Monday 30 April 2018

MSIKITI WA KWANZA KIJIJINI NYANDA ZA JUU KUSINI NA BAKARI MWAKANGWALE


WAISLAMU wachache wa Mwakaleli, mkoani Mbeya wameanza harakati za ujenzi wa msikiti huku wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wenyeji katika mji huo.

Msikiti huo unajengwa katika Kijiji cha Mpunguti Kata Luteba Kitongoji cha Kamasulu mpakani mwa Kata ya Luteba na Kandeta, bonde la Mwakaleli katika Wilaya mpya ya Busokelo, Mkoani Mbeya.

Mwandishi wa habari hizi, akiwa hapo Mwakaleli, alibaini kuwa katika wilaya hiyo mpya ya Busokelo, iliyogawanywa kutoka katika Wilaya ya Rungwe, haina msikiti hata mmoja na huo ndio msikiti wa kwanza kujengwa katika ardhi hiyo ya Mwakaleli.

Baadhi ya wenyeji wameeleza kuwa Mwakaleli, ina jumla ya kata nne ambazo ni Isange, Mpombo, Kandete, Luteba, ambapo sasa Waislamu wachache kutoka katika kata hizo watalazimika kutumia msikiti huo pindi utakapo kamilika.

Akielezea harakati hizo za ujenzi wa msikiti huo Bw. Majid Adam Mpangoji, ambae ni mwakakilishi wa Jumuiya ya Waislamu Mwakaleli, katika Wilaya ya Busokelo, alisema wameanza ujenzi wa msikiti chini ya Jumuiya hiyo katika hali ya upinzani mkali baada ya wenyeji kubaini kuwa wanajenga Msikiti.

“Awali tulipata upinzani mkubwa kutoka kwa wenyeji baada ya kubaini kuwa katika eneo hilo unajengwa msikiti kwa ajili ya Waislamu hii ni kutokana na kuamini na kuelewa tofauti kuhusu Uislamu na kutokuwepo kwa msikiti kwa miaka yote katika ukanda huu kwa ujumla, ukilinganisha na wingi wa Makanisa, hivyo kuona kama wanawekewa kitu kigeni katika mji wao.”

Amesema Bw. Majid. Akifafanua zaidi, alisema ilifikia hatua hata viongozi wa kitongoji kilipo kiwanja cha msikiti huo kuungana na wakazi kupinga kujengwa msikiti katika eneo hilo lakini akasema baada ya mvutano mkubwa walishinda kwa hoja na kuanza ujenzi wa msikiti huo.

 Alisema, harakati za kuhakikisha unapatikana msikiti katika ardhi hiyo zinafanywa na jumuiya hiyo ambayo mpaka sasa ina mwaka mmoja na nusu tangu kuundwa kwake ambayo ina mchanganyiko wa Waislamu wageni na wenyeji.

Bw. Majid, ambae ni mmoja wa Waislamu wageni na aliyechachu ya harakati hizo, amesema mpaka sasa Jumiya hiyo imefanya harakati za kununua ardhi kupitia michango ya Waislamu hao wachache waliopo hapo.

“Katika azima ya kupata msikiti changamoto kubwa tuliyokutana nayo hapa Mwakaleli ni kupata eneo (ardhi) wengi hawakuwa tayari kuuza ardhi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti lakini pia ilikuwa shida na ngumu kukutana kwa pamoja kama Waislamu na kujadili kuhusu umuhimu wa kuwa na msikiti katika mji wetu.” Amesema Bw. Majid.

Lakini alisema, zilifanyika juhudi za makusudi kwa kumpitia Muislamu mmoja mmoja na kuwaelimisha na baadae waliona kweli, upo umuhimu wa kutafuta eneo na kujenga msikiti ili na wao wawe na sehemu maalum ya kuabudia na kuwa na kituo cha kufanyia shughuli zao za kiibada kama wanavyofanya wenzao Wakristo.

Alisema, juhudi hizo zilizaa matunda baada ya kuungwa mkono na Waislamu wachache wenyeji na kuweza kufanikisha kuanza harakati hizo na kuweza kufikia hatua hiyo huku malengo zaidi yakiwa kujenga kituo kikubwa, huku msikiti huo ukiwa ni hatua za awali kwani ni matarajio yake baada ya kukamilika utakusanya Waislamu na kupanga mipango mingine zaidi.

Alisema, katika ukanda huo wa Mwakaleli na pengine Wilaya nzima ya Busokelo, hakuna msikiti na kwa Waislamu wachache waliopo hapo (Mwakaleli) ama huswalia majumbani mwao au hujumuika na Wanafunzi wa Kiislamu wa Shule ya Sekondari Mwakaleli, kuswali haswa swala ya Ijumaa, Shuleni hapo.

“Shule hiyo imetoa chumba kimoja kwa ajili ya matumizi ya msikiti kwa wanafunzi wa Kiislamu (wanaotoka mikoani) waliopo katika shule hiyo kwa ajili ya kufanya ibada zao hivyo na sisi Waislamu wa nje ya shule huungana nao kufanya ibada zetu hapo na haswa Ijumaa wenyeji tunaungana na wanafunzi wa Kiislamu pale sekondari kwa ajili swala ya Ijumaa, hata hivyo ni chumba ambacho hakina hadhi ya kuwa msikiti lakini kwa kuwa ni dharura, hamna namna ibada inafanyika hivyo hivyo.” Amesema Bw. Majid.

Aidha, Bw. Majid, alisema Jumuiya yao ina malengo mengi na kwa sasa ni kuhakikisha msikiti huo unasimama na kuanza kufanyiwa ibada kisha hatua itakayofata ni kuanzisha madrasa na shule ya awali. Bw. Majid, alisema mpaka sasa ana mwaka wa tano tangu aingie katika mji huo na kubaini kuwa hali ya Uislamu ipo chini na hakuna harakati zozote za kuuhisha Uislamu kwani karibia wenyeji wote ni Wakristo. Waislamu ni wachache mno.

Hata hivyo, Bw. Majid, alisema ujio wa watumishi katika idara tofauti tofauti za serikali kutoka katika mikoa mbalimbali na kupangiwa majukumu katika mji huo ndio kumepeleka hamasa ya kupatikana kwa msikiti huo.

Alisema, ujenzi huo wa msikiti mpya upo katika hatua ya msingi kutokana na michango na nguvu za Waislamu hao wachache waliopo hata hivyo akasema wanaomba kuungwa mkono katika juhudi hizo kutoka kwa Waislamu popote walipo. “Mahitaji ni mengi lakini vifaa kama matofali, Nondo na siment vinahitajika kwa haraka ili kuwezesha msikiti kwenda kwa kasi.” Amesema Bw. Majid.

Kwa upande wake, Bw. Singolile Ngolako Mwakisenjele, aliye mzaliwa wa Kandete Mwakaleli, alisema wenyeji wa mji huo wanashuhudia msikiti wa kwanza kujengwa katika ardhi ya Mwakaleli tokea enzi za mababu zao.

 Bw. Mwakisenjele, alisema pamoja na kuwa wana fahamu kuwa dini zipo nyingi ikiwemo Uislamu, lakini baada ya Waislamu wachache waliopo hapo kwa sasa kuanza harakati za ujenzi wenyeji walistuka maana wamezoea kuona makanisa ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali na si misikiti.

Bw. Mwakisenjele, anasema tokea utoto wake na sasa ni mtu mzima akiwa katika ukanda huo alimjua Muislamu mmoja tu ambaye alikuwa ni maarufu kwa jina la Alwatan Mwafisi, hata hivyo nae aliupata Uislamu baada ya kwenda Mikoa ya Pwani.

Baadae, akasema aliingia Muislamu mwingine aliyekuwa akiitwa Majid, hivyo na kufanya mji kuwa na Waislamu wawili kwa miaka mingi hata hivyo pamoja na uwepo wao hapakuwa na fikra kuwa kutakuja kuwa na msikiti katika Mji huo.

“Lakini miaka inavyozidi kwenda na serikali kusambaza watumishi na wengine kupangiwa katika mji huo wa Mwakaleli, katika Taasisi za Serikali swa uchache wakaanza kuingia Waislamu japo sio wengi.

“Lakini kwa uchache wao huo na kukosekana kwa msikiti kila mmoja anaabudia nyumbani kwake, lakini naona kwa sasa wameamua kuunda Jumuiya yao ya Kiislamu na kuamua kujenga Miskiti kwa ajili ya kufanya ibada zao.” Amesema Bw. Mwakisenjele.

Bw. Mwakisenjele, alisema yeye haoni tatizo la ujenzi wa msikiti huo kwa sababu anaamini ni sehemu ya maendeleo na kwamba Serikali haina Dini ila wananchi wake ndio wana dini hivyo akasema si haki kuwapinga Waislamu kuwa na msikiti kwani ni haki yao ya msingi kikatiba katika haki za kuabudu.

No comments: