Mchango wa Waislamu Katika Maendeleo ya Dunia
Ibn Battuta
(2)
na Ben Rijal
Makala hii itamuangalia mweledi wa
safari Ibn Battuta na mchango wake katika maendeleo ya Sayari yetu hii. Ninani
Ibn Battuta? Jina hili katika uga wa elimu ya Jiografia lilihitajika
lizungumzwe kwa mapana na marefu kwa nchi za Kiafrika na hata katika ulingo wa
historia Ibn Battuta ana mchango wake alioutoa. Kinyume chake jina la Ibn
Battuta linaonekana haliingii katika mizani kwasababu za wanalolikataa
wanazijua wenywe, aidha kinachosikitisha nikuwa hata katika nchi za Kiislamu na
za Kiarabu katika mitaala yao hawamzungumzi na wale wanaomzungumza
hawamzungumzi anavyo stahiki.
Ibn Battuta jina lake khasa ni Abu
Abdullah Muhammad Ibn Battuta mzaliwa wa Morocco alizaliwa tarehe 24 Februari
mwaka wa 703 Hijria (1304 CE) wakati wa utawala uliokuwa ukijulikana kama
Marinid, akifahamika zaidi kwa jina la Shams -ad-Din. Wazazi wake ni wakabila
la Kiberber na walikuwa na utamaduni wa kabila hilo kufanya kazi za uhakimu.
Baada ya kupata elimu nyumbani kwao Morocco
katika fani ya Sheria ya Kiislamu akaamua kuondoka na kuanza safari kiguu na
njia ili kuweza kuujua ulimwengu, alianza safari zake hizo akiwa kijana mwenye umri
wa miaka 21.
Safari yake ya mwanzo kutoka
Morocco ilikuwa kuelekea Makka na kupata fursa ya kutimiza nguzo ya Hijja hata
hivyo safari hio ilikuwa ni refu kwani ilimchukua
miezi 16 kutoka Morocco hadi Makka, baada ya kukamilisha Hijja akaamua kutorudi
nyumbani na ilimchukua muda wa maiaka 24 kuizunguka sehemu ya dunia mpaka kurudi
kwao Morocco.
Ibn Battuta aliweza kusafiri
takribana katika nchi zote zile ambazo zikikaliwa na Waislamu kwa wingi katika
wakati wake. Katika safari zake akipendelea zaidi kusafiri kwa kupitia njia za
nchi kavu koliko njia za baharini kwa kuchelea kuhujumiwa na maharamia ambao
walikuwa wakitamba katika maeneo ya baharini, alikuwa akipendelea kujiunga na
misafara ya wafanya biashara.
Alipofika katika mji wa Sfax
alipiga chuo na kubakia hapo kwa muda, katika mji huo wa Sfax aliponea
chupuchupu kuweza kupoteza maisha yake pale jahazi alilosafiria kuzama na
alipofanikiwa kufika nchi kavu ikawa ule msemo usemao kutoka kikangoni
kuangukia motoni, alikuta mapambano yaliopamba moto vikiwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe alifanikiwa
kuokoka.

Mvumbuzi wa nchi
mbalimbali Ibn Battuta
Baada
ya kukaa Sfax kwa muda aliendelea na safari zake kuujuwa ulimwengu, safari hii alifanikiwa kuwasili katika maeneo ya Mashariki
ya kati, akateremkia Bahari Nyekundu (Red sea) kupitia mji mtakatifu wa Makka, kisha
akalivuka jangwa la Uarabuni na kuendelea na safari zake zilizomfikisha nchi za
Iran na Iraq.
Ulipofika
mwaka wa 1330 akapita kwa mara nyengine tena katika Bahari Nyekundu hadi kufika
visiwa vya Zanzibar ambapo katika maandishi yake alielezea kuwa alikutana na
watu wa kisiwa hicho wakiwa ni Waislamu watu walio wakarimu na akazungumza nao
kwa Kiarabu akasali nao, aidha aliyasifu maji ya hapo kwa utamu wake. Kutoka
Unguja akaelekea Kilwa nako huko hakupata tabu kuwasiliana na watu wa Kilwa, aliwasiliana nao kwa
lugha ya Kiarabu na alivutiwa kukuta kuwa watu wake wana ustaarabu na wanaishi
katika nyumba za mbao zilizoezekwa mapaa
yake kwa makuti. Alibahatika kukutana na Mtawala wa Kilwa Sultan al-Hasan ibn
Sulaiman akiwa ni katika kizazi cha Ali ibn al-Hassan Shirazi, alivutiwa na
mpango wa majenzi ya Kilwa yalivyokuwa ya kimpangilio na kuelezea kama ni mji
uliokuwa na maendeleo. Aliuelezea Msikiti Mkuu wa Kilwa, Msikiti uliokuwa
mkubwa wenye kuvutia uliojengwa kwa mawe ya matumbawe.
Ulipofika mwaka wa 1332 aliendelea na safari
zake kuelekea India ambapo ilimchukua miaka 8 kuweza kufika huko India bada ya
kutoka maeneo ya Afrika ya Mashariki. India alipokelewa kwa mikono miwili na
Sultan wa India, baada ya kustakimu hapo kwa muda akamua kuendelea na safari zake zilizoweza kumfikisha
China, katika mwaka wa 1352 mshipa wa kurudi nyumbani ulimpiga akarudia hata
katika maeneo ya Bahari Nyekundu na kuelekea Magharibi ya Afrika katika nchi ya
Mali nchi ambayo ina urithi mkubwa wa utamaduni
wa Kiislamu, alikaa katika mji wa Timbuktu akaitumia maktaba kubwa ya Timbuktu
kujiongezea taaluma. Mji wa Timbuktu unaringia kazi kubwa iliofanywa na Mfalme
Mansa Mussa ambaye ndio aliowapeleka walimu kutoka Misri kwenda kusomesha watu
dini na kuandika vitabu mbalimbali. (Mansa Mussa ana makala zake 2 siku za
mbele nitamuelezea).

Ramani
inayoonyesha njia alizopita Ibn Battuta
Anapozungumzwa Ibn Battuta
huzungumzwa zaidi juu ya safari zake bila ya kutajwa utaalamu wa masuala ya
kidunia. Mbali ya taaluma ya Jiografia alikuwa mtaalamu wa fani ya Sayansi ya
mimea (Botany) aidha alibobea katika elimu ya Sayansi ya jamii. Tunafaidika pakubwa
na kazi za Ibn Battuta kutokana na maandishi yake mengi aliyoyaandika. Fani ya
uandishi kwa wasomi wa Kislamu imepotea, waliopita waliandika sana na maandishi
yao yalitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sayari yetu hii.

Maandishi ya Ibn
Battuta
Maandishi yake
Baadhi ya maandishi yake unapoyasoma unapata ladha namna alivyokuwa anazielezea
jamii za Kiislamu zilivyokuwa zinaishi na ustaarabu waliokuwa nao, nitadokowa
mawili matatu juu ya hayo.
Alipokuwa nchini Syria aliona mambo yaliomvutia kabisa, Syria iliojaa
utamaduni na huruma, Syria yaleo inavurugwa na kupotezewa alama zote za athari
za Kiislamu, Ibn Battuta aliandika yafawtayo: “Utapojumlisha matumizi ambayo serikali katika nchi ya Syria
yakifanyika katika karne ya 14 yalikuwa hayana kifani. Kukitengwa fungu la
kuwasaidia wale wote wasiokuwa na uwezo wa kwenda Kuhiji Makka sio tu kusaidiwa
kufika huko bali na matumizi yao ya kula na mambo madogo madogo, aidha
wakisaidiwa wale ambao hawana pesa za mahari ya kuolea, aidha kukitengwa fedha za kuwapa familia ya bibi
harusi waliokuwa wanyonge hawana vitu vya kumpa bi harusi, vilevile kukitengwa fedha kuwasaidia wasafari
walioishiwa kwa kuwasaidia chakula na nguo na usafiri wakuwafikisha makwao.
Kulikuwa na fungu la kuwaweka huru wafungwa na kuwasaidia maisha yao bada
yakutoka gerezani, aidha kukitengwa fungu la kuweka taa za barabarani na
kuimarisha njia ya wapitao kwa miguu na vipando.”
Alipofika Iraq aliandika haya: “Kisha tukawasili Baghdad mji mkuu wa Iraq ikiwa ni mwahali paliokua na
amani mji kati ya miji ya Kiislamu. Tulizikabili
daraja mbili kama Hilla, ikiwa daraja hizo watu wanazipita usiku na mchana,
kike kwa kiume. Sehemu za kukogea zilijaa watu pomoni, sehemu hizo zilijengwa
kwa kiufundi kabisa na kupakwa rangi za kupendeza na kuta zake zikiwa za mramar
nyeusi. Maeneo hayo yakukogea yalikuwa yanamaji ambayo yakitokea Kufa na Basra
saa zote na siku zote maji hayo yakiwa yakitiririka. Sehemu hizo za kukogea zilikuwa zikimilikiwa na watu
binafsi, unapokwenda kukoga unapewa taula za kujifutia maji tatu, mmoja ikiwa
ya kujifunga kiunoni unapoingia kukoga na nyengine ya kujifutia maji na
nyengine kuvaa kiunoni unapotoka kukoga.”
Vilevile aliandika mambo aliyoyayaona Uturuki, Mongolia
na visiwa vya Maldives. Aliyoyaona Uturuki na Mongolia yalimsataajabisha kuona
jamii ya watu wa hapo kuwapa uhuru ulio mkubwa
wanawake, aidha kilichomvutia katika kisiwa cha Maldives ni kuona wanawake vivazi
vyao ni nguo za ming’aro.
Baada ya safari zake za miaka mingi kwa kipindi
cha miaka 24 kuwa nje ya nyumbani mshipa wa kurudi nyumbani ulianza kumpiga na ulipofika
mwaka wa 1355 aliwasili Morocco katika
mji wa Tangier sehemu ambayo ndio alipofia na kuzikwa katika mwaka wa 1368
na kaburi lake limewekwa kuwa alama ya mvumbuzi huyu na wengi hulizuru kama
tunavyotakiwa kuzuru waliokufa na kuomba dua.
Wataalamu
wa Kimagharibi hawaamini kuwa Ibn Battuta alifanya safari hizi bali wakionacho
nikuwa alinukuu kazi za watu wengine, hio yote ni kuwa kila kinachohusiana na
taaluma na maendeleo ni cha mzungu, hutajwa mvumbuzi Vasco Dagama bila ya
kudhukuriwa Tiro aliokuwa mjuzi wa kuongoza safari za baharini, Tiro alikuwa
mtu mweusi.

Eneo aliozikwa Ibn Battuta sehemu ya Tangier
Makala
ijayo tutamuelezea Ibn Rushd na mchango wake katika maendeleo ya Sayari yetu
hii.
No comments:
Post a Comment