MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI RUYAGWA ZITTO, MB KWENYE
MAKADIRIO YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
''Hatuwashi tena mwenge na kuuweka mlimani Kilimanjaro, hatumuliki tena nje ya mipaka yetu, hatuleti tena matumaini pale pasipo na matumaini, hatupeleki tena upendo kule kuliko na chuki, na hatuleti heshima pale palipojaa dharau. Sisi si Tanzania ya Mwalimu Nyerere, sisi sasa ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya, Taifa lililokiuka misingi yake, Taifa linalowaacha Wapelestina wakiuawa kinyama, na sasa linalosapoti waonevu.''
1. Sisi si Tanzania ya Nyerere,
Ni Tanzania Mpya, Tanzania Mbaya - Inayokalia Kimya Mauaji ya Kinyama ya
Wapalestina, na Kusapoti Waonevu.
[Sehemu ya Kwanza na ya Hotuba ya
ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]
Mheshimiwa Spika,
Msimamo wa Tanzania kuhusu
mgogoro wa Israel na Palestine unaelezwa vizuri sana na nukuu hii ya Mwalimu
Nyerere aliyoitoa Mwaka 1967 na ndio umekuwa Msingi wa Sera yetu ya Mambo ya
Nje kwa miaka mingi kabla ya utawala wa sasa wa CCM mpya:
“[......]
Tanzania’s position. We recognize Israel and wish to be friendly with her as
well as with the Arab nations. But we cannot condone aggression on any pretext,
nor accept victory in war as a justification for the exploitation of other
lands, or government over other peoples.”
Kwamba Tanzania inaitambua Israel
na inapenda kuwa na urafiki nayo pamoja na urafiki na mataifa mengine ya
kiarabu. Lakini hatuwezi kukalia kimya uvamizi kwa namna yeyote ile. Pia
ushindi vitani hauhalalishi unyonyaji dhidi ya ardhi ya wengine au dhidi ya
Serikali za watu wengine. Msingi huu unaendana kabisa na dhamira ya sasa ya Sera ya Mambo nje. Hata hivyo hali
ni tofauti kabisa. Mambo tunayoyafanya kwenye sera yetu ya Mambo ya Nje
yanamfanya Mwalimu Nyerere ageuke huko kaburini kwake. Nitaeleza kwa mifano.
Mheshimiwa Spika,
Oktoba 26, 2016 kulikuwa na kikao
cha wajumbe wa Nchi 21 zinazounda ‘Kamati ya Urithi wa Dunia’ ya UNESCO -
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, kupiga kura ya
kupitisha makubaliano ya kuridhia kuupa hadhi ya Urithi wa Dunia Mji wa
Jerusalem pamoja na moja ya majengo ya mji huo (Temple Mount), na
kufungamanishwa na uasili wake na si hali ya sasa inayotokana na uvamizi wa
Israel juu ya eneo hilo la lililoko Jerusalem Mashariki (lililovamiwa mwaka
1967 na mpaka leo kutambuliwa na UN kama eneo la Palestina, ambao wanauona ndio
Mji Mkuu wa nchi ya Palestina iwapo makubaliano ya ’Two States Solution’
yatafikiwa).
Tanzania ilikuwa ni mjumbe wa
Kamati hiyo ya nchi 21, na kwa mshangao wa wengi duniani, ilipiga kura kuzuia
Azimio hilo, na kutaka azimio ‘Laini’ zaidi kwa Israel. Nchi marafiki zetu wa
asili kule Umoja wa Mataifa (UN) ambazo nazo ni wajumbe wa kamati ile, kama
Cuba, Vietnam na Angola zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo, zikitushangaa
mno kwa utetezi wetu kwa Israel ambao haukutarajiwa, hasa ikiwa msimamo wetu
kama nchi siku zote umekuwa ni kutambua Jerusalem Mashariki kama eneo la
Wapalestina ili kupata muafaka wa nchi mbili.
Sisi ACT Wazalendo tulihoji juu
ya jambo hili linalokwenda kinyume na Sera ya Nje ya Nchi yetu. Msimamo wa
Tanzania ni kukubaliana na UN kupinga uvamizi wa eneo hilo uliofanywa na
Israel. Serikali ilitoa majibu mepesi tu, tena pembeni, kuwa upigaji kura ule
haukuwa msimamo rasmi wa nchi yetu, ni ukiukwaji wa sera yetu ya mambo ya nje,
na kuwa ni jambo ambalo Afisa wetu kwenye mkutano ule wa UNESCO alilifanya kwa
makosa, na hivyo hatua zingechukuliwa dhidi yake.
Ni dhahiri majibu hayo yalikuwa
ni ghiliba tu, matukio ya karibuni yameonyesha kwa uwazi sura mpya ya Taifa
letu, pamoja na msimamo mpya wa Sera yetu ya mambo ya nje. Kwenye Diplomasia
matendo ya nchi huwa na maana zaidi kuliko maneno ya wanadiplomasia wake.
Matendo yetu yafuatayo ya karibuni yameonyesha kuwa Tanzania hatuisapoti tena
Palestina:
1. Baada ya kuwaangusha
Wapalestina kule Paris kwenye Mkutano wa UNESCO, Serikali iliahidi kuwa
ingemchukulia hatua Afisa yule wa Wizara ya Mambo ya Nje aliyekwenda kinyume na
Sera yetu ya Mambo ya Nje, hatujafanya hilo, zaidi tumempandisha cheo na
kumteua kuwa Balozi wetu wa Ankara, Uturuki. Jambo hilo linaonyesha kuwa
tulimtuma Balozi Elizabeth Kiondo apige kura namna ile kule UNESCO, na sasa
tumempa cheo zaidi kwa kazi njema aliyoifanya. Jambo hili linaonyesha kuwa kwa
sasa tunawaunga mkono Waisrael, na hatuko tena na Wapalestina.
2. Kwa sasa tumeamua kufungua
ubalozi wetu Israel, Tel Aviv, kuongeza uchungu kwenye Kidonda, tukachagua
wakati huu wa maazimisho ya miaka 70 ya Uvamizi wa Israel katika ardhi ya Taifa
la Palestina kuzindua ubalozi wetu huo. Jambo hili linafanyika kukiwa na tuhuma
kuwa hata huo Ubalozi unagharamiwa na Israel yenyewe, ndio maana tumepangiwa
hata kipindi cha kuufungua. Kidiplomasia kuufungua ubalozi wetu katika wakati
huu ni kuazimisha uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina. Maana tulikuwa
na uwezo wa kuchagua wakati mwengine wowote kufanya uzinduzi wa ubalozi wetu,
lakini kwa kuwa aliyegharamia uwepo wa ubalozi huo (Israel) alitaka tuufungue
wakati huu wa maazimisho ya miaka 70 ya Uvamizi wa Israel kwa Palestina,
ilitubidi tufanye hivyo. Jambo hilo limeonyesha kuwa kwa sasa hatuungi mkono
tena utu (Palestina) bali tunamtumikia Kila mwenye kitu (Israel).
3. Wakati akiwa ziarani Israel,
Balozi Mahiga alifika sehemu ya miji inayokaliwa kimabavu na Israel ambayo
inapakana na Ukanda wa Gaza. Na baadaye alihojiwa na Televisheni ya Taifa ya
Israel, ambako alionyesha tu masikitiko yake kwa Waisrael wanaokaa maeneo hayo
kwa kusumbuliwa na mashambulizi ya Hamas. Lakini hakulaani kabisa uendelezaji
wa Israel kujenga makazi kwenye maeneo hayo ya uvamizi kama Wanadiplomasia
wengine wa nchi zenye msimamo wa ‘Two States Solution’ kama sisi wanavyofanya.
Balozi Mahiga mwanadiplomasia mzoefu na mbobezi, Kutokulaani kwake makazi yale
haramu ni jambo la makusudi kabisa, si bahati mbaya. Ni kitendo cha kutuma
salamu kwa Wapalestina kuwa tunaunga mkono uendelezaji makazi wa Israel katika
maeneo hayo iliyoyavamia.
4. Tanzania imetajwa na vituo
mbalimbali vya habari vya Kimataifa kuwa ni katika nchi 33 ambazo zilihudhuria
ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem, Mei 14, kilele cha maazimisho
ya miaka 70 tangu uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina. Chanzo cha
taarifa ya Tanzania kuhudhuria ni Serikali ya Israel, ikitaja nchi ilizozialika
na zilizohudhuria. Serikali yetu inasema inapinga uwepo wa Ubalozi wa Marekani
mjini Jerusalem, lakini hapo hapo inatajwa kuhudhuria uzinduzi huo. Picha
tunayoitoa hapa kwa Wapalestina ni kuwa tunaunga mkono jambo hili la ufunguzi
wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem.
5. Siku ya uzinduzi huo wa
ubalozi wa nchi ya Marekani mjini Jerusalem, Jeshi la Israel liliwaua kwa
risasi zaidi ya watu 54 wa Palestina, wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na
hata wanahabari. Nchi mbalimbali duniani zimelaani mauaji hayo. Nchi ya Afrika
ya Kusini imekwenda mbali zaidi kwa kumrudisha nyumbani Balozi wake aliyeko
Israel. Sisi Tanzania tulioikomboa Afrika Kusini tumekaa kimya, tumeshindwa
hata kutoa kauli ya kulaani mauaji hayo. Kuhudhuria kwetu ufunguzi wa ubalozi
na kukaa kimya juu ya mauaji hayo kunaonyesha tumewaacha rasmi Wapalestina.
Mambo hayo matano yanaonyesha
kuwa sisi si tena ile Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere, sisi kwa sasa ni
Tanzania Mpya (kama yasemavyo matangazo ya Ikulu yetu) - Tanzania mpya
inayosimama na Waonevu wa dunia, Wauaji na Wavunja haki za wanyonge. Sisi si
tena Tanzania ya kusimama na wanyonge, bali ni Tanzania ya kusimama na
Wanyongaji kwa sababu ya maslahi ya kiuchumi.
Si ile Tanzania iliyoongoza
Ukombozi wa Bara la Afrika kutoka kwenye makucha ya Ukoloni, bali ni Tanzania
Mpya inayounga mkono na kushabikia ukoloni na Uvamizi. Sisi si ile Tanzania
yenye msimamo mkali tuliyolipinga Taifa kubwa la Marekani dhidi ya Uvamizi wake
kwa wanyonge wa taifa la Vietnam, bali sasa ni Tanzania mpya ya kuunga mkono
Uvamizi wa Taifa onevu la Israel kule Palestina. Sisi si Tanzania ile
iliyoitetea China ipate nafasi na kiti chake stahili kule UNO, bali sasa sisi
ni Tanzania mpya inayowaacha watu wa Palestina bila utetezi wa hadhi, kiti na
nafasi yake stahili kule UNESCO.
Sisi si ile Tanzania huru tena ya
Mwalimu Nyerere, iliyowaheshimu watu na mataifa kwa sababu ya Utu wao na
kuamini kwamba binaadam wote ni sawa. Sasa sisi ni Tanzania mpya, inayowapa
heshima watu kwa sababu ya kitu inachotuhonga, tukiuza usuli wa Utaifa wetu kwa
maslahi machache ya kifedha au kiuchumi.
Hatuwashi tena mwenge na kuuweka
mlimani Kilimanjaro, hatumuliki tena nje ya mipaka yetu, hatuleti tena
matumaini pale pasipo na matumaini, hatupeleki tena upendo kule kuliko na
chuki, na hatuleti heshima pale palipojaa dharau. Sisi si Tanzania ya Mwalimu
Nyerere, sisi sasa ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya, Taifa lililokiuka misingi
yake, Taifa linalowaacha Wapelestina wakiuawa kinyama, na sasa linalosapoti
waonevu.
2. Kujengewa Uwanja wa Mpira na
Msikiti Visiifanye Tanzania Iikumbatie Morocco na Kuacha Kuiunga Mkono Sahara
Magharibi
[Sehemu ya Pili ya Hotuba ya
ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]
Mheshimiwa Spika
Bado niko kwenye Sera ya mambo ya
nje ya nchi yetu, si hii ya Tanzania mpya, bali ile Tanzania ya tangu wakati wa
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ya kusimama na wanyonge. Wakati tulipoamua
kufuata ‘Diplomasia ya Uchumi’ bado msingi wetu huu wa kusimama na wanyonge
ulibaki pale pale. Ndio maana wakati wa Rais Ben Mkapa na Jakaya Kikwete bado
tulibaki kuwa ni sauti ya mataifa yanayoonewa kama Cuba (tukipinga vikwazo vya
Marekani dhidi yao), Palestina na Sahara Magharibi.
Msingi huo wa kusimama na
wanyonge ni muhimu zaidi kwa chama chetu cha ACT Wazalendo, ndio maana
tulipinga ujio wa Mfalme wa Morocco hapa nchini Oktoba 23 - 25, 2016. Kwa kuwa
Taifa hilo bado linaikalia kimabavu ardhi ya wanyonge wa Sahara Magharibi. Ndio
msingi pia wa kutangaza wazi mahusiano yetu rasmi na Chama cha cha siasa na
ukombozi wa Taifa hilo cha Polisario kinachopigania Uhuru wa nchi ya Sahara
Magharibi.
Umoja wa Afrika (AU) uliamua
kukubali ombi la Morocco kurudi bila masharti kwenye jumuiya hiyo. Ikimbukwe
kuwa kwa zaidi ya miaka 33 Morocco haikuwa na mahusiano na jumuiya hiyo (tangu
OAU mpaka sasa AU) baada ya kujitoa kwa kupinga OAU kuitambua Sahara Magharibi
kama Taifa huru na kupewa kiti rasmi ndani ya OAU mwaka 1984.
Uamuzi wa OAU wa kuiruhusu Sahara
Magharibi Kuwa mwanachama wa Umoja huo ulitokana na hukumu ya Mahakama ya
Kimataifa ya Haki (International Court of Justice - ICJ) ya mwaka 1975
iliyopinga madai ya Morocco kuwa ina mahusiano ya kihistoria na kisheria na
Sahara Magharibi (na hivyo kuitawala kinguvu) na kutoa haki ya kujitawala kwa Taifa hilo.
Tunaheshimu maamuzi yale mkutano
wa AU wa Januari 2017, ulioirudisha Morocco kwenye AU. Lakini tabia za Taifa
hilo onevu bado hazijabadilika, ni muhimu tulieleze bunge masuala yafuatayo ili
liweke msimamo wake kwa Serikali juu ya kuminywa kwa watu wa Sahara Magharibi:
1. Kikao cha AU cha Januari 28 -
29, 2018 kiliazimia kuwa Morocco iruhusu Kamati Maalum ya Uangalizi ya AU iende
kwenye maeneo ya Sahara Magharibi ambayo inayakalia kimabavu ili kuja
kuijulisha AU hali ya mambo ilivyo.
2. Machi 29, 2018 Morocco
iliwajulisha UN juu ya kutoruhusu waangalizi wowote wa AU kwenda kwenye maeneo
yote ya Sahara Magharibi inayoyakalia.
3. Tangu mwaka 1991 Morocco
imetumia mbinu, hila, na uzandiki ili kuzuia Tume ya Umoja wa Mataifa kwaajili
ya Kura ya Maoni ya Uhuru wa Sahara Magharibi (MINURSO) kufanya kazi yake
kwenye maeneo inayoyakalia kimabavu ya Sahara Magharibi. Siku za karibuni,
Umoja wa Mataifa, UN ulipitisha azimio namba 2414 (2018) la kuongeza muda wa
mamlaka, uahai na madaraka ya (MINURSO) kwa miezi sita. Morocco imepinga jambo
hilo na kutishia kufanya mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo ya Sahara
Magharibi ambayo yameshakombolewa (Liberated Zones).
4. Bado Morocco inaendeleza
uvunjaji mkubwa wa haki za binaadam kwa watu wote wa Sahara Magharibi wanaodai
Uhuru wao.
5. Kurudishwa kwa Morocco kwenye
AU kulienda pamoja na Taifa hilo kuridhia ‘AU Constitutive Act’ inayoyataka
mataifa ya Afrika kuheshimu maazimio ya AU na hata yale ya UN yanatolewa kwa
ushirikiano na AU. Lakini kwa matendo yake tuliyoyaainisha hapo juu ni dhahiri
kuwa Morocco haitaki usuluhishi na Sahara Magharibi, bado inataka kuitawala na
kuikalia kimabavu, bado Morocco inataka kuendelea kuwa mkoloni. Ndio maana
imekataa hata kumpa ushirikiano msuluhishi wa mgogoro huu, ndugu Horst Köhler,
Rais wa zamani wa Ujerumani
6. Matendo ya Serikali yetu kwa
sasa yanaonyesha hatuna msimamo kwenye mambo ya msingi ya kidiplomasia, namna
tulivyoenenda kwenye mahusiano yetu na wanyonge wa Palestina ni mfano hai, sasa
tukijali vitu kuliko utu kama ilivyo zamani.
Hivyo basi, nataka kulishawishi
Bunge lako litoe muongozo kwa Serikali juu ya kuenenda kwenye hili jambo la
Morocco na Sahara Magharibi, ili kuzuia ahadi ya kujengewa Uwanja na Msikiti na
Serikali ya Morocco (Vitu) isitufanye tu waache ndugu zetu Wanyonge wa Sahara
Magharibi.
Nchi yetu ni kimbilio la Nchi ya
Sahara, Serikali yetu chini ya Mwalimu Nyerere ililitambua Taifa la Sahara
Magharibi tangu siku za mwanzo kabisa za harakati zao, ndio maana wanao Ubalozi
hapa nchini. Kumuenzi baba wa Taifa na kulinda misingi ya Taifa letu ni lazima
tusimame na watu wa Sahara Magharibi, na tusiwatupe kama tulivyofanya kwa watu
wa Palestina.
Naliomba Bunge liibane Serikali
ili itoe ahadi hiyo hapa Bungeni, pamoja na kuitaka Serikali kutumia ushawishi
wake kule AU na UN kuibana Morocco iruhusu kura ya maoni ya kuamua mustakabali
wa watu wa Sahara Magharibi kama ilivyoridhiwa kwenye Azimio la UN.
Viva Sahara Magharibi
Viva Polisario
Mungu Ibariki Afrika
3. Hakuna Diplomasia Bila
Wanadiplomasia: Tuna Uhaba Mkubwa wa Watumishi Kwenye Balozi Zetu
[Sehemu ya Tatu ya Hotuba ya
ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]
Mheshimiwa Spika
Msingi wa tano wa Sera ya Mambo
ya Nje ya Tanzania unatutaka tushirikiane kikamilifu na Nchi, Mashirika pamoja
na Taasisi mbalimbali katika nyanja za Diplomasia, Siasa, Uchumi, Utaalam na
Teknolojia. Wizara hii ina jukumu la kubuni na kusimami utekelezaji wa misingi
yote ya Sera yetu ya Mambo ya Nje.
Pia Wizara hii pia ina jukumu la
kusimamia na kuratibu mahusiano kati ya Tanzania na nchi pamoja na mashirika
mbalimbali. Utimizaji wa jambo hilo unafanyika kupitia balozi zetu
zilizotapakaa kwenye nchi mbalimbali ulimwenguni. Kwa sasa ufanisi wetu ni mkubwa
kwa sababu ya uhaba wa watumishi kwenye balozi zetu mbalimbali duniani.
Kwa wastani ukimuondoa Balozi,
kila kituo cha Ubalozi wetu nje ya nchi kinapaswa kuwa na Mhasibu, mtu wa TISS
na pamoja na Mwanadiplomasia (FSO). Vituo vingi vya balozi zetu havina kabisa
Maafisa wa Diplomasia (FSO’s). Wale wachache waliokuwepo awali walirudishwa
nchini kwa sababu mbalimbali (ikiwemo kumaliza muda wao wa utumishi Nje ya
Nchi). Tumerudisha watu bila kupeleka mbadala wao.
Kwenye balozi zetu mbalimbali
watendaji hasa wa kazi za Kibalozi na kidiplomasia ni hawa maafisa wa
Diplomasia (FSO’s). Sasa kwa uhaba huu tunawezaje kufanya Diplomasia ya nchi
yetu? Hiyo Diplomasia ya Uchumi tunafanyaje bila kuwa na hao Wanadiplomasia?
Nitatoa tu mfano wa balozi zetu
chache ulimwenguni. China, nchi ambayo ni mshirika wetu mkubwa kidiplomasia na
kiuchumi, hatuna kabisa FSO huko, labda ndio sababu mauzo yetu kwenda China
yameshuka mno, maana biashara ya nje ni Diplomasia, sasa wakati Spika unamtaka
ndugu yangu Mwijage asafiri, ni nani atakayemuandalia hiyo mikutano ya kupata
wawekezaji huko China kama hatuna FSO hata mmoja? Wenzetu Uganda wana FSO’s 8
huko China, Kenya na Sudan wao wanao 9 Kila mmoja.
Nchi nyengine ambayo hatuna
kabisa FSO ni Ethiopia - Makao Makuu ya AU, utaona tunavyodharau nafasi yetu
katika Afrika. Pia hatuna FSO Afrika Kusini, nchi rafiki na moja ya zenye
uchumi mkubwa Afrika, hatuna kabisa FSO Ujerumani - Nchi kubwa zaidi kiuchumi
katika Umoja wa Ulaya (EU). Hata India ambako tangu Bunge lianze wabunge tunalalamikia
kukosa soko la mbaazi kutoka huko nako hatuna FSO hata mmoja. Tumeufanya kuwa
ubalozi wa kupokea wagonjwa tu.
Nchi za Brics (ukiondoa China,
India na Afrika Kusini ambazo hatuna kabisa FSO’s) zilizobaki, Brazil na Urusi
tuna FSO mmoja mmoja tu. Hata DRC Congo - Nchi ambayo zaidi ya theluthi moja ya
mizigo ya Transit inayopita kwenye bandari ya Dar inatoka, nayo tuna FSO mmoja
tu tofauti na watatu ilivyozoeleka. Kenya - Nchi ya Afrika Mashariki
tunayofanya nayo biashara zaidi nayo ina FSO mmoja tu.
Hali iko hivyo karibu katika
balozi zetu nyingi ulimwenguni. FSO’s ndio maafisa hasa waliofundwa na kupikwa
kutekeleza Sera yetu ya mambo ya Nje. Foreign Service Officers (FSO’s) ndio
diplomats (wanadiplomasia wetu). Kama hawapo vituoni, na hatuwatumii maana yake
hatufanyi diplomasia, na kwa kuangalia mbali tunaua diplomasia yetu.
Mimi sitapitisha bajeti hii mpaka
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itakaponihakikishia kuwa
itapeleka Maafisa wa Diplomasia (FSO’s) katika vituo ambavyo hatuna kabisa na
pia kuwaongeza katika vile vituo ambavyo wako wachache.
Tunasimama na Iran na Qatar,
Uonevu Dhidi Yao Si Sawa - Tanzania Tusaidie Amani ya Ulimwengu.
Tunasimama na Iran na Qatar -
Uonevu Dhidi Yao Si Sawa. Tanzania Tusaidie Amani ya Ulimwengu.
[Sehemu ya Nne na ya Mwisho ya
Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]
Mheshimiwa Spika
Jambo la mwisho kwenye mchango
wangu ni juu ya hali ya ulinzi na usalama duniani. Usiku wa kuamkia Disemba 9,
2017, tulipoteza askari wetu 14 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa huko DRC
Congo, wakiwa kwenye Jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Mataifa. Nachukua nafasi
hii kuwaombea kwa Mola awalaze pema, pamoja na kutoa pole kwa familia zao na
kwa Jeshi zima la JWTZ.
Taifa letu linachangia pakubwa
katika kulinda amani ya ulimwengu, wanajeshi wetu wakaiwa karibu katika nchi
nane duniani. Naamini tunao wajibu kama Taifa kusaidia uwepo wa amani
Ulimwenguni ili kuzuia nchi zilizo kwenye machafuko kama DRC Congo kuongezeka
na askari wetu wa kulinda amani kupotea.
Tayari, katika siku za karibuni,
dunia imeshughudia maafa makubwa ya vita nchini Libya (ambako Rais Kikwete ni
msuluhishi), Iraq, Afghanistan, Somalia, Syria, Sudan Kusini na Yemen. Mwenendo
wa migogoro na uonevu unofanyika Qatar na unaotaka kufanyika Iran unapaswa
kukemewa mapema ili kuchochea amani ulimwenguni, hasa eneo la mashariki ya kati
ambalo tayari limeharibiwa na vita.
Hotuba ya Waziri ya Bajeti ya
Wizara hii kwa mwaka 2016/17 ilibeba pongezi kwa nchi za Iran, Marekani, China,
Urusi, UN na Umoja wa Ulaya (hasa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) kwa
makubaliano ya Nyuklia ya yaliyoiondolea vikwazo Iran kwa masharti ya kutoendeleza
urutubishaji wa nyuklia. Makubaliano yale ni muhimu kwa kuwa iliondoa hali ya
mashaka iliyokuwa imetanda duniani.
Tumeona Marekani imejitoa kwenye
makubaliano hayo, na kutishia kuweka vikwazo vipya kwa Iran. Huku wajumbe
wengine wa wakiendelea kubaki kwa kuwa bado Iran imeendelea kutekeleza
makubaliano husika, na kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki,
IAEA ni kuwa bado Iran inafuata masharti ya makubaliano husika.
Uamuzi huu wa Marekani si mzuri,
unarudisha hali ya mashaka kwenye eneo la mashariki ya kati, ni uonevu dhidi ya
Iran, hasa kwa kuwa IAEA imethibitisha kuwa Iran haina makosa. Ni maamuzi ya
uonevu tu na usiochochea amani, ni uamuzi unaopaswa kupingwa. Serikali yetu
iitumie nafasi yake kule UN kupinga uamuzi huu, na kuitaka Marekani kurudi
kwenye makubaliano haya ili kudumisha amani.
Pia Julai 26, 2017 Wizara hii
ilitoa taarifa yake juu ya mgogoro wa nchi za Ghuba (GCC), baada ya hatua ya
nchi nne za Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri kuiwekea vikwazo vya anga,
bahari na ardhini nchi ya Qatar. Msimamo wa Serikali ni kuunga mkono upatanishi
unaongozwa na Amir wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Jaber, tunaunga mkono msimamo
huo.
Lakini bado pia sisi ACT
Wazalendo tunasimamia tamko letu la kupinga uonevu dhidi ya Qatar tulilolitoa
July 24, 2017. Kwa karibu miezi 10 sasa watu wa Qatar wamewekewa vikwazo vya
kiuchumi na kiusafiri, kwenye anga, ardhi na bahari na nchi hizo nne jirani,
jambo hilo si sawa, hasa kwa kuwa masharti yaliyotolewa ili kuondoa vikwazo
hivyo yanaingilia uhuru wa nchi hiyo.
Tunaitaka Serikali yetu, pamoja
na kusapoti usuluhishi huu wa Kuwait, itumie nafasi yake pia kule UN
kuhakikisha inachangia usuluhishi wa jambo hili ili mashaka yaliyoko na vikwazo
kwa Qatar viondoshwe.
Ahsanteni kwa Kunisikiliza.
Naomba Kuwasilisha
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Bungeni Dodoma
Mei 23, 2018
No comments:
Post a Comment