Monday, 28 April 2014

KUTOKA JAMII FORUMS 2011: PITIO LA KITABU - MAISHA NA NYAKATI ZA ABDULWAHID SYKES (1924 - 1968)

Default 

Kitabu: Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968)





Pitio la Kitabu 

Kitabu hiki kilipochapwa kwa mara ya kwanza 1998 kwa Kiingereza nchini Uingereza na kilipoanza kuzagaa katika maktaba na maduka ya vitabu mjini London yanayouza vitabu kuhusu Afrika Watanzania wengi waliokuwa Uingereza walisisimuliwa na yale yaliyokuwa ndani ya kitabu hiki. Kubwa zaidi ilikuwa kule kufunuliwa kwa mara ya kwanza kuwa kumbe TANU chimbuko lake si Julius Nyerere bali ni marehemu Abdulwahid Sykes. Hii ilikuwa habari mpya kwa wengi hasa ikizingatiwa kuwa Nyerere mwenyewe hakuwahi kumtaja Abdulwahid Sykes kama mwenzake katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Hili lilikuwa la kwanza. Kitu cha pili kilichosisimua wasomaji ni kuwa mwandishi kwa kutulia kabisa alionyesha bila woga na kutafuna maneno kuwa TANU kilikuwa chama kilichojengwa katika migongo ya Waislam. Hili alilishaijisha kwa kueleza wazalendo waliokuwa bara ambao kwa umoja wao na wengi wao wakiwa Waislam walipambana na ukoloni wa Kiingereza.


Kubwa zaidi la kusisimua ilikuwa kitabu kilieleza bila kupepesa macho au kutafuna maneno njama alizofanya Nyerere kwanza kumfuta Abdulwahid Sykes katika historia yake binafsi, TANU na katika harakati za kudai uhuru. Lakini kilichotibua sege la nyuki ni pale katika kuhitimisha kitabu mwandishi alipoweka wazi mipango ya Nyerere akishirikiana na Kanisa Katoliki baada ya uhuru kupatikana kupanga njama za kuzuia maendeleo ya Waislam. Katika kipande hiki msomaji atakutana na Mufti Sheikh Hassan bin Amir aliyekuwa mufti wa Tanganyika na Zanzibar na mwanasiasa shupavu. Msomaji ataziona juhudi za Sheikh Hassan bin Amir katika kupambana na njama za Nyerere na Kanisa Katoliki na nini kilimfika msomi huyu maarufu wa Kiislam. Kwa wakati ule Nyerere akiwa hai ilihitaji ujasiri mkubwa kwa yeyote yule kusema au kuandika hayo. 



Nakala za kitabu zilifika Tanzania na kila aliyesoma alipatwa na mshtuko mkubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na nje yake. Kitabu kiliwaudhi wapenzi wa Nyerere na wapo waliomwendea kwa kutaka afanye jambo kukomesha “uongo” wa mwandishi. Wengine hawakuamini kuwa huyo anayejiita Mohamed Said kama kweli yupo. Wengine walitaka kujua kama kweli akina Sykes na baba yao ndio waasisi wa vyama vya Waafrika katika Tanganyika katika 1929 hadi 1954 TANU ilipoasisiwa. Hii ilikuwa bahari kubwa kwa wapenzi wa Nyerere ambao wasingeweza kuogelea bila ya msaada wake Baba wa Taifa. Mawimbi ya bahari hii yalikuwa marefu na yakija kwa kasi. Juu ya haya yote Waswahili wana msemo “penye ukweli uongo hujitenga.” Nyerere asingeweza kuthubutu kukana mchango wa marehemu Abdulwahid kwake yeye binafsi na kwa TANU. Abdulwahid ndiye aliyempokoea Dar es Salaam ile ya miaka ya 1950 na akamjulisha kwa wenyeji wa mji. Wapenzi wa Nyerere hadi leo ukiwauliza Nyerere alisema nini kuhusu ukweli kuwa si yeye aliyeasisi TANU wamekuwa kimya. 



Msomi maarufu wa Chuo Kikuu cha Cambridge John Iliffe ambae ameandika sana historia ya Tanganyika alikasirishwa na msimamo wa mwandishi khasa pale aliposema kuwa inastaajabisha kuwa Illife ingawa alitegemea nyaraka za akina Sykes katika kuandika historia ya African Association inastaajabisha hakuona umuhimu wa kutaka kumhoji marehemu Abduwahid aliyekuwa katibu na rais wake kati ya 1951 hadi 1953. Akiandika pitio la kitabu hiki katika Cambridge Journal of African History Iliffe alimshambulia mwandishi katika njia ambayo haikuwa staili yake msomi mkubwa kama yeye. Iliffe alikuwa ameghadhibishwa kwa kuambiwa katika kitabu kuwa alimzuia mwanafunzi wake katika Idara ya Historia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka wa 1969, Daisy Sykes ambae alikuwa binti ya Abdulwahid asiandike maisha ya baba yake. Daisy wakati huo msichana mdogo alikuwa amekasirishwa na jinsi TANU na magazeti yake yote, “The Nationalist” chini ya uhariri wa Benjamin Mkapa na “Uhuru” yalivyoshindwa kumwandika baba yake kwa hadhi aliyostahili. Magazeti hayo yaliripoti kifo cha Abdulwahid Sykes kwa kuwa Nyerere alikwenda mazikoni. Hapakuwa na jingine. Brendon Grimshaw ambae alikuwa Mhariri Mkuu wa “The Tanganyika Standard” na akimfahamu vyema Abdulwahid ndiye aliyendika tanzia ya maana katika “Sunday News” akasema kuwa Nyerere asingelifika pale alipofika kama si kwa msaada wa Abdulwahid Sykes na ni juhudi za ukoo wa Kleist ndiyo uliowezesha watu wa Tanganyika kuwa na chama cha siasa. “The Standard” na “Sunday News” wakati ule lilikuwa gazeti huru halikuwa na hofu ya Nyerere. Hii ilikuwa mwaka 1968.



Kilipotoka kitabu hiki mwaka 1998 walikuwepo watu walioona ukweli wa kuwa historia ya TANU bado haijaandikwa na kuna baadhi ya shutuma zilizoelekezwa kwake Nyerere ni muhimu yeye mwenyewe akazijibu akiwa hai kwa faida ya jamii isijesemwa kuwa kasingiziwa, walimsubiri afe ndipo wamzushie la kumzushia. Mmoja wa kundi hili la pili alikuwa marehemu Prof. Haroub Othman. Yeye alimkabili Nyerere uso kwa macho na kumuomba atoe majibu kujibu shutuma za waandishi wawili. Kwanza ajibu shutuma za Sheikh Ali Muhsin Barwani aliiyekuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) katika kitabu chake “Conflict and Harmony in Zanzibar” na kitabu cha Mohamed Said “The Life and Times of Abdulwahid Sykes (19241968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika.” Sheikh Ali Muhsin akimtuhumu Nyerere kwa kupeleka mamluki Zanzibar kuipindua serikali ya wananchi na Mohamed Said akimtuhumu kwa chuki dhidi ya Waislam na kupotosha historia ya uhuru wa Tangnayika. Prof. Haroub alimshauri Nyerere kuwa njia nzuri ya kuiweka historia yake na uhusiano wake na Waislam sawa ni kwa yeye kuandika historia ya maisha yake. Hadi Nyerere anaingia kaburini hiili halikufanyika. 



Kitabu hiki ni muhimu kwa Waislam na wananchi wote kwa ujumla kukisoma na kuwahimiza watoto wao nao wakisome wapate kujifahamu na kufahamu changamoto za udini na chanzo chake. Ndani ya kitabu hiki mwandishi amejitahidi kukusanya mashujaa waliotupwa waliopigania uhuru wa Tanganyika hata kabla hawajasikia jina la Nyerere wala kuona sura yake, wazalendo kama Hassan Suleiman na Juma Ponda wa Dodoma. Wazalendo waliohutubia mikutano ya hadhara na kuhamasisha watu kudai uhuru hata Nyerere hawamjui kama  Bi Titi Mohamed na wengine wengi kutoka katika majimbo ya Tanganyika. Ukikianza kitabu hiki huwezi kukiweka chini hadi umefika mwisho.



Kitabu hiki kinapatikana Ibn Hazim Bookshop Mtoro na Manyema na Tanzania Publishing House, Samora Avenue.

Last edited by Mohamed Said; 13th March 2011 at 20:45.


Kichwa cha gramafoni kilichokwama kwenye sahani ya santuri HMV.
Kila kikifika kwenye kishimo kinakwama hakendi mbele kinajirudia hapo
hapo hadi aje mtu kukisogeza mbele...
Kichwa cha gramafoni ndiyo wewe na maswali yako yanayochusha.
Nami nikiona unachusha nakupuuza sikujibu.
Wenzako walikusanya magazeti ya Africa Events wakayachoma moto.
Hilo ndilo lilikuwa jibu lao.
Kanisa limejibu.
Au huna taarifa?
Soma tamko la Maaskofu la Xmas.
Ukiwa hukuliona jibu lao rudi hapa uniulize kwa adabu nitakupa jibu.
Nyerere ameandika hadi anakwenda hospitali akiandika...
Au hujui?
Saida Othman Yahya (mke wa marehemu Prof. Haroub Othman) na
Prof. Issa Shivji wanaandika hivi sasa maisha ya Nyerere.
Au na hili hujui?
Chanzo cha kazi hii ya kuandika maisha ya Nyerere ni kitabu changu na
cha Ali Muhsin ''Conflict and Harmony in Zanzibar.''
Wewe huna moja ujualo katika mawanda haya.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Historia...
Mie sitakupa jibu hebu wewe nenda pale kaulize kwa nini mko kimya sasa
mwaka wa 15 hamjaandika kitabu kujibu ''ngano'' za Mohamed Said.
Au ukipenda waulize mbona hamkufanya ''review'' ya kitabu chake?
Kimya chao hadi leo ndiyo jibu lao.
Sikukimbilia Marekani na Ulaya.
Vyuo Vikuu mtu hakimbilii.
Unaalikwa kwa sifa zako.
Au hili nalo hulijui?
Au we hapa JF ndiyo unaona umefika huna tena safari?
Ushatua mizigo yako.
Unataka kutamba kwa kuuliza swali JF...
Kwanza hebu jiangalie unavyoandika wewe na fananisha ninavyoandika...
Jitathmini mwenyewe.
''Paper'' nilizoandika na makala wala sijui hesabu zake.
Hakuna gazeti na jarida ambalo sijaandika kuanzia ''Africa Confidential'' hadi
''The Economist.''
Hakuna radio station ambayo sijafanyanayo mahojiano.
Zisizopenda kuzungumza na mimi ni hizi za hapa nyumbani.
Ni baada ya kitabu kutangazwa na ''publisher'' katika duru za kisomi na ''riviews'' kuandikwa ndipo nikaanza kutafutwa.
Sifa kubwa ya kitabu chochote cha kisomi ni kuja na habari mpya iliyokuwa haijulikani.
Habari mpya katika kitabu changu ilikuwa ''Islam and Politics in Colonial Tanganyika.''Angalia katika ''catalogue'' hiyo ndiyo ''classification'' ya kitabu changu.
Kitabu kikapata ''reviews'' mbili katika Cambridge Journal of African History.
Hapa nyumbani kitabu kikapewa ''serialisation'' tatu katika The East African.
Naamini juu ya hayo yote unajua hadhi ya The East African.
Zitafute hizo ''series'' utazipata ilikuwa December 1998.
Narudia tena kukuambia wewe peke yako huniwezi wewe njoo na wenzako 20 au na zaidi mimi nitakuwa peke yangu.
Sifanyi maskhara.
Mjikusanye kama mnavyojikusanya JF...
Wewe peke yako huniwezi.
Kuna mtu hapa jamvini alikuonya akakuambia, ''Huyu mume mkubwa humuwezi.''
Bado hujaamini?
Au ulidhania anakufanyia utani?
Utabaki hivyo hivo na hizo chuki, kejeli, choyo na husda zako.
Kama hujui maana khasa ya ''hasad'' Ritz au Zomba watakufahamisha.
Nimerudi kukata hicho kibri chako.
Nakusihi ukae kimya sitopenda Insha Allah kusemezana na wewe tena baada ya leo.


(Hili ni jibu nilimpa mmoja wa watu ''walioumizwa'' na kitabu changu ambae alinitukana na alikuwa akinibughudhi sana katika Jamii Forums).

No comments: