Monday, 23 April 2018

SHEIKH YAHYA HUSSEIN SEHEMU YA PILI NA ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA

Shajara ya Mwana Mzizima
Sheikh Yahya Hussein
‘Mjawiid,’ Mnajimu, Tabibu na Mtabiri Bingwa
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Raia Mwema
23 - 24 April 2018



Sheikh Yahya Hussein na King Hussen wa Jordan,  Amaan 1950s

JUMA lilopita kwenye safu hii ya Shajara ya Mwana Mzizima, tulimwangazia hayati Sheikh Yahya Hussein, aliyefariki dunia miaka kama 7 iliyopita na tuliona misukosuko aliyoipitia maishani mwake mpaka hatimaye kuja kuweza kupata mialiko ya mazungumzo na watu mashuhuri duniani wakiwamo wafalme wa kule nchi za Mashiriki ya Kati na Mashariki ya Mbali— Middle and Far East. Ile ilikuwa ni sehemu ya kwanza; sasa endelea na sehemu ya pili…

Mzee Juma Hussein Juma Karanda, ni babake mkuu Sheikh Yahya Hussein. Mzee Hussein, alipata elimu yake miongo mingi nyuma kutoka kwenye vyuo mbalimbali nchini Yemen; elimu ambayo aliitumia vizuri kwa kuwatoa ujingani vijana wengi sana wa Kitanzania wakati huo pale madrassani kwake Al- Hassnain Muslim School, Dar es Salaam.

Kitendo hicho cha kupigiwa mfano cha Mzee Hussein, kilisaidia sana kuziba pengo la kukosa elimu bora kwa wengi wa watu wa hapa Mzizima wakati ule wa utawala wa kidhalimu wa Kiingereza. Elimu ya Waingereza ilikuwa ikitolewa kwa upendeleo na ubaguzi mkubwa kwa watu wenye asili ya Kiafrika, ambao tuliwekwa kwenye daraja la nne baada ya Wazungu, Wahindi na Waarabu.

Madrassa ya Al Hassnain pale Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam, iliyomilikiwa na Sheikh Hussein na nduguye Sheikh Hassan, ilijitoa muhanga kwa kutoa elimu ya dini ya Kiislamu na ile ya Kidunia (sekula) kwa kiwango kikubwa sana, pengine kuzidi ile iliyokuwa ikitolewa na serikali ya kikoloni. Hili lilithibitika pale Sheikh Yahya alipojiunga na shule za serikali, kwani alikuwa akiwaacha kwa mbali wanafunzi wenzake kwenye matokeo ya kila siku darasani na mitihani ya mwisho pia.

Kwa hili la elimu, Mzee Hussein Juma –babake Sheikh Yahya - ameweza kutupatia majibu na kufuta usemi unaonezwa kwamba ‘jamii ya Kiislamu haipendi kusoma elimu dunia hata kidogo’. Ni uzushi ambao watu wamekuwa wakiuamini bila ushahidi kwa sababu umekuwa ukirejewarejewa mara kwa mara na kuzoeleka.

Msomaji, hebu fanya tafakuri ndogo tu; kwenye miaka hiyo ya 1920 na 1930, Sheikh Hussein Juma amewezaje kutoa watoto wake mwenyewe kama watatu hivi wakiwa wasomi wa hali ya juu; kama huko siyo kuthamini elimu tukuiteje?

Miongoni mwao yumo Professa Mansour Hussein Juma, msomi bobezi wa hisabati anayehadhiri kule Ibadan, Nigeria mpaka leo. Mwengine ni hayati Muhiddin Hussein, aliyekuwa Inspekta wa Jeshi la Polisi kabla uhuru. Inspekta ndio cheo cha juu kabisa alichoweza kushika mtu mweusi kwenye serikali ya kibaguzi ya Kikoloni. Muhiddin yeye alipata degree yake Makerere kabla ya uhuru.

