Dk. Mahathir ‘Role Model’ wa Zitto Kabwe, Mwenye Maajabu
Na Yusufu Lulungu
Zitto Kabwe na Mahathir Mohamed
Kuala Lumpur
Mara kadhaa Mbunge wa Kigoma mjini(ACT-Wazalendo), Zitto
Kabwe amekuwa akiandika mambo kumuhusu Mzee huyu Dk. Mahathir Mohamad.
Miongoni mwa maandiko yake kwa Mzee huyu ni lile la mwaka
2013 katika gazeti la Raia Mwema lililokuwa na anuani ya “Uhuru wa fikra
utawango’a madikteta,” na lile la hivi karibuni la kumtakia heri ya kuzaliwa na
kutimiza miaka 92.
Pia baadhi ya watu wakaribu na Zitto Kabwe wamewahi kunijuza
kuwa mbunge huyo anamchukuliwa Dk Mahathir kama mmoja wa ‘kioo’ chake muhimu
kuelekea harakati zake za kisiasa huko mbeleni na ujenzi wa nchi.
Sababu moja wapo ya Zitto kumchukulia Dk. Mahathir kama mfano
wake wa kuigwa ni uwepo wa mshabaha kiasi katika historia zao za kisiasa.
Nitaeleza hili huko mbeleni kwenye makala haya.
Kwenye anuani ya makala haya nimedokeza kuhusu maajabu
anayoendelea kuyafanya Dk. Mahathiri ambae alikuwa Waziri Mkuu wa nne wa
Malaysia kuanzia mwaka 1981 hadi mwaka
2003 alipojiuzulu.
Moja ya maajabu hayo yanatokana na matokeo ya Uchaguzi mkuu
uliofanyika nchini Malaysia Jumatano
iliyopita ambapo Muungano wa vyama vya Upinzani(Pakatan Harapan au Alliance of
Hope) ukiongozwa na Dk. Mahathir ulishinda uchaguzi huo.
Upinzani huo ulinyakuwa viti vya wabunge 113 na kuubwaga
Muungano uliyokuwa madarakani, Barisan Nasional (BN), ukiongozwa na waziri mkuu
aliyenyofolewa kitini ndugu Najib Razak. BN waliambulia viti 79.
Matokeo hayo yanatoa maajabu haya, Mosi, ni kuwa Dk. Mahathir
aliyeshika nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka 22 na kustaafu siasa kwa muda wa
miaka 15 amerejea tena kwenye nafasi hiyo wakati huu akitokea chama cha
Upinzani.
Na kwa sasa Dk. Mahathir mwenye umri wa miaka 92 ndio anakuwa
kiongozi mwenye umri mkuwa duniani kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kisiasa.
Dk. Mahathir ndiye anatajwa kuwa ‘Baba wa taifa’ wa Malaysia
kwa kulifanya taifa hilo kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi na kisiasa na hata
kuingia kwenye ‘Asian Tigers’.
Pili, Dk. Mahathir amechangia kuung’oa madarakani Muungano
huo wa BN ambamo ndani yake kuna chama chake cha UMNO alichokulia kwa zaidi ya
miaka 50. Mahathir alikihama chama hicho hapo mwaka 2016 na kujiunga na
Muungano wa vyama vya upinzani.
Miongoni mwa sababu za Dk. Mahathir kukihama chama hicho ni
shutuma za ufisadi zinazomkabili Razak, ambapo anadaiwa kupokea kiasi cha dola
milioni 700 kutoka taasisi moja ya maendeleo nchini humo.
Pia Dk. Mahathir anamtuhumu Razak kwa kuongoza nchi kinyume
na katiba ikiwemo kuharibu uchumi wa nchi.
Tatu, Dk. Mahathir amemngo’a mtu ambae alimkuza kisiasa kwa
lugha nyingine mwanafunzi wake. Ni Dk. Mahathir ndiye aliyemuwezesha Najib
Razak kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama na kisha nafasi ya naibu Waziri
mkuu na hapo mwaka 2009 kuwa Waziri Mkuu wa sita.
Akiandika kwenye kitabu cha wasifu wake ‘A Doctor in the
House,’ cha mwaka 2011 ukurasa wa 768 Dk. Mahathir anasema: “Katika moja ya
hotuba zangu za kushtukiza kabla sijastaafu, nilisema bayana kuwa natarajia Tun
Abdullah(naibu waziri mkuu wakati huo) angemchagua Najib kuwa naibu wake.”
Tun Abdullah ndio alikuwa anachukuwa nafasi ya Uwazir mkuu
baada ya kustaafu Dk.Mahathir mwaka 2003.
Ajabu la nne ni kuwa Dk. Mahathir ameshinda uchaguzi huo
kupitia Muungano huo wa vyama vya Upinzani ulioundwa na hasimu wake mkubwa kisiasa Anwar Ibrahim.
Wawili hao walikiingia kwenye ugomvi hapo mwaka 1998 baada ya
Dk. Mahathir kumtimua Anwar kwenye nafasi ya unaibu Waziri mkuu na baadae
kutimuliwa kwenye chama kwa madai ya ulawiti.
Anwar ambae alitajwa kuwa muumini mzuri wa dini, alishutumiwa
kuwa na tabia ya kulawiti wasaidizi wake na wengineo. Madai hayo
yalitajwa(yanatajwa) kuwa ni ya kisiasa na kudaiwa kuratibiwa na Dk.Mahathir
ili kumzuia Anwar asiwe Waziri Mkuu.
Madai hayo baadae yalimpelekea Anwar kufungwa jela na mpaka
sasa yupo gerezani. Licha ya kuwemo gerezani, Anwar ndio anatajwa kuwa kinara
wa Muungano huo wa upinzani (Pakatan
Alliance).
Ajabu la tano, ni kuwa mke wa Anwar, Wan Azizah binti Wan
Ismail aligombea kwenye muungano huo pamoja na Dk. Mahathir, akiwania nafasi ya
unaibu Waziri Mkuu.
Tangu kutimuliwa kwa Anwar, Azizah, familia nzima na
wapinzani wamekuwa wakimuangalia kwa jicho baya Dk. Mahathir. Wanamuona ndio
mtu aliyeharibu maisha ya Anwar.
Leo hii mke wa Anwar na Dk. Mahathir wanafanya kazi pamoja,
Dk. Mahathir akiwa Waziri Mkuu, Wan Azizah akiwa naibu wake.
Katika moja ya mahojiano yake na runinga ya Aljazeera, Dk.
Mahathir ameonekana kumuonea huruma Anwar akihisi ni kweli anateseka kutokana
na hatua yake ya kumfukuza Serikalini.
Lakini kwenye kitabu chake cha ‘A Doctor in The House’
ukurasa wa 698 Dk Mahathir anaonekana kutojutia hilo akisema: “Leo hii Anwar
angekuwa waziri Mkuu wa Malaysia”. Lakini kwa kuwa hajawa, ni kwa sababu ya
matendo yake mwenyewe. Sikuwa na chaguo lolote bali kumuondoa Serikalini na
nilifanya nilichokiona ni sahihi kwa ajili ya nchi. Huenda nimefanya makosa
mengi lakini la kumfukuza Anwar sio miongoni mwa makosa hayo.”
Hata hivyo Mahathir ameahidi kuwa atatawala kwa muda wa miaka
2 kisha kumpisha Anwar awe Waziri Mkuu.
Kwanini ni ‘Role Model’ wa Zitto?
Moja ya eneo ambalo linatajwa kumfanya Zitto Kabwe amuone Dk.
Mahathir kama ni mtu wanaofanana kisiasa ni wote wawili kufukuzwa uanachama
ndani ya vyama vyao kwa tuhuma za usaliti.
Kama ilivyokuwa kwa Zitto Kabwe ambae hapo mwaka 2013
alifukuzwa uanachama ndani ya Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)
kwa tuhuma za usaliti, yakiwemo madai ya kutaka kumpindua Mwenyekiti Freeman
Mbowe ndivyo ilivyokuwa kwa Dk. Mahathir.
Hapo mwaka 1969, Dk. Mahathir alifukuzwa uanachama kwa tuhuma
za uchochezi na kutaka kumpindua aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Tunku
Abdul Rahman.
Chanzo cha yote ni hatua ya Dk. Mahathir kuandika barua kali
iliyomtuhumu Tunku kuwa alikuwa ameshindwa kukiongoza chama(UMNO) mara baada ya
chama hicho kushindwa kiasi kwenye uchaguzi mwa mwaka huo 1969.
Pia Dk. Mahathir alimtuhumu Tunku kuwa ameshindwa kuongoza
Serikali, hapendwi na wananchi wake, na ameshindwa kulilinda kabila la Malay
dhidi ya jamii ya Wachina ambao walijiona kuwa ndio Malaysia halisi na kuanza
kuwatenga wenzao ikiwemo kuwafanyia vurugu.
Barua hiyo iliyosambazwa nchi nzima, ilimfanya Dk. Mahathir
aonekane msaliti na mchochezi na kufanywa aitwe mbele ya Baraza kuu ili
ajieleze na kufuta yaliomo kwenye barua hiyo. Hata hivyo Mahathir aligoma
kuondoa maneno hayo, akishikilia msimamo wake kuwa alichokisema ni ukweli.
Dk. Mahathir anaetajwa kuwa ‘mbishi’ na ‘mbabe’ aliandika
barua hiyo katika wakati ambao wakosoaji wa Serikali walikuwa wakikamatwa na
kusekwa jela.
Hata hivyo kufukuzwa kwenye vyama vyao, haukuwa mwisho wao kisiasa, Dk. Mahathir
alirejea kwenye chama mwaka 1974 kwa msaada wa watu kadhaa akiwemo Harun Idris
aliyekuwa makamu wa Rais wa UMNO.
Jambo la ajabu tena, hapo baadae Dk. Mahathir akagombea
nafasi hiyo ya Harun, mtu aliyemsaidia kurudi chamani, na kummbwaga ‘muokozi’
wake huyo.
Nae Zitto licha ya kwamba hakuwa nje kabisa ya kisiasa, baada
ya kutimuliwa, alihamia chama kingine
cha ACT Wazalendo na kugombea ubunge mwaka 2015 ambapo nae alimmbwaga
mwalimu wake, marehemu Dk. Aman Walid Kaborou.
Moja ya tofauti zao ni kuwa Dk. Mahathir ameweza kufikia
nafasi ya uwaziri mkuu, nafasi ya juu nchini Malaysia huku Zitto Kabwe akiwa
bado kwenye Ubunge.
Kwa kuwa Zitto Kabwe anamtazama Dk. Mahathir kama kioo chake
kisiasa huenda nae anatamani siku moja awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kufikia rikodi ya ‘mwalimu’ wake huyo.
Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, simu
0625592471.
No comments:
Post a Comment