Shajara
ya Mwana Mzizima:
WAJUE WANA
SAIGON CLUB WA MZIZIMA
Na
Alhaji Abdallah Tambaza
Saigon Khitma Jumapili 13 May 2018 |
JUMA hili, shajara imeonelea ichepuke kidogo kutoka kwenye siasa na
kuangalia mambo ya kijamii kidogo ili wasomaji wasichoshwe na historia ya siasa
peke yake; leo tutaangazia habari
nyengine kutoka katika jamii tunamoishi.
Vijijini kule tunakotoka, ukitaja neno ‘klabu’ au klabuni, basi moja
kwa moja hiyo inamaanisha kwamba umekusudia mahala ambapo watu – wanawake kwa
wanaume—watakuwa wamejazana wakinywa ‘mapombe’ yale ya kienyeji yaliyovunda na
kutoa harufu mbaya kabisa.
Mijini hali kadhalika, ukisema ‘nakwenda klabu’ maana yake ni kwamba
unakusudia klabu cha usiku (Night Club), ili pia ukalewe na, au kukesha huko
ukicheza muziki na mambo mengine ya anasa kama kucheza kamari na kuvinjari na warembo
wa mjini hapo. Klabu pia inaweza kuwa kama vile klabu za mpira za Simba, Azam
na Yanga ili kwenda kujumuika na wapenzi na marafiki mzungumzie masuala ya soka
na michezo mengine kama tenisi na gofu (Gymkhana) na Leaders Club (Klabu ya
Viongozi pale Barabara ya Ali Hassan Mwinyi), siasa na biashara—basi hakuna
zaidi.
Jijini Dar es Salaam, hususan maeneo ya katikati ya Kariakoo,
inapatikana klabu moja mashuhuri sana inayojulikana kama Saigon Club, yenye
maskani yake pale Mtaa wa Narung’ombe na Livingstone. Ni klabu kongwe ambayo
umaarufu wake umezagaa kila pembe, ambapo hakuna mwenyeji wa jiji hili, atasema
haijui au hajawahi kuisikia. Saigon kabla ya kuhamia Mtaa wa Narung’ombe na
Livingstone ilikuwa Mtaa wa Sikukuu na Narung’ombe.
Madhumuni ya klabu hiyo—‘raison d’etre’— ni tofauti kabisa na vilabu
vingine vyote tulivyovizoea katika maisha ya kawaida. Hapo hapachezwi mpira
(ingawa wanachama wake labda kwa kiasi fulani ni wapenzi wa mpira), wala mchezo
wa aina yoyote ile kama karata, drafti na dhumna. Hii siyo kusema kuwa Saigon
haikuwa klabu ya mpira. Saigon ilianza kama klub ya mpira ya watoto wadogo wa
shule za msingi na wakakua nayo hadi ukubwani na walipokuwa sasa hawawezi tena
kucheza mpira Saigon ikabaki kama barza, mahali wanakutana kwa mazungumzo.
Klabu hii ya kupigiwa mfano au yenye mfano wa kuigwa, ni mahala ambapo
watu huenda jioni na kuzungumza mambo mbali mbali ya kijamii na namna ya
kuyatafutia ufumbuzi wa haraka kwa mustakabali wa jiji la Dar es Salaam na watu
wake.
Orodha ya wanachama wake imekusanya watu kutoka katika kada mbalimbali
wakiwamo kwanza hao wanamichezo, wapenzi wa michezo, masheikh, maimamu, walimu
wa skuli na madrassa; pamoja na wanasiasa waandamizi wakiwamo mpaka marais,
mawaziri, wabunge na madiwani.
Wamo pia wanajeshi la Ulinzi, Polisi, Usalama wa Taifa, Madaktari na
wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa mjini Dar es Salaam wa jinsia zote.
Klabu ya Saigon ina madhumuni tofauti na vilabu vyengine na mambo
yanayofanyika pale ni aghlabu kuyakuta kwenye vilabu vya kawaida
tulivyovielezea hapo awali.
Kwanza, uanachama wake hauangalii umri, jinsia, dini, kabila, itikadi
ya vyama vya siasa, cheo, na mambo kama hayo. Utanzania wako ndiyo kigezo kikuu
cha kuwa mwanachama ingawa klabu ni ya watu wa Dar es Salaam.
Katika kalenda yake ya mwaka, Klabu ya Saigon huadhimisha mambo
makubwa matatu hivi.
Kwanza, ni kuandaa shughuli kubwa siku chache kabla ya kuingia mwezi
mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaalika watu mashuhuri kuja kujumuika na jamii ya
kawaida kuja kuwaombea dua wanachama wa klabu hiyo waliotangulia mbele ya haki,
pamoja na wakazi wa jiji hili ambao maisha na matendo yao walipokuwa hai,
yaliacha athari na kumbukumbu kwa watu wa jiji hili.
Kushoto Brigadier General Mstaafu Simba Waziri, Mwinyi Mangara na Boi Risasi katika futari ya mwaka wa 2010 |
Hao ni pamoja na wasanii wa fani mbalimbali; mashekhe na walimu wakubwa;
wazee mashuhuri pamoja na viongozi waliopata kushika nyadhifa mbalimbali jijini
Dar es Salaam na kugusa nyoyo za watu.
Katikati Abdallah Tambaza mwandishi wa makala hii na kulia Mussa Shagow na kushoto ni Mwinyikhamis Mwinyimadi |
Shughuli hiyo ya khitma, husababisha kufungwa kwa matumizi ya kawaida,
barabara yote ya Narung’ombe kuanzia Sikukuu mpaka ile ya Livingstone. Idadi ya
wahudhuriaji huwa zaidi ya watu elfu 4000 mpaka 5000. Vyakula vya aina
mbalimbali hupikwa kwa wingi sana siku hiyo na vinywaji baridi na matunda hutolewa
kwa wageni.
Sherehe hii, ambayo huwa si ya kukosa kuhudhuria kwa wenyeji, hufana
sana maana huwa imepangiliwa kwa ustadi mkubwa kuanzia madua na visomo
mbalimbali, pamoja na wazungumzaji wa kutoa nasaha zenye mazingatio kwa
waalikwa.
Kila mwaka huwa inaushinda mwaka uliotangulia kwa ubora. Huwa ni
hadhara ya aina yake iliyojaa vicheko, utani na vitimbi mbalimbali vya Usimba
na Uyanga kwa watu kupigana vijembe vya upendo.
Pili, ni kuandaa futari maalumu katika siku moja ya Ramadhani na
kufuturisha watu wa jiji hili bila ubaguzi, hata kama mtu hukufunga au si
Mwislamu huwa anakaribishwa kujumuika. Kitendo hicho, si tu kinajenga udugu
miongoni mwa wanachama, bali hutoa fursa kwa watu mbalimbali kukutana na kula
pamoja futari hiyo katika hali ya furaha na upendo.
Daima kwenye futari hizo za kimrima, waandaaji huhakikisha vile vitu
vyote vizuri vinakuwamo sahanini, siniani na vyanoni—iwe ndizi mzuzu na mihogo
kwa papa; tambi, kaiamati na maandazi; mikate ya kusukuma na ya kumimina;
bajia, sambusa na kachori pia huwamo. Uji wa pilipili manga na ‘chai za zatari’
huhanikiza kwa harufu nzuri mahala hapo. Waandaji huweka pia makombe (mabakuli
makubwa) ya michuzi ya kuku, maini na mbuzi pia. Vitu huwa vimekamilika
kisawasawa vyenye kutamanisha machoni na mdomoni!
Wazalendo hawa wa Saigon huwa hawaishii hapo, bali pia huandaa sherehe
ya usiku mmoja ya kasida za Mtume Muhammad, kwa ajili ya mahujaji wa jijini
ambao walibahatika kwenda kufanya Ibada ya Hija na kurejea salama. Hii nayo
hupendeza kwelikweli, maana hutoa fursa kwa mahujaji, wakiwa kwenye kanzu zao
nzuri zenye kumeremeta, kuja kuelezea waliyoyaona na kuyadiriki walipokuwa kule
kwenye miji mitukufu ya Makkah na Madina katika Hijja na Umra kwa kuwaburudisha
kwa kasida zinazoimbwa na kughaniwa kwa sauti nyororo.
Hii huwa ni nafasi nzuri kwa wasiobahatika kuwenda Hijja ya kuombewa
dua na watu wale watukufu siku za mwanzo kabisa, kwani imesemwa kwamba dua za mahujaji
kabla ya siku 40 kwisha huwa mustajaba (hukubaliwa na anayeombwa).
Saigon Sports Club, hapo mwanzoni iliundwa na vijana wadogo wa skuli za
Mchikichini na Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, mwaka 1966, ikiwa kama klabu
ya mtaani kwa madhumuni ya kucheza mpira na watoto wenzao wa mitaa mingine.
Kwa mujibu wa Alhaji Mussa Mohammed Shaggow, mwanachama mwandamizi, waanzilishi
wachache wa mwanzo wa klabu hii wakati huo ikijulikana kama Everton ni pamoja
na Mussa Shaggow mwenyewe, Harudiki Kabunju, Yaakub Mbamba, Atika Kombo, Abdu
Shiba, Dachi na Salum Khalil akiwa Golikipa wa mwanzo klabuni.
Kulia Atika Kombo, Harudiki Kabunju na Sunday Kayuni wakijikinga mvua katika khiyma ya mwaka wa 2017
|
Timu nyingine za watoto wa mitaani siku hizo hapa Kariakoo, ni pamoja
na iliyokuwa jirani yao, Cuba Rovers, New Take Time, New Port (mwandishi huyu
alikuwa mwanachama), Dundee, Young Kenya na Young Boys. Zote hizo ziliundwa na
vijana wadogo wa umri wa wastani wa miaka 14 wa maeneo ya Kariakoo, ili kutoa
ushindani wa kimpira.
Sasa kadri miaka ilivyokuwa inakwenda mbele na vijana wale kuondoka
kutoka utoto na kwenda ukubwani, wakabadilisha madhumuni ya klabu yao na kuwa
haya sasa ili kudumisha udugu wao pamoja na kuwapokea wanachama wapya wakiwamo
wanawake na wazee pia.
Kwa sasa, Saigon mpya yenye malengo mapya na maono mapya, inaongozwa na
Mahmoud Mbarak kama Mwenyekiti, akisaidiwa na Juma Abeid ‘Spencer’. Boi Juma ni
Katibu wa Klabu akisaidiwa na Mohammed Msitu na Alhaji Mussa Shaggow Mweka
Hazina akisaidiana na Abdul Risasi. Kwenye orodha ya wajumbe yumo Muharram
Mkamba, Mohammed Tall, R. Sultan na wanawake Hamida Simba na Awena Kitama.
Iddi Simba, mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kugombea urais wa nchi hii,
kupitia CCM ndiye mlezi wa Saigon ambaye kila mara amekuwa mstari wa mbele
kuitetea na kuihami pale inapotaka kutetereka au kwenda kombo, kwani klabu hii
ni kioo cha uzalendo uliotutuka kwa kufanya mambo makubwa ambayo wengi
wamejaribu kuyaiga lakini wameshindwa vibaya.
Dr. Gharib Bilal akitoa nasaha katika Khitma ya Saigon |
Wamo pia katika wanachama na wapenzi wakubwa wa Klabu ya Saigon, Rais
mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wake Dk. Mohammed
Gharib Bilal. Wengine ni Mwanasiasa mashuhuri wa nchi hii hayati Ali Sykes na
nduguye Balozi Abbas Sykes pamoja na watoto wao Kleist Sykes (sasa marehemu),
Abraham na Ayoub Sykes. Yumo pia Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala, na marehemu
Balozi Abdul Cisco Mtiro na ACP Kamanda Mohammed Chico (sasa marehemu).
Kulia Ally Sykes, Sheikh Issa ''Smart Boy'' Ausi, mwisho kushoto Juma ''Spencer'' Abeid |
Kulia marehemu Balozi Cisco Mtiro, Mrehemu Sheikh Hussein, Sheikh Shomari na Abraham Sykes katika Khitma ya Saigon |
Mheshimiwa Mussa Zungu katikati akifuturu |
Madhumuni mapya ya uwepo wa Klabu hiyo, pamoja na hayo niliyaeleza hapo
juu ni pamoja na kusaidiana kwa shida; kufa na kuzikana. Saigon pia imekuwa
kimbilio kubwa la wanasiasa wakubwa na wadogo wanaowania nafasi za uongozi
katika ngazi mbali mbali hapa nchini ili kupata kuungwa (endorsement).
Hivyo basi kutokana na kuwa na wanachama wa rika na kada mbalimbali inakuwa
rahisi kwa mgombea kukubalika jijini kama watu wa Saigon watamridhia na ‘kumpigia
debe’ tiketi yake. Hiyo imethibitika mara nyingi na hivyo kuwa na ulazima wa
kujitambulisha mapema kwa wana Saigon pale mgombea anapotangaza nia. Cha ajabu
ni kwamba, hiyo si kwa wanasiasa peke yao bali hata wale wanaogombea kwenye
vilabu vya mpira vya Simba na Yanga na kwenye ofisi za TFF za Taifa—Saigon wana
mkono mrefu na nguvu kote huko. Fitna za siasa na mpira wanajua kuzicheza.
Lakini basi pamoja na mafanikio yote hayo mazuri, klabu
ya Saigon imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha
kuwepo na makundi mawili hasimu yasiyoiva pamoja. Jitihada mbalimbali
zimefanywa kuwarudisha pamoja kwa faida ya watu wa Dar es Salaam, mpaka leo
hazijazaa matunda. Hivyo ni jukumu letu kuzidi kumwomba Allah (SWT) aipeperushe
fitna hii kwa mbali na amani nzuri irejee pale Saigon ili Dar es Salaam yetu
iendelee kustawi. Wahenga walisema; ‘wengi huitwa wale na mmoja huitwa yule!’
Hiyo ndiyo Saigon Club, yenye kuunganisha watu kwa namna
ya kipekee ambayo haijapata kufanywa, kuwepo au kutokea mfano wake hapa
Tanzania katika huu umri wa miaka 60 wa kujitawala.
Jana tarehe 13 May 2018 Saigon walifanya khitma ambayo
juu ya kuwa ilinyesha mvua kubwa wengi walihudhuria.
Alamsiki!
Simu: 0715808864
atambaza@yahoo.com
No comments:
Post a Comment