JINAMIZI LA UDINI TANZANIA
UTABIRI WA SHEIKH SULEIMAN TAKADIR

Kutoka Kushoto:
Sheikh Suleiman Takadir, Mbutta Milando, JohnRupia na Julius Nyerere Hao
Waliowazunguka na Silaha za Jadi ni Bantu Group Kundi la Vijana wa TANU
lililokuwa linatoa Ulinzi kwa Viongozi wa TANU. Picha Hii Ilipigwa Mwaka wa
1955.
Jina la Sheikh Suleiman
Takadir halijapatwa kutajwa popote katika historia ya kupigania uhuru wa
Tanganyika wala katika historia ya TANU. Hatajwi na hakupata kutajwa baada ya
uhuru kupatikana mwaka 1961 na sidhani hata kama atakuja kutajwa au kukumbukwa
na hawa viongozi walio katika madaraka hivi sasa. Lakini naamini viongozi hawa
walio madarakani hivi sasa ambao wakati wa kudai uhuru walikuwa watoto wadogo
lazima watakuwa wamesikia jina hili likitajwa na wazee wao. Sheikh Suleiman
Takadir hutajwa kila linapotokea jambo ambalo Waislam huonekana wanadhulumiwa
na serikali kwani ilikuwa Sheikh Suleiman Takadir ndiye aliyeweka agenda ya
hali ya baadae ya Waislam na Uislam katika Tanganyika huru mwaka 1958. Jambo
hili alipolileta lilitishia kuigawa TANU katika misingi ya dini katika wakati amabo
umoja wa Waafrika ulikuwa unahitajika sana. Mwaka wa 1958 TANU ilikuwa imeenea
nchi nzima na tayari iko katika barabara ya kuelekea kuchukua madaraka ya ndani
na kisha Tanganyika kupata uhuru wake kamili.

Sheikh Suleiman Takadir
alikuwa nani na nini ulikuwa umaarufu wake? Sheikh Suleiman Takadir kwanza
alikuwa ‘’alim,” mwanazuoni kisha alikuwa Mwenyekiti muasisi wa Baraza la Wazee
wa TANU kuanzia TANU ilipoundwa mwaka 1954 hadi “alipotoswa” mwaka 1958 kwa
kosa la “kuchanganya dini na siasa.’’ Sheikh Takadiri alishiriki vilivyo ndani
ya Baraza la Wazee wa TANU katika kutayarisha safari ya Nyerere kwenda UNO
mwaka 1955. Wapenzi wake katika harakati za kupigania uhuru walimpachika jina
la utani wakimwita “Makarios,” wakimlinganisha na Askofu Makarios wa siasa za ukombozi za Cyprus na Ugiriki
aliyekuwa anapambana na ukoloni wa Waingereza wakati yeye alipokuwa
anapambana na Waingereza katika ardhi ya Tanganyika. Sasa kwa kuwa Suleiman
Takadir alikuwa sheikh na mpambanaji ndipo walimpa jina hilo la “Makarios” na
kwa hakika jina hili lilimkaa, likamwenea vyema na yeye akalipenda.
![]() |
| Baraza la Wazee wa TANU Sheikh Suleiman Takadir wa Pili Chini Kulia, Wa Pili Waliosimama Dossa Aziz, Wa Sita Julius Nyerere, Wa Saba John Rupia, Wa Tisa Said Chamwenyewe, Anaefuatia Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate |
Shebe ndiye alinipiga picha yangu ya kwaza nikiwa
na umri wa mwaka mmoja au miwili hivi nMikutano ya mwanzo ya TANU ilikuwa ikifanyika Mnazi Mmoja mbele ya baadae ilipojengwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Wakati ule pale palikuwa hakuna jengo lolote, palikuwa na kiwanja kitupu na ardhi ile ilikuwa mali ya Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU. Kiwanja hiki baaadae Mzee Rupia aliwapa TANU na TANU wakaanzisha Chuo Kikuu pale mara baada ya uhuru. Mikutano ya kwanza ya TANU ikifanyika pale Mnazi Mmoja na kabla Nyerere hajapanda juu kwenye jukwaa kuzungumza na wananchi alikuwa kwanza anatangulia Sheikh Suleiman Takadir kusawazisha uwanja na kuwaweka wananchi tayari kumsikiliza kiongozi wao. Kama alivyokuwa Nyerere, Sheikh Suleiman Takadiri alikuwa na kipaji cha kuongea. Leo hii huenda baadhi ya wasomaji wangu wasiamini lakini ukweli ni kuwa Sheikh Suleiman Takadir alikuwa kabla hajazungumza lolote alikuwa akipiga “fatha,” wananchi wakaitika na kwa umoja wao wakasoma, “Surat Fatha,” sura ya ufunguzi katika Qur’an Tukufu, kisha Sheikh Takadir akaomba dua na wananchi wakawa wanaitika kwa pamoja, “Amin,” Amin,” “Amin.” Baada ya hapo ndipo atapanda Nyerere na kuanza kuhutubia. (Picha za mwanzo za mikutano hii zipo na zilipigwa na Mzee Shebe ambae katika miaka ile ya 1950 alikuwa na studio yake Mtaa wa Livingstone na Kipata. Picha hizi baadhi nimepata kuziona. Mzea picha hii ninayo hadi hii leo.
Inaaminika Mzee Shebe ndiye mpiga picha wa kwanza wa TANU na Nyerere).
Mwandishi Akiwa na Mwaka Mmoja Au Miwili Picha Aliyopigwa na Mzee Shebe
1952/53 Kwenye Studio Yake Mtaa wa Livingstone na Kipata
1952/53 Kwenye Studio Yake Mtaa wa Livingstone na Kipata
![]() |
| Nyerere Akihutubia Mkutano wa TANU Siku za Mwanzo |
Huyu ndiye Sheikh
Suleiman Takadir na huyu ndiye Nyerere kama alivyokuja kutambulishwa kwa watu
wa Dar es Salaam na Sheikh Suleiman Takadir kwa mara ya kwanza mwaka wa 1954.Kabla
ya hapo Nyerere alikuwa akijulikana na watu wachache katika TAA. Sheikh Takadir
alimpenda sana Nyerere kiasi kuwa mwaka 1957 katika hotuba aliyotoa katika
tafrija moja ya taarab Mtaa wa Mvita, alimwita Nyerere, “Mtume wa Afrika,”
aliyetumwa na Mungu kuwaokoa Waafrika. Maneno yale ya Sheikh Suleiman Takadir
alikuwa kama anamtabiria Nyerere makubwa katika mustabali wa Afrika, kwani
miaka mingi baadae Nyerere alikuja kusimama mstari wa mbele katika kuikomboa
Afrika kutoka makucha ya wakoloni. Nyerere akawa hapungui nyumbani kwa Sheikh
Takadir Mtaa wa Swahili. Nyumba hii iko jirani na kilabu ya mpira ya Pan
Africa. Kutembelewa na Nyerere pale nyumbani kwake ikapelekea baba mwenye
nyumba, Jumbe bin Jumaa wa Digosi amuhamishe nyumba Sheikh Takadir asije
kumponza kwa kwani Nyerere alijulikana kama adui mkubwa wa Waingereza. Hii kwa
muhtasari ndiyo historia ya Sheikh Suleiman Takadir na Nyerere. Lakini usuhuba
huu ulikuja kuvunjika na watu wawili hawa wakawa mahasimu wakubwa, Sheikh
Suleiman kafa hasemi na Nyerere na Nyerere kwa upande wake hakupata hata siku
moja kumtaja Sheikh Takadir popote hadi anaingia kaburini. Inaaminika Sheikh
Takadir alikufa kihoro baada ya kupigwa pande na TANU na wakazi wote wa Dar es
Salaam na wanachama wa TANU kwa kosa la “kuchanganya dini na siasa.” (Ikiwa
msomaji wangu ulisoma makala yangu ya juma lililopita utakuwa umeona kuwa TANU
ikiongozwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir ilipitisha azimio la kupiga vita
hisia zozote na chembechembe za Uislam ndani ya TANU). Hakika Uislam ulikuwa na
nguvu ndani ya TANU lakini haukuachiwa uvuke mipaka kuwabagua wengine waliokuwa
si Waislam.
Kilitokea nini hadi
kupelekea Sheikh Suleiman Takadir agombane na Nyerere? Chanzo cha mtafaruku huu
ni Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka 1958. Waingereza waliweka masharti ambayo kwa
hakika yalikuwa ya kibaguzi na yalifanya wananchi wengi wasiweze kukidhi sifa
zilizowekwa za kuweza mtu kupiga au kupigiwa kura. Kulikuwa na sifa ya elimu,
kipato na kazi ya kukubalika na kupiga kura kwa tabaka za rangi. Mpiga kura
Mwafrika alitakiwa ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika. Masharti haya
yalikuwa kisiki kigumu kwa uongozi wa TANU na wanachama wake kutimiza. TANU na
viongozi wake wengi hawakuwa na hiyo elimu iliyokuwa ikitakikana wala kipato
cha maana. Ili mtu asimame kama mgombea kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria
au awe angalau mpiga kura ilibidi azikusanye sifa zote hizo mahali pamoja. Wapiga
Kura na wagombea walitakiwa wawe na kisomo cha darasa la 10 au kipato cha pauni
400 kwa mwaka na kuwa na kazi ya maana. Waafrika waliokuwa na sifa hizi
hawakuwa wengi katika TANU. Wengi katika TANU kama walivyokuwa wakipenda
kujiita wenyewe walikuwa, “Baba Kabwela.” Ikawa sasa ili TANU iweze kuweka
wagombea ilibidi iwatafute watu nje ya uongozi wa TANU. Hapa ndipo lilipokuwa
tatizo.
Nyerere Akitia Sahihi Azimio la Tabora
Nyerere Akitia Sahihi Azimio la Tabora
Ilibidi TANU sasa
iwalete watu wenye sifa nje yake na wengi wa watu hawa walikuwa Wakristo
waliosomeshwa na wamishionari. Jambo
hili lilimkera sana Sheikh Takadir na wanachama wengi wa TANU kwa ujumla wao na
kwa hakika TANU nzima hawakutaka kabisa kuingia uchaguzi ule kwa masharti yale
waliyoyaona ya kibaguzi. Wanachama wa TANU walikuja na kauli mbiu isemayo,
“Kuingia Kura Tatu ni sawa na kujipaka kinyesi.” Ilikuwapo minong’ono kuwa Wakristo wataichukua
nchi lakini kwa muda mrefu hofu hii ilizuiwa kwenye vifua hakuna aliyekuwa na
ujasiri wa kulisema hilo waziwazi kwani jambo la dini lilikuwa mwiko mkubwa
katika TANU. Ikawa tatizo lile la kushiriki kwa TANU katika Uchaguzi wa Kura
Tatu lijadiliwe kwenye Mkutano Mkuu wa TANU wa mwaka 1958 uliopangwa kufanyika
Tabora. Mpinzani mkubwa wa Kura Tatu alikuwa Zuberi Mtemvu, Katibu Mwenezi wa
TANU kwa wakati ule. Ukweli ni kuwa Kura Tatu ilitishia uhai wa TANU na
zilikuwapo dalili za chama kumeguka pande mbili. Kulikuwa na uwezekano mkubwa
sana kuwa Zuberi Mtemvu na Sheikh Takadir wangelikuwa upande mmoja na wangeweza
kuja na chama kingine ingawa agenda zao zilikuwa tofauti. Mtemvu yeye alisimama
kwenye Afrika kwa Waafrika na Sheikh Takadir kwenye Uislam. Mkutano wa Tabora
ni kisa kirefu In Sha Allah tutakitafutia wakati wake makhsusi tukizungumze. (Nimekiandikia
kitabu kizima “Uamuzi wa Busara,” Abantu Publishers 2007, Dar es Salaam) Sheikh
Suleiman Takadir na baadhi ya wazee katika Baraza la Wazee wa TANU walikuwa
wajumbe katika mkutano wa Tabora. Kufupisha kisa TANU ilipiga kura kukubali
kuingia kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu na manusruna kura zifungane kati ya wale
wanaounga mkono na wale waliokuwa wakipinga. TANU iliingia katika Uchaguzi wa
Kura Tatu na ikapata ushindi mkubwa.
Hofu aliyokuwanayo
Sheikh Takadir ilikuwa kuwa watu walioingia katika TANU kuchukua uongozi ni
Wakristo. Sheikh Takadir alikuwa anajua nguvu ya madaraka waliyokuwa
wanakabidhiwa akawa na hofu kama uongozi huu mpya utakuja kutoa haki kwa
Waislam uhuru utakapopatikana. Sheikh Takadir alitaka uhakika wa hali ya baadae
ya Waislam katika Tanganyika huru. Katika mkutano wa Halmashauri Kuu Makao
Makuu ya TANU, New Street Sheikh Takadir alimkabili Nyerere akamshutumu kuwa hakuwa
na nia nzuri na Waislam, atakuja wapendelea ndugu zake Wakristo katika
Tanganyika huru. Sheikh Takadir akawageukia wenzake katika Baraza la Wazee wa
TANU akasema, “Tuzibe ufa tusije tukajenga ukuta.” Jambo lile lilikuwa zito.
Nyerere alijiinamia na aliponyanyua uso wake machozi yalikua yanambubujika.
Mkutano haukuweza kujadili jambo lile na kikako kile kikavunjika pale pale na
wajumbe wakawatawanyika.
Sheikh Takadir ‘’akatoswa,’’
kwani alikuwa amevunja mwiko mkubwa katika TANU. Mzee Iddi Tulio akachaguliwa
kushika nafasi yake. Huku kutoswa na
kutengwa na jamii ndiko kulikosababisha kifo cha Sheikh Takadir. Alikuwa hata
akitoa salamu hakuna aliyeitika. Akienda sokoni Kariakoo kununua chochote kile
hakuna aliyekuwa tayari kupokea hela yake. Haikuchukua muda mrefu Sheikh
Takadir akaaga dunia. Kabla Sheikh Takadir hajafa TANU ilifanya mkutano mkubwa
sana na Nyerere akamshambulia Sheikh Takadir kwa kutaka kuwagawa Watanganyika
katika misingi ya dini. Baada ya mkutano kundi kubwa lilikwenda nyumbani kwa
Sheikh Takadir Mtaa wa Msimbazi kuzomea huku wakiimba, “Takadir Mtaka Dini.” Sheikh
Takadir alitoka nje akasimama kizingitini akasema maneno haya, “Ndugu zangu In
Sha Allah iko siku mtakuja kunikumbuka.” Haukupita muda mrefu Sheikh Takadir
akatangulia mbele ya haki na kwa kipindi kirefu katika historia ya uhuru wa
Tanganyika hakuna aliyemkumbuka Sheikh Suleiman Takadir, Askofu Makarios wa
Tanganyika. Hivi sasa Sheikh Suleiman Takadir anatajwa sana na kizazi cha leo.
Utabiri wake kuwa ndugu zake watakuja kumkumbuka umetimia. Swali la kujiuliza
ni iweje hii leo baada ya miaka 57 kupita Sheikh Suleiman Takadir anarejeshwa
upya katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika? Hiki ni kitendawili
kinachongoja kuteguliwa.
| Kushoto: Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mohamed Mtamila na Bi. Titi Mohamed Aliyesimama chini ya Jukwaa ni Joseph Nyerere Nyuma ya Nyerere ni Mama Maria Nyerere na Nyuma ya Sheikh Takadir ni John Rupia |


No comments:
Post a Comment