Wednesday, 25 March 2015

MCHANGO WA WAISLAM KATIKA MAENDELEO YA DUNIA - Muhammad Ibn Musa Al-Khwarizm (780 – 850) - HAMZAH Z. ZUBEIR


Mchango wa Waislamu Katika Maendeleo ya Dunia
na Hamza Z. Rijal
Katika makala iliopita ikiwa ni utangulizi wa maudhui ya Mchango wa Waislmau katika maendeleo ya dunia nilijaribu kutoa ufafanuzi kuwa Waislmau sivyo wanavyoonekana na kunasibishwa na ugaidi lakini Waislamu wameweza kutoa michango mikubwa ya kuifanikisha dunia hii tunayoishi kuwa katika maendeleo na mafanikio.

Kati ya vigogo mbalimbali wa Kiislamu ambao wamefanya kazi kubwa ambao wataelezewa katika mfululizo wa makala hizi ni pamoja na : Muhammad Ibn Musa Al-Khwarizm (780 – 850), Ibn Battuta (1304 – 1369), Ibn Rushd (1126 – 1198), Omar Khayyam (1048 – 1131), Thabit Ibn Qurra (826 – 901), Abu Bakr Al-Razi (865 – 925), Jabir Ibn Haiyan (722 – 804), Ibn Ishaq Al-Kindi (801 – 873), Ibn Al-Haytham (965 – 1040), Ibn Zuhr (1091 – 1161), Ibn Khaldun (1332 – 1406), Ibn Al-Baitar (1197 – 1248), Abu nasr Al-Farabi (872 – 950), Al-BattanI (858 – 929), Ibn Sina (980 – 1037).

Muhammad ibn Musa Al-Khwarizmi
Msomi Al-Khwarizmi
Mjuwe Muhammad Ibn Musa Al-Khwarizm (780 – 850)

Muhammad ibn Mussa Al-Khawarizimi ni Mfursi aliobobea katika fani nyingi za kitaluma ikiwa Hesabati, Elimu ya nyota, Jiografia na elimu nyenginezo, hizo nilizokwisha kuzinukulu ndizo alizozifanyia kazi kwa kiwango kikubwa.

Al-Khawarizimi amezaliwa huko Uajemi katika mwaka wa 780AD. Katika historia tunamsoma Kiongozi Haroun Rashid ambaye katika uongozi wake aliusukuma na kupeleka Uislamu mbele katika fani ya elimu na ndio nyakati hizo zikijulikana kama nyakati za dhahabu kumanisha kuwa ninyakati ambapo Waislamu walifanikiwa na kutekeleza mengi katika elimu na maendeleo au kwa kifupi tunaweza kuita ni wakati wa mafanikio na maendeleo makubwa. Kujulikana kwa Al-Khawarizimi na kuweza kufanya kazi zake kwa upana ni pale alipokuwa Baghdad katika Nyumba ya Hekima (house of wisdom) chini ya Kiongozi al-Mamun huyu akiwa ni mwana wa Kiongozi Haroun Rashid.

Kubakia kwake Baghdad Al-Khawarizimi aliweza kuja na nadharia mbalimbali za hesabati na ufanyaji wa hesabu kwa njia rahis kabisa kwa kutumia Logarithm inaeleweka kuwa alibobea mno katika fani hii ya Algorithm ambayo fani hii ndio inayotumika katika Computer kuwezesha kufanya kazi kwa kirahisi. Baadhi ya wasomi hupenda kumwita Al-Khawarizimi kuwa ni babu wa somo la Computer kwa kuwa dhana nzima inayotumika katika Compure mizizi yake imetokana nayeye.

Juu ya kazi kubwa iliofanywana Al-Jabir katika somo la Algebra lakini Al-Khawarizimi naye amefanya kazi kubwa ndani ya fani hii hasa unaposoma kitabu kinachojulikana Hisab al-Jabr wa-al-Muqabala. Kitabu hiki katika taaluma ya sayansi kilibidi kufasiriwa mara mbili kwa lugha ya Kilatino lugha ambayo huko nyuma ikijulikana kama ni lugha ya taaluma. Walikuwa Gerard wa Cremona na  Robert wa Chester katika karne ya  12  walipoifanyia tafsiri kazi yake hiyo ya Hisab al-Jabr wa-al-Muqabala.

Al-Khwarizm aliidhibiti taaluma ya utambuzi wa hesabu zijulikanazo kama Quadratic equations ambazo alitoa mifano zaidi ya 100 katika kuweza kupata jawabu unapofanya Quadratic equations  aidha aliweza kufahamisha somo la Geometry na kuweka mifano mbalimbali ya kuweza kulielewa somo hilo. Fani hizi mbili ambazo nimezielezea, aliweza kurahisisha kugawa mirathi kwa njia ya kirahisi kabisa kwa kutumia Quadratic equations na mifano yake ya Geometry ndio yalioleta chimbuko la upimaji wa ardhi ambao hadi hii leo njia alizozipita ndizo zinazotumika.

Bahati mbaya katika taaluma tunazozisoma jina lake huwa haliguswi kwa uchoyo wa nchi za Magharibi uchoyo huu sio kwa Waislamu tu bali hata watu wa jamii nyengine waliokuwa sio Waislamu walifanyiwa uchoyo huo, kwa mfano V. N. Sukachov katika mwaka wa 1910 huyo akiwa ni Mrusi ni mtu wa mwanzo ambaye alielezea kuwa kila kiumbe kina mwahali pake anaposihi na hapo ndipo panakuwa na maingiliano ya maisha na mazingira yaliokizunguka kiumbe hicho nadharia ya kisomi inajulikana kama Ecosystem, akiwa Sukachev alioasisi neno hilo na kuwa anayasomesha na kuyaelezea katika vyuo vya Urusi nchi za magharibi hawana habari au waliibeza kazi hii mpaka alipokuja A. G. Tansley mwaka wa 1935 na kuielezea suala zima la ecosystem na kubatizwa kuwa Tansley ni muanzilishi wa dhana nzima ya ecosystem, na katika makala hizi utaona msomaji kuwa hata yale majina yao wataalamu hawa wa Kiislamu yanaojitambulisha kuwa ni watu wa maeneo gani yamebadilishwa na kufanywa majina yao yatamkwe kizungu, mfano Al-Khawarizimi anatamkwa kama Algoritmi au Algaurizin
Al-Khwarizmi amefanya kazi kubwa katika elimu ya nyota na kuandaa kalenda, kufanya hesabu na kujua kwa dhati sehemu ya jua mwezi na sayari zinapokuwa huyu  ndio muasisi wa table kwa wasomi wa hesabu za sine na tangents.  Katika kitabu chake cha Zij al- sindhind ambacho kimejikita katika elimu ya nyota, Al-Khawarizimi alichukua rejea nyingi tu kutoka Uhindini na kwengineko kuweza kukifanikisha kitabu chake.

Al-Khawarizmi akiwa amefanya hesabu kwa njia ya Alogarithm miaka 200 iliopita hii leo ndio taaluma hii inatumika kwa kiwango kikubwa, ni yeye Al-Khawarizimi alizozijulisha nambari za kiarabu kutumika katika nchi za Magharibi na kuifanya Zero nayo itumike katika kujumuisha ingawa wengi wanasema kuwa Zero iliasisiwa katika Bara la Uhindi na Al-Khawarizimi alisoma maandiko mengi ya Uhindini lakini kujulikna kwa Zero huko Ulaya inatokana na maandiko yake Al-Khawarizimi.

Al-Khawarizimi amefanya kazi nzito katika somo la Jiografia, pale aliporekebisha kazi ya Ptolemy ya utafiti wa Jiografia  juu ya umbo la dunia katika kazi yake maarufu ijulikanayo Surat al-Ard. Kazi yake hii haijachapishwa ilikuwa kazi iliyoandikwa kwa mkono, na ramani  alizozichora bahati mbaya nazo zilipotea lakini maelezo yake wanataaluma wengine waliweza kuunganisha na kupata sura kamili ya ramani hizo alizozitaarisha. Inafahamika kuwa aliwasimamia wasomi kama 70 katika somo la Jiografia katika kutekeleza kazi hio ndio iliomwezesha kutengeneza ramani ya dunia ambayo ndio hii inayotumika sasa, kazi zake zilipotafsiriwa kwa lugha ya Kilatino ndio ikatia msukumo wa sayansi kusonga mbele katika nchi za magharibi.

Al-Khawarizimi ameweza kusaidia katika kuifanikisha kazi ilioanzwa na wataalamu wengine kujua nyakati kwa kutumia chombo kinachoitwa Sundial, chombo hicho ambacho hutumika kujua wakati katika siku wakati jua linawaka. Al-Khawarizimi alikitengeneza chombo hichi kwa njia nyengine kinyume na watangulizi wake wa Kihindi na Hellenistic. Kazi hii ya Sundial imetumika katika kujua nyakati za sala na huko nyuma kilikuwa chombo hicho kinawekwa juu ya Misikiti. Al-Khawarizimi alisaidia katika kuifanikisha kuiandaa kalenda ya Kiyahudi katika kitabu alichokiandika kinachojulikana Istikhraj Tarikh al-Yahud

Baadhi ya kazi zake ni pamoja na kitabu alichokiandika kwa kiarabu na kutafsiriwa kwa lugha ya Kilatino katika karne ya 12 kitabu hicho ni Kitab al-Jam'a wal- Tafreeq bil Hisab al-Hindi, kitabu hichi lau ingekuwa hakijafanyiwa tafsiri kwa Kilatino kingepotea wala kisingezungumzwa kwani maandishi ya awali ya kiarabu yalipotea. Kitabu chake cha Algebra kijulikanacho kama Al-Maqala fi Hisab-al Jabr wa-al- Muqabilah hichi kimesaidia sana wasomi wa nyakati zake nacho kilitafsiriwa kwa Kilatino kikiwa kimetoa mchango mkubwa wa sayansi kwa nchi za Magharibi. Msomi huyu aliweza kutengeneza Jadweli ya nyota na mwenendo wake na kutafsiriwa kwa lugha mbalimbali za nchi za Magharibi na kufanyiwa tafsiri hata kwa Kichina, bila ya kusahau ju ya kazi ya Sun-dials alipoandika kitabu kijulinacho Kitab al-Rukhmat.

Ukitaka kumuelewa Al-Khawarizimi na kuwafanya wasomaji wamuelewe itabidi kwa uchache uandike kitabu kisichopunguwa kurasa 2,000 ndipo utapoweza kumuelezea akafahamika, juu ya hayo azma ya makala hizi ni kutoa mwanga na kueleza kwa mukhtasari Waislamu na michango yao katika maendeleo ya dunia yetu hii.
Makala itakayofwata itamuangalia Ibn Battuta.
















No comments: