Wednesday, 1 April 2015

SAYYID MANSAB BIN ALI - Hamza Z. Rijal

SAYYID MANSAB BIN ALI

Na Hamza Z. Rijal

 Mwanachuoni aliyekuwa na Maajab

Alisoma mpaka uchoraji katika kanisa
Alikuwa akisoma sana majarida ya Misri
Alivutiwa sana Muhammad Abdoo wa Misri

Katika safu ya wanavyuoni wetu safari hii tutamzungumzia Sayyid Ahmad bin Ali Itibar bin Mwinyi Mkuu Sultan Ahmad bin Ali bin Abi Bakr bin Salim, zaidi akijulikana kwa jina la Sayyid Mansab bin Ali.

Sayyid Mansab alizaliwa Ukutani mwaka wa 1279 A.H (1863), akiwa ametokana na mtoto wa kike wa Sayyid Ahmad bin Salim aliyekuwa kadhi wa Sayyid Said.

Inafahamika kuwa Sayyid Mansab babu yake alikuwa ni mfalme huko Ngazija. Wengi wa wafalme wa Ngazija walikuwa ni wa Ngazija wenyewe kinyume na wafalme wa Zanzibar.

Babu yake Sayyid Mansab inasemekana alikuwa ni mpenzi mkuu wa miti (ameature botanist) na mapenzi yake ya miti ilimuwezesha kupeleka miti mingi ya vyakula nchini Ngazija, bwana huyu ananasibishwa na Masharifu wote Moroni kutokana na asili yake, kama ilivyokuwa Masharifu wa Jamalil-Leyl wanavyonasibishwa na Mwinyi Bahasani wa Tsujini.

Sayyid Mansab alianza kusoma elimu ya dini kwa mjomba wake Sayyid Muhammad bin Ahmad bin Salim, na alielimika vya kutosha kisha akasogea kwenda kupiga goti kwa Sheikh Ali bin Khamis. Sheikh Ali bin Khamis siku hizo alikuwa akivuma sana kwa kukusanya elimu nyingi za dini, na baada ya kutoka hapo Sayyid Mansaba alisogea kwa Sheikh Muhammad Al-Murony.

Kwa kuwa Sayyid Mansab alikuwa na sifa za kipekee na mwenye kiu ya kukusanya elimu mbali mbali, hakusita hapo bali alikwenda kujifunza uchoraji wa picha kwa bibi wa Kimisheni wa Kingereza kwenye kanisa la Mkunazini, U.M.C.A (Kimoto).

Kwa kufanya hivyo Sayyid Mansab akapata pingamzi kubwa kwa mashekhe wa siku hizo ambao walikuwa wakimpinga na kumuona mtu asiyofahamika.
Vile vile alimfuata gwiji wa elimu ya tarekhe na elimu ya fani nyenginezo mjuzi aliyekuwa akijulikna kwa jina la Hakim Daud Ali Khan.

Hapo wengi ndipo walipozidi kumuona Sayyid Mansab anakuwa na nadharia zisofahamika na kumuona kuwa atakuja kuleta athari kubwa kwa vizazi vijavyo ikiwa haja dhibitiwa, na hayo yalikuja kuleta ithibati pale alipokuwa akipenda kujisomea gazeti la "Manara" lililokuwa likichapishwa nchini Misri. Sayyid Mansab alilipenda gazeti hilo kwa kuwa lilikuwa na maudhui mengi ambayo yakipinga mambo ya uzushi ndani ya uislam, na alikuwa ni mtu peke yake katika Unguja nzima akipokea gazeti hilo kwa njia ya posta, tena zama hizo. Mwangalie Sheikh huyo alivyokwenda mbali na namna alivyokuwa akipenda kuwa na uono mpana wa kielimu, ambao hata masheikh wetu wa leo ambao wamefika vyuo vikuu mbali mbali hawana mtizamo wa aina hiyo.

Sayyid Mansab alikuwa akivutiwa sana na Muhammad Abdoo mwanafunzi wa Jamaludini Afghani, na alikuwa akiitumia zaidi tafsiri ya Sheikh Muhammad Abdoo na ikawa anavyosomesha yeye tafsiri ilikuwa ni tafauti sana na masheikh wenzake na wale vijana waliokuwa wakisoma skuli za kizungu wakihudhuria darasa zake walikuwa wakivutiwa mno kwani alikuwa akiweza kuelezea ulimwengu kwa upana sana.

Hii ilitokana na kusoma magazeti mengi yaliyokuwa yakitokea Misri, kama: Al-Hilal, Al-Muktatatf, Al-Liwaa, Al-Muayyad na mengi mengine. Matokeo ya kupenda kuwa msomi wa fani mbali mbali yalitokana na kupenda kukaa na wageni kama Sayyid Abdulrahman Jamal wa Misri, Sheikh Muhammad Bakashmar, Sheikh Abdallah bin Salim Al-Khemry, Sheikh Muhammad Al-Izz na wengi kama hao.

Mfalme wa nne katika wafalme wa Kibusaidy, Sayyid Khalifa bin Said, mfalme huyu alikuwa hakubali kupigwa picha na alikuwa hajawahi kupigwa picha, na Waingereza wakiheshimu jambo hilo, lakini Sayyid Mansab alimpiga "drawing", kwa siri pasina mwenyewe kujua. Lakini kama nilivyokwisha eleza kuwa masheikh wenzake walikuwa wakimpiga vita kwa hivyo walifikisha habari kwa mfalme na Sayyid Mansab kuitwa na kuulizwa "Kweli umeniandika sura yangu?" Sayyid Mansab akajibu na huku anatetemeka "La, bwana wangu sithubutu".

Sayyid Khalifa akamwambia "Nikipata picha hiyo utaona cha mtema kuni na ushuhudie kilichomtoa kanga manyoya, kwani nitachokifanya nitakukata kichwa chako!". Na pale pale wakapelekwa watu nyumbani kwa Sayyid Mansab kupekua, na kulipekuliwa kila mwahali kwenye nyumba yake na hata mitungini kulimurikwa na kurunzi labda humo kuna chochote kile, lakini kama waswahili wasemavyo "Wastara hazumbuki", alistirika Sheikh na hakujapatikana chochote kile lau ingekuwa sio Sayyid Mansab picha ya Sayyid Kahalifa isengekuwepo.

Ama wangeiona lazima Sayyid Khalifa angemkata kichwa chake kama alivyosema. Sayyid Khalifa alikuwa hana mchezo atakalo ndilo huwa., alikuwa akiwakata vichwa wahalifu kila siku ya Jumanne na Alkhamis.

Sayyid Mansab alikuwa khatibu wa msikiti wa Ijumaa Forodhani kuanzia mwaka wa 1299 A.H (Septemba 1882) hadi 1337 A.H (Septemba 1919) alipomwachia mwanawe Sayyid Hamid. Alikuwa akisoma kwa kufuata kawaida zote, kwa hivyo hata katika mashughuli mbali mbali akitangulizwa yeye kusoma.

Juu ya kupigwa vita na baadhi ya masheikh lakini watu hao waliokuwa wakimpiga vita walikuwa wakielewa kuwa Sayyid Mansab alikuwa gwiji, na iliposaliwa sala ya kuomba mvua wakati wa Sayyid Hamuud na zama za Sayyid Khalifa bin Haroub alitangulizwa yeye kusalisha na hakuna aliyethubutu kupinga hilo.

Sayyid Mansab alikuwa hatoki ila wakati maalumu, wala haendi pahali ila mahali maalumu katika saa maalumu wala hafanyi jambo maalumu ila katika muda maalumu pia. Alikuwa akiyafanya haya sio kwa kufuata manazil ila alijiwekea taratibu hizo mwenyewe.

Sayyid Mansab alikuwa akitunza siha yake vilivyo na yalikuwa maradhi ya kipuuzi hayamsogelei, lakini alipigwa na maradhi ya ghafla yaliyodumu kwa masaa kumi na nne tu na ilipofika asubuhi ya Jumatatu mwezi 13 Mfungo saba mwaka wa 1346 A.H (10 Octoba 1927) akiwa metimiza miaka 67, Sheikh alifunga macho na kuwachia watu pengo kubwa ambalo lilikaa kwa muda mrefu pasi kuzibwa.

Ewe! Mola tupe nasi tuliopo hima kama aliyokuwa nayo Sayyid Mansab na tufanikishe katika mambo ya kheri "AMIN".

(Maelezo haya nimeyapata kutokana na kitabu cha Sheikh Abdallah Farsy "Baadhi ya Wanavyuoni wa Kishafi wa Mashariki ya Afrika", na wazee wa Msikiti Gofu)







No comments: