Tuesday, 10 February 2015

Kipi Kilichokwenda Kombo? Na Ben Rijal


Kipi Kilichokwenda Kombo?
Na Ben Rijal

Bila ya kujiuliza pale ulipopakosea kutaka kujirekebisha basi elewa fika utakuwa unaendelea kukosea kwa kuwa hujajiuliza na kutaka kujirekebisha.

Mila, utamaduni na silka ni katika mambo muhimu katika jamii yoyote ile itakayo taka kuwa na mafanikio.

Anuwani ya makala hii ni kipi kilichokwenda kombo? 

Hapa najaribu kutafuta suluhisho la kuona maadili ya kizanzibari kuwa yamekwenda arijojo na kuna hatari kwa kasi inayokwenda kuja kujikuta ni kuwa taifa lilokosa mtizamo na muelekeo katika maadili.

Inaweza kuwa kuna sababu tele zinazosababisha kuona vijana hata wazee kila mmoja amepoteza mwelekeo na kujiuliza kipi kilichowasibu Wazanzibari? 

Mara nyingi unapokuwa unaliachia jambo ima kwa kutokusudia au kwa makusudi jambo ambalo baadaye litakuja kuwa na madhara basi ujuwe hakutokuwa wa kulaumiwa isipokuwe wewe ulilolichangia liwe hivyo.

Zanzibar yetu ambayo tunaililia ilikuwa ni kituo au nchi ambayo atakaitia mguu wake tu anaona ameingia katika nchi iliojaa nidhamu ya hali ya juu n utamaduni wakupigiwa sifa. 

Ilikuwa mwiko kumuona mwanamke kava vazi lilokuwa sio la stara na kupita njiani huku akijishau na hakuna anaye thubutu kumwambia elee. 

Leo mwanamke kuwa katika hali kama hio ni jambo la kawaida. 

Leo vijana wamekuja na mtindo wao wa kuvaa suruali na kuona suruali ya ndani na akapita kijana huyo katika kadamnasi ya watu na hakuna hata atakayethubutu kulikaripia hilo. Leo vijana wamekuwa hata hawaoni shida kutumia uraibu wa sigereti mbele ya wazazi wao na wanapoulizwa hujibu kuwa wanaondoa mawazo, wakati huko nyuma hata kijana akiingia katika dimbwi la uvutaji sigereti basi atahakikisha kuwa anavuta kwa kujificha.

Leo hata kwenye ibada imekuwa watu kushambuliana yule anajua zaidi huyu hajui, huyu usimzikileze almuradi kumekorogeka, utajiuliza haya yanatokea hata Misikitini? 

Iweje kwenye Msikiti sadaka iliyoletwa wapate kila aliopo kwa wakati ule Msikitini, imelizikie sadaka ile kwa Imamu na muadhini wake tu? 

Yakiwa Msikitini yanajiri hayo yataweza kuvuka penginepo?

Barabarani kulikuwa na nidhamu ya hali ya juu kabisa, iwe unakwenda kwa miguu, umepanda baskeli au umo kwenye gari, leo ukiwa unatoka nyumbani kwako iwe umetoka kwa miguu au umepanda chombo chochote kile basi utakuwa umo kwenye khofu kama utafika salama huko ulipokusudia. 

Leo njia ya upande mmoja tu ambayo ndio kawaida iliowekewa utaona njia hio imegeuzwa kuwa njia ya pande mbili, utajiuliza kwani wataalamu wa mawasiliano kuona njia ile iwe inakwenda na vyombo kwa upande mmoja walikosea? Waendeshaji baskeli nao hao hawasemeki wao hujifanyia watakavyo, lakini baya zaidi huwa hawachukui kurunzi wakati wa usiku na hio sio kama ni sheria tu lakini inakuwa kwa usalama wa mwendeshaji wa baskeli na usalama kwa waendeshaji wa magari.

Utajiuliza kwanini leo watoto wanaokwenda skuli kuwa humo njiani wanamopita ni kelele tupu na kusema maneno yasiostahiki, basi tena usadifu kupanda daladala nao hapo utayasikia usioyapata kuyasikia. Walimu huko nyuma ndio waliokuwa kioo kwa wanafunzi na jamii kwa jumla leo aghlabia ya walimu mienendo yao sio yenye maadili. Siku hizi kusikia walimu wa madrasa baada ya kuelekeza kutendwa mwenendo mwema wao ndio sasa wanaowaharibu watoto, inasikitisha kusikia humo kwenye madrasa watoto ndio wanaharibiwa. 

Hivi sasa unasikia fukuto lilokuwa sio la chini kwa chini lakini lishatoa moto wala sio moshi kusikia mapenzi yanayofanywa na watu wa jinsia mmoja, halafu kumsikia mtu analizungumzia kama  ni jambo la kawaida katika jamii , anatamka mtu yule mpenzi wake, huyo anayoambiwa ni mpenzi wake ni wote wawili ni watu wa jinsia moja, hapa ndipo unapojiuliza hao wanaopiga zumari kuhalalishwa matendo hayo machafu sio watapata mwanya kusema yahalalisheni koliko kuwachia kuwa hayatendeki na kuwakosesha mashetani hao uhondo?

Leo madanguro yapo na unapouliza unaambiwa laa hio ni gesti tu, inafahamika fika kuwa nyumba hizo zinaruhusiwa na wamiliki wake watu kwenda kujifanyia watakavyo, la kujiuliza kweli nahuo UKIMWI utatoweka? Siku hizi kuna maeneo ukipita nyakati za usiku utakutana na wale wanaouza miili yao na soko hilo huambiwa nila watalii lakini na wenyeji nao sio kalili.

Zamani ilikuwa mtu akiwa na haja ya nazi huwenda kwa mmiliki wa shamba na kumuomba nazi, hapo mmiliki ama atamgea kama zipo au atamwambia kama unaweza kuukwea mnazi basi kajichukulie zitazokidhi haja zako, huko nyuma utaikuta ndizi imekaa kwenye mgomba kila ukipita imekutumbulia macho, leo wizi wa mazao umeshika kasi na kupamba moto, mwenye ndizi anaikata ingalichanga kwa kuhofia isije kuibiwa, leo lakusikitisha nikuona mifugo inavyoangamizwa, mtu anamchinja ng’ombe aliomuiba kisha akachukua paja moja tu na kumwacha ng’ombe na sehemu zake zilizobaki kama mzoga, wakulima na wafugaji kila mmoja anafanya amali hizo kwa kuwa ni mazoea tu lakini sio wenye matumaini na kupata kipato kutokana na kazi hizo.

Mvuvi amekuwa mfano wa yule anawekea kinyesi sahani anayokulia, inasikitisha kuwa mvuvi anajua kuwa matumbawe ndio makazi n amazalia ya samaki na ndipo sehemu inahitajia kuhifdhiwa kwa hali ya juu ili aweze kupata kuvua samaki wakutosha, leo mvuvi huyo ndio anayeongoza kuyaharibu na kuyafisidi hayo matumbawe tena kufanya hayo kwa makusudi.

Wengi wetu kutokana na hali zetu za vipato huwenda kutibiwa katika hospitali za serikali, eeeh, hapo utaumwa mara mbili unafika unaambiwa daktari hayupo, mara yupo lakini anaingia na kutoka, wengine watakutajia vya kuchangia visivyo na hesabu kwamfano mtu anataka kupasuliwa kumbe nusu ya vitu hivyo vinakuwa mali yake na anapokuja mwengine anamtajia hivyo hivyo lakini atamwambia vipo hapo alipo na kumpiga bei atakayo, hapo anakua daktari anawakanga wagonjwa kwa mafuta yao, leo tukimbile wapi kwakufahamu daktari ndio mtu mwenye huruma ya hali ya juu leo madaktari nao wameingia ngomani.

Ukiyachukua na kuyafasili hayo yote niliojaribu kuyaelezea utaona Wazanzibari tumetoka katika msatari ule tuliokuwa nao uliokuwa wakupigiwa mfano sio tu Afrika ya Mashariki lakini kwa dunia nzima. 

Unaposoma maandishi mbalimbali utaona tulivyokuwa tukisifiwa, leo anayekuja kutoka nje hakuulizi ya karibuni anakuuliza ya kale, lakujiuliza kwanini yawe hayo? Tujiulize kipi kilichokwenda kombo? 

Tuendelee hivi hivi au kuna haja ya kutafuta mwaarubaini wakuweza kuyatatua haya machache nilioweza kuyanukulu? 

Watu sio wale wale, sasa kipi kilichowabadilisha wawe sivyo kama walivyokuwa waliopita?

Kipi kilichokwenda kombo? 

Utakpoyasoma makala hii hebu jiulize kisha jaribu kupata jawabu.

No comments: