisi na iliyotulia kiasi kwamba inatufanya tuzikumbuke
kazi nzito iliyofanywa na muimbaji wakati wa kuimba”
Tungo za Rochereau ambazo zilikuwa
chanzo cha nguvu za African Jazz zilileta muziki wenye hadhi na hisia sawa
katika African Fiesta vile vile. Kurekodiwa kwa ‘Ndaya Paradis’ (tungo ya
Rochereau) kuliwakilisha uhalisia wa aina ya muziki wa African Fiesta.
Utangulizi wa Nico kwa gitaa la Hawaii, sauti peke ya Rochereau ikipanda na
kuongezeka kwa huba kwa ajili ya mpenzi wake Ndaya, ikiambatana na changamsho
la Nico na Dechaud lilitoa mdundo ulioandaliwa kwa uangalifu na kujitosheleza.
Ubunifu wa Nico na vionjo vyake vya
upigaji gitaa havikuweza kulinganishwa na vile vya bendi nyingine za Kongo.
Dechaud, aliyefunga nyuzi za gitaa lake, kama Jhimmy, kwa staili ya
‘Mi-Compose’ alitengeneza jamvi la mlio wa gitaa uliooana na mapigo ya Nico.
Ndugu wawili wakawa wameanzisha muundo maalumu wa upigaji magitaa.
African Fiesta ilizidi kujijenga kwa
kumuongezea Joseph Mwena, mwanamuziki wa miaka mingi toka kundi na NGOMA,
aliyechukuliwa kama mpiga gitaa la besi wa kudumu. Kadiri muda ulivyopita
wanamuziki wengine walijiunga na African Fiesta; ikiwa ni pamoja na Faugus,
mdogo wake Roger Izeidi, aliyekuwa akipiga gitaa la tatu (Rhythm), muimbaji
Paul Mizzele na muimbaji kijana wa kike aliyeitwa Photas Myosotis (Photas
usinisahau).
Kulikuwa na jambo moja lililoifanya
African Fiesta kutambulika miongoni mwa washindani wake wa karibu. Wakati OK
Jazz na Orchestre Bantou walikuwa wakiongozwa katika ‘Saxophone’, African
Fiesta walijibu kwa tarumbeta la Dominique ‘Willy’ Kuntima. Willy, ambaye ndiye
aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote katika kundi, alianzia Orchestre Odeon
Kinois katika miaka ya mwisho ya mwongo wa 1940. Alienda kurekodi santuri
katika kituo cha NGOMA na kwa kipindi kifupi alijiunga na LONINGISA ambako
alifanya kazi na kundi la OK Jazz lililokuwa linaanza kujitokeza. Lakini ni
katika ESENGO, Kampuni ya Kabasele na Dechaud, ambako Willy alipata nafasi.
Alikuwa makini na mwenye hamasa, kama asemavyo mwandishi mmoja wa habari wa Kongo,
Willy ‘alinyanyasa tarumbeta kwa nguvu iliyokuwa vigumu kuaminika. Akiwa
amesimama kwa miguu yote miwili, viwiko vya mikono vikiwa vimejikunja, akicheza
na kujipinda pinda mwenyewe huku jasho likimdondoka toka puani, kidevuni na
shingoni alikuwa akionekana kama anataka kulazimisha tarumbeta lisalimu amri.
Kwa sauti zenye vionjo vya Kilatini na vionjo vya Jazz, Willy aliziongezea
hadhi tungo za wenzake.
Wakati African Fiesta inajitokeza;
Joseph Kabasele alijaribu kuiunda upya African Jazz yake. Kwanza alimshawishi
Papa Noel kutoka Orchestre Bantou. Walisafiri hadi Kampala, Uganda mwaka 1963
ambako kundi jingine la Kikongo, ‘Vox Africa’ lilikuwa katika wakati mgumu.
Muimbaji Jean Bombenga, mwana African Jazz kipenzi cha Kalle, alianzisha kundi
la Vox Africa wakati Kongo Leopoldville ilikuwa inakaribia kupata uhuru.
Bombenga na Kabasele walikubaliana kuunganisha nguvu. Umoja wao ulizaa African
Jazz mpya iliyowajumuisha Kabasele, Bombenga na Mathieu Kouka katika safu ya
waimbaji na Papa Noel, Andre ‘Damoiseau’ Kambite, na Casimir ‘Casino’ Mutshipule
katika safu ya wapiga magitaa. Miezi michache baadaye Papa Noel alijiondoa
katika kundi. Lakini hata pamoja na Papa Noel kuwemo katika safu ya wanamuziki,
African Jazz Mpya haikuwa na mashiko kama ile ya mwanzo.
No comments:
Post a Comment