TAMKO LA TAASISI YA
MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA KAULI YA MAASKOFU
KUINGILIA MADARAKA YA BUNGE NA KULITAKA LISIJADILI JUU YA MAHAKAMA YA KADHI
1. Hivi karibuni ndugu
zetu, viongozi wenzetu wa Dini ya Kikristo chini ya “mwamvuli” wa Jukwaa la
Wakristo Tanzania, wametoa Tamko la kuitaka Serikali isitishe Mchakato wa
Mahakama ya Kadhi kwa kuondoa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali Na. 02 wa Mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375(The
Islamic Law(Restatement) Act, Cap.375) na ambao unatarajiwa kujadiliwa katika
Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoendelea hivi sasa
Dodoma, ikiwa ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Mizengo Kayanza Pinda mwishoni mwa Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba.
2. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imelipitia Tamko hilo la Jukwaa la Wakristo
Tanzania kwa umakini mkubwa na baada ya tafakuri ya kina juu ya kadhia hii,
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inaweka bayana
yafuatayo:-
3. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imesikitishwa sana na Tamko la Maaskofu chini ya
Jukwaa la Wakristo Tanzania kuingilia kwa hila madaraka ya Bunge na kutaka kuifanya
Serikali iliyotoa ahadi kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ionekane
imewadanganya Waislamu ili Waislamu waichukie Serikali yao. Ikumbukwe kwamba
Ahadi ya Marekebisho ya Sheria kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara ni
Ahadi ya Serikali.
4. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawanasihi na kuwaomba Maaskofu wawaachie “uhuru”
Wabunge Waumini wa Dini ya Kikristo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
waujadili muswada huo bila ya shinikizo la kiimani la kuukataa.
5. Mbinu zozote za
kuwashawishi Wabunge kiimani kutekeleza Maazimio ya Maaskofu chini ya Jukwaa la
Wakristo Tanzania, huo ni “udini” ambao ni hatari sana kwa Umoja na Mustakabali
wa Taifa letu.
6. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawakumbusha Maaskofu kwamba Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Vyombo vya Uchunguzi na Utafiti vyenye
uwezo wa kubaini maeneo yanayovunja Umoja wetu wa Kitaifa, na hata mambo
yanayopingana na Katiba ya nchi yetu tuliyo nayo sasa na ile inayopendekezwa.
Kamwe Maaskofu si sehemu ya vyombo hivyo. Ni vizuri wakaendelea kuongoza Ibada
na kazi hizo za Uchunguzi wakawaachia walioaminiwa kuzifanya.
7. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inachukua fursa hii kuwakumbusha Maaskofu na
Watanzania kwa ujumla kwamba “Hofu” ya kuwepo Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara
ni hofu “bandia”, kwani kesi zinazohukumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kiislam
zinazohusiana na Ndoa ya Kiislamu, Talaka, Miirathi, Wasia, Waqfu na Malezi ya
Watoto zinapatiwa uamuzi (hukumu) katika Mahakama zilizopo na kwa miaka kadhaa
na wala Maaskofu hawajapata kudai ziondolewe kwa kuwa ni za kidini. Ieleweke
kuwa wanachoomba Waislamu ni kubadilishiwa Hakimu ili aje Kadhi ambaye ana
taaluma na uelewa mpana wa Sheria ya Kiislamu. Je, ni vipi kasoro ya Dini
ionekane baada ya kuletwa Kadhi atakayezipatia hukumu za kesi hizo na
isionekane sasa wakati zipo Mahakamani kwa Hakimu anayezikosea hukumu hizo?
8. Kuhusu hofu ya Maaskofu
kwamba, kwa kuwa baadhi ya Taasisi za Kiislamu hazikubaliani na Mamlaka ya
Mufti wa Tanzania kwenye masuala yao, na hivyo kuijumlisha hoja hiyo kama hoja
ya kutaka muswada huo uondolewe kwa ujumla wake, tunapenda kuwakumbusha na
kuwataka viongozi wa kikristo wayaache mambo ya ndani ya waislamu
yashughulikiwe na waislamu wenyewe. Kadhalika wakumbuke kauli yao “ Ya Kaizari
mpe Kaizari, na ya Mungu mpe Mungu” na hivyo basi waiache Serikali na Bunge
kutekeleza majukumu yao bila ya kuingiliwa kiimani. Viongozi wa Kikristo
watambue kuwa Waislamu wanajua migongano na mifarakano iliyopo ndani ya
makanisa lakini waislamu hawajathubutu kuyaingilia mambo ya ndani ya wakristo
kwa namna yoyote na wamewaachia Wakristo watatue matatizo yao wao wenyewe. Viongozi
wa Kikristo waache kuwadanganya Waislamu kwa “huruma ya mamba” na ikiwa kweli
Viongozi hawa wa Kikristo ni wasikivu wa sauti ya Baadhi ya Taasisi za Kiislamu
wangefanyia kazi madai ya uwepo wa “Mfumo Kristo” yaliyotolewa hadharani na
Taasisi hizo.
9. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania itashangazwa sana iwapo Serikali itaamua
kuuondoa Bungeni Muswada unaolenga kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara
kwa kisingizio cha kupingwa na baadhi ya Taasisi za Kiislamu na chembilecho
itadhihirika wazi kuwa Serikali imeuondoa Muswada huo kutokana na shinikizo la
Jukwaa la kikristo, kwa kuwa ni Serikali hii iliyoamua kuendelea na mchakato wa
SENSA mwaka 2012 pamoja na kupingwa na baadhi ya Taasisi za Kiislamu.
10.
Taasisi
ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawaomba Waheshimiwa Wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wazingatie viapo vyao vya kuitumikia
nchi hii na watu wake kwa uadilifu na bila ya kuathiriwa na shinikizo la
kiimani lililotolewa na Maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania waupokee
Muswada huo na waupime kwa hoja na kutoa majibu yenye hoja, na kamwe wasikubali
wagawanywe kiimani kwani jaribio la kuligawa Bunge kiimani ni jambo la hatari
linalotishia kuligawa Taifa la Tanzania.
11. Taasisi ya Masheikh na
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania haina pingamizi na dhamira ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kuwafahamisha “wenye hofu” na uwepo wa Mahakama ya Kadhi Tanzania
Bara kuwa Mahakama hiyo haina madhara yoyote kwa Umoja, Mshikamano na
Mustakabali wa Taifa la Tanzania. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania inaahidi kumpa ushirikiano wowote atakaouhitaji katika utoaji wa elimu
hiyo.
12. Mwisho, Taasisi ya
Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawaomba Waislamu wote nchi nzima
kuwa watulivu na kuendelea kuiombea nchi yetu isiingie katika machafuko yoyote.
Wabillahit Tawfiiq
SHEIKH
KHAMIS MATAKA
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment