‘’...hoja
unazo lakini tujaaliwe hakuna (Waislam wenye elimu). Hapa tujiulize kwa nini hakuna. Ikiwa hakuna
Waislam waliosoma jibu ni jepesi nalo ni kuwa Waislam tunabinywa kwenye elimu
na hili tumeshaieleza serikali toka 1980s...ndani ya barua ya Warsha kwa Waislam,
Wabunge na Serikali...mimi ndiye nilibeba upupu ule nikenda kuumwaga Karimjee Hall
siku hizo Bunge linakutana hapo. Upupu tuliudurufu Masjid Quba. Hela ya kununua
karatasi hatuna tulipokuwa njiani tunahangaika tukakutana na mtu baada ya
kumueleza shida yetu akatuchukua hadi ofisini kwake akatupa karatasi...’’
Haukupita
siku tukavamia Bunge Karimjee Hall baada ya Sala ya L’Asr kimya kimya tukitokea
upande wa Independence Avenue na upupu wetu, tukaanza kuumwaga katika magari
yaliyokuwa yameegeshwa nje.
Kisha
taratibu tukaingia ndani ya viwanja vya Bunge na kuendelea na kazi yetu.
Taratibu
na kimya kimya kama tulivyoingia ndivyo tulivyoondoka katika viwanja vya Karimjee Hall.
Ilikuwa siku ya Ijumaa.
Mjini katika misikiti yote inayoswaliwa Ijumaa waraka ule wa Warsha uligawiwa misikitini.
‘’Upupu,’’
ulikuwa unakwenda kwa Waislam Wote wa Tanzania, Wabunge na Serikali.
Katika waraka ule Warsha
walieleza kuwa ipo njama ya kuwabana viijana wa Kiiislam katika elimu na
takwimu zikaonyeshwa katika ule ‘’upupu,’’ kuwa Waislam wako wengi katika shule
za msingi lakini kuelekea sekondari idadi yao inapunguzwa kiasi ikifika Chuo Kikuu
Waislam idadi yao inakuwa haivuki asilimia 10.
Haya
yakiwa yanafanyika kwa miaka yote toka uhuru wa Tanganyika upatikane mwaka wa 1961.
Waraka huu wa Warsha ulimwagwa nchi nzima kwa wakati mmoja.
Waraka
huu ulisababisha mshtuko mkubwa ndani ya Bunge na katika Serikali lakini hakuna
aliyetaka ijulikane kuwa Waislam wametoa Waraka huo.
Nimepokea
kwa masikitiko taarifa ya msiba wa
Sheikh Yusuf Salum.
Ndugu
yetu marehemu Sheikh Yusuf Salum wakati ule miaka ya mwanzo 1980 akiwa kijana
mdogo kama tulivyokuwa sote alisaidia sana pale Masjid Quba katika utayarishaji
wa waraka huu.
Mwenzangu alimpa jina Sheikh Yusuf akimwita, ''Mass Support,'' lakini yeye mwenyewe hakujua kama kapewa lakabu hiyo.
Ikawa kila tunapomzungumza tukilitaja jina hilo na naamini Sheikh Yusuf kaondoka duniani halijui jina hili.
Mwenzangu alimpa jina Sheikh Yusuf akimwita, ''Mass Support,'' lakini yeye mwenyewe hakujua kama kapewa lakabu hiyo.
Ikawa kila tunapomzungumza tukilitaja jina hilo na naamini Sheikh Yusuf kaondoka duniani halijui jina hili.
Allah amghufirie dhambi zake na amuingize mahali pema peponi.
No comments:
Post a Comment