Shajara ya Mwana Mzizima
Rashidi Mfaume Kawawa
Mtetezi Wanyonge aliyekuja kuwa
Waziri Mkuu
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Raia Mwema Aprili 30 - May 1, 2018 |
UTAWALA dhalimu wa Kikoloni wa Ulaya Ingereza hapa
kwetu, ulijaa uonevu, udhalilishaji na ukandamizaji katika utoaji wake wa
huduma muhimu miongoni mwa wanajamii. Raia tuliwekwa kwa madaraja ambayo
Wazungu walikuwa daraja 1; Wahindi daraja II; Waarabu daraja III na Watu weusi
tukawa kwenye daraja la IV la mwisho.
Miongoni mwa mateso hayo ni pamoja na watu ‘mababa
majitu mazima’, kuchapwa viboko Bomani na Ma-DC na PC (wote walikuwa Wazungu
wanaotisha na masharubu yao mazito) pindi inapotokea ukawa umefanya kosa la
aina fulani, ambalo kwa wakubwa itabidi upigwe viboko.
Tiba, makazi pamoja na elimu, ilikuwa kwa matabaka
vilevile, hata ikawa kwa sisi wananchi wenyewe kutokuwa na sehemu bora ya
kuishi; tukiumwa tiba yetu ni panadol tu; kujifungua ni kienyeji nyumbani
ambako wengi wa wazazi walipoteza maisha; na shule zilikuwa chache tu za
‘Kayumba’, utake usitake. Katu, haikuwezekana watu weusi kuchanganywa na Wazungu
ama Wahindi kwenye elimu hata kama baba yako anao uwezo wa kukulipia ada kubwa
- afadhali ilikuwapo kidogo kwa watoto wa machifu.
Watesaji wakubwa kwenye ajira walikuwa ni Wahindi wakati
huo, maana wao ndio waliokuwa wakilimiliki uchumi pamoja na nyenzo zake zote
kuu (maduka, viwanda, mashamba, pamoja na ajira za nyumbani). Wenyewe wakituita
‘golo’, jina ambalo maana yake pengine ni fisi, sokwe au nyani
mweusi - walitudharau sana hata ni aibu kuhadithia.
Malkia wa Uingereza, pamoja na kwamba alikuwa ni
mkubwa wa Kanisa Anglikana duniani, alishindwa kutuona sisi kama binadamu kama
alivyo yeye na watu wa kwao; na akashindwa kutufanyia uadilifu kwa miaka yote
aliyoikalia nchi yetu.
Hali ikawa mbaya sana isiyovumilika kwa Waafrika
wanyonge hata ikasababisha kuwaibua watetezi wengi wa haki waje kuongoza
mapambano ya kupigania haki kwenye ajira
na utumishi. Miongoni mwao alikuwamo mwanaharakati wa kukumbukwa na kupigiwa
mfano, hayati Rashidi Mfaume Kawawa.
Hayati Mzee
Kawawa, ambaye baadaye alikuja kuwa mpaka Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi
hii, alikuwa ni kiongozi asiyetetereka kwenye masuala ya utetesi wa Haki za
Binadamu kwenye masuala ya wafanyakazi.
Alipambana vikali sana wakati huo wa ukoloni, kwani
anasifika na kukumbukwa kwa kuandaa migomo bila woga pamoja na kwamba ilipigwa
marufuku na Serikali ya Kikoloni. Habari
zinasema, Kawawa alikuwa na sauti na nguvu kubwa kwa jamii ya wanyonge wakati
huo kiasi kwamba alichokisema yeye basi kilitekelezwa mara moja.
Aliongoza muungano wa vyama vingi vya wafanyakazi hapa
nchini wakati huo kikiwemo kile cha ‘Makuli’
(wapakiaji na wapakuaji mizigo melini) wa bandarini cha Dockworkers Union 1948,
Tanganyika Railways African Union, African Cooks Union na Domestic Workers
Union (Chama cha Watumishi wa Majumbani)
Wakati ule, ukiacha Serikali na Railways, mwajiri
mwengine mkubwa alikuwa ni Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kazi nyingi za
Waafrika pale Pwani zilikuwa za ‘daily pay’, yaani ya malipo kila siku jioni.
Iliwezekana kufanya hivyo kwa sababu kazi za bandarini ni za msimu maana kuna
wakati meli zinakuwa nyingi na wakati mwengine zinaadimika; hivyo watu wachache
sana walikuwa na ajira za mwezi hata mwezi.
Kazi zile za Bandari zilikuwa ni za kuhatarisha maisha
sana. Wengi wa watu walipata vilema ama kupoteza maisha, hivyo kufanyishwa kazi
za namna ile bila mikataba stahili ulikuwa ni uonevu mkubwa sana. Hali hiyo
ilisababisha migomo isiyokwisha kutoka kwa wafanyakazi kwa kule kutotendewa
ipasavyo.
‘’Katika miaka ile kazi ya bandarini ilikuwa ni
hatari, ikishindana na kazi ya migodi.
“Lakini bado serikali ya kikoloni ilijifanya kutoelewa
ukweli kwamba Mwafrika alikuwa mwanadamu kama alivyo Mzungu Muasia au Mwarabu
…Serikali ilikuwa na dhana ya ajabu na wakati mwengine ya kusikitisha kuhusu
Mwafrika kama binadamu,”anaandika Mohammed Said, Uk 64 katika kitabu chake
mashuhuri cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, kinachosambazwa na Kampuni
ya Ibn Hazm Media Center, Dar es Salaam.
Wanaharakati wawili wakubwa ndio waliojitokeza mbele
zaidi katika kuwapigania na kuwatetea Waafrika wenzao wakati huo. Abdulwahid
Sykes akajikita kwenye Dockworkers Union
na Rashidi Kawawa akiwa zaidi kule TRAU; huku
wakisaidiwa kwa karibu na watetezi wengine shupavu wakati huo kama vile
Kassanga Tumbo, Michael Kamaliza, Alfred Tandau na Jacob Namfua.
Vuguvugu hizi na mwamko huu mkubwa ukazaa chombo
kikubwa zaidi kilichounganisha vyama vya wafanyakazi wote wakati huo
kilichojulikana kama Tanganyika Federation of Labour na Rashidi Mfaume Kawawa
akawa ndiye Katibu Mkuu wa mwanzo. Chama kingine machachari wakati huo ni kile
cha madereva na hasa madereva Teksi, kilichoongozwa na kada mashuhuri wa CCM,
Mustapha Songambele.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa harakati za vyama vya
wafanyakazi, kwenye harakati za kudai uhuru chama cha TANU kilikuwa kikihitaji
sana kuungwa mkono na kila sekta ya wazalendo wa Tanganyika wakati huo. Rashidi
Kawawa, haraka akaunganisha nguvu na TANU kwa kupeleka umma wote ule wa
watumishi kutoka vyama vilivyoungana na kuwa wanachama wa rasmi wa TANU.
Kwa namna ile viongozi wote wale waandamizi kutoka TFL
wakachukua nafasi za juu na kuwa na sauti kwenye masuala ya ukombozi wa taifa
hili. Chama cha TANU kikawa hakishikiki kutokana na chachu mpya aliyoingiza
Kawawa kwenye mapambano. Huo ukawa ndio mwanzo wa Kawawa kuwa karibu na Nyerere
kiasi kile.
Nilimfahamu Rashidi Mfaume Kawawa, nikiwa bado kijana
mdogo kabisa kwenye miaka ya mwanzo 1950s pale alipokuwa Ofisa kwenye Idara ya
Ustawi wa Jamii (Community Development Department) ya Serikali ya Kikoloni,
alipokuwa akicheza filamu za vichekesho. Filamu alizocheza hayati Mzee Kawawa
zilikuwa zikitupa burudani tosha sisi vijana wadogo wa wakati huo, kwani filamu
zile hazikuwa za kuburudisha peke yake, lakini pia kuelimisha jamii katika
masuala mbalimbali. Jina lake la kwenye sinema lilikuwa ‘Muhogo Mchungu’.
Sinema nyingine maarufu aliyoicheza Mzee Kawawa ni ile
iliyojulikana kama, ‘’Mgeni Mwema,’’ ambapo kila mwanzo wa mwezi kwa jiji la
Dar es Salaam zilikuwa zikionyeshwa pale viwanja vya Mnazi Mmoja, Ilala na
Magomeni na baadaye kuhamia sehemu nyengine mikoani. Pamoja na sinema za Muhogo
Mchungu, usiku huohuo huonyeshwa pia sinema nyingine za wale Wazungu wawili
wasanii, Stan Laurel na Oliver Hardy, hapa kwetu Dar es Salaam tukiwaita ‘Chale
Ndute na Chale Mbwambwambwa’, ambao vichekesho vyao kwenye zile sinema vimekuwa
kivutio mpaka leo duniani kote.
Kwa sababu
ambazo hazikuelezwa sawasawa mpaka leo, jamii ya Watanzania wamenyimwa nafasi
ya kuburudika na uhondo wa filamu za Mzee Rashidi Kawawa - hatujui zilipo,
zimevichwa kama zilivyofichwa nyaraka nyingi za historia ya muhimu ya nchi
yetu.
Katika miaka ile ya 50s, nikiwa mwanafunzi pale Shule
ya Msingi Mnazi Mmoja, mjini Dar es Salaam kila mara nilikuwa namwona Mzee Kawawa
akirandaranda nje ya nyumba ile ndogo iliyokuwa mkabala na shule yetu akiwa ama
anatoka au kuingia mle ndani kukutana na wapigania uhuru wenzake. Pale Ofisi
ndogo ya Makao Makuu ya CCM, ndipo yalipokuwa makao makuu ya Chama TANU wakati
wa kudai uhuru.
Hayati Mzee Kawawa, wakati ule alikuwa kijana
mtanashati kwelikweli; kila mara akiwa amependeza kimavazi, hasa pale alipokuwa
akivaa ile migolole ya vitenge vya Afrika Magharibi, hususan kutoka Ghana na
Nigeria, iliyokuwa ikipendwa na wapigania uhuru wengi sana wakati ule, akiwamo
Dk Kenneth Kaunda na Harry Chipembere wa Zambia; Kanyama Chiume na Yatuta
Chisiza wa Malawi; na Nyerere, Kassanga Tumbo na Michael Kamaliza wa Tanganyika.
Mtoto mkubwa wa hayati Mzee Kawawa, dadangu Rehema,
nilikuwa nasoma naye darasa moja pale shuleni Mnazi Mmoja pamoja na Silas
Munanka mtoto wa Mzee Bhoke Munanka. Wengine waliokuwapo pale wakati ule ni
pamoja na Wendo, mtoto wa Mzee Hamza Kibwana Mwapachu, Muharrami Kilongola na
Mohammed Rashid Sisso, ambao baba zao walikuwa viongozi waandamizi pale Lumumba
Makao Makuu.
Sasa asubuhi moja ya mwaka 1960, nchi ikiwa ndio
kwanza imepata Utawala wa Ndani (Internal Government), ambayo hata maana yake hatukuijua
ni nini siku hizo; tuliiona gari nyeusi aina ya Humber yenye kibao cha namba
kilichosomeka MWP, kwa maana ya Minister Without Portfolio inaingia mpaka ndani
mle shuleni. Dereva akiwa amevalia sare zinazomereta kabisa akashuka kuja
kumfungulia mlango abiria wake. Abiria alikuwa ni Rehema Rashidi Kawawa, ambaye
sasa hakuwa mwenzetu tena, kwani babake alikuwa amechaguliwa kuwa “Waziri
Asiyekuwa na Wizara Maalumu’ katika Serikali ile ya Madaraka ya Ndani.
Kwetu sisi vijana wadogo siku zile, lile lilikuwa ni
tukio kubwa la kukumbukwa, kwa sababu haikupata kutokea hata siku moja pale
shuleni, mwenzetu au mwalimu, akaletwa na gari mpaka ndani.
Kama vile sinema ndoto usingizini! Tulianza kuona
cheche za kuelekea uhuru kamili. ‘Golo mdogo’ anakuja shule na gari la aina
yake! Ule ukawa ni wakati kutafakari na kusubiri lini na sisi wengine tutahamia
kwenye magorofa ya Upanga na Uhindini wanakokaa Wahindi; kwani moja ya ilani au
ahadi za wanasiasa siku zile ni kwamba huru utakapopatikana, basi sisi
‘makabwela’ tutachupa kutoka raia daraja la IV hadi la kwanza.
Tumesubiri sana; na mpaka leo bado tunaendelea
kusubiri siku hiyo ifike. Ni mapambano ambayo bado yanaendelea mpaka leo
tumefikisha miaka zaidi ya 60 ya uhuru wetu na bado hayajafikiwa kisawasawa.
Kwa sababu ambazo mpaka leo hazijawekwa hadharani,
kipande hiki cha historia yetu hakitajwi, hakiadhimishwi na wala hakienziwi
hata kidogo. Nilidhani, kuwa na madaraka ya ndani lilikuwa jambo zuri sana
katika safari ya kuelekea kupata uhuru kamili. Pale nchini Kenya, ambako
mwandishi huyu alipata kuishi zaidi ya miaka mitano kwenye miaka ya 1970s,
Sikukuu ya Madaraka Day, husherehekewa kwa shangwe, nderemo na vifijo vikubwa
sana pengine kuliko hata siku ya uhuru kamili mwaka 1962.
Shermax Ngahemera, ni mhariri mwandamizi wa gazeti la
Kiingereza la The African, linalochapishwa kila siku na Kampuni ya New Habari (2006)
Ltd, pale Sinza, Kijiweni. Siku moja wakati ilipotangazwa kwamba Rashidi Kawawa
hatunaye tena hapa duniani; watu wakawa wanahaha kujaribu kumpamba na kumpembua
ili wapate kuandika taazia iliyo bora kuhusu mwanamajumui yule shupavu. Shermax
alisema hivi:
“Unajua huyu mzee ana mchango mkubwa sana katika
kufanikisha kupatikana kwa haraka uhuru wa nchi hii pengine kuliko mtu mwengine
Mwalimu, wakati fulani aliitwa na Gavana Sir Richard Turnbull na kuulizwa
anafikiri lini tutakuwa tayari kujitawala ili maandalizi yaanze mara moja. Nyerere
aliruka mita 100 juu akikataa kabisa kupewa uhuru kwa haraka hivyo kwa sababu
nchi ilikuwa bado haina wasomi ambao wangeweza kusaidiana na Mwalimu kuendesha
nchi,” anasimulia Shermax na kuendelea, ‘’ ”Siku kadhaa baadaye Nyerere
aliulizwa na Kawawa juu ya safari yake
kwa Gavana. Nyerere alimwambia Kawawa kwamba Gavana alikuwa anataka tumwambie
kama tuko tayari kujitawala maana yeye alikuwa amechoka na anataka kurudi
kwao,” amesema Shermax na kuendelea, “Nyerere alimwambia Kawawa kwamba hakutaka
kupata uhuru wakati ule maana watu wa kuweza kufanya kazi nyeti za kisomi za
Serikali hawakuwapo bado. Kawawa akamwambia Mwalimu akachukue nchi hata saa ile,
maana tuko kwetu na kama tutaanguka basi lazima tutasimama tena. Hatuna wa
kumwogopa hata kidogo. Nyerere alirudi tena kwa Gavana na kumwambia kwamba amefuta
usemi wake yuko tayari kujitawala wenyewe!” alimaliza Ngahemera.
Uhuru ulipopatikana mwaka 1961, hayati Mzee Kawawa
alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini, na ile Humber yake
nyeusi iliendelea kumleta shuleni Rehema.
Habari zinasema, baada ya miezi kadhaa ya kuwa huru,
hayati Mwalimu Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu na kumpisha Rashidi Kawawa
aongoze serikali maana ni yeye aliyesema ‘tutaweza tu hatumwogopi mtu’. Mwalimu
alirudi uraiani na kuzunguka nchi nzima kutafuta wasomi japo walikuwa wachache
waje kuchukua nafasi kwenye serikali ifikapo 1962 tutakapokuwa Jamhuri, yaani
mamlaka kamili.
Rashidi Kawawa, aliitumia vyema nafasi hii, kwani
hakusita hata kidogo, pale alipoona kuna Mwafrika mwenye ujuzi wa kazi ambayo
imeshikwa na Mzungu, basi mara moja alimpa mzalendo kazi hiyo. Kipindi hicho
kilijulikana maarufu kama Afrikanizesheni (Africanisation). Watu wengi
walipandishwa vyeo bila kutegemea. Mmoja wa watu hao alikuwa Mzee Mangara Tabu
Mangara, aliyekuwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali (Government Printer), nafasi
ambayo haikuwa inashikwa na Mwafrika kabla uhuru.
Nakumbuka pia shule za sekondari hapa jijini ambazo
zikiongozwa na Wazungu siku zote wakapewa kuwa Headmasters wake akina
Abdulrahman Mwalongo (Azania), Borry Lilla (Agha Khan), Rahma Mwapachu (Zanaki).
Huyo ndiye Rashidi Mfaume Kawawa; msanii wa filamu za
maigizo; mtetezi wa wanyonge wakati wa ukoloni; kiongozi wa vyama vya
wafanyakazi; Waziri Mkuu na Makamu wa Rais nchini; Waziri wa Ulinzi na ‘Simba
wa Vita’; Mwanasiasa nguli aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM.
Alamsiki!
sim
No comments:
Post a Comment