Shajara ya Mwana Mzizima:
TAARABU NA UHURU WA TANGANYIKA
Mwalimu Subeti Salum Subeti (1903 - 1974) mmoja katika wapiga fidla (violin) maarufu wa Egyptian katika miaka ya 1940 |
KUPATIKANA
kwa Uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961, kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na
uhodari, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi na umahiri wa viongozi wa
vyama vya siasa wakati huo; hasa chama cha TANU kilichoongozwa na hayati Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Lakini, kwa
upande mwengine, harakati za kudai uhuru zilinogeshwa (spiced) na uwepo wa
vikundi mbalimbali vya burudani na sanaa vilivyokuwa vikihamasisha na kuwatia
hamasa wananchi kila palipokuwa pakifanyika mikutano— hususan ile ya hadhara—
kwa kutoa burudani mbalimbali zilizoleta shamrashamra, nderemo, vifijo na hoihoi.
Kwenye
mikutano ile ya wazi hapa Dar es Salaam, kabla ya kuhutubiwa na wale viongozi
waandamizi wa TANU—Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi na Nyerere—kulitanguliwa
na usomaji wa mashairi pamoja na tenzi zilizobeba ujumbe mzito kwa
waliohudhuria.
Pia, nyimbo
za kwaya zenye kusisimua zilizoimbwa kwa madaha na weledi mkubwa na bingwa wa
kwaya siku hizo, hayati Mzee Makongoro; zilibeba ujumbe mzito: Uhuru! Uhuru!
Uhuru na Umoja.
Kwa upande wa
ngoma alikuwapo Mzee Morris Nyunyusa (alikuwa haoni kabisa), ambaye pia alikuwa
akipata nafasi ya kupiga kwa ustadi mkubwa zile ngoma zake kumi kwa wakati
mmoja. Mmoja wa nyimbo zake ni ule mashuhuri unaopigwa kwenye Radio Tanzania
mpaka leo kuashiria kwamba ni wakati mwengine tena wa kusomewa taarifa ya
habari.
Mzee Ramadhani Mwinamila wa Unyanyembe Tabora,
pia alikuwa akihanikiza na kikundi chake cha ngoma ya kiasili ya Kinyamwezi
kilichojulikana kama ‘’Hiyari ya Moyo,’’ huku akiwa amejiviringisha na joka
kubwa ambalo hurandaranda nalo mgongoni akienda huku na kule kwa midundo ya
kiasili ya Kinyamwezi ya ‘igembe nsabo’ na ‘mipanga lolo’.
Mwamko ule;
hamasa ile; na vuguvugu lile lililosababisha maelfu kwa maelfu ya Wananchi
kufurika kwenye mikutano, ulimtisha na
kumshitua Gavana wa Kiingereza, Lord Twinning. Hakukuwa na namna nyingine bali TANU
kuipenda tu!
Kutokana na
watu wengi mno kupokea na kuelewa ujumbe, sasa ikawa ni lazima mikutano ile ifanyike
viwanjani Jangwani, kwani Mnazi Mmoja pakawa hapatoshi tena kubeba mzigo ule
mkubwa.
Nyerere wakati
fulani, alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara, hali iliyosababisha
harakati za ukombozi kudorora.
Wananchi wa
Dar es Salaam, walisononeka sana kukatishwa kwa uhondo ule wa kumsikiliza
kijana mdogo wa Kizanaki, msomi kutoka Butiama, akiwaliwaza na maneno yake
mazuri yaliyojaa lafudhi ya Kikurya, lakini yaliyobeba ujumbe mzito wenye
mazingatio na matumaini makubwa.
Mmoja wa watu
walioathirika kwa kusitishwa na kutokuwapo kwa mikutano ile, ni mama yangu
mlezi nyumbani kwetu, hayati Bi. Fatuma Kigwe, ambaye daima alikuwa akituchukua
sisi tukiwa bado vijana wadogo siku hizo— iwe Mnazi Mmoja au Jangwani— kwenda
kumsikiliza Nyerere na Titi na yale waliokuja nayo.
Mama, alikuwa
na kipaji kikubwa sana cha kuigiza sauti za watu (personification). Sasa, jioni
baada ya mikutano ile, wakati tumekusanyika kwenye mduara wa chakula cha usiku,
alikuwa akitoa burudani upya kwa kumwigiza ‘Nyerere wa Butiama’ na namna
alivyokuwa akizungumza mkutanoni.
“Nisikilizeni
… ‘babe zangu’ na ‘mame zangu’, Mkoloni Mwingereza huyu anatapatapa tu,
anatapatapa tu …ataondoka, ataondoka tu
…ataondoka atuachie nchi yetu, ndiyo…ndiyo, ni mtu mbaya sana …hana
huruma huyu hata kidogo!” Mama alikuwa akimpatia kweli kweli Mwalimu, hasa pale
alipokuwa akirudiarudia neno moja mara mbili. Hapo tulikuwa tukipata burudani
upya kumsikiliza ‘Nyerere wa Butiama’ akikonga nyoyo za Watanganyika wenzake
waliokuwa wamechoshwa na kutawaliwa.
Sasa, pamoja
na mambo mengine mengi, mbinu mpya ikabuniwa ya kumpiku Gavana Twinning na amri
yake ya kukataza mikutano: Watu wa kawaida tu, wakawa wanaandaa shughuli
majumbani mwao; hasa zile za harusi, ambapo kwa zamani, kwa mila ya watu wa Mrima,
ni kawaida Bwana na Bibi Harusi watolewe uwanjani kuonyeshwa kwa ndugu na jamaa
huku muziki wa taarabu ukitumbuiza.
Sasa, ikawa inapotokea
mtaani kuna harusi, viongozi wa chama wa eneo husika humwendea mwenye shughuli
kumtaka kutumia shughuli yake kwa kumwalika Nyerere kuja kuwa mmoja wa wageni ili
baadaye apate nafasi ya kuhutubia hafla ile. Halikuwa jambo gumu lile
kutekelezeka, kwa sababu wakati huo Nyerere alikuwa ni raia wa kawaida tu,
ambaye kuhudhuria kwake kwenye shughuli yoyote halikuwa jambo lililowahusu watu wa usalama ama
wakoloni wenyewe.
Mbinu ile, ikawa na mafanikio makubwa sana,
kwani kila fursa ilipopatikana, ilizungumzwa siasa tupu na maendeleo ya
harakati za chini kwa chini za kudai nchi yetu kutoka kwa Wazungu wale
wababaishaji kutoka Ulaya Ingereza. Vinanda na nyimbo za hamasa za taarabu pia
huchukua nafasi hiyo kuimba nyimbo za siasa tu, badala ya ‘kimasomaso mwanangu
usimwone’. Kadi mpya ziliuzwa hapo pia.
Egyptian
Musical Club, ni moja ya vikundi vikongwe vya muziki wa taarabu hapa nchini ambayo ilisheni
waimbaji wazuri na wenye vipaji haswa, pamoja na wapigaji ala mahiri sana kwa
ukanda huu wa Afrika Mashariki. Wao ndio waliofanya kazi hiyo kwa kiwango cha
juu sana. Maskani ya bendi hiyo, kwa muda mrefu yalikuwa palepale New Street
(sasa Lumumba) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mita chache tu—mkabala— na mahala
lilipokuwepo jengo la Makao Makuu ya Chama cha TANU.
Muziki wa
Taarabu asilia, asili yake ni mchanganyiko wa muziki wa Kiswahili na ule wa
Afrika Kaskazini (kwenye nchi kama Egypt, Tunisia na Morocco) uliosheheni ala
mbalimbali mithili ya Ochestra ya bendi za Muziki ya Kizungu ama kihindi
inayohusisha zaidi vinanda na ala nyingine kama vile accordion, magitaa ya bass
na rythim, udi, ghanoon, tumba na violin.
Vifaa
vyengine ni saxophone, organ, tarumbeta, piano na marimba. Ukiacha mpigaji wa
gitaa la bass na mwimbaji, wapigaji wengine wote huwa wamekaa kwenye viti vyao
wakivurumisha vinanda kwa mpangilio na uongozaji wa kiongozi wa bendi (band
master).
Mpiga violin |
Egyptian
Musical Club, ni bendi iliyoanzishwa miaka mingi nyuma mnamo karne ya 18 hivi,
jijini Dar es Salaam ikiwa moja ya uendelezaji wa utamaduni wa Mswahili wa
Mrima uliochanganyika na ujio wa walowezi wa Kiarabu kutoka nchi za Kaskazini
mwa Afrika.
Mara zote
nyimbo zake, pamoja na kubeba ujumbe, hutungwa kwa kuzingatia maadili na
utamaduni wa Mswahili wa Mwambao na lugha yake adhimu ya Kiswahili ndiyo
iliyotumika, ingawa mara chache nyimbo
hizo hupigwa kwa mahadhi ya Kihindi na Kiarabu. Ni aghlabu sana taarabu
kuimbwa kwa Kingereza ingawa wasanii wajanja wa kileo wamefanikiwa kufanya
hivyo.
Ukiacha bendi
hii ya Egyptian, bendi nyengine zilizokuwepo wakati huo jijini Dar es Salaam ni
Alwatan Musical Club na Bombay Musical Club (baadaye ikajiita Jamhuri pale uhuru
ulipopatikana). Tofauti na sasa, muziki huu siku za nyuma ulikuwa ukipigwa kwa
ajili ya kuburudisha watu na si kwa ajili ya kujipatia chochote kwa wasanii
husika kama ambavyo sasa imezoeleka.
Kule Tanga
nako kulikuwa na bendi kadhaa za muziki huu, ikiwamo Lucky Star ya mwimbaji
maarufu hayati Bi Shakila, aliyejizolea sifa kemkem hapa nyumbani na Afrika
Mashariki yote kwa sauti yake nyororo na maudhui yenye mafunzo. Habari zinasema
mbinu hii iliyokuwa ikitumika hapa Dar es Salaam kutumia taarabu kisiasa
ilifanikiwa pia kule Tanga na kwengineko.
Kule
Zanzibar, ingawa hakukuwa na marufuku yoyote kukataza wanasiasa kufanya kazi za
ukombozi, lakini pia nako taarabu ilitumika kwa kutunga nyimbo zenye maudhui ya
kudai kujitawala wenyewe miongoni mwa jamii ya Waafrika.
Mara zote
wakati wa Sikukuu za Pasaka, Wazanzibari wakati ule walishuhudia kumwona
Nyerere akihutubia kwenye kukaribisha wageni wa ‘Sports’ kulikokuwa kukifanywa
na vilabu vya mpira vya Sunderland (sasa Simba) na Yanga.
Wimbo kama,
Abeid nenda, Oya! Oya!; Tunakutuma, Oya! Oya! Ulitungwa mahsusi na Bendi ya
Culture ya Unguja kumhamasisha Abeid Karume katika safari yake ya kule kwenye
Mkutano wa Lancaster House, mjini London uliojadili mustakabali wa Zanzibar
mpya baada ya kujitawala.
Kwa muktadha
huu basi, hapana budi kwa wale wasomi watakaokuja kuandika historia sahihi ya
mapambano ya uhuru wa nchi yetu kutilia maanani jambo hili la kuwakumbuka
wapigaji vinanda wale wa Bendi ya Egyptian Musical Club. Ni ukweli ulio wazi
kabisa kwamba kwa kiasi kikubwa tu katika kipindi kile kigumu, kwa kushirikiana
na wazalendo wa kawaida tu, waliweza kupeleka mbele harakati zile.
Mara chache
hupata watu wakaitaja klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kwamba ilikuwa na mchango
mkubwa katika ukombozi wa taifa hili. Kwa kiasi fulani ni kweli maana wengi wa
wanachama wake walikuwa ni watu weusi, hivyo wakawa pia na kadi za TANU, lakini
vyovyote vile iwavyo, Yanga hawakuwa na mchango unaoikaribia au kuipiku bendi
ya Egyptian Musical Club; kwani wao walipiga na kutumbuiza kwenye shughuli
nyingi ambazo ‘Mheshimiwa’ Julius Nyerere alipata fursa ya kupenyeza maneno
yake, wanawake wakapiga vigelegele na wanaume kushangilia kwa makofi
kuchangamsha harusi na harakati za ukombozi kuzipa nguvu.
Bendi ya
Egyptian ya miaka hiyo ya 1950 na 60s, ilikuwa na wazee kama Mzee Bom Ambaroni
aliyeshirikiana na Mzee Salum Mboga na Mwalimu Subeti Salum katika upigaji wa ‘violin’. Maalim Abubakar
Mzinga yeye ghanoon na kuimba nyimbo pia.
Shamas bin
Abubakar, Hamis George, Abbas Mzee,
Saleh Mtumwa na Muhiddin Kingaru, hawa wao walikuwa waimbaji wa zile nyimbo
maarufu zilizotokea kupendwa kwa muda mrefu za: ‘’Kharusi Jambo la Kheri;’’ ‘’Kila
Mwenye Uwezo Asaidie Yatima;’’ na ‘’Umaridadi si Kufua Nguo, Bali Usafishe Wako
Moyo.’’ Nuru bint Suud na Mtumwa Rajab wao walikuwa miongoni mwa waimbaji
wanawake.
Bendi
nyengine iliyoundwa baada ya uhuru kupatikana kwa msaada mkubwa wa mwanasiasa
nguli kutoka hapa Mzizima hayati Kitwana Kondo, ilikuwa ni New Extra Musical
Club. Ikiwa na makao yake pale Mtaa wa Mafia na Livingstone jijini Dar es
Salaam, New Extra ilitumika sana katika kuhamasisha wananchi kutilia maanani suala
la kilimo kwa kutunga wimbo maarufu wa ‘Shambani Mazao Bora Shambani’. Khamis
Juma Mzinga ndiye aliyeuimba wimbo huo ambao mpaka leo unatumika na kupigwa na
Radio Tanzania linapokuja suala la Kilimo Kwanza.
Ni bahati
mbaya sana muziki huu wa Taarabu Asilia umetoweka katika medani ya muziki hapa
kwetu Tanzania Bara, kule Zanzibar ndio kwanza ‘mkoko unaalika maua’, kwani
huwaambi kitu katika kumuenzi na kumtukuza hayati Bi Kidude na Siti bint Saad
aliyekufa miongo kadhaa nyuma kabla uhuru kupatikana.
Ni sehemu
muhimu sana ya utamaduni wa Mtanzania ukiangalia kule nyuma tulikotoka. Ilikuwa
ni muziki huu wa taarabu asilia, serikali ya awamu ya kwanza ya hayati Baba wa
Taifa, iliyoutumia kwa kuwastarehesha wageni wote wakubwa wa siserikali
walioitembelea nchi yetu siku za nyuma, kwenye dhifa za chakula cha usiku
(state banquets), pale Ikulu na kwenye holi la Diamond Jubilee, Upanga.
Wageni wakubwa
wa kukumbukwa ambao walipigiwa taarabu ni
pamoja na Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkurumah wa Ghana, Kenneth
Kaunda wa Zambia, Huophet Boigny wa Corte de Voire na Chou en Lai wa Jamhuri ya
Watu wa China.
Wengine ni
Rais Tubman wa Liberia, Modibo Keita wa Mali, Ahmed Sekou Toure wa Guinea,
Houari Boumedienne wa Algeria na Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria pamoja
na wengine wengi.
Taarabu
Asilia, ilikuwa kwenye programu zote za mikutano mikuu ya Chama cha TANU na
baadaye CCM, kwa kuwaburudisha wajumbe baada ya mchoko wa mikutano.
Hivyo, kama
ulivyopotea muziki wa dansi wa kina Mbaraka Mwinshehe, Juma Kilaza, Michael
Enock – huu wa kina TX Moshi William na Muhiddin Gurumo nao unaelekea huko
huko— taarabu asilia nayo imekwenda na maji mbele ya macho yetu! Ni msiba
mkubwa.
Alamsiki!
Simu:
0715808864
No comments:
Post a Comment