Saturday, 9 May 2015

TATIZO NI MADRASA AU NI AJENDA YA KUUDHURU UISLAMU - SHEIKH KOMBO HASSAN


http://www.iium.edu.my/deed/quran/swahili/1_0.gif
TATIZO NI MADRASA AU NI AJENDA YA KUUDHURU UISLAMU?
Sehemu ya Kwanza

na 
Kombo Hassan 

Asalaam Aleikum,
Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu Swala na Amani zimfikiye Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na jamaa zake.

USULI WA TATIZO

Historia ya Elimu ya Madrasa Tanzania inasibiana na Historia ya kuenea kwa Uislam katika Afrika Mashariki kuanzia Pwani hadi bara. 
  • Elimu itolewayo na Madrasa zetu ilichipuka tangu wakati walivyoanza kuja Waarabu kutoka Saudia, Oman, Uajemi, Hadhramaut na Yemen. Karne ya 9 na 10 wahamiaji kutoka Saudia walianza kusini BENADIR (Pwani ya Somalia). 
  • Karne ya 12 Waarabu walianza kufika hadi mji wa Kilwa. 
  • Karne ya 12 wageni kutoka Hadhramawt na Yemen waliingia Afrika Mashariki.  Wageni hawa nao pia walitoa elimu inayohusu Uislam. 

Kustawi kwa Elimu ya Madrasa Afrika Mashariki:

Mwaka 1332, Mwarabu aitwaye IBN BATUTA alipotembelea Kilwa alikuta mji umekaliwa na  waliokuwa wakitumia lugha ya Kiswahili. Baadaye miji ya Tanga, Dar-es-Salaam, Mombasa, Lamu, Malindi, na Mikindani vikawa vituo vya kueneza uislam na elimu ya kiislam katika miji ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Zaire, Msumbiji, Malawi na Burundi.

Wajerumani walipofika Tanganyika waliwakuta Waislam wanafahamu kuandika, kusoma na walikuwa wameelimika katika hesabu. Mmishionari Ludwig Krapt alipofika kwa Chifu Kimweri wa Usambara mwaka 1848 walikuta yeye na  wanae wote wanajua kusoma. Rejea: (I.N. Kimambo, na A.J.A. Temu, "History of Tanganyika," EAPH, Nairobi, 1969 uk. 126).
Herufi walizokuwa wakitumia zilikuwa za Kiarabu. Wajerumani kwa ajili hii basi waliwaajiri Waislamu kama walimu, wakalimani na makarani serikalini. Elimu hii yote na utamaduni wa ustarabu wa hali ya juu  ulikuwa unatokana na Uislamu  na shule za Madrasa. Hapo ndipo ilipoanza mbinu  ya kuvunja maendeleo  haya yote.

Herufi za Kiarabu zikapigwa marufuku kutumika na badala yake watu wakalazimishwa kujifunza herufi za Kirumi. Muislamu ambaye jana alipoingia kulala alikuwa anaitwa ameelimika akaamka asubuhi yake mjinga, hana elimu, hajui kusoma wala kuandika. Njama zote hizi dhidi yaUislam ilikuwa sehemu ya makubaliano kama ilivyoandikwa katika kifungu IV cha Mkutano wa Berlin  wa mwaka 1884. Kifungu hicho kilikuwa kinasema kuwa Ukristo ni lazima ulindwe dhidi ya Uislam. (Rejea: H.B Hansen, “Mission, Church and State in Colonial Setting: Uganda 1890-1925,” London 1984, uk. 26, vile vile angalia Ali M. Kirunda, Uganda Muslims and their Problems,” The Monitor June 4-June 8, 1993).

Na wamishonari  walifuata nyayo za Madrasa na walimu wa kwanza katika shule za misheni  walikuwa Waislam ambao  hawakusoma katika shule za kanisa bali  katika Madrasa. Rejea: (Abel Ishuwi, “Education and Social Change,” (1980).
Mwaka 1882, Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Gladstone, akiwa ameinua juu  Qur’an, alisema kuwaambia wabunge wa Uingereza (House of Commons):
“So long as the Egyptions have got this book with them, we will never be able to enjoy quite of peace in that land.” (Muhammed Qutb 1972: xi)

Tafsiri:
“Madhali Wamisri wanacho kitabu hiki hatuwezi kamwe kufurahia utulivu au amani katika nchi ile.”

Katika miaka 1900, kauli kama hiyo ilitolewa na Waziri wa Makoloni ya Uingereza huko Uturuki pale aliposema:

“Muda wa kuwa Waislamu wanayo Qur’an, basi watakuwa kikwazo kwetu. Kwahiyo ni lazima tuiondowe kutoka maishani mwao.”

Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimekuja na mbinu ya kistratejia kama wahisani kwa njia ya kuwashajihisha Waislamu kujioganaizi kwa kuwa na mtaala mmoja wa dini,  kuanzisha “NGO’s” za  ujasiriamali ili kuweza kukabiliana na makali wa umasikini uliowapiga Waislamu wengi n.k. 

Marekani kwa kupitia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa zamani Bw. Collin Powell, na Waziri wa Ulinzi Bw. Dolnad Rumfeld, wamesema kuwa umadhubuti wa Waislamu unatokana na wao kusoma, kufundisha, kuiamini na kuifuta Qur’an. Hivyo ufumbuzi wa kudumu ni kuwatoa Waislamu katika Uislamu wao kwa kuingilia mafundisho ya Qur’an. Na njia nzuri ni kuanzia kwenye Madrasa zao. Kampeni hiyo iwe ya dunia nzima. Hapa tutaangalia tu wanayoyafanya Tanzania na mafanikio yao ukilinganisha na yetu sisi Waislamu.

Njia ya kwanza waliona ni kutoa misaada kwenye madrasa ili iwe ni mwanya na hatimaye kubadilisha mitaala ya madrasa. Huko Kenya wakaenda kwa pupa kwa balozi wa Marekani kutoa rundo la misaada ya vitabu na pesa kwa madrasa. Waislamu wakashituka na wakakataa. Makafiri hawakukata tamaa walijifunza kosa lao. Hapa Tanzania, wakaamua kuwa kwanza kabisa waanze na utafiti utakaowajulisha ukweli halisi juu ya madrasa. Nawakaona ili Marekani wasionekane waziwazi. Wakawatumia watu wengine, yaani Shirika la Kijerumani liitwalo Konrad Adeneur Stiftung. Mwezi Mei/Juni 2003 walifanya utafiti wao walioita “Qur’an Madrasa Baseline Survey.”

Yaani utafiti wenye lengo la kujua hali halisi ya madrasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam. Waligundua mengi, lakini kwa sasa tuseme tu kuwa baadhi ya waliyojua ni kuwa karibu ya nusu ya walimu wa madrasa wanapata mshahara wa mdogo. Wengine hawalipwi kabisa. Theluthi mbili ya madrasa zinamilikiwa na watu binafsi na zipo vibarazani. Kwa ufupi ni kuwa Serikali ya Marekani kwa kupitia Shirika lake Liitwalo USAID linasaidia madrasa huko Zanzibar. Hivyo Waislamu tunasaidiwa kwa kupitia mifuko mikubwa minne:

ð  Mfuko wa Rais Bush wa Elimu ya Waislamu (President Bush’s Muslim Education  Initiative).
ð  Mfuko wa Rais Bush wa Kupambana na Ugaidi Afrika Mashariki (President Bush’s East African Counter-terrorism Initiative).
ð  Skolaship za Balozi kwa Wasichana (The Ambassador’s Girls’ Scholarship Program).
ð  Mfuko wa Elimu Afrika (African education initiative).

Wanazitumia pesa hizo kuwasomeshea Waalimu wa Kiislamu, kuandaa mitaala na vitabu, kuwalipa mishahara waalimu, na viongozi wa jamii, na kusaidia pia kipesa watoto wa masikini. Wameanzisha pia Kituo cha Vitabu vya rejea vya Madrasa Zanzibar (The Zanzibar Madrasa Resource Centre). Misaada hiyo Marekani kwa kupitia mradi wa MKEZA (Mradi wa Kuendeleza Elimu Zanzibar) imekwisha kujenga madrasa 16 (mpaka mwaka 2007) moja ya madrasa hizo aliyotembelea mke wa Bush, Laura, Julai 2005. Kwa mujibu wa USAID wenyewe Marekani ni wafadhili wakubwa kwenye nyanda ya elimu huko Zanzibar.
***
Kwa upande wa Tanzania bara USAID kwa kushirikiana na BAKWATA wametoa kitabu cha Mwongozo wa kufundishia waalimu wa Kiislamu. USAID pia imetoa mafunzo kwa  waalimu 54 wa madrasa ya kuwafundisha watoto wa kiislamu namana ya kupambana na UKIMWI. Mwongozo huo waVitabu 2,500 uligawanywa kwa waalimu wa madarasa Dares Salaam na Iringa. (Taarifa hizi zote zimepatikana  kutoka katika tovati ya USAID/Tanzania). Rejea: Islamic Propagation Centre (2007).  

Kwa mujibu wa  Hotuba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali  (SMZ) kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2013/2014: 

“Elimu ya Madrasa na Vyuo vya Kuran

          52. Mheshimiwa Spika, Idara hii inashughulikia jumla ya madrasa/vyuo vya Kur-  ani 2,251.  Aidha zipo skuli za maandalizi za madrasa 84, Unguja na Pemba zinazosimamiwa na kuhudumiwa kupitia Kituo cha Zanzibar Madrasa Resource Centre (ZMRC), ambazo ufundishaji wake unafuata misingi ya dini ya kiislamu.

        53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF inakusudia kutoa mafunzo kwa walimu wa madrasa/vyuo vya Kur-ani 350, Unguja 200 na Pemba 150. Pia itaendelea kufanya ziara mbali mbali za kikazi katika madrasa na vyuo vya Kur-ani pamoja na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kushajiisha kufanya ziara za pamoja za kubadilishana uzoefu.”  (Mwisho wa kunukuu).

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“217...Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.” (Al Baqara 2:217)
“120. Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.” ( Al Baqara 2:120).

Kwa mujibu maelezo hayo hapo juu hii ni  “Strategic Plan” (Mpango Mkakati) wa vita dhidi ya Uislamu na Waislamu ili kulizivuga na kuingilia/kuharibu mafundi yake ili ziwe ni zenye kuzalisha Waislamu “Mazezeta”.

HALI ILIVYO SASA  KUHUSIANA NA MADRASA NA VITUO VYA KULELEA WATOTO WALIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

Hivi sasa hapa nchini kumeibuka kadhia  ya serikali kuzifunga baadhi ya madrasa na vituo vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu nk. Hatua hiyo imechukuliwa kwa kile kinachodaiwa kutofuatwa sheria, kanuni na sera za nchi.

No comments: