Monday, 28 April 2014

NI WAKATI GANI KUNA UDINI NA WAKATI GANI UDINI HAUPO?

NKAMIA KASEMA KWELI:
WAISLAMU TUZUNGUMZE NA MWENYE MBWA

Mwezi Februari 2007, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Jakaya Mrisho Kikwete alimteuwa Profesa Idris Kikula kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma yaani UDOM na Profesa Shaaban Mlacha kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho kwa upande wa Utawala na Fedha. Aidha Mhe Kikwete alimteuwa Profesa Ludovick Kinabo kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho kwa upande wa Taaluma. Viongozi hawa wakubwa watatu wamekuwa wakifanya kazi chini ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya uteuzi wao, viongozi hao walishughulikia kujenga Chuo cha UDOM ambapo ilipofika mwezi Agosti 2007, wanafunzi wapatao 5,000 walidahiliwa chuoni hapo na masomo yakaanza.

Mara tu baada ya chuo kufunguliwa, tuhuma kadhaa zenye hisia kali za kidini zilianza kuelekezwa kwenye uongozi wa Chuo na hasa kwa Profesa Kikula na Profesa Mlacha. Baadhi tu ya shutuhuma hizo ni kuwa Chuo cha UDOM kinafungwa kabisa siku za Ijumaa ili kuwapa nafasi wanafunzi waende kuswali msikitini. Kwa upande wa udahili wa wanafunzi, shutuma kali zimeelekezwa kwa MaProfesa hawa wawili kuwa wanadahili wanafunzi wa Kiislamu tu na kuwanyima Wakristo nafasi ya kusoma hapo chuoni. Shutuma hizo hazikuishia hapo. Wapo watu waliodai kuwa wanafunzi WOTE wa kike wanaosoma Chuoni hapo, bila kujali dini zao, wanalazimishwa kuvaa “Hijab”, vazi la stara kwa mabinti wa Kiislamu.

Tuhumu hizi na nyingine nyingi zimeendelea tokea chuo kianzishwe. Waislamu wamekuwa wakizipuuza tuhuma hizi kwa sababu ni UWONGO MTUPU na walidhani kuwa wanaotoa tuhuma hizi ni watu wasiojua kitu. Jambo la kushangaza na kusitusha sana ni kitendo cha Mhe Joseph Roman Selasini Shao Mbunge wa Rombo (CHADEMA) alipojiunga na kundi hilo na kutoa kauli Bungeni zilizoashiria kuwa UDOM kuna udini kwa maana ya kuwa Waislamu wanawakandamiza Wakristo.

Akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu siku ya tarehe 15 Aprili 2013, Mhe Selasini alitoa shutuma nzito dhidi ya Uongozi wa UDOM kuwa kuna kundi la wanafunzi na waalimu wa Kiislamu wanaofanya vikao vya siri na kupanga njama dhidi ya Wakristo. Kwa mapana yake, kauli ya Mhe Selasini ina maana ya kuwa ukimya unaoonyeshwa na uongozi wa juu wa UDOM kuhusu suala hili, unathibitisha kuwa uongozi wa Chuo unalijua suala hilo vizuri au unashiriki moja kwa moja katika njama hizo dhidi wa Wakristo hapo chuoni. Kauli hii inawalenga Profesa Idris Kikula na Profesa Shaaban Mlacha kwa sababu wao ndio Waislamu.

Shutuma alizozitoa Mhe Selasini ni nzito na hazifai kupuuzwa. Kwa kulijua hilo, Mhe Juma Selemani Nkamia Mbunge wa Kondoa Kusini alizingatia ushauri wa Wazaramo unaosema kuwa “akutukanae kenye pombe, nawe mjibu kwenye pombe”. Akichangia Bajeti hiyo hiyo, siku hiyo hiyo, Mhe Nkamia alisema kuwa yeye ni mwanafunzi hapo UDOM na hajawahi kusikia ubaguzi ambao Mhe Selasini anaouzungumzia. Majibu ya Mhe Nkamia yanazaa maswali kadhaa ambayo ni vyema Waislamu tukajiuliza. Hivi ni kwa nini shutuma nyingi na hasa za udini zimekuwa zikielekezwa kwenye Taasisi kubwa ambazo zinaongozwa na Waislamu? Ni kwa nini Wakristo wamekuwa na tabia ya kuamini na kutaka jamii yote iamini kuwa Muislamu akipewa nafasi ya juu ya uongozi atakuwa amepewa kwa sababu tu ya Uislamu wake na wala si sifa zake? Ni kwa nini akiwepo Muislamu zaidi ya mmoja kwenye uongozi wa juu (kama ilivyo UDOM), Wakristo wanaamini kuwa Waislamu hao wamependelewa na kuwepo kwao hapo hawatotenda haki kwa Wakristo? Kwa nini Wakristo wakiwa wengi kwenye uongozi wa juu wa Taasisi yoyote ile wanaamini kuwa hiyo ni haki yao?

