Tuesday, 6 January 2015

TAMSYA TAARIFA FUPI YA UTENDAJI KAZI KWA MWAKA WA 2014


TAMSYA
TAARIFA FUPI YA UTENDAJI KAZI I
DARA YA HABARI NA MAHUSIANO YA JAMII 2014 (HQ)

1.      Dondoo
2.    Historia fupi ya TAMSYA na malengo yake
3.     Changamoto za JKT na ufumbuzi wake
4.    Changamoto za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu
5.     Fursa za udhamini wa Masomo na Jitihada za Tamsya (scholarship)
6.     Kadhia ya Wizara ya Nishati na Madini,fursa zitakazopatikana na jitihada za TAMSYA
7.     Ripoti hii imeambatanishwa na ripoti fupi ya kongamano la kimataifa lilofanyika Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM)
8.     Changamoto ya kuondolewa masomo ya Arabic na Islamic Knowledge
9.     Jitihada za kuanzishwa Blog ya TAMSYA
10.            Mabadiliko ya Elimu yaliyofanyika na fursa zilizopo
11.   Changamoto ya kupokwa fikra ya Jihad, Mitaala na Ziara Matawini

Kwa jina la Allah (SW) Mwingi wa Rehema na Mwenye kurehemu, Allah ambaye huneemesha ndogo ndogo na neema kubwa kwa wanaomshukuru na wanaomkufuru.

Ifuatayo ni ripoti fupi ya utendaji kazi ya mwaka 2014,kabkla ya kuanza na ripoti ni vema tukajikumbusha, historia fupi ya TAMSYA na malengo yake.
Jumuiya ya wanafunzi na vijana wa Kiislamu ilianzishwa rasmi mwaka (1993). Hapo awali jumuiya ikiafaamika kwa jina la TAMSA yaani Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu Tanzania. Tamsya ni jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu  inayojitegemea  na kushirikiana na vijana wote wa Tanzania. Wanachama wa Tamsya wapo wanachama wa asili na wanachama wa heshima. Jumuiya inasimamia wanafunzi wote kuanzia ngazi ya shule za awali, shule za misingi, sekondari,vyuo vya kati na vyuo vikuu. Madrasa na shule zote zinazosomesha dini ni matawi ya Tamsya. Jumuiya ya Tamsya imepata usajili wa kudumu kutoka serikalini kupitia Wizara ya Mambo ya ndani tarehe 13 mwezi wa 10 mwaka 2010,kwa namba ya usajili S.A 17021 na kutambulika rasmi Tanzania Bara na Visiwani kisheria. Quran na Sunnah za Mtume Muhammad (SAW) ndiyo muongozo wa jumuiya yetu ya Tamsya.

MALENGO YA JUMUIYA YA WANAFUNZI NA VIJANA WA KIISLAMU TANZANIA (TAMSYA)

1.      Kusambaza na kutoa elimu sahihi ya Uislamu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
2.    Kuwajengea uwezo wanafunzi na vijana katika kupambana dhidi ya umaskini, maradhi, ujinga na mmomonyoko wa maadili.
3.     Kuwaongezea utambuzi wanafunzi wa Kiislamu na vijana na kutoa ufumbuzi sahihi dhidi ya matatizo mbalimbali ya kijamii.
4.    Kuendeleza udugu wa Kiislamu na ushirikiano kwa kushirikiana na taasisi zingine zenye malengo sawa na Tamsya.
5.     Kusimamia, kulinda na  kutetea haki za wanafunzi Waislamu na vijana wa Kiislamu Tanzania.
6.     Kuendesha na kusimamia miradi mbalimbalikama huduma za kijamii na kumiliki mali zinazoamishika na zisizoamishika.
7.     Kujitolea katika kazi mbalimbali za kijamii zenye maaslahi na wanafunzi Waislamu, vijana na jamii kwa ujumla.
8.     Kuwasaidia wanafunzi wa Kiislamu na vijana kujenga tabia njema za Kiislamu, maadili kwa kupitia mafundisho ya kiroho, kimwili, kiakili na kijamii.

MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZINAUZOIKUMBA JUMUIYA YA WANAFUNZI NA VIJANA WA KIISLAMU TANZANIA

Ifahamike wazi kuwa Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa Kiislamu si kitu cha mtu mmoja au mali ya kikundi cha watu wachache, Jumuiya ni mali ya Waislamu wote wa kike na  wa kiume. Ndiyo maana mara kwa mara huwa tukisisitiza motto wetu usemao ‘’Tamsya is I and You’’ yaani Tamsya ni mimi na wewe hivyo basi kwa kuunganisha mikono yetu kwa pamoja na nguvu zetu kwa pamoja kuanzia matawi ya wilaya, mikoa mpaka ngazi ya taifa ndipo tunapoweza kupiga hatua na kuweza kuyafikia malengo tuliyojiwekea. Kama ilivyo ada hakuna jumuiya au taasisi isiyokuwa na changamoto hivyo basi na Tamsya nayo ina changamoto mbili tatu:

1.      Jumuiya inakabiliwa na changamoto ya kiuchumi katika kuyaendea malengo mbalimbali iliyojiwekea kama kutekeleza na kukamilisha miradi iliyoanzishwa kwa wakati, kufanya ziara za mara kwa mara ili kuwafikia walengwa moja kwa moja kulingana na changamoto hii kuwa kubwa  ndipo Tamsya ikaamua kuanzisha ‘’Tamsya fund raising proposal’’ ili kukusanya pesa za kutosha na kuweza kutekeleza maazimio ya Mkutano Mkuu ya kila mwaka na kutekeleza mipango mikakati tuliyojiwekea.
2.    Jumuiya inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wanajumuiya kutokuifahamu vyema jumuiya yao.

3.     Jumuiya inakabiliwa na changamoto ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Ieleweke wazi kwamba Tamsya haipingi suala la kurejeshwa mafunzo ya JKT tangu yaliposimama miaka ya 1990’s na kurejeshwa mwaka 2013 kwa sasa mafunzo hayo ni lazima kwa walimu wa ngazi ya cheti, stashahada na wanafunzi waliohitimu kidato cha sita. Tamsya inapinga mfumo wa mafunzo ya JKT unavyoendeshwa kwa kuwanyima vijana uhuru wao wa kuabudu hususani watoto wa kike ambao tuna taarifa za kutosha za kila kambi juu ya mavazi wanayovaa, vitendo vya ukikwaji wa haki za kibinadamu na mmonyoko wa maadili. Tamsya bado inaendelea kulipigania suala hili hatua ya awali iliyochukuliwa ni kuandaa ripoti kwa kila kambi itakayobainisha faida, hasara na changamoto zinazowakabili vijana kwa kila kambi, pili ni kuwashirikisha wadau hususani wazazi katika kuliendea jambo jambo hili kwani ni la kijamii zaidi na mpaka sasa tuko mbioni kukutana na waziri mwenye dhamana ili kujadiliana nae kwa pamoja ili kuweza kupunguza au kuondosha kabisa baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana katika mafunzo yao.

SUALA LA JKT NA UNYETI WAKE

Changamoto kubwa iliyowakumba vijana waliohudhuria mafunzo ya JKT mwaka 2014 ziko baadhi ya kambi ambazo Idara ya Habari imefanya jitihada ya kukusanya ripoti zifuatazo ni baadhi ya kambi zilizokuwa na changamoto kubwa Kambi ya MAFINGA-IRINGA, KAMBI YA BULOMBOLA KIGOMA,KAMBI YA MARAMBA JKT,KAMBI YA MGAMBO JKT- TANGA,KAMBI YA MSANGE JKT-TABORA,KAMBI YA RUVU JKT NA NYINGINEZO.

Changamoto kubwa ilyowakumba vijana katika kambi zilizooorodheshwa hapo juu, ni suala zima la ukaguzi wa kuwakagua vijana kama wameathirika na vitendo vya ushoga au usagaji. Tunazo taarifa za ndani kuhusiana na ukiukwaji wa haki za kibinadamu juu ya zoezi hili kwa namna lilivyoendeshwa na kuratibiwa kwani vijana hulazimika kuvua nguo zote na kubaki uchi wa nyama kama walivyozaliwa ili wakaguliwe na madaktari wa kijeshi ilhali wakiwa wamechutama kibaya zaidi ziko baadhi ya kambi kama kambi ya MAFINGA-IRINGA ambazo watoto wa kike w3alikaguliwa na madaktari wa kiume, ambae alikuwa akiwashika sehemu zao za siri na kuwatomasa matiti pasi na woga, hili ni jambo lisilovumilika hata kidogo. Zoezi hili huchochea vitendo vya uzinzi na wengine kufikiwa kubakwa kama taarifa tuliyopokea kutoka kambi ya BULOMBOLA ambayo mpaka sasa kesi ya mwanafunzi aliyebakwa na afande mkufunzi ipo katika Mahakama ya Kijeshi na hukoleza vitendo vingi vya utovu wa nidhamu ambayo ni kinyume na maadili ya kijeshi.  Ziko baadhi ya kambi imefikia hali baadhi ya wakufunzi huwapa mazoezi makali makuruta pindi wanapokataliwa na baadhi ya wasichana au kukosa kabisa wakulala nae, Lugha za matusi, kutokujali hali za makuruta pindi wanapougua na wengine kufikia kufariki. Tamsya ina taarifa za vijana wanne waliofariki kutokana mafunzo yanayoendelea kwa ujumla. Kwa namna mafunzo haya yanavyoratibiwa ni wazi kuwa shabaha ya serikali ya kuwajengea vijana uzalendo haitafikiwa ila ni kwa kiwango kidogo. Idara ya Habari inakamilisha ripoti ya sehemu ya pili kuhusu faida, madhara na changamoto za suala la JKT kwa ngazi zote.

