Thursday 7 August 2014

MAADHIMISHO YA MIAKA 100 VITA VYA KWANZA VYA DUNIA 1914 - 1918 : SHAJARA ZA LANCE CORPORAL KLEIST SYKES


Picha ya Bismini
(Askari Monument)


Ndugu msomaji,

Mwezi huu katika juma hili kulifanyika maadhimisho makubwa Uingereza kuadhimisha miaka 100 toka Vita Vya Kwanza Dunia vilipoanza Ulaya mwaka wa 1914.

Wakati ule Tanganyika ilikuwa ikitawaliwa na Wajerumani.

Kwa ajili hii basi Tanganyika ikiwa chini ya ukoloni wa Wajerumani ikajikuta iko vitani ikipigana na Waingereza.

Tanzania haikuadhimisha kuanza kwa vita hivi.
Labda serikali imeona hapakuwa na haja yoyote.

Lakini ukweli utabaki kuwa wazee wetu walipigana vita hivi na walipoteza maisha yao katika vita vile.

Baadhi ya askari hawa wa Vita Kuu ya Kwanza walikuja kuwa mti wa mgongo wa harakati ya kupigania uhuru wa Tanganyika pale vuguvugu la kuunda TANU lilipoanza mwaka 1950.

Mzalendo maarufu katika harakati hizo za kudai uhuru kutoka kwa Waingereza na alishirika katika kuunda TANU alikuwa Schneider Plantan.

Katika askari waliopigana vita vile vya kwanza kutoka Tanganyika katika jeshi la Wajerumani alikuwa Kleist Sykes.

Kwa miaka mingi sana Kleist Sykes hajaacha kunishangaza kila ninapopitia maisha yake.

Ndugu msomaji natayarisha maandishi aliyoacha Kleist kuhusu Vita Kuu Vya Kwanza pale aliponyanyua kalamu kuandika kuhusu maisha yake na ndani ya maelezo hayo akaeleza jinsi Tanganyika ilivyoingia vitani, vita ambavyo alipigana kikosi kimoja na ndugu yake, Schneider Plantan dhidi ya Waingereza.

Tafadhali fuatilia ukurasa huu.



Jeshi la Wajerumani Tanganyika wakikota mzinga.
Nyuma ni askari wa Kijeruamni na mbele yao wakivuta mzinga
ni askari wa Kiafrika


General Paul Emil von Lettow-Vorbeck surrendering his forces to the British at Abercon (present-day Mbala) in Northern Rhodesia.

Ndugu msomaji,
Picha zote nilizobandika hapa nimezinyambua kutoka katika mtandao.

Picha hiyo hapo juu ya Paul Emil von Lettow - Vorbeck imechorwa na Mtanzania lakini kwa bahati mbaya sana jina lake halikuonyeshwa popote hata hivyo picha hii ipo Makumbusho ya Taifa.

Katika vita vile Kleist Sykes alikuwa ndiye mpambe wa Vorbeck.

Hapo chini ndivyo nilivyomwandika Kleist Sykes katika Vita Vya Kwanza Vya Dunia.


Vita Vya Kwanza Vya Dunia 1914- 1918

Miezi michache kabla vita haijaanza Ujerumani ilimteua Lettow-von Vorbeck kama Kamanda wa Majeshi ya Ulinzi ya Ujerumani katika Tanganyika. Askari wa zamani Waafrika waliopigana chini yake, pamoja na Kleist wanamkumbuka kwa mapenzi kama mtu mwema na askari shujaa. Kleist aliingizwa ndani ya jeshi la Wajerumani tarehe 13 November 1906 akiwa kijana mdogo sana wa umri miaka kumi na mbili na akapigana katika vita Vya Kwanza Vya Dunia (1914 - 1918). Katika jeshi Kleist alipata mafunzo ya mawasiliano. Baada ya miezi mitatu alihamishwa na kupelekwa Bataliani ya Pili kama karani katika Makao Makuu ya Jeshi Dar es Salaam. Alibakia hapo hadi mwaka 1914. Vita vilipoanza, bataliani ya Kleist iliondoka Ukonga ikaelekea Mwakijembe, Tanga ambako kulikuwa na mashambulizi kutoka majeshi ya Waingereza kupitia mpaka wa Kenya. Katika bataliani hiyo alikuwapo Schneider, mtoto wa Affande Plantan.

Kleist alikuwa anazungumza Kijerumani na juu ya yote hayo alikuwa vilevile mtoto wa Affande Plantan, kiongozi wa askari wa Kizulu katika utawala wa Wajerumani. Kwa ajili hii Kleist alipewa heshima ya pekee na akapewa nafasi kuwa mpambe wa von Lettow Vorbeck. Kumshuhudia kijana wa Kiafrika katika sare ya jeshi la Kijerumani akiongea Kijerumani huku anatembea nyuma ya von Lettow-Vorbeck, Mkuu wa Majeshi ya Wajerumani Tanganyika, bila shaka kuliwavutia wengi, hata Wajerumani wenyewe. Hii ilikuwa nafasi hasa iliyostahili mtoto wa askari ambae baba yake aliwasaidia Wajerumani kuiteka Tanganyika. Kama mpambe kazi yaje ilikuwa kushughulikia mambo yote ya Kamanda Mkuu. Alikuwa na jukumu la kuangalia chakula na usafi wa sare za von Lettow-Vorbeck, pamoja na mahitaji yake mengine. Alikuwa ndiye mtu wa kwanza Lettow-Vorbeck kukutananae asubuhi na wa mwisho kabla hajalala. Ilikuwa kazi yenye kumpa hadhi, mamlaka na heshima mbele ya askari wenzake. Utanashati wa Kleist katika mavazi na nidhamu yake katika maisha yake ya kawaida tu, yalitokana na kipindi hiki alichokuwa jeshini. Inaaminika kuwa hata ile hulka yake ya kuweka shajara na kuandika kumbukumbu muhimu ya mambo yake, yanatokana na uzoefu aliopata katika kipindi hiki akiwa jeshini. Inasemekana hii ndiyo miaka ambayo ilijenga silka na maisha ya Kleist.

Shajara zake za vita ni kielelezo binafsi kuhusu kampeni za Wajerumani na Waingereza wakati wa Vita Kuu Vya Kwanza. Shajara hizo zinaeleza kwa ukamilifu hali ya mambo yalivyokuwa kwa askari wa Kiafrika katika mapambano waliyoshiriki dhidi ya Waingereza. Kupitia maandishi ya Kleist unaweza ukaelewa ile chuki ambayo Waarabu walikuwanayo dhidi ya Wajerumani. Pambano la Kleist la kwanza dhidi ya Waarabu waliokuwa washirika wa Waingereza lilikuwa katika sehemu moja ijulikanayo kama Mwele Juu karibu ya Tanga.

Mbinu ya Lettow Vorbeck ilikuwa kuvuka mpaka wa Tanganyika na  Kenya ili kukata mawasilano ya reli kati ya Mombasa na Kisumu. Reli hii ilikuwa jirani na mpaka wa Tanganyika. Ilikuwa mwendo wa siku chache kuifikia reli hii na kuikata Kenya na njia yake kuu kutoka Mombasa. Lakini jeshi la wanamaji wa Kiingereza lilikuwa Mombasa kwa hiyo bandari ya Mombasa ilikuwa imesalimika na manowari za Kijerumani. Ilikuwa wakati bataliani ya Kleist ipo Korogwe, mji uliopo maili chache kutoka Tanga, katika kijiji kiitwacho Semanya ndipo Kleist alipopokea habari kuwa Affande Plantan, baba yake Schneider na mlezi wake amefariki Dar es Salaam. Plantan alikuwa amekufa kwa homa ya matumbo tarehe 11 December 1914. Wajerumani walisimamisha vita kwa siku saba kwa heshima ya Affande Plantan. Wajerumani hawakuwa wezi wa fadhila walitambua kuwa alikuwa Affande Plantan waliekujanae kutoka Msumbiji kuja kuiteka Tanganyika. Alistahili kila aina ya heshima aliyostahili askari shujaa, hata kama alikuwa mamluki. Baada ya hapo Kleist na kamapani yake walielekea Tanga ambako kulikuwa  makao makuu ya jeshi la Wajerumani wakati wa vita. Hapo hakukaa kwa muda mrefu kwa kuwa ilibidi kuomba likizo kurudi Dar es Salaam kumuangalia mama yake aliyekuwa mgonjwa. Alikaa Dar es Salaam kwa siku kumi akimuuguza mama yake kisha akarejea Tanga na akapewa kuongoza askari wanane katika divisheni ya kampani. Tarehe 24 December, 1915 kamapani yake iliamuriwa kwenda Mwakijembe na kisha Mwele Ndogo kuipokea 4th Reserve Company.

Waarabu walichukua nafasi hii ya msahambulizi ya Waingereza dhidi ya Wajerumani kulipiza kisasi dhidi yao. Waarabu waliungana na Waingereza kuwatimua Wajerumani Tanganyika. Bado baadhi yao walikuwa na kumbukumbu ya kitendo cha kikatili cha Wajeruani kwa shujaa wao Abushiri ambae walimnyonga mwaka 1889. Historia ikajirudia upya; Kleist na Schneider waliingia katika mapigano Mwele Ndogo dhidi ya adui wa zamani wa baba yao na adui wa Wajerumani - Waarabu. Mapambano haya yalifanyika siku ya mkesha wa Krismasi mwaka wa 1915 katika sehemu ile ile ambayo Sykes Mbuwane na Affande Plantan mamluki wa Kizulu waliteremka kwenye meli kuja kuwaongezea nguvu Wajerumani waliokuwa wakipigana na Waarabu na machifu wenyeji. Kwa saa kumi kuanzia alfajir hadi muda mchache kabla ya jua kuchwa, Wajerumani walibanwa katika mashambulizi makali. Kleist akapandishwa cheo na kuwa Lance Corporal kwa mchango wake katika pambano lile. Siku mbili baada ya pambano hilo Kleist na kampani yake waliamuriwa kwenda Kahe. Kleist Alibakia Kahe kwa mwezi mmoja kisha wakapata amri ya kwenda Voi,Kenya mji uliopo mpakani. Wakati wakiwa njiani kuelekea Voi, Kleist akaugua na ikabidi arudishwe Mombo, mji uliokuwa na mbu wengi kwa ajili ya mto uliokuwa unakatiza hapo mjini. Kleist alibaki akiugua hapo Mombo hospitalini kwa miezi miwili. Kutoka Mombo akaelekea Handeni. Mwezi Aprili 1916 habari zikamfikia bado akiwa katika uwanja wa mapambano kuwa mama yake amefariki dunia.

Mwaka wa 1916 Jeshi la Kiingereza lilikuja kuungwa mkono na askari kutoka Afrika ya Kusini walioshuka na meli Mombasa. Chini ya uongozi wa Jenerali Smuts walivuka mpaka wakaingia Tanganyika kupitia Namanga na Taveta. Haukupita muda mrefu mji wa Moshi ukatekwa. Batalioni ya Kleist ikawa sasa inarudi nyuma kuelekea Dodoma kulipokuwa na boma la Wajerumani. Si tu kuwa kikosi cha Kleist kilikuwa kinaandamwa na majeshi ya Waingereza, vikosi vya Wabelgiji navyo vilikuwa  vimevuka mpaka kutoka Belgian Congo na kuingia Tanganyika. Wabelgiji waliteka Kigoma, Ujiji na Tabora. Mambo yalikuwa yamewachachia Wajerumani. Afya ya Kleist kwa wakati ule ikawa mbaya sana. Alifanyiwa uchunguzi Morogoro na akaonekana hawezi kuendelea kuitumikia katika kampeni yake. Afya yake haikumruhusu kupigana vita na ikabidi aachwe nyuma Mahenge wakati wenzake wakikimbia huku wakifukuzwa na adui. Kampani ya Kleist ilikwenda Chenene ambako walipambana kwa bunduki na vikosi vya Afrika ya Kusini kwa saa mbili. Kampani ile ikakimbilia Gode Gode, wakiponea chupu chupu. Kleist akakamatwa mateka mwezi Septemba 1917. Von Lettow Vorbeck mwishowe alifanikiwa kuvuka reli ya kati akavuka mpaka na kuingia Msumbiji, wakati huo ikijulikana kama Portuguese East Africa, akanusurika kutekwa yeye na askari wake. Kwa askari wa Kizulu hii ikawa ni nusra kwao kwa kuwa walikuwa wamerudishwa nyumbani.

Wakati von Lettow Vorbeck amefanikiwa kuponyoka kukamatwa, mpambe wake Kleist alitekwa na jeshi la Wabelgiji na wao wakamkabidhi kwa Waingereza. Waingereza walimtia Kleist kifungoni katika kambi ya mateka wa vita.  Askari waliokuwa mateka pamoja na wagonjwa walichukuliwa na Waingereza na kutiwa kwenye kambi iliyokuwapo Kilosa. Kleist alikubali ukweli kuwa sasa yeye amepoteza hadhi yake kama askari, ni mateka, kwa hiyo akawa anasubiri hatima yake. Alibakia ndani yake kambi ile na yeye mwenyewe anaeleza katika kumbukumbu zake kuwa hakuwa na kinyongo chochote kwa maadui zake. Kleist aliweza hata kufanya urafiki na maadui zake ambao walikuwa wamemtia kifungoni.  Kutokana na hali yake ya afya, Kleist hakuweza kufanya kazi zote za sulubu kama ilivyo desturi kwa wafungwa. Hali yake ya afya haikuwa inaonyesha dalili zozote za kupata nafuu, Kleist aliachiwa mwaka 1917 kwa hisia labda akiwa nje ya kambi, afya yake itarudi.  Mwezi Novemba 1918 vita vikaisha huko Ulaya.

(Kutoka,  ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968)...''  











Displaying ABDULWAHID SYKES BOOK COVER

Kitabu kwa lugha ya Kiingereza na tafasiri yake kwa Kiswahili Vitakuwa Madukani
Hivi Karibuni. Kitabu Cha Kiingereza ni Toleo la Pili na Cha Kiswahili ni Toleo la Tatu


Itaendelea In Sha Allah...

No comments: