Monday 28 May 2018

Historia ya Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar-es Salaam - Sehemu ya Pili Na Alhaji Abdallah Tambaza


Shajara ya Mwana Mzizima:
Historia ya Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar-es Salaam
Sehemu ya Pili
Na Alhaji Abdallah Tambaza

JUMA lililopita katika safu hii, tulielezea historia ndefu ya eneo la Mnazi Mmoja la hapa jijini Dar es Salaam na matukio au mambo makubwa ya kukumbukwa yaliyokuwa, ama yakifanyika hapo kila wakati; kwa vipindi maalumu, au pale linapotokea tukio muhimu linalohitaji mjumuiko mkubwa wa watu viwanjani.

Kwa muktadha huo basi, tulielezea ile mikutano mikubwa iliyofanyika hapo kabla ya kupatikana uhuru wetu na baada yake; ambayo ilihutubiwa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake wa mwanzo wa TAA na TANU, aliokuwa nao katika mapambano ya kuikomboa nchi yetu hii adhimu ya Tanganyika kutoka kwa wakoloni Waingereza.

Tulipokea simu kadhaa za pongezi kutoka kwa wasomaji wetu ambao walitoa maombi maalumu ya kuendeleza simulizi za mahala pale kwa mara ya pili, kwani bado walikuwa hawajakatika kiu zao; sababu maeneo mengi ama tuliyaruka au kuyaacha kutokana na uhaba wa nafasi gazetini, ambayo haimpi mwandishi uwanda mpana kucheza nao.

Mwisho wa makala ile tulielezea kwa kifupi namna Mwalimu na wenzake serikalini walivyokusudia kuifanya Mnazi Mmoja iwe ndiyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam (kwa maana ya City Center pale ulipopatikana uhuru), kwa kuzileta ofisi kuu na muhimu za Serikali kutoka kule mjini na kuzijenga upya kwenye eneo hilo.

Mpango ule ulishindikana kutekelezwa kutokana na wakazi wengi wa eneo lile kutoridhika kuhamishiwa maeneo mengine, pamoja na kuwapo kwa ushawishi na kampeni iliyofanywa na Mwalimu Nyerere mwenyewe.

Mwanahistoria maarufu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Sheikh Mohammed Said, alipozungumza nami hivi karibuni alinihadithia kwamba katika kutilia mkazo jambo lile, kuna watu ilibidi Mwalimu awaandikie barua yeye binafsi kutokana na kuwaheshimu na uzito wao katika jamii.
Mmoja kati ya hao ni Bi Mruguru bint Mussa wa Mtaa wa Kipata, Gerezani, ambaye ni mama wa wanasiasa mashuhuri wa harakati za kudai uhuru, akina Abbas, Ali na Abdulwahid Sykes. Mohammed anasema:

“…Nimehadithiwa na Balozi Abbas Sykes kwamba katika kadhia ile, Mwalimu alimwandikia mama yao barua binafsi kumtafadhalisha aridhie nyumba yake kuvunjwa na kupewa mbadala ili nchi ipige hatua kimaendeleo kwa kulijenga upya jiji letu… Bwana Abbas alisema: ‘unajua Nyerere akimuheshimu sana mama kwani alimchukulia kama ni mamake mzazi vile.’

“Bi Mluguru kutokana na mapenzi yake kwa Mwalimu, yeye alikubali kuvunjwa kwa nyumba yake.
Sasa tunapoliangalia eneo hilo leo, takriban miaka karibu 60 kupita, ingawa hakuna majumba ya kiserekali mahala hapo, lakini majengo yake si yale tena yalikuwapo kwenye miaka ile ya 1960s; kwani sasa nyumba zote karibu ni za ghorofa tupu zilizojengwa na wafanyabiashara; ama kwa kuzinunua za zamani au kwa kufanya ‘ubia’ na wenye mali.

Jirani na ile Hospitali ya Mnazi Mmoja, ambayo kwa sasa imeboreshwa kwa kuwa na wodi mpaka za wazazi kujifungulia, huduma za macho na meno, wakiwamo pia hata na Madaktari Bingwa (zamani ni Mabwana Mganga tu wa kufunga vidonda na kutoa dawa za kikohozi na mafua); kunapatikanwa jengo mashuhuri la Arnautoglo.

Likijulikana kama Holi la Arnautoglo, mahala hapo palikuwa sehemu muhimu sana iliyokuwa ikitumika kwa kufanyia mikutano ya ndani ya kila aina, ikiwamo ile ya siasa na ya kijamii, vikao muhimu na mambo ya namna hiyo.

Holi hilo pia lilitumika kwa shughuli za harusi, michezo ya kuigiza, michezo ya masumbwi (boxing), na miziki ya dansi kila wakati ikishirikisha bendi mashuhuri za wakati huo za Kilwa Jazz (Dar es Salaam), Moro Jazz (Morogoro), Kiko Kids (Tabora) na Dar Jazz (Dar es Salaam).

Vikundi vya Muziki wa Taarab asilia, ambayo hupigiwa watu wakiwa wamekaa kwenye viti; na si kuruka na kucheza na chupa ya bia mkononi, pia vilikuwa vikiutumia ukumbi huo kwa shughuli zake. Wakati huo vikundi mashuhuri kabisa vilikuwa ni Egyptian Musical Club, Alwatan Musical Club na ile ya Bombay Musical Club, iliyokuwa maeneo ya Kisutu karibu na Makaburi ya Kisutu kabla hakujavunjwa na kujengwa vile vyuo vya Biashara na kile cha Ufundi.

Kwa siku za Jumamosi na Jumapili, vijana wadogo wengi waliokuwa wakisoma shule za sekondari kwenye miaka ile ya mwanzo ya uhuru (1960s), ilikuwa ni zamu yao kuja kucheza ‘’Buggie’’ muziki wa Kizungu, hasa ule wa Kimarekani uliojulikana kama Soul, Jazz na Blues. Wakati huo bendi za vijana wadogo zikipiga nyimbo za kina James Brown, Ottis Redding, Aretha Franklin, Percy Sledge, Ray Charles na Babu BB King.

Mzee Mustafa Songamebele alivyo hivi sasa

Hali hii haikumfurahisha hata kidogo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dar es Salaam wakati huo, Mzee Mustapha Songambele. Haraka haraka, Mzee Songambele akatoa tamko kwa Vyombo vya Habari kwamba Serikali ya Tanganyika imepiga marufuku muziki wa Soul kupigwa kwenye kumbi za starehe na redioni. Tangazo lile lilishitua sana, kwani muziki na uja uzito ni vitu viwili tofauti; na kwamba ule muziki ilikuwa ni sehemu ya utamadauni (culture) wa Wamerekani. 

Bila shaka yeyote, kuitangazia Dunia kwamba Tanganyika imepiga marufuku nchini mwake kupigwa muziki wa Kimarekani, lilikuwa ni tukio baya kidiplomasia, hasa kwa nchi changa kama yetu wakati ule. Haikupita hata wiki moja, likatoka tangazo jengine kwamba ‘ni ruhsa’ sasa kupiga muziki ule nchini bila matatizo. Vijana wakashangilia kwelikweli, kwani ndio waliokuwa wapenzi wakubwa wa muziki huo kama ambavyo labda leo ukataze muziki wa kizazi kipya wa kina Diamond, Ali Kiba, Dully Sykes, sijui Q-Chief na labda Lady JD—utachokoza nyuki wakuume bure!   

Kwa wakati ule wa ukoloni, mtu mweusi hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda kufanya starehe zaidi ya hapo Arnautoglo na Ukumbi wa Amana pale Ilala, wakati huo ukijulikana kama ‘Kwa Ramadhani Minshehe’. Huyu Ramadhani Minshehe ndiye aliyekuwa baba mzazi wa mwanasiasa mashuhuri na kada wa Chama Cha Mapinduzi hapa nchini hayati Ditopile Mzuzuri.

Katika wakati huo mgumu, Mzee Minshehe alikuwa ni mmoja wa wazalendo waliokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha hapa jijini, kwani pamoja na jumba hilo, pia alimiliki mashamba na majumba mengi kule maeneo ya Ilala yaliyokuwa yakimwingizia kipato si haba.

Sehemu nyingine za burudani kwenye mahoteli yale kule mjini, mtu mweusi hakuruhusiwa kuingia humo na kuchanganyika na mabwana wakubwa. Iwe kwenye vilabu vya starehe au mahotelini, utakaribishwa na maandishi mazito milangoni yanayosomeka, tena kwa Kingereza, ‘Members Only’ au ‘Management Reserves the Right of Admission’. Hayo yalifanyika hapa; na huo ndio ukoloni maana yake.

Ni ubaguzi; ubaguzi mtupu kila mahala na kutuona mtu mweusi ni kinyaa! Sasa sijui wale ndugu zangu wanaojiita wao ni Liverpool; sisi Manchester, Arsenal, Chelsea… watasemaje Wazungu wale wakikasirika kunasibishwa na wewe pia kwenye club yao! Ingeeleweka kama pengine mtu angesema anapenda tu namna Manchester inavyocheza, lakini anadiriki kusema “sisi (Chelsea si wa kuchezea) tuna mtoto mpya huyo balaa, lazima tukufungeni tu!” Duh! Tafadhalini tupunguze hiyo. ‘Mazungu yale ni mabaguzi’ wala hayashituki kupendwa na sisi.

Jumba la Arnautoglo pia limekuwa ndio mahala kwa kina mama wakati huo wa zamani za kale kwenda kujifunza kazi za mikono kama ushonaji nguo, ufumaji vitambaa na kazi za nyumbani kama mapishi (wenyewe wakiita domestiki).

Masomo ya Watu Wazima pia yalikuwa yakitolewa hapo kwa wale walioikosa elimu hiyo utotoni, na hivyo ikawa mkombozi mkubwa kwa wale waliotaka kuondoka kwenye ujinga kwa kujua kusoma na kuandika. Kwa sasa, jengo la Arnautoglo limesheheni ofisi mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya na Jiji la Dar es Salaam.

Jamiatul Islamiya ni madrassa kubwa yenye jengo la gorofa moja  iliyojengwa kwa nguvu za wakazi wa jijini hapa chini ya uongozi wa hayati Mzee Kliest Sykes. Taasisi hiyo kongwe ambayo haipo tena sasa, ilianzishwa baada ya Waafrika chini ya Mzee Sykes tena, kuanzisha African Association ili kuja kuziba mapengo makubwa yalikuwamo katika upatikanaji wa elimu miongoni mwa wazalendo wa Kiafrika.

Wakoloni waliwaachia Wamissionari jukumu kubwa la kutoa elimu na hivyo watu wengi wa dini ya Kiislamu wakawa na woga kwamba watoto wao wangebatizwa na kubadilishwa dini kirahisi.

Jamiatul Islamiya, iliyohamiya mjengoni hapo mwaka 1935, ilifanya kazi kubwa kusomesha vijana wa kike na wa kiume elimu zote mbili, kwa maana ya  Sekula na ya Kiislamu, ni mahala ambapo watoto wengi jijini walipitia kupata manufaa yake. Ilikuwa ni mahala hapo ambapo watu mashuhuri walisoma kama vile akina Abdulwahid Sykes na nduguze, baba mzazi wa mwandishi huyu hayat Mzee Mohammed Tambaza, Imam Mkuu wa Masjid Mwinyikheri Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua na nduguze, hayati Mzee Zubeir Mtemvu na nduguze pamoja na wazee wengi ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki.

Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika Muslim School

Jengo lile, ni kielelezo tosha kwamba watu wanapoungana na kuazimia kufanya lao basi Mungu hubariki jambo hilo na bila shaka mafanikio hupatikana. Linaweza likaonekana ni la kimasikini kwa dunia ya leo, lakini ukichukulia mazingira ya ukoloni na hali dhalili za watu wake wa Kiafrika haikuwa kazi ndogo kusimamisha mjengo pale.

“Wazazi wa Kiislamu waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe … Aljamiatul Islamiya ilienda nyumba kwa nyumba ikikusanya michango kutoka kwa Waislamu …

“Kwa bahati nzuri mnamo mwaka 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu ujenzi wa shule ile. Alitoa fedha na shule ikajengwa jirani kabisa na mahala ilipokuwa African Association kwenye Barabara ya New Street (sasa Lumumba).

“Hii ni moja ya shule za mwanzo kabisa kujengwa na Waislamu wa Tanganyika wakati huo wa …ni moja ya mifano hai ya kuonyesha juhudi za Waislamu wa Tanganyika katika kujiletea maendeleo wenyewe…,”anaandika Mohammed Said katika kitabu chake cha Maisha na Nyakati za Abdul Wahid Sykes, ukurasa 45.

Balozi Abbas Sykes, ni mmoja katika wale mashujaa wa mwanzo kabisa walioitoa TAA ilipo na kuifanya iwe TANU mwaka 1954, kwa kuipa meno kuja kupambana na Mwingereza kudai nchi yetu. Ndiye mtu aliyeshika wadhifa wa kuwa Mkuu wa Jimbo la Pwani (PC siku hizo) ikiwamo na mji wa Dar es Salaam na Mzizima yake, akichukua madaraka kutoka kwa PC (Provincial Commissioner) Mzungu.

Abbas Sykes katika miaka ya 1950/60

Wakati huo Balozi Sykes akiwa PC, alifanikiwa kumwoa mmoja wa wanawake warembo kabisa (celebrity) jijini na mtangazaji maarufu na mahiri wa redio; mwenye sauti nyororo na ya kuvutia wa Idhaa ya Kiingereza ya Sauti ya Tanganyika, Tahia Abdulwahaab.

Akiwa bado kijana mdogo na mbichi kama alivyo Mheshimiwa Makonda sasa hivi, utawala wake jimboni ulivuma kweli kweli Pwani nzima; kwani alikuwa mtu asiyetaka masikhara hata kidogo kwa raia na watendaji.

Spidi yake ilikuwa kali kwelikweli, na hivyo Kamishna Sykes hakudumu sana katika wadhifa ule, kwani alibadilishiwa kazi na kupelekwa kuwa balozi kwenye nchi kadhaa duniani.

Miongoni mwa nchi hizo alikopita kwenye safari yake ndefu, ni pamoja na Paris, Ufaransa, Montreal Canada, United Nations, New York na Khartoum, Sudan. Akiwa kule Ufaransa aliwakilisha nchi pia kwenye Shirika la UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni), kama Mwakilishi Mkazi.

Balozi Sykes, amestaafu kazi miaka mingi na sasa amepumzika tu nyumbani kwake pale Sea View. Alamsiki! Tukutane juma lijalo InshaAllah.
Simu: 0715 808 864
atambaza@yahoo.com

No comments: