Shajara ya Mwana Mzizima
Jumbe Muhammad Tambaza
Alimsomea Dua Nyerere, Nyota Yake Ikang’ara
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Jumbe Muhammad Tambaza |
JUMBE Muhammad Tambaza, ni mmoja katika wapigania uhuru
mashuhuri wa nchi hii ambao, historia inawataja kama ni watu waliotoa mchango
mkubwa sana katika kufanikisha kumng’oa Mkoloni Mwingereza, katika ardhi yetu
tukufu.
Hayati Mzee Tambaza, ambaye alifariki mnamo mwaka 1978
hivi, anaingizwa katika kundi moja la watu wa mwanzo kabisa waliompokea kwa
furaha na upendo kijana Julius Nyerere kutoka Butiama, alipofika jijini Dar es
Salaam kwa kumuunga mkono ‘mia kwa mia’, katika harakati zake za kupigania uhuru
wa Tanganyika kwenye miaka ya 1950s.
Wanaharakati wengine aliokuwa nao ni pamoja na Mzee
Mwinjuma Mwinyikambi wa Mwananyamala; Mzee John Rupia wa Mission Quarters;
Sheikh Suleiman Takadir; Sheikh Haidar Mwinyimvua (Kisutu); Mzee Max Mbwana
(Kariakoo); Zubeir Mwinshehe Mtemvu (Gerezani) pamoja na familia ya Mzee Azizi
Ali (Mtoni) na ile ya Kleist Sykes (Gerezani), Dar es Salaam.
Ukoo wa Diwan Tambaza Zarara bin Mwinyi-Kitembe, ndio waliokuwa
wenyeji wa maeneo ya katikati ya jiji wakati huo, wakihodhi eneo la ardhi yote
ya Upanga, iliyosambaa kuanzia Daraja la Selender kuelekea Palm Beach Hotel,
hadi Ikulu ya Magogoni kwa upande mmoja; na kwa upande mwengine maeneo yote
kutoka Aga Khan Hospital, Ocean Road Hospital, Kivukoni Front (makaburi ya
asili ya wanandugu wengine yako pale Wizara ya Utumishi, Magogoni) kwenda Mnara
wa Saa pale Uhuru Street na vilivyomo ndani yake.
Habari zinasema kwamba, katika siku za mwanzo tu za kupambana
na Mwingereza, wazee mashuhuri wa hapa Dar es Salaam walikutana na kuamua
kumfanyia ‘zindiko’ na ‘tambiko’ la kijadi, pamoja na kumwombea dua maalumu
kijana mdogo, Julius Nyerere, ili kumkinga na waovu na pia kuifanya nyota yake
ing’are juu ya wote wenye nia mbaya naye; wakiwamo watawala wa Kiingereza, hasa
Gavana Twinning.
Katika moja ya hotuba zake za kuaga aliyoitoa mnamo
Novemba 5, 1985, Nyerere alilikumbumbuka tukio hilo na hapa chini anasimulia:
“…Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar
es Salaam; na wazee wa Tanzania…na mambo makubwa kama haya kama hayana baraka
za wazee hayaendi… huwa magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi
nilipata baraka za wazee tangu zamani; tangu awali kabisa.
“Sasa siku moja, Dosa akanifuata
Magomeni (nyumbani kwake) akasema: ‘Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe
Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee
wameshakaa wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo wao Waislamu
watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.”
Anahadithia Mwalimu na kuendelea:
“Tulipomaliza wakasema kuna dua pia
za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika… zilikuwa za Korani;
sasa zikaja dua za wazee… za jadi, “…walikuwa na beberu la mbuzi…
wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama beberu akachinjwa huku anaambiwa
Twinning ‘umekwisha’… nikaambiwa tambuka… nikavuka lile shimo na baada ya hapo
nikaambiwa …basi nenda zako kuanzia leo Twinning amekwisha!”
Mwalimu alimaliza kusimulia namna alivyofanyiwa dua na
tambiko nyumbani kwa Mzee Tambaza, Upanga jijini.
(Picha ya Baraza la Wazee wa TANU kutoka kitabu cha Saadan Abdu Kandoro, ''Wito wa Uhuru.'') |
Kutawaliwa na Wazungu kuliwakera na kuwakasirisha watu
wengi sana, kutokana na kule kudharauliwa ndani ya nchi yao wenyewe na watu
wengine; hasa pale walipominywa katika kupatiwa huduma muhimu kama elimu bora,
matibabu na mahala pazuri pa kuishi.
Pamoja na mambo mengi mengine yaliyokuwa mabaya
kutokana na kutawaliwa, yamo pia na yale ya kuwekwa kwa madaraja katika utoaji
huduma muhimu. Sisi, wana wa nchi hii, hatukuwa na shule za maana hata kidogo;
watu wote sisi tukasomee shule moja tu (Mchikichini) mpaka darasa la nne; kwa
nini hasa kama siyo dharau?
Nyumba zetu za kukaa zilikuwa za ovyo zilijengwa kwa
miti na kukandikwa udongo na juu ni makuti, tena hapa hapa mjini Dar es Salaam,
sikwambii vijijini; umeme uko kwenye taa za barabarani na siyo majumbani mwetu.
Tukiwasha vibatari na taa za ‘chemli za Aladin’ kwa wenye uwezo kidogo kila
siku.
Hospitali ziliishia kutoa kama huduma fulani ya mwanzo
tu (First Aid). Haikuwapo hospitali ya Amana, Temeke, Mnazi Mmoja, Mwananyamala
wala Mbagala. Tuliponea kibahatibahati tu kwa mizizi na majani ya porini. Ukiwa
na homa kali basi chemsha mwarobaini; tumbo la kuendesha chemsha majani ya
mpera au mpapai nani akupe ‘antibiotic wewe’.
Hospitali ya Muhimbili, yenye maabara na vipimo pamoja
na madaktari bingwa, ilijengwa mwaka 1957 - ni juzi tu - kwa heshima ya Binti
Mfalme Margareth II, aliyekuwa na ziara ya kutembelea makoloni ili aje kufungua
rasmi hospitali hiyo. Kiwanja kilitolewa kwa hisani ya familia ya Mzee Jumbe Tambaza,
ambapo miembe ile mikubwa inayoonekana mpaka leo pale ilikuwa shambani kwa kina
Tambaza.
Kwa hivyo basi, ukiacha labda homa na vidonda,
magonjwa mengine yote kwetu ilikuwa ni kifo tu. Umri mkubwa wa kuishi kwa
wastani ulikuwa ni miaka 30.
Mzee Jumbe Tambaza, ambaye jina lake linanasibishwa na
shule maarufu ya Sekondari ya Tambaza ya jijini - hana uhusiano wowote na shule
hiyo - shule ilipewa jina lake kutokana na eneo iliyopo na kwa kuthamini
mchango wake katika kupigania uhuru.
Kabla ya hapo, wakati huo wa ubaguzi wa rangi na
matabaka, shule hiyo na ile ya msingi iliyo jirani nayo inayoitwa Muhimbili Primary,
zilikuwa mahsusi kwa vijana wa Kihindi tu – hasa Ismailia - zikijulikana kama
‘Aga Khan Schools’ na kamwe hawakuwa wakisoma Waswahili na Kiswahili pale.
Shamba la Mzee Jumbe Tambaza pale Upanga, lilianzia
mbele kidogo ilipo Shule ya Jangwani Wasichana (ambayo wakati wa ukoloni
ilijengwa na serikali wasome watoto wa kike wa Kihindi tu, na ile Shule ya
Azania ilikuwa kwa watoto wa Kihindi wa kiume), na kutambaa moja kwa moja mpaka
lilipo Daraja la Selender pale baharini.
Eneo la Majengo ya Hospitali ya Muhimbili ilikuwa mali
ya Jumbe Tambaza na marehemu nduguze (Msakara, Kudura na Mwamtoro Tambaza). Kutokana
na kukosekana kwa hospitali ya maana ya rufaa kwa ajili ya Waafrika (kwa sababu
ya ubaguzi tu), hayati Mzee Tambaza alitoa eneo lote lile la Muhimbili ijengwe
hospitali ya Waafrika ili kupunguza vifo vilivyotokana na kukosa tiba sahihi.
Kijihospitali kidogo kwa ajili ya watu Weusi kilikuwapo
pale jirani na Kituo cha Kati cha Polisi (Central Police Station) jijini,
ikiitwa Sewa Haji Hospital, kwa heshima ya mfadhili aliyeijenga kusaidia jamii
masikini. Sewa Haji alikuwa mkazi wa Bagamoyo mwenye asili ya Kibulushi kutoka
Persia. Baada ya kujengwa hospitali ya Muhimbili, jengo moja katika yale matatu
makuu, likaitwa Sewa Haji kama kumbukumbu yake.
Mjini Dar es Salaam wakati huo wa kibaguzibaguzi, serikali ya kikoloni haikutenga sehemu ya kuzikia watu weusi ambao walikuwa
daraja la nne. Yale makaburi mashuhuri ya Kisutu, wakati huo yalikuwa ni ya
watu wenye asili ya Kiarabu tu! Mwengine yoyote, ilibidi apelekwe kijijini kwao
tu nje ya mji – Kunduchi, Mbweni, Msasani, Bagamoyo, Kisarawe, Maneromango na
mikoani pia.
Sasa, ili kuondoa adha hiyo na usumbufu, Babu Mzee
Tambaza, alitoa bure sehemu kubwa ya eneo lake itumike kwa watu wenye kuwa na
shida ya kuzika ndugu zao jijini. Makaburi ya Tambaza siku hizo yalikuwa
maarufu sana kuliko yalivyo yale ya Kisutu kwa sasa. Kamwe watu weusi hawakuwa
wakizikwa Kisutu, kama ilivyo wakati huu.
Kufuatia hali hiyo, Jumbe Tambaza aliwashawishi binamu
zake wawili, Mwinyimkuu Mshindo na Diwan Mwinyi Ndugumbi na wao wakatoa sehemu
watu waweze kuzikana kule maeneo ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa na Ndugumbi,
Magomeni Makuti; makaburi ambayo mpaka leo yameendelea kutumika kuzikia watu
wote.
Neno Tambaza, limetokana na neno kutambaa au kusambaa
eneo kubwa. Diwan Tambaza na nduguze walikuwa watawala wa sehemu mbalimbali za
hapa Mzizima siku za nyuma kabla Waarabu, Wajerumani wa Wangereza kufika hapa.
Nduguze wengine ni Diwan Uweje; Diwan Uzasana; Diwan Mwenye-Kuuchimba na Diwan
Mwinyi Ndugumbi.
Majina hayo walijipachika wenyewe kiushindani,
kujigamba na kujitukuza kuliko ndugu wengine; hivyo kimafumbo mafumbo, huyu
akajiita hivi na yule akamjibu mwenzake vile; mwengine akajiita naye atakavyo,
kutokana na uhodari na tawala thabiti walizoziongoza.
Majina hayo pandikizi, hata hivyo yalikuwa na maana
yake kila moja; kama vile mtu aseme mimi ‘Mobutu Sese Seku Kuku Mbenju wa
Zabanga’, ikiwa na maana ya ushujaa kwa ‘Batu ba Kongo na fasi ya Zairwaa!’
Sasa Diwan Tambaza alipojiita vile, nduguye Diwan
Uweje akamjibu na kumwuliza hata ukiwa umesambaa ndio uweje? Mwengine naye
akasema, ‘’Ah! Uliza sana wewe uambiwe.’’ Hivyo yeye akajita Diwan Uzasana.
Diwan Mwenye-Kuuchimba, yeye alikuwa akitawala maeneo ya Mtoni Kijichi na Mbagala
yake, akasema, ‘’Nyie wote mnacheza tu, ‘mimi ndiye mwenye kuuchimba!’’ Kwa
maana ya kwamba ndio kiboko ya wote. Ilimradi hali ikawa ndiyo hiyo; na hizo
ndio zama zao, kwani husemwa kila zama na kitabu chake.
Mwandishi wa makala haya, jina langu naitwa Abdallah
Mohammed Saleh Tambaza. Babu yangu Mzee Saleh bin Abdallah Tambaza wa Zarara,
anakuwa binamu wa Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, yaani baba zao walikuwa ndugu.
Shamba la babu yangu mimi pamoja na kaka yake Kidato
Tambaza, linasambaa kuanzia Don Bosco, Makao Makuu ya Jeshi, Diamond Jubilee,
Msikiti Maamur (kaburi la babu na babake babu yamo ndani ya Msikiti wa Maamur unapoingia
mkono wa kulia pale ukutani), kuelekea kwenye Jamat la Wahindi mpaka Mahakamani
kule Kisutu.
Miembe, minazi na mizambarau ile ya asili inayoonekana
Upanga, ilipandwa na babu yangu kwa ajili ya urithi wa wajukuu zake,
itakapofika zamu yao kumiliki maeneo yale.
Kwa bahati mbaya sana, Wazungu Waingereza, wakaona
mandhari ile nzuri ya Upanga, hawakustahili watu weusi kuishi pale na wakawaamuru
babu zangu wahame wawapishe Wahindi raia daraja pili. Hii ni baada ya wao
Wazungu daraja la kwanza kuchukua eneo lote la Oysterbay (sasa Masaki). Maeneo
yote hayo mawili yenye upepo mwanana ni karibu kabisa na bahari.
Kitendo cha kumhamisha mtu nyumbani kwake kwa namna
ile, halafu kumpa fidia uitakayo wewe, ni dharau, dhuluma na ukiukwaji mkubwa
wa haki za binadamu. Wazee wale wastaarabu na wajanja hawakuwa na haja ya kuyauza
maeneo yale, kwani ukiyaangalia utaona waliyapangilia ili vizazi na vizazi vya
kwao viishi hapo.
Hii haihitaji mjadala wala maelezo marefu, lakini ni
ushahidi tosha kwamba inaweza ikawa ndiyo sababu kubwa iliyomfanya Mzee Jumbe
Tambaza awe mstari wa mbele kabisa katika kuwachukia watawala wa Kizungu na
kumuunga mkono Nyerere kwa nguvu kubwa kama ile.
Mchango wa Mzee Jumbe Tambaza katika ukombozi wa nchi
yetu haukutetereka hata kidogo, kwani hata pale rafiki yake mpenzi Sheikh
Suleiman Takadir, alipotahadharisha watu kuwa makini na Nyerere maana
ameonyesha kwamba siku za usoni angependelea zaidi jamaa zake, Mzee Jumbe
hakumuunga mkono na akakubali Sheikh Takadiri atengwe na jamii kwa manufaa ya
umoja wa kitaifa.
Jumbe Tambaza pia hakumuunga mkono Zubeir Mtemvu,
kwenye suala la Kura Tatu ambalo ilibaki kidogo tu chama cha Tanu
kingesambaratika na kuwa vipande viwili; lakini yeye alibaki na Nyerere wake
mpaka dakika ya mwisho kule Tabora hadi kukasainiwa waraka wa ‘Uamuzi wa Busara’
ambao uliwapeleka TANU kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu.
Katika picha ya pamoja iliyopigwa baada ya kutangazwa
ushindi wa kuingia kwenye Kura Tatu kwa chama cha TANU, anayeonekana nyuma ya
Mwalimu Nyerere pale Tabora ni Mzee Jumbe Tambaza. (Rejea kitabu Mohammed Said,
‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes… uk 275).
Kutokana na uaminifu wao usiotetereka kwa chama chao,
Mzee Jumbe Tambaza na mwenziwe Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; wazee wale wawili wa
Kimashomvi kutoka Mzizima, kwa muda mrefu wamekuwa wajumbe wa kudumu (permanent
seats) kwenye Kamati Kuu ya TANU bila kupigiwa kura; achilia mbali ule uwepo
wao kwenye Baraza la Wazee wa TANU.
Mnamo mwanzo wa miaka ya mwanzoni 1950, Mzee Tambaza alitumbukizwa
tena kwenye mgogoro mkubwa na serikali pale ilipokuwa inajenga upya Barabara ya
Umoja wa Mataifa kutokea Faya kuelekea Daraja la Selander, ilipoamuliwa kwamba
sehemu ya eneo la makaburi iondoke kupisha ujenzi huo.
Hayati Mzee Tambaza, alifungua kesi mahakamani dhidi
ya serikali, kesi ambayo inatajwa kama moja ya kesi nzito (landmark cases) sana
kutokea hapa nchini na Afrika Mashariki iliyogusa imani ya Dini ya Kiislamu;
kwamba je, ni halali au si halali kufukua makaburi ya watu waliokufa?
Kesi ya Makaburi, kama ilivyokuja kujulikana,
iliunguruma kwa muda mrefu na kujaza kurasa za mbele za magazeti wakati huo,
kutokana na mabishano makali ya hoja (cross examinations) mahakamani baina ya
mawakili wa pande mbili hasimu.
Wakati Serikali ikiwatumia masheikh wazawa wa hapa
waliosema kwamba inakubalika kufukua makaburi, Jumbe Tambaza aliwatumia
masheikh wakubwa kutoka Mombasa na Zanzibar, akiwemo aliyekuwa Kadhi wa
Zanzibar Abdallah Saleh Farsy kupinga hoja hizo.
Kwa kishindo kikubwa, Mzee Tambaza alishinda kesi ile
na ikabidi barabara ile ipindishwe pale kwenye mteremko wa kutokea Faya na
kuyaacha makaburi na vilivyo ndani yake kama yalivyo. Haraka haraka, Hayati
Mzee Tambaza akafanya maamuzi ya kujenga msikiti ambao haukuwapo mahala hapo
kabla ya tukio hili, kuepusha kujirudia.
Huyo ndiye
Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, mwanaharakati wa kupigania uhuru wa taifa hili wa
kupigiwa mfano, aliyetetea na kutoa vyake kusaidia wanyonge wenziwe katika jamii
yetu katika kipindi cha manyanyaso ya utawala dhalimu wa Malkia wa Uingereza. Alimfanyia
madua na matambiko ya jadi Mwalimu Nyerere ili nuru yake ing’are kama mwezi na
jua!
Ewe Mola Mghufirie madhambi yake – Ameen.
No comments:
Post a Comment