Monday, 31 March 2014

NAFASI NA MUSTAKBALI WA WAISLAMU NA UISLAMU KATIKA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA



BARAZA LA KATIBA LA WAISLAMU TANZANIA
 
 
 
BISMILLAHIR RAHMAANI RRAHYIM
 
MPENDWA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
 
Mheshimiwa Rais,
 
Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh!
 
Kwa niaba la Baraza la Katiba la Waislamu Tanzania na kupitia Baraza hili, kwa niaba ya Waislamu Tanzania napenda nikushukuru kwa kuupokea waraka wetu wa pili (baada ya ule wa awali ambao pia uliupokea) na kitabu ambacho kiliambatana na waraka huu. Tunakutumia waraka ule (wa pili)na kitabu kile kwa barua pepe kwa madhumuni ya kurahisisha uwekaji kumbukumbu.
 
Waislamu tunatoa shukrani pia kwa kitendo cha ofisi yako adhimu (Ikulu) kuuona umuhimu wa uwakilishi wa Dini katika mchakato huu nyeti wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (“Sheria Kuu ya Watanzania”). Allah (S.W.) akuongoze. Ofisi yako imekumbuka nafasi ya Mola Wetu Mlezi katika uendeshaji wa maisha yetu haya ya mpito.
 
Mheshimiwa Rais, umetuteuwa Waislamu tisa (9) kuuwakilisha Ummah wa Waislamu Tanzania pamoja na kusimamia, kutetea na kupigania maslahi ya Uislamu katika mchakato huu. Tunapokumbuka maneno ya Mola Wetu Mlezi juu ya mchakato huu, damu zinatusisimka na tunapata yakini kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa, kwa hakika ni mtihani kwa kila aliyejaaliwa na Allah (S.W.) macho ya kuona. Uliotuteua na kututwisha dhima hii tumejiorodhesha hapa chini:
 
1.
SHEIKH MUSSA YUSUF KUNDECHA:  [TANZANIA BARA]
2.
UKHTI SHAMIM KHAN: [TANZANIA BARA]
3.
SHEIKH HAMID MASOUD JONGO: [TANZANIA BARA]
4.
SHEIKH HAMIS ALI TOGWA: [TANZANIA BARA]
5.
SHEIKH THABIT NOUMAN JONGO: [ZANZIBAR]
6.
SHEIKH NASSOR MOHAMED IBRAHIM: [ZANZIBAR]
7.
UKHTI FATMA MOHAMMED HASSAN: [ZANZIBAR]
8.
UKHTI YASMIN YUSUFALI ALLOO: [ZANZIBAR]
9
SHEIKH THUWENI ISSA THUWENI [ZANZIBAR]
Ummah wa Waislamu nchini ulifanya kila uliloweza kuwasilisha hoja na maoni yao kwa mtizamo wa dini yao; vile Mola Wetu Mlezi anavyotaka na kuridhia. Hata hivyo ushahidi wa kimazingira unaonesha bayana kuwa Waislamu hatukufua dafu. Sisi uliotuteua tupo Bungeni kujaribu kwa mara ya mwisho kukumbusha, matakwa na maamrisho ya Mola Wetu Mlezi juu ya mchakato huu, matakwa na maamrisho ambayo bila shaka na wewe unayajua vema. Sisi na wewe tutaulizwa na Allah (S.W.) juu ya hili Siku ambayo na wewe una yakini nayo. Bali kila nafsi ya Muislamu iliyopo katika Bunge Maalumu la Katiba ijiandae kwa hilo. Tuandae majibu yatakayomkinaisha Allah (S.W.). Sisi sote tumetamka shahada mbili, tumekula kiapo cha kumtii Bwana wa viumbe, Mwenye Nguvu na Hekima – Allah (S.W.)    
 
Tunatanguliza shukrani nyingi kwa kukubali kwako kuupokea waraka huu. Maombi yetu kwa Allah (S.W.) akuzidishie hekima, subira, moyo wenye kushukuru kwa neema za Mola Wako kwako na akujaalie kukumbuka kauli yake: “Inna lillahi wa Inna Ilayhi Raajiuun”
 
Wabillah Tawfiq,
SHEIKH MUSSA KUNDECHA
MWENYEKITI BARAZA LA KATIBA LA WAISLAMU TANZANIA
NA
MJUMBE: BUNGE MAALUM LA KATIBA
DODOMA
 
 

1 comment: