Wednesday, 1 April 2015

Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry - Hamza Z. Rijal

Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry
Na Hamza Z. Rijal

Kati ya wanavyuoni wa Zanzibar ambaye si haba alisafiri kwenda sehemu mbali mbali kufuata elimu sio mwengine ila ni Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry.

Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry inasemekana kuwa alizaliwa mwaka 1290 A.H (1873).
Sheikh Ahmad alianza kusoma kwa Sheikh Ali Bin Abdallah Al-Mazrui na ndipo alipopata msingi wa elimu. Baada ya hapo akaelekea Mombasa, na huko alikutana na wanavyuoni mbali mbali na kukaa huko mpaka watu wakadhani kuwa hatorudi tena Zanzibar.

Alirudi Zanzibar baada ya kufa Sheikh Ali bin Abdallah. Kabla hajenda kusoma kwa Seyyid Ahmad bin Sumeyt na Sheikh Abdallah Bakathir, alikwenda kusoma kwa Sheikh Muhammad bin Ahmad Al-Muroni na kwa Sheikh Abdul-rahman Mweze Mbamba.

Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry alikuwa kati ya wanafunzi wakubwa wa Sayyid Ahmad bin Sumeyt na Sheikh Abdallah Bakathir, na akawa mwenye kuhudhuria darsa zao zote walizokuwa wakisomesha na akawa ni mwanafunzi aliyekubalika na Alim wote hao wawili walikuwa wakimtukuza na walimkubali ya kuwa anafahamu vizuri.

Kwa hivyo wakiulizana nae katika baadhi ya mambo yanayofanya matata na wengi wakisema Sheikh Ahmad amepata kufunuliwa elimu na wajuzi hawa wawili.

Hapo mwanzo nilikwishaeleza kuwa Sheikh Ahmad akipenda kusafiri kwa kwenda kutafuta elimu na katika safari zake alitembelea nchi ya Misri, Sham na nchi nyenginezo.

Kati ya aliobahatika kukutana nao Misri alikuwa ni Sheikh Muhammad Abdoo. Huyu alikuwa ni Mufti wa Misri nzima na ni mwanachuoni mkubwa kabisa. Sheikh Ahmad aliweza kudondoa cha hapa na pale kwa Mufti huyo, kisha akahudhuria darsa za Sheikh Salmy Al-Bishry, Sheikh Al-Islam wa Misri na vile vile akaenda kwa Seyyid Ahmad Bey-Al-Husseyny, huyu akiwa ndio mtu wa mwanzo kupiga chapa ‘Al-Umm’ ya Imam Shafi, akampa hiyo Al-Umm na vitabu vyengine Sheikh Ahmad ili iwe hidaya kwake.

Na alipofika Hijaz kati ya aliyekutana nao alikuwemo Sheikh Muhammad Bin Suleiman Hasballah. Huyu ni mtunzi wa kitabu “Riyadhal-Badiah”, na Sheikh Ahmad alimtaka mtunzi huyo ampe ‘Ijaza’ ya kusomesha kitabu hiki na vyenginevyo, naye alimpatia Ijaza. Naye Sheikh Ahmad alivisomesha vitabu hivyo vyote na kuwapa baadhi ya wanafunzi wake Ijaza.

 Katika usomeshaji wa darsa, Sheikh Ahmad alikuwa akisomesha kwake nyakati za usiku na akisomesha nyakati za alasiri na zile nyakati za asubuhi akipatikana Msikiti Barza na katika mwezi mtukufu wa Ramadhani alikuwa na kazi nzito ya kusomesha kwani alikuwa akidarasisha kuanzia saa 5 asubuhi hadi nyakati za alasiri.

Baada ya kustakimu siku nyingi Zanzibar, Sheikh Ahmad alihamia Ngazija na huko alikuwa na wanafunzi wengi, lakini inavyoeleweka Sheikh Ahmad hajaishi siku nyingi nchini Ngazija na alifia mji wa Mitsamihuli Mwezi 23 Mfunguo 7 mwaka 1357 A.H (23 Juni 1936).

Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry ni mtu wa kupigiwa mfano kwa safari zake za nje za kwenda kutafuta elimu na kubahatika vile vile kukutana na vigogo mbali mbali, ambavyo vilimmiminia elimu si haba.

Mola atupe hima nasi kuuiga mfano mzuri wa Sheikh Ahmad Bin Muhammad Mlomry
“Ameen.”      

No comments: