Sheikh Shauri
Al-Shirazy
Na
Hamza Z. Rijal
Zanzibar
ilikuwa ni kituo muhimu cha elimu ya dini ya kiislamu hata
pale waislamu wa Afrika Kusini walipotanzwa juu ya suala zito la kidini na
kukosa wakulisuluhisha suala hilo, ndipo walipoamua kulipeleka suala
hilo Makka ili kuweza kupatiwa ufafanuzi. Maulamaa wa
Makka waliipa kazi hiyo maulamaa wa Zanzibar.
Zanzibar
ilikuwa ni kioo kwa yule atakayekujitizama uwezo wake
kielimu, hayo yalishamiri katika kipindi cha karne ya 19 hadi katikati ya karne
ya 20.
Walipita
masheikh wakubwa wakubwa ambao wakitukuzwa kwa elimu,
adabu na mwenendo mzuri waliokuwa nao. Miongoni mwa wanavyuoni waliokuwa
maarufu zama hizo na kuacha athari kubwa baada ya
kuondoka kwao, mmoja wao alikuwa ni sheikh Shauri Bin Haji Ashirazy mzaliwa wa
Tumbatu.
Sheikh
Shauri inelezwa kuwa alisoma kwa gwiji ambaye
alikusanya fani zote za elimu ya dini ya kiislamu ambae ni Sheikh Muhidin bin
Sheikh. Kati ya wanafunzi ambao Sheikh Shauri alipiga goti nao kwa Sheikh
Muhidini, walikuwa Sayyid Ahmed bin Salim , Sheikh
Abdul Aziz bin Abdul Ghany. Sheikh Suleiman Hayat na wengineo
.
Aidha
inaelezwa kuwa Sheikh Shauri bin Haji alipokuwa katika umri wa
makamo aliondoka Tumbatu na kuelekea mjini kuitafuta elimu kama
tunavyosisitizwa na dini yetu ya kiislamu kuwa tuitafute elimu popote pale kama
hadithi ya bwana mtume isemavyo: "Itafteni elimu hata China".
Kama
nilivyotangulia kueleza kabla, kuwa mwalimu wa sheikh Shauri alikuwa ni Sheikh
Muhidin Bin Abdallah Al-Kahtany, Sheikh Shauri alifika pahala ndipo kwa
kujiendeleza na kujikuza , kwani Sheikh Muhidin
alikuwa na uwezo wa kutoa fatwa mas-ala mbali mbali ya kidini na akisomesha
fani mbali mbali za elimu ya dini. Ilikuwa kupita kwake na
kuambiwa umekubalika ilikuwa ni sawa kwa sasa umefuzu katika chuo kikuu
chochote kile cha kidini.
Kutokana
na kazi zake Sheikh Muhidin kuzimudu vya kutosha ndipo
hata mfalme wa siku hizo Sayyid Said alivutiwa naye na kumpa kazi ya ukadhi.
Sheikh huyu inafahamika kuwa ndiye aliyejenga msikiti
wa Ijumaa wa Forodhani kwa kusaidiwa na mfalme wa wakati huo Seyyid Majid Bin
Said bin Sultani.
Baada
ya Sheikh Shauri kuhitimu masomo yake na kukubalika
kuwa sasa anaweza kudarasisha, Sheikh Muhydin alimpa ruhusa mwanafunzi wake
arudi shamba, lakini safari hii badala ya kurudia Tumbatu alitua Donge. Maskani
yake ya kwanza ilikuwa ni Donge Muwanda, hapo aliweza
kujinunlia shamba na kustakimu. Aliweka darsa kubwa ikawa watu wanatoka maeneo
mbali mbali kwenda kusoma kwake na wengi wa wanafunzi
walikuwa wanatoka Kinyasini, Bumbwini na umbali wa kutokea Tumbatu. Wote hao walikuwa wakifuatia darsa za sheikh huyu mashuhuri.
Mbali
ya darsa za kila siku, vile vile Sheikh Shauri alikuwa akiendesha darsa za
wiki. Inaelezwa kuwa sheikh huyu akiimudu vilivyo darsa ya kutafsiri Qurani kwa kutumia kitabu cha “Jalaleyn”.
Mbali
ya tafsiri ya Qurani aliyokuwa akisomesha vile vile vitabu alivyokuwa
akidarasisha vilikuwa pamoja na Taajul Arusi cha Sheikh Sakandri, Ulbati Sadik , Murshadi Awami, Ghaya na vyenginevyo ambao warithi
wake wote nao walikuwa wakivisomesha na vinaendelea kusomeshwa hadi hii leo.
Baada
ya Sheikh Shauri kuona kazi yake imeweza kutoa matunda alihamia Donge Msalani, kama alivyofanya alipokuwa Donge Muwanda na hapo Donge
Msalani alijinunulia shamba ambalo ndilo lililokuwa likimuendesha maisha yake.
Watu wa daraja za kina sheikh Shauri ni kati ya wale
walioufahamu fika mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) wa mtu kupata riziki yake
kwa jasho lake kinyume cha wale tuliokuwa nao zama hizi.
Aidha
historia inaeleza kuwa Donge Panga Maua ndio kilikuwa ni
kituo cha mwisho cha Sheikh Shauri. Inafahamika kuwa sheikh Shauri aliweka
markaz kubwa hapo Donge Panga Maua na alipata
wanafunzi wengi ambao baadaye walishika makamo yake. Kati ya hao ni Sheikh Haji Bin Vuai Shirazy na Sheikh Suleiman Ali. Hawa
wawili walikuwa ni wazaliwa wa Donge , vile vile
sheikh Ali bin Umar Shirazy huyu alikuwa kati ya wanafunzi wake wakubwa ambaye
hakuwa mkazi wa Donge.
Mbali
na kuwafunza wanaume , aliweza kumuelimisha vya
kutosha mkewe Mwana Alama ambaye naye alikuwa akidarasisha wanawake wenzake na
kuendeleza darasa kwa wanawake. Ilikuwa kwa mwanamke haina haja ya kwenda
kuuliza kwa Sheikh kwani bibi huyu naye alikuwa akizimudu fani nyingi, ambapo
kwa hivi sasa wanakosekana wanawake wa sampuli hiyo.
Sheikh
Shauri alibarikiwa watoto watano akiwemo Shadhili, Moh’d, Mahmond na wawili wakiwa wasichana. Shadhili Shauri Shirazi ni mmoja
kati ya watoto wake ambaye alifanikiwa uzazi na kuzaa watoto saba akiwemo
Haroun, Daud,Farasini, Shauri, Abdulsamad, Ziyabu na
Khadija.
Kwa
mujibu wa simulizi za uhakika Sheikh Shauri Shadhili Shauri
al Shirazy wengi wakipenda kumwita Shauri mdogo, kijana huyu aliweza kuelimika
vya kutosha kutoka kwa baba yake Sheikh Shadhili, na ndipo ukasibu ule
msemo mtoto hufuata kisogo cha mzeee wake. Shauri mdogo alishika usukani naye
baadaye akaziendeleza darsa alizozirithi kwa baba yake
ambaye zinatokana na msingi aliouweka babu yake.
Ni
jitihada ya kushukuriwa ya kina sheikh Machano na
sheikh Shamim ya kuendeleza elimu katika eneo la Donge ambayo mwanzilishi wake
ni Sheikh Shauri. Pamoja na masheikh hawa wawili kuwa na
shughuli nyingi mjini, hawakuitupa Donge na kukumbuka kuwa mtu kwao ugeni sio
kitu chema. Masheikh hawa hutumia siku za mwisho wa
wiki kwenda Donge na kudarasisha.
Leo
Donge zipo darsa, lakini sio kama zilivyokuwa
zikiendeshwa siku za Sheikh Shauri mwenyewe, jitihada zaidi zatakikana kwa
upande wa masheikh na wanafunzi kwa kuweka misingi madhubuti ya kuihuisha dini
yetu na kuirejeshea Donge hadhi yake na Zanzibar kwa jumla.
Tunamuomba “Allah”
atuwafikishie hayo. “AMIN”
No comments:
Post a Comment