Sheikh Hassan Bin Ameir
Na Hamza Z. Rijal
Katika
mfululizo wa makala za wanavyuoni wetu hii leo tutamuangalia alimu mkubwa wa
Zanzibar na Afrika Mashariki kwa jina ni
Shekh Hassan Bin Ameir Bin Mazi Bin Haji Bin Khatib Al-Shirazy
aliyezaliwa mwaka wa 1300 AH (1880 CE).
Sheikh Hassan Bin Ameir amezaliwa Mkoa wa Kusini
Unguja katika kijiji cha Mtegani, Makunduchi. Sheikh Hassan alianza masomo yake
ya Quraan hapo kwao Mtegani, ambapo hakudumu kipindi kirefu na kuhamia Dunga
amabapo nako huko alikuwa akisoma chuwoni, baada ya hapo akelekea Upenja ambapo
alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi waliokuwa wakimudu fani ya tajwidi.
Sheikh Hassan hakusitia hapo, kwani baada ya kuondoka
Upenja aliingia mjini na hapo alipata fursa ya kusoma kwa Maulamaa wa nyakati
hizo ambao kwa leo utawaita kama ni Ma-Professa, kwani walimu hao waliomiminia
elimu walikuwa kila mmoja wao akimwambia mwenzake nipishe. Kati ya hao walimu
wake alikuwa ni Sheikh Hamdani Bin Abdulkadir Al-Qahtan, Sheikh Said Bin
Dahman, Sheikh Muhammed Bin Abdaulla Bin Wazir, Sheikh Ali Bin Mandhry huyu
alisoma kwake huko Pemba, Sheikh Abdulrahman Bin Mahmoud, Sheikh Abdulrahman
Bin Hassan, Sheikh Muhammad Bin Ali Khamis Al-Barwany, Sheikh Abdaullah Bin
Amour bin Muhammed al-Mendhry na Sheikh Abdulla Bin Amour al-Azzi. Mbele ya
mashekhe hao alisoma ilimu zote ikiwa pamoja na Fiqh, tafsiri ya Quraan, fani
zote za lugha, sayansi ya hadithi za Bwana Mtume Muhammad S.A.W na maulamaa
wote hao ! walimkubali kuwa mwanafunzi wao ataweza kuendeleza kile
walichomfunza.
Sheikh Hassan Bin Ameir alianza na kazi ya kusomesha
kabla ya kujiunga na mahkama ya kadhi, na alipokuwa anasomesha aliweka madrsa
yake hapo mtaa wa Misufini madrasa iliyokuwa ikijulikana kwa jina la “Madrasa
el-Shirazi”, watu wengi walinufaika na madrasa hiyo, ingawa kwanza ilikuwa na
wanafunzi wengi kutoka sehemu za kwao Makunduchi lakini kipindi kisichokuwa
kirefu wanafunzi walikuwa wakifurika
kutoka sehemu mbali mbali za Unguja, Pemba, Mrima na baadhi ya sehemu
nyenginezo za maeneo ya Afrika Mashariki na kati kwenda kusoma kwa alimu huyu.
Ingawa Sheikh Hassan alikuwa ameshapea na kuwa mwalimu
lakini alikuwa hajasita na kusoma sio kwa kujisomesha mwenyewe tu lakini
ilikuwa kwa kupiga goto na kwenda popote pale panapotolewa elimu ndipo
alipokuja Unguja Sheikh Abdulbari Al-Aziy kutoka Misri, Sheikh Hassan Bin
Ameir alikuwa mmmoja katika wanafunzi
waliojiunga kwa kupata taaluma kwa mwalimu huyo, na kati ya mengi aliyoyasoma
hapo ilikuwa pamoja na uandikaji wa khati, na inasemekana Sheikh Hassan alikuwa
na khati nzuri sana za kiarabu kwa maandishi ya “nusha” na “rika”, vile vile
alisoma masomo ya hesabu ambayo ni muhimu katika fani ya mirathi na kuna mmoja
aliyowahi kusoma kwake alifika kueleza kuwa “ulipokuwa ukiingia mlango wa
mirathi kila mmoja akisikia raha kutokana na namna Shekhe alivyokuwa akimudu
mada ya mirathi”. Sheikh Hassan alijifunza kis! wahili cha skuli kwa mwalimu wa
kiengereza Mr. River Smith, na alipomaliza msomo hayo akapatiwa cheti
kilichomruhusu kusomesha katika skuli za serekali na kuweza kufanya kazi popote
pale anapotakiwa mtu wa elimu ya dini.
Sheikh Hasasan alisomesha skuli nyingi tu humu visiwani
zikiwemo skuli za Makunduchi, Muyuni, Kiembe Samaki, Chake Chake Pemba na
kwengineko.
Wengi wa wanafunzi wake walishika nyadhifa mbali mbali
katika sehemu zao akiwemo Mufti wa Ngazija Muhammed b Abdulrahman, Sheikh
Fatawi Bin Issa aliyekuwa kadhi baada ya kuwacha Sheikh Abdaalh Farsy, Sheikh
Ameir Tajo Al-Shirazi naye pia alikuwa kadhi mkuu wa Zanzibar, Sheikh Rashid
Bin Haji Al-Shirazi wa Tabora, Sheikh Abdaalh Iddi Chaurembo wa Mrima, Sheikh
Ramadhan Abass wa Mrima, Sheikh Masoud Bin Khatib wa Rufiji, Sheikh Abdulmuhsin
Bin Kitumba wa Ujiji-Kigoma, na wengi wengineo ambao nao wameweza kutoa mchango
mkubwa wa kuelimisha watu elimu ya dini ya kislamu.
Sheikh Hassan Bin Ameir aliwacha kazi ya ualimu na
kujiunga na mahkama akiwa kama karani, na nyakati hizo zilikuwa sio elimu yako
tu ndio inakubalika lakini shakhsia yako nayo ilikuwa ni kiegezo cha kuweza
kupata kazi, aliifanya kazi vilivyo na kwa uadilifu kabisa na hakuna yeyote
yule aliyewahi kumtia ila juu ya kazi yake.
Sheikh Hassan alielekea bara kwa kustakimu na kufanya
kazi kubwa ya tabligh, kuna wengine wanaosema kuwa kule bara aliitwa kwenda
okoa jahazi, kuna wengine wanasema alikwenda kwa hiari yake, itavyokuwa Sheikh
Hassan Bin Ameir alifanya kazi kubwa sana ya kusomesha na hata pale ilipoundwa
jumuia ya “The East African Muslim Welfare Society” iliyokuwa chini ya ulezi wa
Kiongozi Mohammed El Husaini Aga Khan iliyoasisiwa katika mwaka wa 1945, Sheikh
Hassan b Ameir alikuwa katika washauri wakuu na hata pale msafara wakwenda
Misri,Lebnon na nchi nyengine za kislamu kwa kutafuta msada wa kujenga Chuo
Kikuu Cha KIislamu Sheikh Hassan Bin Ameir alichaguliwa kuwa ndio kiongozi wa
msafara huo ukijumuisha watu wengine akiwemo Sheikh Tewa Said, Mwinyi Baraka na
wengineo maelezo zaidi ya msafara huo na kazi zake za Mrima pitia kitabu cha
Ndugu Muhamed Said “The Life and Times of Abdulwahid Sykes.”
Sheikh Hassan alipokwenda Hijja marejeo yake alipitia Chuo
kikuu na kikongwe duniani chuo cha Al-Azhar huko aliweza kupatiwa fursa ya
kutoa mhadhara mdogo ambao wengi walishtuka kuona mtu ambaye amesoma Unguja tu
na Pemba yake kuweza kuwa na umahiri na
umilikaji mkubwa wa lugha ya kiarabu hata Sheikh Mahmoud Zuttuti kumkubali na kusema kuwa “Afrika Masahariki
imepata lulu”.
Dunia mdawari hilo mja ulijue, Shekhe alirejeshwa
Zanzibar katika mwaka wa 1968 kutoka bara, naye alirudi nyumbani bila ya
ukaidi, kurudishwa kwake ni kitandawili kikubwa hakitatuliwa humu, hata hivyo
alipokewa na kupewa kazi katika Mahakama ya Rahaleo, Mahakama ya suluhu.
Sheikh Hassan alibarikiwa kupata fursa ya kuandika
vitabu na kati ya vitabu alivyoviandika ni:
-Wasialatul Rraja (Shrerehe ya Safinatul Najaa)
-Fathul Kabir (Sherhe ya Mukhtasarul Kabir)
-Idhanil Maani Fi-Asamail Husana (Sherehe ya Taibatil Asmai
-Musliku Karib Fi mughnil Muhtaj (Sherehe ya Maslaqul Qarib)
-Madarijul Ulaa (Sherehe ya Tabaraka Dhul Ulaa
Na baadhi ya
vitabu alivyoviandika na kutochapishwa ni pamoja na :
-Tuhfatul Zinjibariya( Sherehe ya Robol Ibada)
-Maulidi barzanji (Sherehe ya Maulidi ya Barzanji)
-Anwaru Saniyyat (Sherehe ya Addurarul Bahiya)
Sheikh hassan Bin Ameir alifunga macho tarehe 8 Oktoba mwaka wa 1979 katika mtaa wa
Michenzani na kuzikwa kijijini mwao Mtegani Makunduchi. Maziko yake yalikuwa
makubwa mno, kwa wale wanayakumbuka, kwani mbali ya wakazi wa Zanzibar watu
wengine walitoka nje ya Zanzibar kwa
kuja kumlaza kigogo hichi.
Nuru yake ipo na inangara hadi leo, lakini bado kazi
nzito inahitajika kufanyika kuanzia Makunduchi hadi mjini Unguja na Pemba ili
Zanzibar iwe katika makamo ya mashekhe zetu hawo waliopita ambao Maarifa wamewavalia njuga
kuwaeleza japo kwa mukhtasari.
Mola tupe kila yalio mema, na utupe satwa ya kufwata
nyayo za watangulizi wetu “AMIN”
(Maelezo haya mafupi nimeyapata kwa Sheikh Salmin Bin
Hafidh ambaye naye amepokea kwa Sheikh Ameir Tajo, Haji Bin Hafidh, Hamid Bin
Hafidh).
No comments:
Post a Comment