Ili kupata majibu ya baadhi ya maswai haya, tuangalie Jukwaa ambalo Mhe Selasini amelitumia kutoa shutuma zake. Jukwaa alilolitumia ni Bunge. Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Waheshimiwa Wabunge walifanya uchaguzi kuchagua Mhe Spilka, Mhe Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge (Presiding Officers) Watatu. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kati ya Wenyeviti Watatu wa Bunge, mmoja lazima atoke Zanzibar. Matokeo ya uchaguzi huo ni kuwa viongozi WOTE walikuwa Wakristo! Uongozi ulikuwa kama ifuatavyo:

Spika           Anna Makinda                                                        Mkristo
Naibu Spika  Job Ndugai                                                             Mkristo
Mwenyekiti   Jenister Mhagama                                                  Mkristo
Mwenyekiti   George Simbachawenye   (baadae Mhe Zungu)        Mkristo
Mwenyekiti   Sylvester Massale Mabumba (Dole, Zanzibar)            Mkristo

La kushangaza ni kuwa hata pale alipotakiwa Mbunge kutoka Zanzibar ili awe Mwenyekiti wa Bunge basi nafasi hiyo pia akapewa Mkristo! Ikumbukwe kuwa Mhe Mabumba ndio Mbunge PEKEE kutoka Zanzibar ambaye ni Mkristo! Kwa upande wa Menejimenti, Katibu wa Bunge (Dr Thomas Kashilila) na Wakuu wa Idara WOTE ni Wakristo! Je, Mhe Joseph Selasini analionaje hili?

Pamoja na unyeti wa Taasisi hii, hata mara moja Waislamu hawajalalamika kuwa Bunge linaongozwa na Wakristo watupu. Wao wamekuwa wakiamini kuwa waliochanguliwa wamechaguliwa kwa uwezo  wao (na sio vinginevyo) na kwamba watatekeleza majukumu yao kwa haki na kwa faida ya taifa. Sasa kwa nini mantiki hiyo hiyo haitumiki pale ambapo Waislamu wamechaguliwa au wameteuliwa kuongoza Taasisi yoyote ya Umma? Kwa nini kuwepo na mashaka kuwa wamepata nafasi hizo kwa sababu tu ya dini zao?

Kama Mhe Selasini anaona kuwepo kwa Profesa Kikula na Profesa Mlacha UDOM ni udini, je ameangalia uongozi wa juu wa Vyuo Vikuu vyote vya Umma hapa nchini? Kwa Mhe Selasini na wale wanaoitakia mema Tanzania, wafahamu kuwa jumla ya Vyuo Vikuu vya Umma na Taasisi za Umma za Elimu ya Juu zinazotoa shahada kwa kiwango cha Digirii hapa nchini ni 19. Ukijumuisha na Tume ya Vyuo Vikuu yaani Tanzania Commission for Universities (TCU) ambaye ndiye Mdhibiti, jumla zinakuwa Taasisi 20. Kati ya Vyuo/Taasisi hizo 20, Wakuu wa Vyuo/Taasisi 17 ni Wakristo na Wakuu 3 tu ndio Waislamu. Kiuwiano hii ni sawa na 85% Wakristo na Waislamu ni 15% tu kama inavyoonekana hapa:

1. Chuo Kikuu cha Dodoma         Prof. Idris Kikula                        Muislamu
2. Chuo Kikuu cha Ardhi             Prof. Idris Mshoro                      Muislamu
3. Taasisi ya Ustawi wa Jamii    Dr. Abuu Mvungi                        Muislamu
4. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam         Prof. Rwekaza Mukandala          Mkristo
5. Chuo Kikuu cha Sokoine                  Prof. Gerald C Monela                Mkristo
6. Chuo Kikuu cha Tiba M’bili     Prof. Kaaya                               Mkristo
7. Chuo Kikuu cha Mzumbe        Prof. Joseph Kuzilwa                 Mkristo
8. Chuo Kikuu Huria                            Prof. Tolly Mbwette                             Mkristo
9. Chuo Kikuu cha Tek. Mbeya    Prof. Joseph Msambichaka         Mkristo
10. Chuo Kikuu cha Katavi                    ???????                                         Mkrsto
11. Chuo cha Moshi MUCCOBS    Prof. Faustine K Bee                  Mkristo
12. Chuo cha Elimu DSM (DUCE) Prof. Mfinanga                          Mkristo
13. Chuo cha Elimu Mkwawa      Prof. Amandina Lihamba           Mkristo       
14. Chuo cha IFM                        Prof. Godwin Mjema                  Mkristo
15. Taasisi ya Nelson Mandela    Prof. Burton Mwamila                Mkristo
16. Taasisi ya Teknolojia DSM    Prof. Kandoro                            Mkristo
17. Chuo cha Biashara (CBE)                Prof. Mjema                              Mkristo
18. Chuo cha Mwalimu Nyerere            Prof. Magotti                                      Mkristo
19. Chuo cha Uhasibu Arusha               Prof. Johannes Monyo               Mkristo
20. Tume ya Vyuo Vikuu                      Prof. Sifune Mchome                  Mkristo
                  
Nadhani wengi watakumbuka kuwa mwaka jana wakati Rais Kikwete ameteuwa wajumbe wa Tume ya Katiba, Bwana Edwin Mtei aliandika kwenye jamiiforums kupinga uteuzi ule kwa madai kuwa wajumbe wengi ni Waislamu. Katika kutetea hoja yake, mzee Mtei amedai kuwa katika utendaji wa kazi si rahisi mtu akaweza kujizuia hisia ya imani (dini) yake isiingilie utendaji wake. Hivyo basi, mzee Mtei alidai kuwa kwa kuwa Tume ya katiba ina wajumbe wengi Waislamu, itakuwa rahisi kwa imani ya dini hiyo kupenyezwa katika Katiba mpya. Kwa kuzingatia hoja ya mze Mtei, kama uongozi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu nchini upo katika sura tuliyoionyesha hapo juu, ni dhahiri kuwa si rahisi kwa vijana wa Kiislamu kupata Elimu ya Juu na hasa ukizingatia kuwa Baraza la Mitihani limesheheni Wakristo na tokea liundwe halijapata HATA MARA MOJA kuongozwa na Mwislamu.

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kuwa Mhe Rais Kikwete anateuwa Waislamu katika nafasi nyeti za uongozi. Mifano mikubwa ambayo imekuwa ikirudiwa mara kwa mara ni Mkuu wa Polisi Saidi Mwema, Mkurugenzi wa Usalama Othman Rashid, Jaji Mkuu Mohamed Chande na Waziri wa Ulinzi Mhe Shamsi Nahodha. Wakati Wakristo wanalalamikia teuzi hizo mbalimbali ambazo zimezingatia uwezo, ujuzi na uzoefu wa Walioteuliwa, wanasahau kabisa kuwa kwa kipindi kirefu wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu Viongozi Waandamizi wa Chama na Serikali walikuwa Wakristo lakini Waislamu hawakuliona kama hilo ni tatizo. Mwaka 1996, mara tu baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu ilipoingia madarakani uongozi ulikuwa hivi:

Serikali

Benjamin William Mkapa            Rais wa Jamhuri ya Muungano             Mkristo
Fredrick T Sumaye                     Waziri Mkuu                                        Mkristo
Maokola Majogo                        Waziri wa Ulinzi                                  Mkristo
C. Apson                                   Mkurugenzi wa Usalama                      Mkristo
Harun Mahundi                          Mkuu wa Polisi                                    Mkristo
Jenerali Robert Mboma              Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi                   Mkristo

Wakristo wamesahau kuwa katika kipindi hicho Wakuu WOTE wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Waziri wa Ulinzi walikuwa Wakristo WATUPU mpaka baadae alipoteuliwa Mahita. Katika utawala wa Rais Kikwete haijatokea HATA MARA MOJA Wakuu wote wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakawa Waislamu watupu! Aidha ni vyema tukajikumbusha kuwa wakati WOTE wa utawala wa Rais Kikwete Mkuu wa Majeshi amekuwa ni Mkristo.

Chama

Benjamin William Mkapa            Mwenyekiti                                         Mkristo
John Samwel Malecela               Makamu Mwenyekiti Bara                    Mkristo
Philip Mangula                           Katibu Mkuu                                        Mkristo

Si hivyo tu, Wakristo pamoja na Mhe Selasini wamesahau kuwa katika kipindi CHOTE cha Serikali ya Awamu ya Tatu Mihimili YOTE ya dola ilikuwa inashikwa na Wakristo kama ifuatavyo:

Benjamin W Mkapa          Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   Mkristo
Pius Msekwa                    Spika wa Bunge                                            Mkristo
Francis Nyalali                 Jaji Mkuu                                                     Mkristo
Barnabas Samatta            Jaji Mkuu                                                     Mkristo

Aidha hali hiyo hiyo ilijitokeza wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Julius Nyerere wakati yeye alipokuwa Rais, Spika wa Bunge Chifu Erasto Mang’enya na Jaji Mkuu Agostino Saidi/Francis Nyalali.  La kushangaza ni kuwa kila alipokuwa Rais Mkristo Mihimili yote Mitatu wa Dola imekuwa chini ya Wakristo. Lakini haikuwahi kutokea hata mara moja wakati Rais ni Muislamu (kama ilivyokuwa wakati wa Rais Mwinyi na sasa Rais Kikwete) Mihimili ya Dola kushikwa na Waislamu watupu. Hili halijawahi kutokea hata mara moja.

Kwa kuzingatia hoja ya Mhe Selasini na wengine wenye fikra kama zake, uongozi wa UDOM ni mbovu kwani umeshindwa kudhibiti upendeleo na ukandamizaji unaofanywa na Waislamu dhidi ya Wakristo. Swali la kumuuliza Mhe Selasini je wakati Waislamu walipodhulumiwa waziwazi na Dr Joyce Ndalichako Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani kwa kufelishwa kwa makusudi kabisa mbona hatukumsikia kusimama Bungeni kuzungumzia dhulma hii? Wakati Getrude Mongella alipokula pesa Dola 200,000 za Bunge la Afrika na Serikali akakubali kulipa deni lile, mbona Mhe Selasini hakusimama Bungeni kupinga hoja hiyo? Au kwa sababu tu Ndalichako na Mongella ni Wakristo?

Wakati Dr Charles Kimei Mkurugenzi wa Benki ya CRDB anatoa maagizo kwa Mameneja wake wote wa Mikoa kuwa watoe Sadaka Kanisani (fungu la 10) kutokana na faida ambayo Benki imepata, mbona Mhe Selasini hakuhoji Bungeni wizi huu wa sehemu ya fedha za Umma (kwa sababu Serikali ina hisa 40% CRDB) zinazopelekwa Kanisani?  Au kwa sababu Dr Kimei ni Mkristo na anatoka Rombo kama yeye? Unafiki huu wa Mhe Selasini na watu wa aina yake mpaka lini?

Mwaka 1993 tumeshuhudia utiaji sahihi wa Makubaliano baina ya Serikali na Makanisa kuhusu Serikali kuwapa fedha Makanisa ili waendeshe huduma za afya katika hospitali zao ambazo zitatumika kwa wananchi pia. Waislamu walilalamikia sana utaratibu ule kwa sababu wajibu wa kutoa huduma ya afya ni wa Serikali. Hivyo basi isingekuwa vyema kwa Serikali kujivua wajibu wake na kuipa Taasisi nyingine. Mantiki ya utaratibu ule ilikuwa ni utaratibu wa muda hadi hapo Serikali itakapopata uwezo wa kujenga hospitali zake. Cha kushangaza ni kuwa kwa miaka 20 sasa tumeshuhudia namna fedha za Umma zinavyoporwa na kupelekwa Makanisani kwa kisingizio cha kuendesha hospitali teule na kwamba Serikali haina dalili ya kujenga hospitali za Umma. Ikiwa Serikali imeweza kujenga shule za Kata nchi nzima kwa chini ya miaka 2, iweje leo Serikali imeshindwa kujenga zahanati za Kata nchi nzima ili kukomesha uporaji wa mali ya Umma unaofanywa na Makanisa?

Kwa kuwa Bunge letu lipo katika kipindi cha kujadili Bajeti ya Serikali namwomba Mhe Selasini wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Afya asimame na kuhoji kwa nguvu zote tokea mwaka 1993 hadi leo Serikali imetumia kiasi gani kuhudumia hospitali za Makanisa? Ni kiasi gani zinahitajika kujenga zahanati za Kata nchi nzima? Kwa nini katika kipindi chote cha miaka 20 Serikali haikuona umuhimu wa kujenga hospitali zake na kutimiza wajibu wake kwa raia ambao wanalipa kodi? Iweje Serikali ishindwe kujenga na kuendesha hospitali hali ya kuwa ina vyanzo vingi vya mapato lakini Kanisa liweze kufanya hivyo kwa kutegemea fedha za Serikali na misaada? Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa hospitali za Umma ili kuachana na utaratibu wa sasa wa kupora fedha za Umma na kupeleka kwenye mahospitali ya Kanisa?

HITIMISHO

Kwa kuhitimisha tunapenda kumfahamisha Mhe Selasini na wenziwe wenye mawazo kama yake kuwa nchi hii imekuwa na amani kwa muda mrefu kutokana na uvumilivu wa Waislamu. Ni vyema Mhe Selasini akafahamu kuwa amani ya kweli inaenda na HAKI. Amani na haki ni sawa na watoto pacha. Tokea nchi yetu ipate uhuru Waislamu wamefanyiwa madhila makubwa sana na kumekuwa na hila nyingi sana za kuwarudisha nyuma kimaendeleo na pia kuwagombanisha na jamii. Mara kadhaa Waislamu wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya uvunjaji wa amani kama vile kusingiziwa kuingiza kontena la majambia nk. Lengo kuu ni kuionyesha jamii kuwa Waislamu ni watu wa shari. Aidha viongozi wa Kiislamu Serikalini wamekuwa wakitupiwa shutuhuma mbalimbali kama ambavyo alivyofanyiwa Profesa Kighoma Malima alipozushiwa uwongo kuwa amejenga msikiti Wizara ya Elimu nambo mengineyo.

La kushangaza ni kuwa wakati haya yote yanaendelea, Wakristo wamekuwa wakifanya vitendo vya kutishia amani waziwazi lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yao. Mfano Wakristo wametangaza kuundwa kwa Tume ya Kijeshi ya Kikristo. Jambo hili ni la hatari sana na linaacha maswali mengi bila kupata majibu. Je Tume hii ipo ndani ya Jeshi letu la Ulinzi au nje ya Jeshi? Je Makamanda wake ni nani na wanaripoti wapi? Je Amiri Jeshi Mkuu wake ni nani? nk.

Kwenye Gazeti la Mtanzania la tarehe 10 Aprili 2013 kuna mwandishi ameandika makala kuhusu vuguvugu la udini linaloendelea hivi sasa nchini. Kwa mujibu wa jina la mwandishi, inaelekea ni Mkristo. Kubwa katika aliyoyaandika ni kuwa Waislamu wanalalamika hawana uwakilishi wa kutosha kwenye vyombo vya maamuzi na Serikalini. Pamoja ya kuwa huo ndio ukweli, mwandishi anasema kuwa si vyema watu wakapewa dhamana kubwa kwa sababu tu za dini zao na kuwa na haja ya kupata uwiano mzuri wa dini hizi mbili. Kama Waislamu hawapati fursa ya kushika nyadhifa kubwa Serikalini kwa sababu ya upungufu wa sifa na hasa elimu, ni vyema basi Serikali ikaliangalia suala la kuwaendeleza Waislamu kielimu. Pamoja na Ukristo wake, mwandishi amekuwa mkweli na anaona hatari iliyopo mbele yetu ya kuliacha kundi kubwa la raia likiwa nyuma kimaedeleo wakati kundi jingine linapiga hatua. Hawa ndio wazalendo wa kweli na wanaoitakia mema Tanzania ili iwe na amani ya kudumu sio kama Mhe Selasini ambae anaongozwa na jazba na mihemuko.


Kwa upande wa Waislamu, nadhani wakati sasa umefika wa kuzungumza na mwenye mbwa. Mhe Juma Nkamia amefikisha ujumbe. Kilichobaki ni wajibu wetu kuufanyia kazi. 

1 comment:

Unknown said...

Mzee Mohamed Said kitu kimoja kinanishangaza sana hapa kwetu Tanzania.
Wakristo wanapoongelea mambo mambo yao HUO UNAKUWA SIO UDINI!
Lakini Waislamu wakifanya hivyo hivyo UNAKUWA NI UDINI.
Sijui lini Viongozi wa Watanzania watakuja kufahamu kuwa Double Standard Mwisho wake huwa mbaya sana.

Elimu unayo itoa hapa Laiti wangeifuatilia basi naimani kubwa Kungekuwa na maendelea na mshikamano mkubwa sana baina ya wananchi wa imani zote mbili.
Mungu ibariki nchi yetu.
Amen.