TAAZIA: SHEIKH MANZI
BIN SAID BIN MANZI
AMIR NA IMAM WA MASJID MWINYIMKUU AMEFARIKI
AMIR NA IMAM WA MASJID MWINYIMKUU AMEFARIKI
Sheikh Manzi bin Said bin Manzi |
Masjid Mwinyimkuu |
Siku mbili zilizopita tulitangaziwa msikitini petu Masjid Nur
Magomeni Mapipa ugonjwa wa Sheikh Manzi. Leo tarehe 4 Shaaban 1435 sawa na 3 Juni 2014 baada ya sala ya
Alfajr tukatangaziwa kifo cha sheikh wetu. Si zaidi ya juma moja nimekutana na
Sheikh Manzi Magomeni Mapipa nyakati za asubuhi. Kama kawaida yake yeye alikuwa
mtu wa kutabasamu nyakati zote. Akanisasalimia kwa bashasha yake niliyoizoea
kisha akaniambai kwa njia ya maskhara, ''Sheikh Mohamed nakusoma.'' Akacheka
sana huku anatingisha kichwa. Ajabu kwa watu wenye ilm kama ya Sheikh Manzi
kutunyanyua watu kama sisi kwa cheo adhim cha usheikh. Sheikh Manzi mimi ni
mzungumzaji wangu sana tukikutana kama kawaida lazima nimuulize ujenzi wa
Msikiti wa Mwinyimkuu ambao amekuwa akiusimamia kwa muda sasa. Akanifahamisha
kuwa msikiti unakwenda vyema. Si kama huu msikiti siujui.
Msikiti wa Mwinyimkuu ni jirani yangu sana na hupita hapo mara kwa
mara na nikiona ghorofa zinavyopanda nami hushukuru. Siku hii Sheikh Manzi
akaniambia kitu ambacho nilikuwa mie sikijui. Katika mazungumzo yetu pale nikamtaja
Sheikh Hassan bin Amir. Sheikh Manzi akanishika mkono akanambia, ''Sheikh
Mohamed, Sheikh Hassan bin Amir ndiyo mwalimu wangu.'' Nilipigwa na butwaa.
Nikamjibu Sheikh Manzi nikamwambia, ''Sheikh Manzi sasa nimekufahamu zaidi.
Nilimsikia Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo akisema tena katika darsa Msikiti wa
Mtoro kuwa, ''Mwanafunzi mwenye akili ya kawaida hendi kusoma kwa Sheikh
Hassan, ukiona mwanafunzi kabeba kitabu anakwenda kusoma kwa Sheikh Hassan bin
Amir basi jua huyo akili yake si ya kawaida.''
Kama kawaida kwa adab ya watu alim akaninilalamikia kunituliza
kuwa yeye alikuwa mwanafunzi mtoto wa kawaida tu. Lakini kwa yule aliyepata
kumsikia Sheikh Manzi akiwaidh utajua kwa hakika amesoma vizuri. Tulipoagana
nikawa sasa naendelea na safari yangu nikawa nawaza ndani ya nafsi yangu, ‘’Kumbe
ndiyo maana katika khitma ya Sheikh Ali bin Abbas miezi michache iliyopoita
alipoombwa amzungumze Sheikh Ali bin Abbas alimzungumza kwa undani kabisa,
kumbe katika miaka ile wote walikuwa wanafunzi watoto kwa Sheikh Hassan bin
Amir.’’
Majuma machache yaliyopita mie na wenzangu wa Masjid Nur tulikuwa
tunazungumza kuhusu mwezi mtukufu wa Ramadhani na matayarisho yake. Yakanijia
mazungungumzo niliyofanya mwaka jana na rafiki yetu mmoja ambae mimi ndiye
aliyenijulisha kwa Sheikh Manzi nikawa nasema, ''Mnajua jamani kwa nini Sheikh
Manzi yeye kila mwaka anatushinda katika kugawa futari kule mtaani kwake? Ni
kwa sababu yeye kwa miaka mingi ametengeneza ''data bank,'' ya wajane, yatima,
wazee na wengineo wanaohitaji futari. Sasa mimi mkinituma kwa yule rafiki yetu
kweli anatupa lakini hatupati kwa wingi kwa kuwa hatuna hesabu iliyokamilika
kwa hiyo mwaka huu kama tutakwenda tena na mikono mitupu tutapata kama kawaida
lakini Sheikh Manzi atatushinda tena yeye mipango yake itakuwa imesimama vizuri
kila mwaka.'' Ikawa sasa sote tumepwelewa hatujui tuanzie wapi kuitengeneza
hiyo ‘’data bank.’’ Ikawa tunasema, ''Hapa la kufanya ni kumwendea Sheikh Manzi
atufundishe namna ya kujenga, ''data base'' kama yake aliyotengeneza pale
Msikiti wa Mwinyimkuu.'' Kufikia umuzi huu ikawa sasa kila mtu anasema lake
kuwa kwa mwaka huu tumechelewa lakini hili tulifanyeni ni jambo zuri. Ndani ya
nafsi yangu nikawa najisemea mwenyewe, ''Lo! Mwaka huu tena Sheikh Manzi
katushinda yule rafiki yetu sijui atatuonaje maana mwaka jana tulilia ngoa,
''Bwana mbona Sheikh Manzi unamjazia na
sisi tunataka kama yeye au tumshinde.'' Rafiki yetu akawa anacheka akajibu,
''Sheikh Manzi ana orodha kamili nyinyi mnayo? Sisi ukweli wa mambo tulikuwa
tumeliendea jambo lile bila ya mipango kamili ya kisanyansi tunategemea uzoefu
tu wa mpata mpatae hatuna orodha kamili ya wahitaji. Sisi tunaomba bila kujua
nani na nani tunataka futari iwafikie, lakini Alhamdulilah hakututoa mikono
mitupu nasi tukakabidhiwa futari. Misikiti yetu ipo jirani kwa hiyo futari
ikishuka Msikiti wa Mwinyimkuu mara moja tushapata taarifa.
Kifo cha Sheikh Manzi kimewasikitisha wengi khasa sisi tuliyekuwa
tunaishi nae Magomeni. Sheikh Manzi amesimamia ujenzi wa msikiti wa Mwinyimkuu
kwa mfanikio makubwa sana na kila ukienda kuswali pale utaona ubao wake ambao
anaeleza mapato na matumizi na maendeleo ya ujenzi. Kwa kweli mtu unasikia
raha. Unaona kazi inavyokwenda na jinsi msikiti unavyopendeza. Dar es Salaam
imefiwa. Shughuli gani utamkosa Sheikh Manzi na akiombwa azungumze kila mtu
atatoka pale si kama alivyokuja. Allah aiweke roho ya ndugu yetu mahali pema
peponi.
Amin.
Sheikh Manzi bin Said bin Manzi |
Waliokaa wa Mwisho Kulia Sheikh Manzi Bin Said bin Manzi Katika Maulid ya Mwinyimkuu 29 Mfungo Sita 1435 31 Januari 2014 |
Maulid Masjid Mwinyimkuu |
No comments:
Post a Comment