Monday 21 May 2018

HISTORIA NDEFU YA MNAZI MMOJA DAR - ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA


Shajara ya Mwana Mzizima:
HISTORIA NDEFU YA MNAZI MMOJA DAR
Na Alhaji Abdallah Tambaza


ENEO la Mnazi Mmoja hapa jijini, lina historia ndefu pengine kama ilivyo historia ya jiji lenyewe la Dar es Salaam liloanza na Mzizima zaidi ya miaka 150 iliyopita.

Hakuna maelezo sahihi yaliyorekodiwa yanayoelezea hasa ni kwa vipi eneo hilo likaitwa Mnazi Mmoja; lakini itoshe tu kusema kwamba majina kama hayo hupewa maeneo, ama kwa kuwepo kwa mti kama huo mahala hapo huko nyuma; na baadaye, pengine kwa sababu yoyote ile, labda ukakatwa usiwepo tena, lakini jina likawa limebakia.

Aidha, jina hilo pia hutolewa kwa sababu ya harakati za mahala hapo kufanana na zile za ki-mnazi mmoja hivi—liko eneo linaitwa Mnazi Mmoja kule Unguja ambako pirikapirika zake zinalingana na hizi za hapa Dar es Salaam. 

Eneo la Mnazi Mmoja ya Dar es Salaam, kiasilia linaanzia mwanzo wa Barabara ya Lumumba (zamani New Street)/Morogoro Road na kuelekea mpaka mwisho wa Lumumba kule Gerezani; halafu ikutane na Bibi Titi Mohammed, na kuja hadi Morogoro Road tena. Mzunguko huo na vilivyomo ndani yake, hasa vile viwanja, ndio Mnazi Mmoja yenyewe.

Kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja pale barabara ya New Street siku hizo, mikutano mikubwa sana ya kihistoria ilifanyika ambayo ilikuja kubadili historia ya nchi ya Tanganyika wakati huo wa utawala dhalimu wa Serikali ya Malkia Elizabeth wa Ulaya Ingereza.

Iliyokuwa Ofisi ya African Association 1929, TANU 1954
na CCM 1977,New Street (Lumumba Avenue)

Mikutano hiyo ni pamoja na ule mashuhuri ulioitishwa na Chama cha TANU siku hizo kuja kuwaelezea wananchi kusudio la kumpeleka Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa (UNO), kwenda kulieleza baraza lile kwamba, ‘wakati umefika sasa Watanganyika wanataka uhuru wao ili wajitawale wenyewe’.

Julius Nyerere alienda  UNO na kurejea nchini Machi 19, 1955 na siku iliyofuata Jumapili, Machi 20,1955, TANU ilifanya mkutano mkubwa sana ambao unakisiwa ulihudhuriwa na watu wasiopungua 40,000 waliokuja kutoka pande zote za nchi hii kusikiliza matokeo ya safari ile ya kihistoria, iliyokuja kubadili kabisa taaswira na mtizamo wa Watanganyika kwa nchi yao.

“Mikutano ya mwanzo kabisa ya TANU ya siku za mwanzo ilifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Kwenye jukwaa kubwa lililojengwa kwa miti walikuwa wakikaa wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU, Bibi Titi Mohammed, John Rupia na Clement Mtamila,” anaandika Mohammed Said kwenye kitabu chake mashuhuri cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, ukurasa 191.

Kulia Sheikh Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman
Takadir, Julius Nyerere, Mnazi Mmoja, 1955

Mkutano mwengine mkubwa alioufanya Mwalimu Nyerere kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ni pamoja na ule aliouita kulielezea taifa kutoroka nchini kwa aliyekuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Oscar Salathiel Kambona. 

Waziri Oscar Kambona, alikimbilia Uingereza baada ya kukosana na Mwalimu Nyerere siku hizo kuhusiana na Azimio la Arusha, ambalo yeye aligoma kuwa muumini wake. Alipopata fununu za kwamba labda angetiwa mbaroni, akakimbilia Kenya na baadaye kuishia London, Uingereza kama mkimbizi wa kisiasa.     

Nyerere, katika mkutano huo, alimshambulia hadharani aliyepata kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Masuala ya Muungano, Abdallah Kassim Hanga, ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Oscar Kambona, na ambaye wakati huo alihusishwa na masuala ya uhaini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika mkutano huo, Hanga, ambaye aliletwa kutoka kizuizini Ukonga, alitukanwa na kufokewa kama mtoto mdogo mbele ya kadamnasi ya watu. Baada ya tukio hilo, Hanga hakuonekana tena na hajulikani mahala alipo mpaka leo hii. Kambona yeye alishambuliwa ‘ghaibu’ (hakuwepo alikuwa yuko London akila ‘bata’).

