Mashujaa
wa Uhuru Waliosahaulika
Na
Alhaj Abdallah Tambaza
KATIKA taifa lolote duniani,
kuna watu huwa wanaenziwa, wanatukuzwa na kutajwatajwa, kama namna ya kukumbuka
michango yao katika uhai wa taifa husika, hata kama hawakuwahi kuwa viongozi wa
juu. Kwa mfano, leo hii huwezi ukazungumzia taifa la India bila kugusa habari
za kina Nehru na Mahatma Gandhi. Hali kadhalika, huwezi kuzungumza habari za
Malawi, bila kuwataja akina Kanyama Chiume, Kamuzu Banda, na Yatuta Chizisa.Vivyo
hivyo, historia ya Kenya, haiwi sawa usipowataja
akina Deedan Kimathi, Kungu Karumba, Bildad Kagia, Njenga Karume, Jaramogi
Oginga, Tom Mboya, Mbiyu Koinange na
Ronald Ngala wa chama cha KADU.Wamarekani nao wanao watu wao waliowafanyia
mambo makubwa mno siku za mwanzo za uhai wao. Mwaka 1776, kule Philadelphia waliketi kwenye chumba
chenye joto kali sana na kuandaa mikakati ya kujitangazia uhuru Julai 4, 1776. Wamarekani
wanawaita watu hao, ‘the framers of Independence’ (waliobuni na kuandaa mipango
ya Uhuru). Majina ya Jefferson, Hamilton, Madison, Washington na Lincoln
yanapatikana kwenye mitaa ya miji yote, katika kila jimbo la Marekani ili
kudumisha kumbukumbu, kuenzi na kufundisha vizazi umuhimu wa watu hao.
Abdallah Tambaza |
Hapa kwetu hali haiko hivyo.
Mashujaa wetu wanabakia kuwa Mwalimu Nyerere peke yake na watu wachache sana
ambao viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wamewateua.Kwa hivyo basi, wakati huu
tukiadhimisha kumbukumbu ya miaka 53 ya Uhuru wa taifa letu, ni vizuri basi,
pamoja na mambo mengine, tukawakumbuka watu ambao nchi imewasahau na kuwaweka
kando (marginalized) ambapo pengine kama si wao historia ya nchi yetu
ingeandikwa kwa namna nyingine. Orodha yao ni ndefu sana, na kwa kweli siyo
kusudio la makala haya kuwaorodhesha wote hapa chini, lakini tujiulize inakuwaje
leo hii watu kama John Rupia, Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe Tambaza, Zuberi
Mtemvu, Haidar Mwinyimvua, Dossa Aziz na Mshume Kiyate wawe ni watu wa kawaida
tu kwetu?
Katika siku za mwanzo za
harakati za kudai uhuru, chama cha TAA na baadaye TANU hakikuwa na fedha za
kujiendesha kufanikisha shughuli zake kubwa na ndogo za kila siku. Katika
kufanya hayo, chama kiliwategemea watu wachache ambao walikuwa na uwezo wa
kifedha kwa wakati huo. Miongoni mwa watu hao ni Mzee John Rupia, Dossa Aziz,
Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Haidar Mwinyimvua pamoja na
familia ya kina Sykes. Hawa wote kwa wakati huo walikuwa ni Waafrika wazalendo
wenye kumiliki mali kama mashamba, majumba na biashara mbalimbali.
Pamoja na kazi nyingine ngumu
walizozifanya usiku na mchana, mabwana wakubwa hawa walijitolea mali zao nyingi
sana kwa ajili ya harakati za kupigania uhuru bila kujali kama watapata hasara
ama kufilisika kwa kufanya hivyo. Mzee Haidar Mwinyimvua alikuwa akiishi Wadigo Street Kisutu, jijini Dar es Salaam, jirani na mahala alipozaliwa mwandishi
huyu. Mzee Haidar alikuwa fundi cherehani lakini pia alimiliki majumba (landlord)
yaliyotapakaa jijini Dar es Salaam wakati huo. Alikuwa pia Mwenyekiti wa Baraza
la Wazee wa TANU kwenye miaka ya 50. Habari zinasema alipata kuuza nyumba yake
na fedha kuzipeleka katika harakati za ukombozi wa taifa hili kutoka minyororo
ya ukoloni. Mzee Haidar, alikuwa na watoto wasiopungua 12 hivi waliohitaji
kula, kulala na kusoma; lakini kwa mapenzi ya nchi hii na kuuchukia ukoloni,
aliona bora awalaze njaa wanawe lakini nchi yetu iwe huru. Mtoto mkubwa wa Mzee
Haidar ni Sheikh Ahmed Haidar, Imam Mkuu wa Msikiti wa Mwinyikheri pale Kisutu,
Dar es Salaam.
Mmoja wa Waafrika waliokuwa na
pesa nyingi kabla ya Uhuru ni Mzee John Rupia. Huyu alimiliki mashamba jijini
Dar es Salaam pamoja na nyumba kadhaa, ikiwamo ya ghorofa (Rupia Building) pale
mtaa wa Kitchwele (sasa Uhuru street). Huyu alikuwamo tokea TAA na wakati TANU
ilipoanzishwa alikuwa Makamu wa Rais. John Rupia alitoa fedha zake nyingi sana
kwa chama kama vile kilikuwa cha kwake binafsi na Julius Nyerere ni mfanyakazi
tu. Alimnunulia suti na kumkatia tiketi ya ndege Nyerere kwenda UNO kuelezea
azma ya Watanganyika kutaka kujitawala wenyewe. Fedha nyingine za kufanikisha
safari zilitolewa na kina Dossa na Sykes. Mzee Mwinjuma Mwinyikambi na Jumbe
Tambaza hawa ni babu zangu katika ukoo wetu. Jumbe Tambaza anakuwa binamu ya
babu yangu mzaa baba. Kwa hiyo nawafahamu vizuri sana wazee hawa wa Kimashomvi.
TANU likuwa ni wao na wao ni TANU. Hawa wazee wawili walikuwa na nafasi za
kudumu (permanent seats) katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya TANU siku hizo;
siyo kwa kupigiwa kura na mtu, bali kwa heshima na nyadhifa zao tu.
Mzee Mwinjuma alilitoa bure
shamba lake lote la inayojulikana Kinondoni kwa Mwinjuma kwa TANU, kama zawadi
yake ya uhuru pale ulipopatikana mwaka 1961. Vivyo hivyo kwa Mzee Tambaza; yeye
alitoa sehemu kubwa ya shamba lake pale Upanga kwa Tambaza, iwe sehemu ya
kuzikia Waafrika bure kwani wakati huo makaburi ya Kisutu walikuwa wanazikwa
watu wenye asili ya Kiarabu tu. Zamani haikuwa rahisi ‘mwenzangu mimi’ kuzikwa
pale kama ilivyo sasa. Fedha zake nyingi nyingine alizitumia kwa kazi ya TANU. Kama
hiyo haitoshi, mahala ilipojengwa hospitali
kubwa ya Waafrika pale Muhimbili—Wazungu walitengewa European Hospital (sasa
Ocean Road) na Wahindi, Hindu Mandal— ilitolewa na Jumbe Tambaza mwaka 1957 tukiwa
bado tunatawaliwa na kufa ovyo kwa kukosa tiba bora.
Mshume Kiyate, yeye pamoja na
mambo mengine, alichukua jukumu la kumlisha Nyerere kila siku akipeleka kapu
kubwa lililosheni kila aina ya chakula nyumbani kwa Mwalimu pale Magomeni, ili
kazi ya kutafuta riziki isimwondoe Nyerere kwenye kufikiria kazi za chama. Aliifanya
kazi hiyo kwa muda wote wa kudai uhuru na mpaka mwaka 1961 ulipopatikana, alitaka
kuendelea kumpelekea Nyerere chakula pale Ikulu, lakini Nyerere akamwambia
‘Mzee Mshume sasa basi tena pumzika’. (Rejea kitabu cha Maisha na Nyakati za
Abdulwahid Sykes cha Mohamed Said). Alipokufa hakuna mtu yeyote aliyejua
miongoni mwa wakuu wa nchi na maziko yake yalikuwa ya kawaida tu pale Mtaa wa
Matumbi, jirani na maeneo ya Faya, Kariakoo, nyumbani kwa mdogo wake Mzee Maguno. Kwa kulipa fadhila
na kuonyesha shukrani zake, kwa kipindi fulani, Nyerere alikuwa anamlea pale
kwake Msasani, mjukuu wa Mzee Mshume aitwaye Mwinyi Kiyate, baada ya babake na
babu kufariki.
![]() |
Kushoto Mohamed Jumbe Tambaza na Kulia ni Mshume Kiyate |
Siku hiyo gari ya Dossa
ilikwenda mpaka mahala iliposimama ndege (apron) na ‘kumbeba’ Nyerere mpaka mjini akipungia watu mkono huku
gari likisukumwa kwa wimbo maarufu wa “baba kabwela Uno” (yaani kwa Kizaramo
baba karudi UNO). Dossa Azizi alikufa na kuzikwa mpweke shambani kwake Mlandizi.
Nyerere hakuhudhuria wala chama alichokitumikia katika nyadhifa mbalimbali
wakati wa uhai wake pia hakikutuma mwakilishi. Inasikitisha sana. Pengine ndio
sababu za misukosuko na kutoelewana kunakotokea nchini sasa hivi ni matokeo ya laana
hizo. Siku zote Mungu huwa hawaachi hivi hivi madhalimu; anazo namna zake nyingi
za kutoa adhabu hapahapa.
![]() |
Waziri Dossa Aziz Kama Alivyokuwa 1955 |
Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu,
ni mwanaharakati mwengine wa kupigiwa mfano katika mapambano ya ukombozi wa
nchi hii kutoka katika madhila na makucha ya ukoloni wa ‘Ulaya Ingereza’. Kwa
ujinga tu na sababu wanazozifahamu wao, watu wengi wamekuwa wakiuchukulia
utawala wa Kingereza kama vile halikuwa jambo baya—wazungu walitutesa sana!
Ma-PC na Ma-DC walikuwa wanachapa watu wazima viboko. Utawala wa
Kiingereza haukuwa na jema lolote kwetu kwani ulituweka sisi Waafrika— wenye
nchi hii— katika daraja la chini kabisa kibaguzi. Ukoloni uliwatukuza Wazungu
kama daraja la kwanza; Wahindi daraja la pili; Waarabu daraja la tatu na Weusi
wote daraja la mwisho; kwenye masomo, tiba, ajira na makazi.
Mzee Saleh Abdallah Tambaza, ni
babu ya mwandishi huyu, ambaye pamoja na kaka yake Mzee Kidato Tambaza,
walikuwa wanamiliki ardhi kubwa sana
Upanga, jijini Dar es Salaam wakati wa ukoloni na kabla ya hapo. Eneo
hilo lilianzia Selander Bridge, mahala walipokuwa wakivua samaki, Palm Beach,
Sea View na kuzunguka mpaka maeneo ya Mahakama ya Kisutu, maeneo ya Diamond
Jubilee, makao makuu ya Jeshi na Hospitali ya Tumaini. Miembe mikubwa ya miaka
mingi, minazi, mikungu na mizambarau ambayo ipo bado hadi sasa ni kielelezo
tosha (classic example) ya dhulma ya wazungu. Wakoloni waliwataka babu zangu
wahame hapo kwa sababu tu hapafai kukaa mtu mweusi tuwaachie Wahindi upepo wa
bahari. Wazungu nao peke yao wakawa wanaburudika kule Oysterbay (sasa Masaki).
Ukionekana huko mtu mweusi ni mpishi au mkata majani (house nigger).
Babu alichachamaa sana, akapambana
sana na DC wa kizungu wakati huo; lakini alishindwa na shamba likaenda kwa
malipo kiduchu waliotaka watawala kutoa. Mzee Saleh alihamia eneo la Mabibo
External kumalizia uhai wake, lakini alipokufa mwaka 1949 alirudishwa kuzikwa
Upanga, na kaburi lake liko pale ulipojengwa Msikiti wa Maamur sasa hivi. Msomaji,
hebu tafakari kidogo inawezekana vipi leo hii mtu akamsahau Zuberi Mtemvu (baba
wa Abbas Mtemvu, mbunge wa sasa wa Temeke), mtu ambaye ndiye aliyekuwa katibu
mkuu wa kwanza wa TANU? Vipi historia ishindwe kumtaja mtu huyu ambaye baada ya
kuhitilafiana na Nyerere alianzisha chama chake cha siasa – African National
Congress—kwa kazi ileile ya kudai uhuru? Vipi asitajwe, wakati chama chake
kilimweka kwenye kinyang’anyiro (ballot box) cha kugombea urais mwaka 1962 na
kama angeshinda ndiye angekuwa rais wetu?
Mtemvu alipata kura nyingi sana
kwenye majimbo ya Bukoba na kuipiku TANU. Alizunguka sehemu nyingi duniani,
hasa nchi za kisoshalisti wakati huo na kupendwa kuliko chama cha TANU. Makao
makuu ya ANC yalikuwa mtaa wa Nyamwezi, Kariakoo Dsm, kwenye ghorofa iliyoitwa
Kiruka Building ya Mzee Nassor Kiruka. Uhuru
haukuletwa na Nyerere na TANU tu. TANU ilikuwa na ushawishi mkubwa tu na hivyo
ikashinda uchaguzi kwa kupata viti vingi, lakini vyama vilikuwa zaidi ya TANU
kwenye mapambano. Pamoja na Congress cha Zuberi Mtemvu, kilikuwapo chama
maarufu cha UTP— United Tanganyika Party— kilichoongozwa na Sheikh Hussein Juma
na nduguye Hassan Juma. Kilikuwapo pia chama cha AMNUT—All Muslim National
Union of Tanganyika, nacho kiliweka mgombea. Hawa wote ni mashujaa wetu, kwani
walifanya kazi ileile ya kudai uhuru. Mtume Muhammad (S.A.W) alipopewa utume
kule Mecca, alipata taabu sana. Hakuweza peke yake kukubalika kirahisi bila ya
msaada wa masahaba akina Abubakar, Omar, Ali, Bilal ibn Rabah, Othman bin Afan
na wengine wengi.
Sasa kwa kuthamini michango ya
watu hao, Mtume Muhammad na dini kwa ujumla inaenzi na kuthamini mchango wa
akina Abubakar kupita kiasi mpaka imefika mahala wametabiriwa pepo kabla ya
kufa wakiwa bado wapo hapa hapa duniani. Bilal Ibn Rabah alikuwa mtumwa wakati
fulani lakini alikuwa akiteswa sana na bwana wake aliyekuwa kafiri kwa sababu
ya kuukubali kwake Uislamu. Ilikuwa ni Sayiddna Abubakar aliyemgomboa kwa
kitika kikubwa cha fedha ili awe huru.
Hadithi imepokewa kwamba kwa kitendo hicho Sayiddna Omar
alimwita Abubakar hivi:
“Abubakar Sayiddna; attaka Sayidduna!!”
Maana yake ni kwamba Abubakar ni mtukufu wetu, lakini leo
ametuokolea mtukufu wetu mwingine!
Sasa nyie Watanzania, watu
waliokufanyieni hayo vipi muwaone kama vile wa kawaida? Tena mnapinga na
kukataa kwamba hawakufanya chochote. Ni wizi wa fadhila huo. Historia ya
Tanganyika kabla ya uhuru inakuwa si sahihi kama hukuwataja au kutambua mchango
wa familia ya kina Sykes.Mzee Kliest Abdallah Sykes, alizaliwa Pangani mkoani
Tanga mnamo mwaka 1894 wakati wa utawala wa Ujerumani hapa Tanganyika. Mzee
Kliest Sykes alikuja kuwa askari shujaa wa Wazungu wa Kijerumani ambao walikuwa
na kambi kubwa ya kivita eneo hilo.Katika uhai wake alijaaliwa watoto watatu wa
kiume akiwamo Abdulwahid, Ali na Abbas.
Alifariki dunia jijini Dar es Salaam mwaka 1949 baada ya kuwa amefanya kazi
kubwa ya kuanzisha 1929, taasisi ya African Association iliyounganisha Waafrika
wote. Historia ya nchi yetu itakuwa imechakachuliwa kama haitazungumza mchango
wa mzee huyu pamoja na ule wa watoto wake katika mapambano dhidi ya ukoloni.
AA ndiyo iliyokuja kuzaa chama
cha TAA na baadaye TANU. Jina la TANU lilibuniwa na Abdulwahid na Ali Sykes
vitani Burma mwaka 1945 wakiwa na usongo wa kuja kuanzisha mapambano ya
kukomboa watakaporudi nyumbani.Katika
kitabu chake kuhusu maisha ya Abdulwahid Sykes, mwanahistoria maarufu nchini
Alhaj Mohamed Said anaandika:
“…ilikuwa hapa siku ya mkesha wa Krismas 1945 Abdul na
askari wengine pamoja na mdogo wake Ali na James Mkande, walifanya makubaliano
ya kuunda chama cha siasa kudai uhuru wa Tanganyika mara tu watakaporudi
nyumbani baada ya vita.’’ (Angalia Said Uk. 62).
![]() |
Abdulwahid Sykes Kama Alivyokuwa 1960 |
Mwaka 1954 wakati TANU
ilipoasisiwa, Ali Sykes ndiye aliyebuni na kugharimia ununuzi wa kadi za chama
kipya yeye mwenyewe akiwa na kadi namba 2. Kakake Abdulwahid namba 3, Dossa
namba 4 na kadi namba 1 ikiwa ya Nyerere. Vipi taifa makini linaweza kuwafanyia
hiyana watu wa namna hiyo? Watu waliohatarisha uhai wao ili leo ili sisi tuwe
huru; haiingi akilini kwamba nchi inaweza kuwasahau kiasi hiki. Mimi bado
nakumbuka, pale mchana ule wa Jumamosi, Oktoba 12, 1968 mji wa Mzizima
ulipozizima baada ya habari kuzagaa kwamba Abdul Sykes ameaga dunia. Alikuwa
mtu mashuhuri sana jijini Dar es Salaam, si tu kwamba alikuwa mwanasiasa lakini
kipenzi na rafiki wa watu wengi akiwemo baba wa mwandishi huyu. Alizikwa na
maelfu ya watu Jumapili Oktoba 13, katika makaburi ya Kisutu katika mazishi
ambayo yalihudhuriwa pia na Mwalimu Nyerere na waasisi wengine wa taifa hili.
Lakini Waswahili wana msemo
kwamba ‘maji hufuata mkondo’. Mtoto wa Abdulwahid, aitwaye Kliest Sykes damu
ilipomchemka mwanzoni mwa mwaka 2000 alikuja kuwa Meya wa Jiji la Dar es
Salaam.Moja ya kazi zake za kujivunia ni kubuni huu mradi mkubwa kabisa wa
mabasi ya mwendo kasi BRT kwa jiji la DSM ambao viongozi kadhaa sasa
wanajinasibisha (attributed) nao. Balozi Abbas Sykes ni mmoja kati ya waasisi
wa TAA baadaye TANU. Huyu ni mdogo wa mwisho wa Abdulwahid Sykes lakini kwa
namna ya pekee kabisa alikuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa
nchi yetu. Mara baada ya Tanganyika kuwa huru 1961, Abbas Sykes, akiwa kijana
mdogo wakati huo, ndiye aliyekuwa Provincial Commissioner wa kwanza mwafrika wa
Jimbo la Dar es Salaam. Katika kipindi
kirefu sana Balozi Sykes aliiwakilisha Tanzania nchini Canada, Italia na Sudan
mpaka alipostaafu kazi hiyo kwa umri. Kwa hiyo Watanzania tufungue ukurasa mpya
tuiandike tena historia ya mapambano ya ukombozi wetu kama
inavyostahili—tunachekwa.
![]() |
Kushoto Kwenda Kulia: Hussein Shebe, Abdallah Awadh, Balozi Abbas Sykes, Mohamed Said na Kleist Sykes Msikiti wa Kipata Katika Hawli ya Marehemu Ally Sykes 2014 |
Simu : 0715 808 864/0784 808 864. Barua pepe:
atambaza@yahoo.com
No comments:
Post a Comment