Sheikh Yahya Hussein mwenyewe, mbali na unajimu na utabibu wake, naye pia tayari alishakuwa mwalimu; si wa madrassa peke yake, bali wa shule pia kwani kule Zanzibar amewahi kufundisha shule moja na Rais (mstaafu) Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Mtoto mwengine mkubwa wa Sheikh Hussein Juma ni Kanali (mstaafu) wa JWTZ Juma Hussein Karanda, ambaye alipata kuwa Mkuu wa Karakana ya Magari ya Kijeshi kule Tabora na Lugalo Barracks. Kwa sasa anaishi Kibaha, mkoani Pwani alikoweka makazi baada ya kulitumikia Jeshi muda mrefu.

Watoto wengine wa Sheikh Hussein Juma ni wale mabinti zake watatu Saphia, Zawadi na Husna ambao mwandishi huyu alisoma nao pale Shule ya Msingi Mnazi Mmoja na Uhuru Middle School hapa jijini kwenye miaka ya mwanzo ya 1960s.

Sheikh Hussein Juma, kwa kuchukia ile dharau ya kutawaliwa iliyosababisha wazawa wawe hawana haki yeyote; alijitosa kwenye kupigania uhuru wa nchi yetu ili tusiwe tena wanyonge, sisi na wanawe wale aliowaenzi na kuwapenda.

Alijiunga na chama cha United Tanganyika Party (UTP), ambacho kilikuwa hasimu mkubwa wa chama cha TANU kwa kutokubaliana kimaono na itikadi. Hussein Juma alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa UTP hapa nchini.

Habari zinasema, UTP kiliundwa kwa msaada mkubwa wa tajiri mmoja wa Kihindi kutoka kwenye mashamba ya Katani ya Tanga, kikiungwa mkono pia kwa karibu na Gavana Lord Twinning, ili kije kukipunguzia makali chama cha TANU; na kwa namna hiyo kiwe mbadala kwa wale wasiokubaliana na siasa za Nyerere kutoka Butiama.     

Sasa wakati babake akijiunga na UTP, Sheikh Yahya yeye, bila shaka kwa ushauri wa babake, akajiunga na chama kingine cha siasa kilichojulikana kama All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), kilichoongozwa na Shneider Plantan na Katibu wake akiwa Marijani Shaaban Marijan, aliyewahi kuwa Kocha wa Mpira wa Miguu wa Timu ya Taifa.

Vyama hivyo viwili, pamoja na kile cha African National Congress (ANC) cha hayati Mzee Zubeir Mtemvu (babake Abbas Mtemvu wa Temeke), vilitoa changamoto kubwa kwa chama cha TANU na hivyo kustawisha upinzani uliokuwapo wakati huo kwenye ulingo wa siasa hapa nchini.

Kuwa mwanachama wa UTP wakati ule, ilikuwa ni majanga makubwa kwa mtu yeyote yule. Umaarufu na upenzi kwa chama cha TANU ulikuwa juu sana kiasi cha yeyote yule anayejaribu kukipinga kuonekana kama ni msaliti anayestahili kutengwa na jamii ya watu weusi.

Kwa kukipinga kwake chama cha TANU, Sheikh Hussein Juma alipoteza heshima, hadhi, umaarufu na mambo kama hayo. Popote pale alipoonekana iwe barabarani, mazikoni au kwenye hafla yeyote alikuwa akizomewa na kutupiwa matusi hata na watoto wadogo tu alioweza kuwajukuu:

“Huyo! hilo! Sheikh Hussein Juma UTP huyoo!!!!” alizomewa Sheikh Hussein pamoja na Sheikh mwengine maarufu hapa jijini Sheikh Hashir wa kule Temeke ambao wote walikuwa wanachama wa UTP.

Masheikh hao waliokuwa wakiheshimika kwelikweli kwenye jamii ya Kiislamu kabla ya siasa za TANU wakawa maadui wakubwa wa jamii inayowazunguka; waliishia kuwa watu wa kukaa ndani tu pekee. Hawakuonekana tena misikitini, misibani au kwenye mijumuiko ya watu. Zuberi Mtemvu na Congress yake, yeye alikaza kamba akaendelea kama kawaida na hakutishwa na jambo lolote.

Uhuru ulipopatikana, watu hao watatu - Sheikh Hussein, Sheikh Takadir, Zubeir Mtemvu - kama vile walikuwa wamekufa, wakatengenezewa majeneza (effigies), yakazungushwa kwenye mitaa ya Dar es Salaam na baadaye yakachomwa moto kuashiria mwisho wao.

Madrassa ya Al - Hassnain, nayo ikafa polepole kwa vile watu walikuwa wakiwatoa watoto wao chuoni hapo mmoja mmoja na mwisho ikafunga milango yake kwa chuki za kisiasa. Wazee wale, pamoja na heshima walizokuwa nazo hapo mwanzoni, wakawa wanaiaga dunia hii kwa kihoro na unyonge, mmoja baada ya mwengine - Inna lillah Waina Illayhi Rajuun!

Sasa basi, wakati hayo tukiyaweka pembeni, hebu tumwangazie tena na kumkumbuka Sheikh Yahya Hussein, katika sifa yake nyengine kubwa ya ukarimu na kusaidia kwa wasiokuwa nacho. Kwa kawaida yao, masheikh wengi tumezoea kuwaona wakiwa wapokeaji na wala si watoaji wa sadaka; huyu hakuwa hivyo!

Wakati ule wa uhai wake, na pale anapokuwapo jijini Dar es Salam, marhum Sheikh Yahya hutoka asubuhi na mapema pale nyumbani kwake Magomeni Mikumi na kufanya mazoezi ya kutembea mpaka Kariakoo akiwa ameongozana na kundi la jamaa na nduguze wa karibu.   

Safari yao hiyo huwachukua mpaka Seiyun Hotel, pale Msimbazi, Kariakoo, jirani kabisa na ile Madrassa ya kwao ya Al-Hassnain. Wakiingia hapo, kila mmoja huagiza chakula akitakacho kwa ajili ya kifungua kinywa.

Seiyun Hotel, ni hoteli maarufu sana jijini inayokaribia uwepo wake kwa zaidi ya miaka 70 au 80 hivi, ikisifika sana kwa kutengeneza maandazi mazuri na laini pamoja na michuzi ya kuku na mbuzi iliyopikika sawasawa.

Sasa, Sheikh Yahya anapofika na kundi lake, huwa anamlipia kila aliyemo mle hotelini bili yake ya chakula hata kama hakuja naye yeye, ile michuzi, vitafunio na chai. Chai ya Seiyun, nadhani inaweza kuingizwa ndani ya mashindano ya Zawadi za Guinness duniani na ikashika namba moja!

“Ah! Mwache tu kila mtu aende zake sisi tutalipa hiyo bili,” husikika Sheikh Yahya akiwaambia wenye hoteli wasichukue pesa kwa yeyote yule anayemaliza kula.

Wakati akiyafanya hayo hapo hotelini, mara zote anakuwa tayari asubuhi ile, ameshatoa sadaka nyingi nyingine kule nyumbani kwake kwa watu wengine waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake atoke na kuwapa ‘chochote kitu’ wakajikimu.

Basi huyo ndiye Sheikh Yahya; hakuwa Sheikh mpokeaji sadaka, bali mtoaji sadaka mara zote. Kama siku hiyo hakwenda Kariakoo basi hufika pale hoteli ya Shibam, Magomeni Mapipa na kufanya kama alivyofanya kule Seiyun, Kariakoo.

Tumwombe Mungu na sisi atupe uwezo wa kuyafanya hayo ili tulipwe malipo mema kesho mbele ya hesabu.

Jamil Hizam, ni Mtanzania mwengine aliyehamia Dubai kule Falme za Kiarabu. Alikuwa mchezaji mpira mashuhuri wa timu za Dar Young Africans na Cosmos ya Dar es Salaam pia kwenye miaka ya 70s kabla hajahamia Arabuni.

Wapenzi wake mpirani walimbatiza jina wakimwita ‘Dennis Law’ (mchezaji mpira wa zamani wa Timu ya taifa ya Uingereza), kwa umahiri wake wa kusakata ‘kabumbu’. Jamil ni mzungumzaji ‘barzani’ kwenye kijiwe chetu pale Kariakoo kila anapokuja Dar es Salaam.

Siku moja tulikuwa tunamzungumzia Sheikh Yahya na mikasa yake. Jamil akasema ngoja nikupeni kisa kimoja; kisa ambacho na mimi mwandishi naona nikisimulie kwa wasomaji wangu leo hii tucheke pamoja.

Jamil anasema:

“…Mwaka 1967 kulikuwa na mechi kati ya Yanga na Sunderland (sasa Simba) ambapo Sheikh Yahya alitabiri Abdulrahman Lukongo angefunga goli kwenye mechi hiyo.

“Mechi ilivyoendelea Abdulrahman Lukongo aligongana kichwa na beki wa Simba aitwaye Durban, katika kugombania mpira wa juu ambapo marehemu Lukongo akapasuka juu ya jicho ikabidi atolewe nje asiendelee tena na mchezo; Lukongo aligoma katukatu kutoka akapewa ‘handkerchief’ kushikilia kuzuia damu na akaendelea kucheza kusubiria utabiri utimie;

“hatimaye, ingawa Simba walishinda 2-1, hilo bao moja la Yanga alilifunga Lukongo ambaye hakukubali kutoka mpaka alipofunga goli alilotabiriwa na Sheikh Yahya …teh! …teh! …teh!”

Mambo ya Sheikh Yahya hayo, ilimradi ni mikasa na mazingatio.

Mkasa mwengine ulitokea kule Nairobi bungeni wakati wabunge wa Kenya walipochachamaa wakitaka Sheikh Yahya kutoka Tanzania afukuzwe arudi kwao, kwani alikuwa akiwanyonya Wakenya na kupata utajiri mkubwa.

Sheikh Yahya Hussein akimpa Rais Jomo Kenyatta zawadi
ya bakora ya kutembelea

Akiwa kule Nairobi, Sheikh Yahya, wateja wake wakubwa walikuwa watu matajiri wa kibiashara, wabunge, mawaziri, wakiwamo viongozi wakuu kama vile Mzee Jomo Kenyatta mwenyewe na familia yake na za nduguze. Alikuwamo pia Rais Daniel Arap Moi. Alikuwamo pia aliyekuwa Meya wa Jiji la Nairobi, Alderman Charles Rubia. 

Mjadala mkali ulizuka bungeni kwa ajili ya chuki tu na kuuchukia Utanzania wake. Kwenye fani ya utabiri alikuwapo mtu mwengine kutoka Kongo DRC alijulikana kama Dk. Ng’ombe, lakini hakuna mtu aliyepiga kelele zozote kama afukuzwe au vipi:

“…Mr. Speaker… hii mutu kutoka pande ya Tandhania ni vizuri akwende kwa nchi yake, yeye  ako na pesa mingi anapata hapa kwa nchi yetu tukufu ya Kenya na kufanya yeye kuwa tajiri kupindukia…

“Mr. Speaker… ni bora akwende kwao kule, maana wao natukana tukana Kenya yetu kila mara…”

hayo ni baadhi ya maneno ya wabunge wa Kenya na Kiswahili chao kibovu wakimlalamikia Sheikh Yahya.

Daniel Arap Moi, aliyekuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo y Ndani (Home Affairs Minister) na Kiongozi wa Serikali bungeni; ndiye aliyekuja kuumaliza mgogoro kwa kuufunga mjadala ule na kusema Sheikh hakuvunja sheria yoyote pale Kenya; na hivyo aachiwe aendelee na shughuli zake kama kawaida.

Sheikh alipanua zaidi shughuli zake kwa kuwa na ofisi sehemu mbalimbali hapa Afrika Mashariki na Kati na nyengine akafungua pale London, Uingereza ambako Wazungu walitokea kumkubali vizuri kutokana na uwezo wake wa kuzungumza lugha kwa ufasaha kama amesomea pale kwao Oxford na Cambridge!

Alamsiki! Tukutane wiki ijayo InshaAllah.
simu : 0715808864

1 comment:

walmirsablan said...

PokerStars Casino Launches In Maryland | jtmhub.com
The PokerStars Casino 광주 출장마사지 in Hanover, MD is located at 경산 출장마사지 2111 Seminole Way, the sportsbook 수원 출장샵 is located at 3111 Seminole Way, 인천광역 출장마사지 Poker 광주광역 출장마사지 Stars Casino: Poker Room.