Mama yetu mpendwa Bibi Titi Mohammed, pia alifanya ule mkutano wake mashuhuri wa mwanzo kabisa uliomjenga kisiasa kwenye viwanja hivyo hivyo vya Mnazi Mmoja, pale alipoweza kuwahamasisha wanawake wenzake kujiunga kwa wingi kwenye harakati za ukombozi wa taifa hili. Huo ukawa ndio mwanzo wa safari ndefu ya kisiasa ya Bibi Titi Mohammed, ambaye jina lake lilivuma na kuvuka mipaka mpaka kwenye nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia na Malawi.

Viwanja hivyo pia, vilikuwa maarufu na mahsusi kwa shughuli za kidini hasa ya Kiislamu wakati huo, kwani ndipo mahala ambapo sherehe za Maulid ya Mfungo Sita (mazazi ya Mtume Muhammad SAW) kwa jiji la Dar es Salaam na Mzizima, zilipokuwa zikifanyika na kuhudhuriwa na Gavana mwenyewe.

Pia, sala za Eid zote zote mbili zilikuwa zikisaliwa viwanjani hapo huku misikiti yote ya jijini, ukiacha michache sana, ilikuwa ikifungwa ili watu waweze kujumuika pamoja kwenye sala na sherehe hizo za sikukuu ya Eid.

Sala ya Eid Mnazi Mmoja 2006
Mnazi Mmoja nyuma ni iliyokuja kuwa Titi Street 1966

Sherehe hizo zote zilikuwa zikipangwa na kuratibiwa na kamati maalumu iliyoshirikisha madhehebu zote za dini ya Kiislamu (Sunni, Bohra, Shia, Ibadhi, Ismailia n.k) iliyojulikana kama Maulid Committee na mwenyekiti wake kwa muda mrefu alikuwa Ismailia mmoja aliyeitwa Aziz Khaki. Hakukuwa na Bakwata siku hizo, ambayo kimtazamo inaonekana kama ni ya Waislamu Waafrika au weusi.

Kwa siku za sikukuu ya Eid, viwanja vya Mnazi Mmoja ilikuwa ndipo panapofanyika sherehe zote kwa kuandaliwa mambo mbalimbali ya kufurahisha, hasa kwa watoto kupata burudani ya michezo mbalimbali ya kubembea na vichekesho pamoja na vyakula vyenye kufurahisha nyoyo kama vile sharbati, askirimu, gubiti na mishikaki. Ngoma za asili pia hupigwa hapo kuwaburidisha watu kwa muda wa takriban siku tatu mpaka nne kila jioni. Zile zilikuwa ni siku za kukumbukwa kweli, kwani mambo kama yale sasa hayapo tena sijui yamepotelea wapi.

Sasa kwa siku nyingine za kawaida, viwanja vya Mnazi Mmoja vilikuwa ni kimbilio la wakazi wengi wa hapa mjini kuja kushuhudia mechi mbalimbali za mpira wa miguu zilizokuwa zikichezwa hapo kwa kushirikisha timu mbalimbali za hapa mjini kuwania ama vikombe au kucheza kirafiki tu pamoja.

Mjini hapa siku hizo, ukiacha Sunderland (sasa Simba) na Yanga, kulikuwapo na vilabu vingine maeneo ya Kariakoo, Ilala na Magomeni vilivyokuwa vikitoa burudani tosha kabisa katika medani ya soka kwa wenyeji wa jijini.

Eneo la Gerezani kulikuwa na timu kali sana ikiitwa Victoria, ambapo inapopambana na New Take Time ya Kariakoo, basi huwa patashika kweli kweli. Klabu ya Kahe ya Kariakoo inapomenyana na Rover Fire ya Msimbazi Center pale Ilala, huwa ni kama vile ‘asiye na mwana aeleke jiwe’. Hali kadhalika klabu ya New Port ilipokuwa ikicheza na Young Boys, basi siku hiyo macho yote huelekezwa Mnazi Mmoja au kwa jina jengine viwanja hivyo vikijulikana kama ‘Tua Tugawe’.

Tua Tugawe, ni jina pia la eneo hilo la asili kwa vile pale mbele, ambapo kwa sasa imejengwa ile Shule ya Msingi ya Mnazi Mmoja, kulikuwa na mbuyu mkubwa uliojulikana kwa jina ‘Mbuyu wa Simbamwene’. Simbamwene alikuwa ni mzee mmoja ‘babubabu’ hivi, ambaye kutwa alikuwa akishinda kwenye mbuyu huo. Mara nyingi jijini Dar, mibuyu huwa na majina ya watu. Kwa mfano mbuyu ule uliopo pale St. Peters, Oysterbay, ulikuwa ukiitwa ‘Mbuyu wa Kigwe’, jina la kiasili hilo ambalo limekufa kabisa. Kigwe ni moja ya majina makubwa ya wazawa wa Msasani kule baharini.

Sasa, mahala pale kwenye mbuyu wa Simbamwene kulikuwa na wahuni wakishinda hapo kuwasumbua watu wanaopita njia hiyo kuelekea Kisutu, Stesheni au Gerezani. Kama itatokea wewe mpita njia ukawa umebeba kitu, basi ghafla hukutokea na kukutisha wakikwambia “tuwa hicho ulichonacho tugawe!” Wanyonge wao mara nyingi huwa ni akina mama ambao walikuwa wakiitumia njia hiyo kwenda hospitali ya Sewa Haji iliyokuwapo maeneo ya kule Polisi Kati (Central Police Station) jijini, wakiwa wamebeba chakula kuwapelekea wagonjwa. Kadhia hiyo pia iliwakumba wasafiri kutoka mikoani ambao walikuwa wakitoka Stesheni ya Treni, ambayo haiko mbali na ‘Tua Tugawe.’

Jirani na Tua Tugawe na Mbuyu wa Simbamwene, ndipo ilipoasisiwa Madrassa maarufu jijini ya Maalim Ramadhan Abbas, ambapo wakazi wengi wa asili ya jiji hili walipitia kupata elimu yao ya Dini ya Kiislamu. Madrassa ya Abbasiya, kwa sasa imehamia maeneo ya Kariakoo jirani na Msikiti wa Idrissa. Miongoni mwa wanafunzi mashuhuri ni pamoja na Sheikh Zubeir Yahya wa Msikiti wa Mtoro, Sheikh Ali Azan wa Msasani na hayati Maalim Badi Ali, aliyepata kuwa mchezaji na kocha wa timu ya mpira ya Yanga ya Dar es Salaam.

Sasa, pamoja na mambo yote mazuri hayo yaliyopo eneo la Mnazi Mmoja hapa jijini; Mnazi Mmoja ndipo ilipoasisiwa TAA, TANU na baadaye CCM (chama kikuu cha siasa nchini) ambayo ilikuwa na makao yake makuu pale New Street/Lumumba kabla kuhamia Dodoma.

Mkabala na Ofisi za CCM, inapatikana shule maarufu ya Msingi ya Mnazi Mmoja, iliyojengwa mwaka 1957 kuja kuisaidia shule pekee ya msingi ya Mchikichini kusomesha Waafrika wajue kusoma na kuandika waje kusaidiana na watawala kweye kazi za daraja la chini—hasa hasa kuhesabu magunia na marobota ya bidhaa. Watu wengi walipitia hapo kwa elimu hiyo, akiwamo mwandishi huyu.

Wengine ni pamoja na Balozi Asha Rose Migiro, Alhaji Ramadhani Madabida aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, Wendo Mwapachu mfanyabiashara mashuhuri jijini Dar es Salaam na Alhaji Mussa Shaggow Mweka Fedha wa Klabu ya Saigon ya Dar es Salaam.

Historia ya Mnazi Mmoja haikuishia hapo, kwani kule upande wa pili inapatikana hospitali pekee iliyokuwa ikihudumia watu weusi wakati huo wa ukoloni uliogubikwa na ubaguzi wa rangi kwenye kila jambo. Hospitali ya Mnazi Mmoja ilikuwa inatibia magonjwa madogo madogo sana kama homa, kukohoa, kufunga vidonda na labda majipu na mapunye uliokuwa ugonjwa mkubwa kwa watoto majumbani.

Magonjwa mengine ni kichocho na kisonono ambayo yalikuwa yakiwakumba watoto mashuleni kwa sababu sera ya serikali ya kikoloni wakati huo ni kwenda shule ‘pekupeku’ (hakuna ruhusa kuvaa viatu shuleni), hivyo wanafunzi walikuwa wakiambukizana magonjwa hayo kwa sababu ya kukanyaga uchafu vyooni.

Jumba la Sukita na lile la Ushirika pale Lumumba ni majengo yenye historia ya kipekee kabisa kwenye miaka hiyo ya nyuma hasa kabla ya uhuru na mwanzoni mwa miaka ya 1960s mara tulipoanza kujitawala wenyewe.
Jumba la Ushirika Lumumba Avenue

Msomaji, amini usiamini lile Jumba la Ushirika ndilo lilokuwa jumba la kwanza refu hapa Dar es Salam likiyapita majengo yote mengine. Wachoraji ramani na wajenzi walitokea nchini Israel.

Hii inaweza ikawa ni kichekesho kwa watu wengi, lakini ukweli unabakia kwamba jumba lile lilipotangazwa kwamba litafunguliwa rasmi kwa kukamilika ujenzi wake, wakazi wengi walisikika wakilalamika ‘inakuwaje linafunguliwa bila kupigwa rangi nje; hawajui kujenga hao!’ Watu kwa mara ya kwanza tulishuhudia nyumba zikiwa na rangi ile ya cementi nje ili kupunguza vumbi, kwani baada ya jengo hilo likafuatia lile la Kilimanjaro Hotel nalo likafunguliwa bila kupigwa rangi nje. Mambo yakawa yaleyale, ‘ujenzi gani huu, nyumba zinapigwa lipu tu bila rangi!’

Jumba la Sukita, wakati huo likijulikana kama Jengo la Elimu ya Watu Wazima kwenye miaka ya 1960s, ndipo kilipoanzia Chuo Kikuu cha mwanzo Tanganyika kabla majengo ya kule UDSM Mlimani hayajajengwa. Nchi hii, kabla ya kupatikana uhuru hakukuwa na elimu ya shahada inayotolewa. Wazungu kwa miaka yote waliyokaa hapa hilo hawakulitaka litokee, maana shahada huzalisha watu wajanja na werevu ambao wangekuwa hatari kwa utawala wao. Udini na uchifu ndio uliowaibua na kuwapaisha akina Nyerere, Mareale, Fundikira, Kunambi na Kidaha Makwaia; ingawa hawakusomeshwa waje wadai uhuru baadaye.

Kushoto ni Mnazi Mmoja 2010

Msomaji historia ya Mnazi Mmoja ni pana sana kuelezeka kwa kikamilifu. Kwa hiyo naona kwa kumalizia nizungumzie sakata la kutaka kuibadilisha Mnazi Mmoja ili ichukue sura ya mpya ya kupendeza zaidi kulikoanzishwa na serikali ya Nyerere na chama chake cha TANU pale uhuru ulipopatikana.

Kwa nia nzuri tu, Mwalimu na viongozi wenzake waandamizi kwenye ile miaka ya mwanzo ya kujitawala walipanga kujenga jengo kubwa la chama chao cha TANU pale Lumumba; kujenga jengo jipya la Bunge pamoja na majengo mengine ya serikali yasambae kwenye eneo lile la Mnazi Mmoja na mitaa ya jirani.

Mpango huo ulikuwa utekelezwe kwa kuvunjwa nyumba nyingi sana mahala pale ukiwamo na Msikiti maarufu wa Manyema. Walipofuatwa kutakiwa kuvunja msikiti wao kupisha ujenzi mpya, wazee wa Kimanyema jijini waligoma kabisa wakasema wao hawawezi kuvunja nyumba ya Mwenyezi Mungu.

Mazungumzo mbalimbali ya kutaka wabadili msimamo yalishindikana hata pale Mwalimu mwenyewe alipoingilia kati kushawishi jambo hilo. Bado walikataa wakasema labda yeye kama rais wa nchi anaweza kutoa amri hiyo.

Nyerere alikasirika sana kupita kiasi; na hapo ndipo alipoanza mikakati ya kuhamisha kabisa makao makuu ya serikali kuhamia Dodoma. Haikuwa kwa kufuata mji wa katikati wala nini. Alijua Dar es Salaam angepata changamoto nyingi bora akaanze upya mahala pengine kama Dodoma, ambako wakazi wangelipokea kwa mikono miwili jambo hilo. Hivyo ndivyo ilivyokuwa serikali kuhamia Dodoma kwa kinyongo!

Basi tukutane juma lijalo. Alamsiki!
Simu: 0715808864

No comments: