Monday, 5 January 2015

JUHUDI YA SHEIKH PONDA ISSA PONDA KUNUSURU MALI ZA WAKFU ZA WAISLAM WA TANZANIA

Sheikh Ponda akiwa kwenye pingu mahakamani

Historia ya Waislam wa Tanzania itakapokuja kuandikwa jina la Sheikh Ponda Issa Ponda litaunganishwa na jina la Mufti Sheikh Hassan bin Amir kwa kitu kimoja nacho ni ardhi ya Chang'ombe Dar es Salaam ambako Waislam chini ya uongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) walikusudia kujenga Chuo Kikuu mwaka wa 1968. Katika uwanja huu ndipo Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere akishuhudiwa na Tewa Said Tewa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir aliweka jiwe la msingi la chuo hicho. Chuo hakikujengwa na EAMWS ikapigwa marufuku na serikali. Mambo hayakuishia hapo. Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa na kufukuzwa nchini akarudishwa ''kwao'' Zanzibar. Serikali ikaunda BAKWATA na Chuo Kikuu cha Waislam hakikujengwa. Nini kilisababisha nakma hii? Waliokuwa karibu na Sheikh Hassan bin Amir wanasema katika siku zake za mwisho kila alipotajiwa ule mradi wa chuo kikuu alikuwa akilia na kusema ilikuwa hamu yake kujenga chuo Kikuu kama Azhar ya Misri na akifika hapo alikuwa akibubujikwa na machozi. Wakati ule Sheikh Hassan bin alikuwa na miaka zaidi ya 90 na aliishi na simanzi hizi hadi alipokufa mwaka 1979.

Sheikh Hassan bin Amir aliyeshika bakora

Kwa takriban miaka 40 Waislam wakawa wanapata taarifa kuwa ule uwanja ambao ulikuwa wakfu ulikuwa ukimegwa na viongozi wa BAKWATA na kuuziwa wafanyabiashara wakubwa matajiri.Waislam hawakuwa na uwezo wa kuzuia dhulma hii ikawa wao ni kulalamika tu na kila miaka ilivyozidi kwenda ndivyo kiwanja kile cha wakfu kilivyozidi kumegwa, kukatwa na kuuzwa. Ghafla siku moja Waislam wakasikia kupitia vyombo vya habari kuwa Sheikh Ponda na baadhi ya vijana wa Kiislam wamekwenda kwenye kiwanja cha wakfu na kutangaza kuwa wamekirudisha kwa wenyewe Waislam na watajenga Msikiti utakaoitwa Masjid Hassan bin Amir ikiwa ni kumbukumbu kwa mwanazuoni huyu wa Kiislam, mwanasiasa na mmoja katika watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Ujenzi wa Masjid Hassan bin Amir ulianza ukiwa ni msikiti wa muda ''temporary,'' na Waislam walianza kuswali hapo. Haukupita muda askari waliwavamia wale vijana usiku wakakamatwa pamoja na Sheikh Ponda na kufunguliwa mashtaka. Waislam wale walipigwa na askari waliingia hadi Markaz pale na kuvunja baahi ya computer kwa kile kilichoelezwa kuwasaka wahalifu.

Askari wakikabiliana na Waislam nje ya mahakama Morogoro


Hivi sasa karibu mwaka mmoja Sheikh Ponda kanyimwa dhamana na yuko rumande akisubiri kesi yake. Leo hii mwandishi alihudhuria kesi ya Sheikh Ponda kwenye Mahakama ya Mkoa Morogoro. Bahati mbaya palitokea purukushani kati ya Waislam na polisi. Wakati Sheikh Ponda analetwa mahakamani akisindikizwa na ulinzi mkali, alipofika langoni mmoja kati ya Waislam kama ilivyo ada alipiga ''takbir'' kwa sauti kubwa, ''Takbir.'' Waislam waliitika kwa sauti kubwa ya kishindo, ''Allahu Akbar.'' Inaelekea hili halikuwafurahisha polisi na askari mmoja akaagizwa amkamate yule aliyepiga ''takbir,'' hapo ndipo Waislam kwa umoja wao wakamkabili yule askari na vurugu ikatokea. Hata hivyo viongozi wa polisi alizungumza na Amir wa Waislam na utulivu ukarejea ingawa yule askari aliumia halikadhalika yule Muislam aliyekuwa akamatwe. Wote walikwenda kupata huduma ya kwanza hospitali ya mkoa. Lakini iko siku wote watasimama mbele ya Allah Hakimu Muadilifu na wao wataulizwa ni nani aliyestahili kuwa rumande akifungwa pingu na kuteseka yeye na familia yake. Ni yule aliyedhulumu haki ya Allah au yule aliyetaka kuinusuru?

Kwenye Uwanja wa Changombe Mwaka 1968 Mufti Sheikh Hassan bin Amir
Akimkaribisha Mwalimu Julius Nyerere Kuweka Jiwe la Msingi la
 Chuo Kikuu Cha Waislam Kati yao ni Tewa Said Tewa

Sheikh Ponda Akizungumza na Mawakili Wake Kulia ni Advocate Nassor






Kushoto ni Mzee Bilali Rehani Waikela Muasisi wa TANU Tabora 1955,
Katibu wa EAMWS Jimbo la Magharibi na Inaaminika ni Yeye Peke Yake
Aliyehai Aneijua Historia Yote ya Kiwanja Cha Chang'ombe na Ujenzi wa Chuo
Kikuu Cha Waislam.






Sheikh Ponda Akipelekwa Mahabusi Mwanzo wa Kesi Dar es Salaam

Waislam Wakiondoka Mahakamani kwa Maandamano




Picha ya Mwaka 2012 ya Sheikh Ponda Akisimama Kuomba Dua Mbele ya
Kibla Cha Msikiti wa Kichangani, Magomeni Dar es Salaam Kabla ya 
Kuongoza Maandamano ya Waislam Kupinga Dhulma Dhidi ya Wanafunzi 
Waislam Katika Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)




No comments: