PETER
MHANDO
MUASISI
WA TANU TANGA
1955
Utangulizi
Historia
hii ya vipi TANU iliundwa Tanga nimeiandika kutokana na mazungumzo niliyofanya
na Mohamed Kajembe, Ngamiani Tanga ndani ya duka lake. Mzee kajembe
alinionyesha kijitabu cha mwaka 1955 kilichoandikwa kwa penseli ambamo ndani
yake aliandika tarehe za mikutano na majina ya wanachama waasisi wa TANU. Mzee
Kajembe alifariki Juni, 1996.
***
Jimbo
la Tanga lilibarikiwa na kuwa na Waafrika walioelimika sana. Waafrika hawa
walikuwa kutoka kabila la Wabondei. UMCA ilikuwa imehama kutoka Zanzibar kwenda
Magila katika Jimbo la Tanga mwaka 1875. Ukristo ulianzishwa na kustawi katika
nchi ya Wabondei, na vivyo hivyo nafasi za elimu kwa watoto wa Wabondei. Katika
lile wimbi la kuwania nafasi za elimu, watoto wengi wa Kiislamu walibatizwa. Ni
jambo la kawaida miongoni mwa Wabondei kukuta majina kama Peter Saidi au John
Ramadhani. Huu ni ukumbusho wa damu ya Kiislam katika Wabondei. Wabondei wengi
walikwenda Makerere College na siasa za kizalendo zilipoanza baada ya Vita Kuu
ya Pili (1938 – 1945), Wabondei walikuwa wamejaa katika utumishi wa serikali ya
kikoloni. Gurudumu la historia ya Tanganyika likizungushwa na baadhi ya
Wabondei, maarufu miongoni mwao wakiwa watu kama Martin Kayamba aliyejikomba
sana kwa wakoloni, George Magembe mtu ambae huku hayuko kule hayuko, hujui kama
yupo na wazalendo au na wakoloni, Stephen Mhando; mzalendo mwenye msimamo mkali
na mdogo wake Peter ambae alikuja kufanya makubwa katika harakati za kuunda
TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika lakini alifariki akiwa kijana sana kabla
ya uhuru kupatikana.
Wabondei
walikuwa ndiyo walimu, makarani, wakalimani mahakamani na maofisa wa ustawi wa
jamii katika serikali ya kikoloni. Hili lilikuwa tabaka maalum la Waafrika,
waliosomeshwa na wamishonari kuitumikia serikali ya kikoloni na katika kufanya
hivyo kulitumikia Kanisa na Ukristo, uhusiano ambao ulikuwa wenye manufaa kwa
pande zote mbili zilizokuwa
zikishirikiana. Ilikuwa vigumu sana kwa Wabondei kutokana na upendeleo huo wasifikirie kwamba wana uhusiano
maalum na Kanisa na serikali ya kikoloni. Hawa Waafrika wasomi kutoka shule za
misheni na Makerere walikuwa watiifu kwa taasisi mbili zanye nguvu nchini,
yaani serikali ya kikoloni na Kanisa. Kwa ajili hii basi, ilibakia kwa Wadigo
Waislam wasiokuwa na elimu kama elimu ilivyokuwa ikiitikadiwa, kuunda TANU na
kuongoza harakati za kudai uhuru.
TANU
iliasisiwa Tanga mwaka 1955 kukabiliana na serikali ya kikoloni kupitia juhudi
binafsi za kikundi cha wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Ngamiani.
Kikundi hiki kiliongozwa na kijana mdogo Peter Mhando, ambae kabla ya hapo katika
siku za nyuma alikuwa katibu wa kikundi cha majadiliano cha wasomi wa Kibondei
kilichojulikana kama Discussion Group. Peter Mhando alikuwa akifanya kazi kama
mhandisi katika Noran Industries- wanunuzi wa nazi na watengenezaji sabuni pale
Tanga. TAA ilikuwapo mjini hapo lakini ilikosa umoja baina ya wakazi wa mji kwa
kubaguana kwa dini, kabila, rangi na kiwango cha elimu. Discssion Group na vyama
hivi vilikuwa vimeshikwa na Wabondei wasomi wengi wao wakiwa Wakristo. Hali hii
iliviza juhudi za kuunda TANU. Vikundi hivi vya majadiliano, vilitarajiwa
kutojihusisha na siasa na vilitiwa nguvu na serikali vikihimizwa kufanya mijadala
na kusoma vitabu. Katika muda wote wa uhai wa vikundi hivyo hawa wasomi wa Kibondei
walikuwa chini ya usimamizi wa afisa Mzungu.
Akikiongoza
kikundi hiki cha wafanya biashara wa Soko la Ngamiani, alikuwa baharia mstaafu,
Hamis Heri Ayemba. Hamis Heri alikuwa Mmanyema kutoka kabila la Wakusu wazee wake
wakitokea Belgian Congo. Hamisi Heri alikuwa na umri wa katikati na katika
ujana wake alikuwa baharia na alipata kusafiri chombo kimoja na Abeid Amani
Karume, ambae baadae alikuja kuwa rais wa Zanzibar. Baada ya Vita Kuu ya Pili,
Hamisi Heri alirudi kwao Tanga ili aanze biashara. Hamiri Heri alikuwa mtu
aliyejikuza na kujielimisha mwenyewe; na alikuwa amesafiri sana. Hamisi Heri
alizungumza vizuri sana Kiingereza na Kiarabu. Katika miaka yake ya mwanzo
katika biashara, alikuwa dalali. Heri aliwashangaza wateja wake kwa uhodari
wake wa lugha mbali mbali, akinadi bei kwa Kihindi au Kiarabu, kutegemea utaifa
wa watu waliokuwepo pale mnadani.
Harakati
za kudai uhuru zilipoanza Heri alikuwa ametajirika na mmoja wa Waafrika wenye
kuheshimiwa sana mjini Tanga. Peter Mhando alipochoshwa na kile kikundi cha
majadiliano, alijiunga na Hamisi Heri na kikundi cha wafanya biashara wa
Ngamiani pale mjni ambao walikuwa wakijitahidi sana kuunda tawi la TANU. Wakati
huo mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa kuliko wote mjini Tanga alikuwa Mwalimu
Kihere.Lakini siasa za mapambano baina
ya ule uongozi wa TAA na kikundi cha majadiliano zilimzuia kutoa mchango
wowote wa maana. Mwalimu Kihere alikuwa amehudhuria mikutano kadhaa ya African
Association tangu mwaka 1946. Wakati wa uongozi wa Abdulwahid Sykes katika TAA
Mwalimu Kihere alikuwa amedumisha uhusiano mkubwa sana baina yake yeye mwenyewe
binafsi, Abdulwahid na Dossa Aziz. Hii ilifanya vilevile adumishe mawasiliano
ya karibu sana na makao makuu ya TAA. Lakini kwa sababu ya mizozo katika siasa
hapo Tanga, ule mkutano mkuu wa kuasisiwa TANU uliofanyika Dar es Salaam mwaka
wa 1954 ulipita bila ya Tanga kupeleka mjumbe.
Kile
kikundi cha wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Ngamiani kiliitisha
mkutano katika Ukumbi wa Tangamano tarehe 5 Septemba, 1955. Waliohudhuria
mkutano huo walikuwa Hamis Heri, Peter Mhando, Mohamed Kajembe,Tuwa Abdallah,
Dhili Mgunya, Abdallah Rashid Sembe, Victor Mkello, Mohamed Sadik, Hassan,
Peter Ramadhani Jembe na Ali Mohamed. Peter Ramadhani tayari alikuwa mwanachama
wa TANU huko Arusha na alikaribishwa mkutanoni ili waasisi wa TANU wanufaike
kutokana na uzoefu wake. Wasomi wa Makerere, uongozi wa TAA chini ya Waarabu na
Mwalimu Kihere hawakuwepo kwenye mkutano huu muhimu. Mkutano ulifunguliwa na
Hamis Heri saa tisa adhuhuri na ulifungwa saa mbili baadae kwa uamuzi kuwa
mkutano mwingine wa kuchagua viongozi wa chama ufanyike tarehe 23 Oktoba.
Mkutano uliamua vilevile kuwa juhudi zifanyike kupata waanachama wengi
iwezekanavyo. Kiasi kidogo cha fedha kilikusanywa na Harir Omari Siagi alipewa
aende makao makuu ya TANU, Dar es Salaam kununua kadi 70 za TANU.
Tarehe
23 Oktoba, wanachama wa mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua uongozi
wao chama. Hamisi Heri alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Peter Mhando katibu.
Jumla ya watu arobaini na tano walihudhuria mkutano huo na wakapewa kadi za
TANU. Mwalimu Kihere alihudhuria mkutano ule lakini hakuchaguliwa katika nafasi
yoyote ya uongozi. Kamati ya wanachama iliundwa kutokana na wale wanachama kumi
na moja waasisi waliokutana katika ule mkutano wa kwanza mwezi uliopita. Kamati
hiyo ilikuwa na wajumbe wafuatao: Abdallah Rashid Sembe, Mohamed Kajembe,
Victor Mkello, Dhili Mgunya, Ali Mohamed, Abdallah Mohamed na Mohamed Sadik.
Peter Mhando alijitolea nyumba yake kuwa ofisi ya kwanza ya tawi la TANU mjini
Tanga. Mara tu baada ya mkutano huu wazee wa Tanga wakiongozwa na Makoko
Rashid, mwanachama wa zamani wa TAA walianza kufanya kampeni kwa ajili ya TANU.
Chama kilipata msukumo mwingine na kuongezeka nguvu wakati Sadik Ali Patwa
Muasia tajiri alipoingia TANU.
Patwa
alikuwa Muislam wa madhehebu ya Shia. Patwa alikuwa amehamia Tanganyika kutoka
Zanzibar mwaka 1918 baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza. Pale Tanga
Patwa alianzisha kiwanda cha soda na akatajirika. Wakati huo wa zama za ukoloni
wakati Waasia wenzake walikuwa wakiwabagua Waafrika, Patwa alikuwa akikaa na
Waafrika wa rika lake akinywa nao kahawa. Halikadhalika watoto wake wakawa
wanacheza kandanda na vijana wenzao wa Kiafrika katika vilabu vya Tanga. Hili
lilikuwa jambo geni na lisilokuwa la kawaida kutoka kwa familia ya Kiasia
wakati wa ukoloni. Patwa alisaidia harakati za kudai uhuru kwa hali na mali, na
akaifanyia kampeni TANU miongoni mwa jamii yake mwenyewe ya Kiasia. Wakati wa
harakati Nyerere alikuwa akifanyiana maskhara na Patwa akimwambia, ‘’Mzee Patwa baada ya
kupata uhuru nadhani tukuteuwe uwe balozi wetu India.’’ Lakini Patwa hakuiona
Tanganyika huru, alifariki kabla ya uhuru kupatikana.
Baada
ya kufungua tawi la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius
Nyerere, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando kufanya ziara Tanga.
Nyerere alifikia nyumbani kwa Hamisi Heri. Ujumbe huu kutoka makao makuu ya
TANU ulipata makaribisho makubwa yaliyoandaliwa na vyama vya lelemama ambavyo
kwa kawaida vilikuwa vingi sana katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka
Mombasa nchini Kenya hadi Mikindani, Tanganyika. Kiongozi wa akina mama hawa
mjini Tanga aliyesaidia kuieneza TANU alikuwa Bibi Mwanamwema bint Sultan,
ndugu wa mbali wa mwenyekiti wa TANU Tanga, Hamisi Heri.
Matokeo
ya ziara ya Nyerere Tanga ilikuwa ni kumrudisha Mwalimu Kihere katika siasa.
Baada ya kushindwa kupata nafasi yoyote katika chama, Mwalimu Kihere alipoteza
shauku ya siasa. Nyerere alipokuja Tanga kuifanyia kampeni TANU ndipo Mwalimu
Kihere alikaribishwa kujiunga na chama. Mwalimu Kihere alifahamiana na Nyerere
mwaka 1946 walipokutana Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka wa African
Association. Nyerere alipozuru Tanga Mwalimu Kihere alitaka kufanya dhifa
nyumbani kwake kwa heshima yake. Uongozi wa TANU, hususan Hamisi Heri na Mzee
Makoko walikataa kumruhusu Nyerere kuhudhuria dhifa hiyo kwa sababu Mwalimu
Kihere alikuwa hajaonesha nia ya kuiunga mkono TANU. Nyerere akitambua utu
uzima wa Mwalimu Kihere, uzoefu na sifa yake ya uongozi katika African
Association, alishauri uongozi wa TANU Tanga usiache fursa ile ipite bure.
Nyerere alitoa hoja kuwa, ilikuwa muhimu kukubali mwaliko wa Mwalimu Kihere na
kutumia fursa hiyo kumuomba arudi kwenye harakati kwa kuwa TANU ingefaidika
kutokana na uzoefu wake alioupata katika African Association. Kwa ajili ya
nasaa hiyo TANU ilikubali mwaliko wa Mwalimu Kihere na Nyerere alihudhuria
dhifa ile nyumbani kwa Mwalimu Kihere pamoja na wanachama wengine.
Mwalimu
Kihere alikuwa mwanasiasa wa msimamo wa wastani, alikuwa mbali na msimamo mkali
dhidi ya serikali. Kwa ajili hii Mwalimu Kihere alielewana vizuri na utawala wa
kikoloni. Hii ilikuwa kinyume kabisa na wazalendo wengine kama Mzee Makoko
Rashid ambaye kwa miaka mingi alijulikana kwa chuki yake dhidi ya Waingereza.
Inasadikiwa kwamba watu wawili wataingia katika historia kwa chuki zao mahsusi
dhidi ya Waingereza, mtu wa kwanza ni Abdillah Schneider Plantan na wa pili ni
Mzee Makoko Rashid. Wote wawili walifungwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao
dhidi ya serikali ya kikoloni. PC na DC wake wote wawili walikukubali mwaliko
wa Mwalimu Kihere. Mwalimu Kihere alimtambulisha Nyerere kwa wageni mashuhuri na
alimuomba azungumze maneno machache. Nyerere kwa kipaji chake cha ufasaha wa
kuzungumza alitoa hotuba kuhusu lengo la TANU na kanuni za kidemokrasia kama
zilivyoelezwa na Umoja wa Mataifa. P.C. alisimama baada ya Nyerere kuzungumza
na akatoa hotuba kwa niaba ya serikali. P.C. alimsifu Nyerere kuwa ni
mwanasiasa mzuri kinyume na vile alivyosikia kabla ya kukutana naye. Hapo hapo
alitoa ruhusa kwa Nyerere na TANU kufanya mikutano ya hadhara katika wilaya
zote za jimbo hilo. Lakini uhusiano huu haukudumu, serkali iliyapiga marufuku
matawi kadhaa ya TANU Tanga mara tu baada ya kuundwa kwa United Tanganyika
Party (UTP).
Siku
iliyofuata mabingwa wa hotuba wa TANU, Julius Nyerere na Bibi Titi Mohamed
walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua
kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni pale Tanga. Ilikuwa muda mrefu umepita tangu zile siku za
zile siasa za wasomi katika Discussion Group, kikundi cha majadiliano; na ile
mizozo baina yao na ule uongozi uliokuwa katika TAA. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Tanga badala ya Hamisi Heri na Amos
Kissenge alichaguliwa katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama waasisi
wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya
TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga. Haukupita muda mrerfu mpangaji mikakati mzuri
Peter Mhando akahamishiwa Makao Makuu ya TANU Dar es Salaam na kutoka hapo
alipelekwa Tabora ambako kulikuwa na matatizo.
Tabora
TANU ilichelewa kuundwa na mara tu chama kilipoundwa kukazuka ugomvi baina ya
ofisi ya wilaya na ile ya jimbo. Ilipoingia mwaka 1956, matawi ya TANU yalikuwa
yamefunguliwa katika wilaya zote nane za Tabora kwa nguvu za uongozi wa wilaya.
Mwaka 1957 malalamiko yaliyokuwa yakitoka ofisi ya wilaya mjini Tabora
iliyokuwa chini ya uongozi wa Wamanyema ilikuwa kwamba ofisi ya jimbo chini ya
Germano Pacha haikuwa imara kwa hiyo ulitaka uchaguzi ufanywe ili kuchagua
katibu na mwenyekiti mpya wa jimbo na kumng’oa Pacha toka kwenye uongozi.
Katika jimbo pale Tabora mjini TANU kwa hakika haikuwa na ofisi yake yenyewe na
hii iliathiri sana utendaji kazi wa Pacha. Ijapokuwa kulikuwa na ukweli kidogo
katika zile tuhuma, Pacha aliyachukulia matokeo yote haya mapya kama ni
kisingizio na juhudi za makusudi za kumtoa yeye madarakani.
Mzee
Fundi Mhindi, mwanasiasa mkongwe na mwanachama muasisi wa African Association
mwaka 1945 na mmoja wa waasisi wa TANU mwaka wa 1955 katika Jimbo la Magharibi
na sasa akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU Tabora, alitumwa kwenda
makao makuu ya TANU Dar es Salaam kujadili tatizo la uchaguzi katika Jimbo la
Magharibi. Mzee Fundi Mhindi alifanya
majadiliano na Julius Nyerere na John Rupia. Makao makuu ya TANU yaliamua
kumtuma Peter Mhando kwenda Tabora kufanya uchunguzi na kuandika taarifa ambayo
ingetoa msingi wa ufumbuzi wa kudumu kuhusu matatizo yanayoisibu TANU pale
Tabora. Wakati ule Peter Mhando alikuwa kijana wa kiasi cha miaka ishirini hivi.
Peter Mhando aliifanya kazi ile akishirikiana na vijana wengine kama Bilal Rehani
Waikela, Ramadhani Abdallah Singo, Abdallah Saidi Kassongo na vijana wengineo. Peter
Mhando alikamilisha taarifa ya mgogoro wa TANU Jimbo la Magharibi na kuituma
makao makuu. Makuu makuu ya TANU ilichukua hatua kutokana na ile taarifa ya
Mhando na kumpeleka Said Ali Maswaya Tabora kutoka Shinyanga kuwa katibu wa
mkoa badala ya Pacha. Katika taarifa yake kwa makao makuu ya TANU, Peter Mhando
alipendekeza kuwa mkutano mkuu wa mwaka wa 1958 wa TANU uliokuwa unakaribia,
ufanyike Tabora ili kukipa chama nguvu zaidi katika Jimbo la Magharibi. Hivi ndivyo
Tabora ilivyokuja kuandaa na kuwa mwenyeji wa ule mkutano muhimu wa TANU
uliojadili kura tatu. Hii ilikuwa ndiyo kazi ya mwisho ya Mhando kuifanyia TANU
kwani alifariki kwa ugonjwa wa kisukari mara tu baada ya kutayarisha na kutuma
taarifa yake makao makuu ya TANU.
No comments:
Post a Comment