CHANGAMOTO YA MIKOPO KWA ELIMU YA JUU
Jumuiya inakabiliwa na ukosefu wa fedha katika kuwawezesha vijana. Kwa mfano mwaka wa masomo 2013/2014 tangu bodi ya mikopo itaangaze kwamba ina uwezo wa kuwapa mikopo wanafunzi 38,000 na wengine watafute njia mbadala za kuweza kujisomesha, changamoto hii ni kubwa na uko uwezekano mkubwa vijana waliopata kuchaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini wameshindwa  kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa mkopo. Changamoto hiyo imeambata pia na tatizo la mikopo hiyo kuwa na asilimia 6% ya riba kwenye mikopo ya vyuo vikuu jambo ambalo limeendelea kulalamikiwa na wadau na wengine kufikia hatua ya kuacha masomo lakini Tamsya imefanya jitihada kubwa katika kulipigania hili kwa kuwaandikia barua bodi ya mikopo ili iweze kutoa ufafanuzi juu ya tatizo hili la riba ingawa majibu ya Bodi ya Mikopo yalikuwa ni ya kiufundi  zaidi, kwamba hiyo asilimia 6% ni ‘’retention fee’’ yaani ni tozo na siyo riba. Tamsya imekwenda mbali zaidi kwa kuwashirikisha maulamaa wa Kiislamu wakiwepo HAY-YATU-LI –ULAMAA ili kutoa fatwah juu ya kadhia hii na In Sha Allah tutaisambaza fatwah hiyo hivi karibuni. Sambamba na hilo Tamsya iko katika kufanya jitihada za dhati kuwashirikisha wadau ili kuweza kuratibu na kuwa na mfuko wetu utakaotuwezesha kuwapa mikopo vijana isiyokuwa na riba ili kuwawezesha kuweza kutekeleza masomo yao katika fani mbalimbali ikiwepo masomo ya Udaktari, Uchumi, Biashara, Sheria na Utawala. Jitihada zilizofanywa na Idara ya Habari ni kuiunganisha Tamsya na Taasisi iliyosajiliwa ambayo ina lengo la kuwawezesha vijana kwa kuwapa msaada kwa wale walioshindwa kujisomesha, Taasisi hiyo huitwa NEB (Nitasoma Education Bridge). Bado jitihada zinaendelea kufanyika In Sha Allah na tunatarajia kuanzia Mwaka wa masomo ujao jitihada hizi zitazaa matunda.

FURSA ZA UDHAMINI WA MASOMO NA JITIHADA ZA TAMSYA

Tamsya imefanikiwa kutengeneza mtandao nzuri na wadau mbalimbali wanaosimamia udhamini wa masomo ndani na nje ya nchi kama tulivyowahi kueleza siku za nyuma ‘’scholarship’’ zimegawanyika katika makundi matatu:

1.      Scholarship zinazotolewa na watu binafsi
2.    Asasi za kidini
3.     Serikali

TAMSYA ilifanikiwa kupata scholarship takriban 200 kupitia shirika la JICA kwa ngazi ya shahada ya pili, ambazo nafasi hizo zilitolewa na muhisani mmoja aliyeko masomoni nchini Japan, sambamba na hilo TAMSYA ilifanikiwa kupata nafasi 5 za vijana kwenda kusoma Sudan. Pia Tamsya imefanikiwa kutengeneza mahusiano mazuri na mratibu wa scholarship za vyuo vya China Bwana Abbas. Yapo matarajio makubwa ya kupata scholarship nyingine kwa inatake ya mwezi wa Januari na Septemba kwa ngazi zote na fani mbalimbali ikiwepo fani ya Mafuta na Gesi. Udhamini wa masomo hayo umegawanyika katika makundi mawili yaani ‘’ Full  Scholarship” na ‘’Partial Scholarship. ’’

KADHIA YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI NA FURSA ZINAZOTARAJIWA KUPATIKANA

Ripoti hii imeambatanishwa na barua iliyoandikwa na TAMSYA kwenda Wizara ya Nishati ya Madini, Ikulu na Tume ya Maadili ya Viongozi baada ya kutolewa majina ya wanafunzi waliopata udhamini wa masomo nchini China Katika fani ya Mafuta na Gesi kupitia Serikali ya China ambao wote walikuwa ni Wakristo. Tunaipongeza TAMSYA kusimama kidete na kuwatetea vijana wa Kiislam ambapo vijana 5 walifanikiwa kuongezwa kwenda kufanya Shahada ya Uzamili na Uzamivu nchini China. Sambamba na hilo Waziri mwenye dhamana PROF. Sospeter Muhongo alitoa taarifa ya kwamba kupitia ziara walioifanya hivi karibuni yeye na Mheshimiwa Rais wamefanikiwa kupata scholarship 200, hivyo basi serikali itakapotangaza nafasi hizo vijana waombe.

CHANGAMOTO YA KUONDOLEWA MASOMO YA ARABIC NA ISLAMIC KNOWELDGE

Tamsya imefanya jitihada mbalimbali kupitia Idara ya Habari kuhudhuria vikao 20 vIilivyofanyika Tampro na Baraza Kuu. Vikao hivyo vilivyoandaliwa na Baraza Kuu na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, juu ya kujadili kuondoshwa masomo ya Arabic na Islamic Knowledge. Masomo haya yameondoshwa katika kuhesabu ‘’Agregate Points’’ kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka huu. Mabadiliko haya yalikuwa ni ya ghafla mno Tamsya kushirikiana na taasisi nyingine ikiwepo Tampro na Baraza Kuu kuandika barua kwenda Wizara ya Elimu na kwenda kwa Kamishna wa Elimu. Majibu ya Wizara ni kwamba mpaka sasa wanaendelea kukusanya maoni juu ya mabadiliko ya tahasusi na michepuo. Tunaipongeza Tampro kwa jitihada zake za kukusanya maoni. Sambamba na hilo tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wadau walioshiriki kutoa maoni ya kuboresha tahasusi na michepuo kupitia TENMET (Tanzania Education Network au Mtandao wa Elimu Tanzania) akiwepo Amiri Ust. Mohamed Wage, Ust Msafiri Mpendu, Ust Mpinga na wengineo Allah awlipe kila la kheri.

KUANZISHA BLOG YA TAMSYA

Alhamdulillah Idara ya habari imefanikiwa kuanzisha blog ya TAMSYA kwa anuani ya www.tamsyablog.org ili kuweza kusambaza taarifa mbalimbali kama habari picha fursa za elimu, kadhia mbalimbali zinzowakumba vijana mashuleni, Idara ya Wanawake bado blog hii hajaanza kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kusokena kwa nyaraka mbalimbali ambazo zipo katika mfumo wa softcopy, kuhama kwa Katibu Mkuu wa Idara ya Habari Kutoka Dar-es-Salaam kwenda Arusha lakini bado ziko jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuimarisha Blog hiyo ambayo  ina link ya online Library,pamoja na blog nyingine ikiwepo blog ya mwanahistoria bobezi Mohamed Said. Bado mpaka sasa ziko kadhia mbalimbali zinazowakumba wanafunzi mashuleni kwa kukosa haki ya kuabudu kama kuvaa Hijab,kutekeleza sala, kukosa vipindi vya dini na wengine kufukuzwa kwa sbabu zisizokuwa rasmi kama ilivyotoke kwa vijana wa Ndanda High School, Mbekenyera Secondary School, Ifunda na shule nyinginezo. Matukio haya yanahitajika kurushwa hewani katika mitandao ya kijamii ili yafahamike na kutafuta ufumbuzi wake. Changamoto ya mwisho ni kutokuwa na takwimu sahihi za wanachama wa Tamsya hususani wanafunzi ndio maana Tamasya imeandaa mpango kabambe wa usajili kufanya ’’Centrallazation’’ ya wanafunzi na kupata takwimu sahihi za idadi kamili ya Wanachama.

MABADILIKO YA KIELIMU, MIFUMO, FURSA NA CHANGAMOTO YA KIMAADILI

1.      Mabadiliko mbalimbali yamefanyika ya kielimu yamefanyika mwaka huu mengi haykuhusisha wadau wa elimu mojamoja
2.    Mabadiliko ya mfumo wa usahihishaji
3.     Mabadiliko ya mihula.
4.    Mabadiliko ya madaraja
5.     Mabadiliko ya michepuo na tahasusi na kuondoshwa Dkt.Joyce Ndalichako.
6.     Kutokuhesabiwa Masomo ya dini na somo la lugha ya Kiarabu.
7.     Kufutwa kwa mfumo wa ‘’Equivalent’’ kwa upande wa masomo ya dini.

IDARA YA HABARI IMEBAANI MIFUMO INAYOWEZA KUWAKWAMUA VIJANA KUZIFIKIA NDOTO ZAO KIMASOMO

Mifumo yenyewe tutaianisha kwa kifupi kama ifuatavyo:

1.      Mfumo wa RPL(Recognition of Prior Learning)
2.    Mfumo wa EDEXCEL NA Cambridge (kutumia mitaala ya nje)
3.     Mfumo wa Foundation, NABE, NACTE.
4.    Mfumo wa VETA (Vocational Educational Training).
5.     Mfumo wa “Equivalent”
6.     Mfumo unaotumiwa na Chuo Kikuu cha St. Joseph  (5 years dergree program).
7. Mifumo ya mitaala ya nje, Pen Foster na program nyinginezo kama Home Schooling ambazo kwa nchini kwetu program hii ni ‘’haramu.’’

WITO
Idara ya Habari inapenda kutoa wito kwa Maamiri wa Mikoa na Wilaya kupitia taarifa mbalimbali zinazotolewa kwenye tovuti zifuaatazo:

 1.      Tovuti ya Wizara ya Wizara ya Elimu
2.    Tovuti ya Baraza la Mitihani
3.     Tovuti ya TCU
4.    Tovuti ya Wizara ya Kazi na Ajira
5.     Tovuti ya Wizara ya Fedha

Hii itasaidia kujua mabadiliko mbalimbali ambayo yana athari kubwa kwa mustakabali wa maisha ya wanafunzi.

CHANGAMOTO YA MMONYOKO WA MAADILI

Ripoti iliyotolewa na Mradi wa “Prepare” walioshirikana na Idara ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Muhimbili ambayo ilikiita ‘’pilot’’ ilikuwa ni Dar-es-Salaam kwa Mkoa wa Kinondoni. Ambapo asilimia 65% ya wanafunzi wa shule za misingi walibainika kujihusisha na ngono, wakati asilimi 6.5% wamejihusisha na ngono kinyume na maumbile, asilimia 32% wamekwishafanya ngono bila ya kutumia kinga. Dhahiri shahiri ya kwamba hali ya mmonyoko wa maadili inaonyesha wazi kuwa hali inatisha zaidi na kukithiri kwa wimbi la “ushoga” kwa wanafunzi. Takwimu za matokeo ya mwaka huu zinakuonyesha ya kwamba mikoa yenye idadi kubwa ya Waislamu ndiyo waathirika wakubwa.



REJEA MATOKEO YA DARASA LA SABA YA MWAKA HUU

Jumla ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mitihani walikuwa 808,085 lakini waliofanya walikuwa ni 792,122. Wavulana wanongoza kwa kuchaguliwa zaidi kwa idadi ya 219,964 (asilimia 92%) na wasichana idadi ya 218,996 (asilimia 97.2) ukirejea kitabu cha ‘’Basic Education Stastics in Tanzania,’’ utaona mikoa yenye idadi kubwa ya Waislamu kuwa kiwango cha chini cha ufaulu.

MWISHO
Idara ya Habari imefanikiwa kusimamia semina mbalimbali zilizofanywa na Tamsya Taifa kwa kushirikiana na TAMSYA Mkoa wa Dar-es-Salaam kuwasaidia wanafunzi katika udahili wa vyuo viku na board ya mikopo, kushiriki kwenye mahafali mballimbali Mkoa wa Dar es Salaam na mingineyo.
Tunamuomba Allah (SW) awatie nguvu viongozi wajao ili waweze kutimiza mikakati na malengo tuliyojiwekea.
Amiin.

Ripoti imeandaliwa na Katibu wa Idara ya Habari Akhiy Kassim I Chubwa Ndimuabo

No comments: