Wednesday, 1 April 2015

Sheikh Muhyiddin Bin Sheikh - Hamza Z. Rijal

Sheikh Muhyiddin Bin Sheikh

Na Hamza Z. Rijal

Kati ya maalim wa Kishafi waliotia msingi wa elimu ya dini Visiwani ni watatu, nao ni: Sheikh Muhyiddin, Sheikh Ahmed Bin Sumeyt na Sheikh Abdul-Aziz Bin Abdul-Ghany Al-Amawy.

Sheikh Muhyiddin Bin Sheikh alizaliwa Barawa mwaka wa 1206 AH(1718 AD). Katika zama zake katika uwanja wa elimu ya dini ya kiislam, ilikuwa huwezi kutaja wasomi wa kiislam wawili asiwe yeye ni mmoja.

Makaazi yake yalikuwa ni Mombasa wakati wa zama za Sayyid Said, wengine wanasema kuwa Sheikh Muhyiddin kuja kwake Zanzibar kulitokana na kutakiwa kufanya hivyo na Mfalme Seyyid Said.

Alitokea kupendwa sana na Mfalme huyo na alikuwa akipelekwa nchi mbali mbali zilizokuwemo chini ya himaya ya Ufalme, akafanya suluhu pale panapotokea mtafaruku na mara nyingi alifaulu kutekeleza kazi hiyo.

Sheikh Muhyiddin ndiye mjenzi wa Msikiti wa Ijumaa wa Malindi, ambao hivi sasa umejengwa tena kwa kufuatwa kigezo kile kile cha mwanzo.

Sayyid Majid Bin Said Sultan alimsaidia sana katika ujenzi wa Msikiti huo. Baada ya ujenzi wa Msikiti huo, Sheikh Muhyiddin alijisogeza Msikiti wa Kiponda uliokuwa karibu na Sharif Dewji, lakini kwa siku hizi tutaita kwa Makapu.

Sheikh Muhyiddin alisomesha wanafunzi wengi, ambao baadae walikuja kuwa ni walimu wakubwa kabisa, kati ya hao ni Sayyid Ahmad Bin Salim Bin Abubakar Salim, Sheikh Abdul-Aziz Bin Abdul-Ghany Al- Amawy, Sheikh Suleiman Hayat, Sheikh Muhammed bin Ahmed Bin Hassan Al-Murony, Sheikh Hassan Bin Yussuf Mugazija, Sayyid Omar Bin Salim Baalawy, Sheikh Ahmad Bin Salmin As-Sabahy, Sheikh Fadhil Bin Ali Mugazija, na Sheikh Shauri Bin Haji Shirazy. (Toleo litalofuata nitawazungumza hawa wote kwa Mukhtasar, yaani wanafunzi wa Sheikh Muhyiddin.)

Katika sifa nzuri alizokuwa nazo Sheikh Muhyiddin, ni alikuwa mtu mwenye uadilifu. Hukumu zake zote zilikuwa hazina upendeleo, ilitokea safari moja Sayyid Bakarish Shatry alikuwa na kesi yake na mwenziwe, basi akenda kwa Sheikh Muhyiddin akampa riali 50, Sheikh Muhyiddin alipomuuliza za nini? Sayyid Bakarish akamwambia hiyo ni zawadi tu, hiyo ni tunu. Sheikh Muhyiddin akapokea akenda nazo ndani akazifunga vizuri, zote pamoja na roboto moja, akaandika juu ya roboto "Hii dhamana ya Sayyid Bakarish Shatry, nikifa apelekewe mwenyewe", basi alipokufa agizo lake lilitekelezwa. Angalia insafu ya watu waliokuwa nayo ya mtoaji wasia na watekelezaji wa wasia.
Sheikh Muhyiddin alitunga vitabu vingi kati ya hivyo ni:

- Kitabu kidogo cha Tawhid,
- Mashairi ya Kiarabu,
- Mashairi ya Kiswahili,
- Tarehe ya Kilwa (Sulwa fy Akhbar Kulwa),
- Utenzi wa Hadithi ya Miraji,
- Kitabu kidogo cha kufundishia Sarfu na
- Sherhe ndogo ya Khutba ya Minhaj.

Vile vile aliandika shairi la dua ya kuomba mvua katika mwaka 1278 AH (1862)
Hebu na tuzisome beti saba za shairi hilo.

1. Naanza kubtadi, Kwa isimu yake Karima
Kuomba Wadudi, Mtukufu mwenye adhama
Nabii Muhammadi, Msalie kiumbe chema
Tupate miradi, Ifurahi yetu mitima(nyoyo)
Siku ya tanadi(kiama), Waja asi wakilalama

2. Na alize thama(kadhalika), Watukufu wenye ajiri(thawabu)
Wenye sifa njema, Simba zake tumwa bashiri
Na waliosimama, Kuendesha mambo ya kheri
Hao wa qadima(zamani), Na nyengine zote dahari
Siku ya qiyama, Tuokoke na Jahannama

3. Nimetia tama(nimemaliza), Dibaji sitakithiri
Nina mambo mema, Nayawaza kiyafikiri
Haya makulima, Yadhiika kwa nyingi hari
Twaomba rehema, Kwa Wahabu mwenye amri
Tutuze mitima, Kwa rehema yako Karima

4. Mola Subhana, Mola wetu uso shirika
Ndiwe Rahmana, Na Rahima uso shaka
Warehemu wana, Na wazee wenye mashaka
Waijua sana, Hali yetu kati ya chaka(kukosa mvua)
Jua la mchana, Na usiku lisilokoma

5. Ilete mvua, Iondoke nyota(kiu) na jua
Ndiwe mwenye quwa(nguvu), Ufishao na kufufua
Hali waijua, Huhitaji kuarifiwa
Hasha kuemewa, Ni amri ‘KUN’ ikawa
Wala kutendewa, Jalla Rabbi mwenye adhama

6. Wengi waaayisi(wamekata tamaa), Kwa mateso kuwa tawili
Wana wasi wasi, Kwa madhambi yao thaqili
Rabbi tunafisi, Mola wetu uso mithali
Na yawe mepesi, Iwe ‘KUN’ yako kakima

7. Rabbi twafikie, Toba njema yenye nadama(majuto)
Utughufurie, Kuu dhambi ziwe lamama(ndogo)
Wewe unenee, ‘Ud-uni’ yako kalima
Tuwasalie, Kwa isimu yako adhima
Dua na ipae, Na qabuli ije kwa hima.

Sheikh Muhyiddin alifariki katika mwezi wa Shaaban tarehe 27 mwaka 1286 AH (Disemba 1869). Akiwa ameacha pengo kubwa baada ya kuaga dunia, lakini si haba kwani aliacha wanafunzi wengi ambao walikuwa wakisifika na kuifanya kazi aliyoiacha Sheikh wao barabara.

"Ewe Mola tupe hima na juhudi za watangulizi wetu hawa waliopita Ameen,"


No comments: