Baada ya kupokea picha hii kutoka katika nyaraka na picha alizoacha marehemu Ali Msham picha ambazo alinipatia mwanae Abdulrahman Ali Msham na kwa kuzingatia pia kabla sijapatapo kuona picha ambayo Zuberi Mtemvu alipiga na Nyerere imenijia hamu ya kuweka hapa historia ya hawa wazalendo wawili ambao baadae walikuja kuwa maadui wakubwa kila mmoja akimwita mwenzake kibaraka.
![]() |
| Kushoto John Rupia Makamu Rais wa TANU, Julius Nyerere Rais wa TANU na Zuberi Mtemvu Katibu Mwenezi wa TANU, Ali Msham ni wa pili katika waliosimama nyuma |
Ilikuwa
miaka ya 1980 tuko nyumbani kwa marehemu Bi. Mluguru bint Mussa, mama yake Ally
Sykes Mtaa wa Lindi. Pametokea msiba. Bi. Mariamu, shangazi yake Bwana Ally
Sykes amefariki. Watu wamejazana mtaa umefungwa wanasubiri muda wa mazishi.
Bwana Ally mwenyewe kakaa jamvini kazungukwa na jamaa zake wa Gerezani, wamekukuja
kuungananae katika msiba wa shangazi yake. Watu ni wengi sana. Bwana Ally yeye
mwenyewe ni mzishi sasa leo limemfika ndugu zake wamemwitika kwa wingi sana,
wamekuja kumzika. Bwana Ally kuniona ananita nende nikakae nae mbele. Basi
nanyanyuka pale nyuma nilipokuwa kwa unyonge maana umma mzima unaniangalia huyu
anaeitwa mbele pale ana umuhimu gani. Katika lile jamvi alokuwa Bwana Ally ni
“nani aliye nani katika mji wa Dar es Salaam,” Waingereza wanasema “Who is Who”
wenyewe watoto wa Gerezani na Dar es Salaam wametanda. Sasa Bwana Ally anawanadia watu, “Nyie mnamjua
huyu? Mtoto wa Said pale Kipata mwandishi hodari sana…”
Utambulisho
umekwisha nakaa pembeni Ally Sykes na Zuberi Mtemvu wanashambuliana kwa maneno.
Bwana Ally kalalamika kuhusu hali ya nchi mambo hayendi vyema. Zuberi Mtemvu
kadakia anawashahidisha watu, “Jamani mnasikia Ally analalamika ati mambo
hayendi sawa…” Mtemvu anaangua kicheko cha kejeli huku akitingisha kichwa. Watu
sasa weshakuwa hadhir wanasubiri Mtemvu atasema kitu gani? “Huyu Ally na
marehemu kaka yake (Mungu amrehemu) walikuwa wanashirikiana na Nyerere kukipiga
vita chama changu kife, leo Ally huyu huyu keshageuka ati nchi
imeharibika…”Wasikizaji wanacheka wengine wanamuunga mkono Bwana Ally wengine
Zuberi Mtemvu. Bwana Ally hakubali kushindwa anarudisha kombora, “Ala kumbe
Congress bado mko hadi leo nilidhania tulishakumalizeni.” Vicheko. Mzee mmoja
kwa mbali anaita, “Ally sikiza bwana, Congress tupo sana. Congress ni mwamba
usiovunjika.” Vicheko vinaendelea. Hii “Congress ni mwamba usiovunjika,” ni
maneno yaliyokuwa katika nyimbo ya Congress wakati wa harakati za kudai uhuru.
Kwangu
mimi pale nilikuwa nasoma na kupata mazingatio. Nilikuwa nikiifahamu vema
historia ya Zuberi Mtemvu na mwalimu wangu alikuwa Ally Sykes. Nilikuwa
nimemsoma Mtemvu katika nyaraka za Sykes. Mtemvu ni mmoja wa wanachama wa
mwanzo shupavu na msomi kabisa kujiunga na TANU. Katika nyaraka za Sykes kuna
“note” ya mwaka 1954 aliyoandika Zuberi Mtemvu kwa penseli kumpelekea Ally
Sykes akimtaarifu kuwa kakutana na Ally Mwinyi Tambwe na amemweleza kuhusu
chama kipya cha siasa kinachotaka kuanzishwa. Katika “note” ile Mtemvu
anamfahamisha Ally Sykes kuwa Ally Mwinyi Tambwe kakubali kukiunga mkono chama
hicho kipya. Mtemvu alimjulisha Ally Sykes kuwa Tambwe kukubali kujiunga na
TANU lilikuwa jambo zuri sana. Tambwe,
Mngazija wakati huo alikuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.
Tambwe alimwahidi Mtemvu kuwaingiza TANU wanachama wengine wanaounga mkono harakati
zile.
Mtemvu
alimfahamu Nyerere siku zile za mwanzo
alipokuwa akija Mtaa wa Kipata kwa Ally Sykes. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe
Manga Mtemvu, alikuwa amejenga nyumba yake nyuma ya nyumba ya Kleist Sykes,
baba yake Ally. Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuzungumza kama alichokuwanacho
Nyerere, Bibi Titi na Sheikh Suleiman Takadir. Mtemvu alikuwa na kipaji cha
kuweza kushawishi na kuwashirikisha watu katika harakati. Takriban mwezi mmoja
baada ya kuundwa kwa TANU Nyerere na Mtemvu walikwenda kuifanyia kampeni TANU
huko Morogoro ambako ndiko ilipokuwa asili ya ukoo wa Mtemvu. Baba yake Mtemvu,
Mzee Mwinshehe, alikuwa ameongea na baadhi ya wezee wenzake kuhusu TANU.
Ijapokuwa Nyerere alijaribu kwa uwezo wake wote kuwafikishia watu ujumbe wa
TANU matokeo hayakuwa mazuri. Katika barua ambayo Mtemvu alimwandikia Ally
Sykes mnamo Agosti, 1954 aliwaelezea watu wa kabila lake kama “wagumu.” Mtemvu
alimuelezea Ally kwa ufupi juu ya mkutano wao na Nyerere Morogoro mjini na
aliomba apewe mara moja kadi 200 za TANU.
Ally aliwaandikia na kuwapa kadi za uanachama wa TANU, Mtemvu na Tambwe
na akamwambia mdogo wake Abbas, awaalike wote wawili kwenye mkutano wa uzinduzi
wa tawi la TANU la Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Arnatouglo ambao ulikuwa
ufanyike Jumamosi inayofuata. Nilipokuwa
nawatazama pale mazikoni Ally Sykes na Zuberi Mtemvu walivyokuwa wakitaniana
nilizidi kupata uhakika kuwa kwa hakika wazalendo hawa walikuwa wakijuana vyema
na historia yao ni ndefu na inatoka mbali.
Si
watu wengi sana wenye kujua kuwa ni Nyerere ndiye alimshauri Mtemvu aache kazi
serikalini ajiriwe na TANU. Mtemvu alikubali ushauri ule na akaacha kazi. Kwa ajili
hii basi Mtemvu akaja kuwa katibu wa kwanza wa TANU na Waingereza wakimchukulia
Mtemvu kama mtu mwenye siasa za upande wa
kushoto sana katika TANU. Hivi ndivyo ilivyokuwa Zuberi Mwinshehe Manga
Mtemvu akaja kuwa mmoja wa viongozi wa juu katika TANU. Katika siku za mwanzo nafasi ya katibu
mwenezi ilikuwa ikishikwa na viongozi mbali mbali baina ya Mtemvu Denis
Phombeah, Oscar Kambona, Iddi Faizi Mafongo na Stephen Mhando. Mtemvu akiwa
katibu mwenezi alikuwa na kazi ngumu ya kuwashawishi na kuushirikisha umma
katika harakati za kudai uhuru na kusajili matawi ya TANU. Ili kampeni ya
kuwaingiza wanachama katika TANU ifanikiwe na ujumbe wake uwafikie wananchi
ilibidi TANU ifanye mikutano ya hadhara. Kwa bahati mbaya serikali ikawa
haitaki kutoa kibali kwa TANU ifanye mikutano. TANU ilijikuta katika hali
ambayo haiwezi kuwasiliana na umma kuutayarisha katika harakati za kudai nchi
yao. Katika hatua kadhaa za ujasiri Mtemvu alifanya mikutano ya hadhara bila ya
kupata kibali cha serikali. Nyerere mtu wa hadhari hakutaka kuonekana anavunja
sheria. Alifahamu kwamba vitendo kama hivyo vingesababisha matatizo kutoka
serikalini.
Jambo
kama hilo lilikuwa sawa na kuikaribisha misukosuko bila sababu ambayo
ingeathiri TANU na uongozi wake wote. Nyerere, kama rais wa TANU, alikuwa
amepokea barua kadhaa kutoka kwa Chief Secretary, T. Griffith-Jones, kuhusu
mikutano isiyokuwa na kibali aliyokuwa akiifanya Mtemvu. Lakini kwa hakika kwa
TANU kunyimwa haki ya kuitisha mikutano ilikuwa sawasawa na kuifunga mikono.
Hakukuwa na namna nyingine TANU ingeweza kufanya ili iwasiliane na watu. Kuacha
kufanya mikutano TANU ingebakia dhaifu na harakati zingekufa. Mtemvu alikuwa
akifahamu kuwa serikali ilikuwa imedhamiria kabisa kuiua TANU ingali bado
changa. Akiwa bado amenaswa katika kitendawili hicho cha kibali cha kufanya
mkutano, Mtemvu alipata nakala ya mkutano wa 674 wa Baraza la Udhamini la Umoja
wa Mataifa ambayo Attorney General, Gratten Below, alifafanua juu ya msimamo wa
serikali kuhusu suala hilo. Mwanasheria Mkuu aliarifu kwamba watu wanaweza
kuanza shughuli za chama mara tu maombi ya usajili ya chama cha siasa
yatakapowakilishwa; na wanaweza kuendelea na shughuli za siasa mpaka majibu
kutoka kwa Msajili Mkuu yamepokelewa kwamba tasjili imekataliwa. Uongozi wa
TANU katika makao makuu ulisisimka kwa taarifa hiyo iliyofukuliwa na Mtemvu. TANU
daima itamkumbuka Mtemvu kwa juhudi zake za kuiingiza TANU Mafia ambako alihutubia
mikutano iliyofurika watu. Nyerere alimwambia Mtemvu watu wa Mafia watakuelewa
wewe zaidi ya mimi.
Bahati
mbaya sana Mtemvu alitupana mkono na Nyerere na TANU mwaka 1958 pale serikali
ya kikoloni ilipoandaa uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa
vishindaniwe kwa misingi ya utaifa. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu,
Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura
yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na
kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi
maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza
kukubalika na TANU. Mtemvu hakuona mantiki ya kuwaingiza Wazungu na Waasia
katika Baraza la Kutunga Sheria na hakuficha msimamo wake na kwa hakika
wanachama takriban wote wa TANU walipinga kura tatu. Wana TANU walikuwa na
kauli mbiu yao wakisema kuingia kura tatu ni sawasawa na “kujipaka kinyesi.” Mtemvu
na wengi waliokuwa wakimuunga mkono walisisitiza, “Afrika kwa Waafrika.” Lakini
hili jambo likawa linasubiri uamuzi wa mkutano mkuu wa TANU wa mwaka 1958 ambao
ulikuwa ufanyike Tabora.
TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa
1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari kujadili miongoni mwa mambo
mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya masharti haya ya kibaguzi
yaliyowekwa na Waingereza au wasuse. Mkutano ule ulitishia kuigawa TANU katika
kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea
kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali
waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza
kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama
Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao
makuu, na Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi
ambayo yangekigawa chama kama isingelikuwa busara ya Julius Nyerere, Rais wa
TANU na mkakati wa siri alioupanga na viongozi wa TANU Tanga, Mwalimu Kihere na
Sheikh Rashid Sembe.
Lakini
kumuelewa Mtemvu na hisia za wanachama wa TANU, fikra za uongozi wake na nguvu
zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa
kwa nini kura tatu ilileta mgogoro na kutoelewana katika uongozi hata kupelekea
TANU kumegeka kwa mara ya kwanza na Mtemvu kuanzisha chama kingeine cha siasa,
inatubidi turudi nyuma tufuatilie mwanzo wa siasa mjini Tabora, mahala ambapo
TANU ilifanya uamuzi wake ya kihistoria na kuwanasa Waingereza katika mtego wao
wenyewe. Tunahitaji kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo Nyerere
na uongozi wa TANU pale Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa
Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika ule
mkutano ambao wajumbe wa TANU walikutana katika ukumbi wa Parish wa Kanisa
Katoliki, Tabora. Hii itatuwezesha kujua kwa nini mkutano mkuu huu ulikuwa
muhimu. Akiiandikia Fabian Colonial Bureau, Katibu Mwenezi wa TANU, Zuberi
Mtemvu ambae alikuwa amelichambua jambo hili la utatanishi wa kura tatu aliandika
maneno haya,”Katika nchi kama Tanganyika, utajiri na elimu vimo mikononi mwa
wageni. Mwafrika ni maskini na hana elimu. Upigaji kura wenye masharti magumu
yaliyoegemezwa kwenye mali na elimu utawaathiri Waafrika peke yao bila kuwagusa
Wazungu na Waasia hata kidogo. “
Ungozi
wa TANU makao makuu kulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza hata kidogo
kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao makuu ya
TANU palikuwa na viongozi kama hawa, Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir,
Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi,
Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd
Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu
Diwani.Katika hawa ni wachache tu ndiyo waliokuwa na sifa za kusimama kupigiwa
kura au kupiga kura. Na hali ilikuwa kama hivi Tanga, Tabora, Dodoma na mahala
pengine kwingi nchini Tanganyika. Kwa
hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi wa kura tatu.
Mkutano wa Tabora ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na
kushindana na UTP au ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake
mkubwa na hasimu wake ushindi wa bure bila jasho.
Mkutano
wa Tabora kwa shida sana uliamua kuwa TANU ishiriki katika kura tatu. Baada ya kutia saini kwa Azimio la Tabora
Mzee Fundi Mhindi, Nyerere, Dossa, Mwalimu Kihere na Mohamed Mangiringiri
waliondoka pale Parish Hall na kwenda mjini kutafuta simu ili kumpigia Zuberi
Mtemvu makao makuu Dar es Salaam kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU
imepiga kura kuingia katika uchaguzi wa kura tatu. Mangiringiri alimchukua
Nyerere hadi kwa mwajiri wake wa Kiasia, G. B. Somji kupiga simu kwa Mtemvu.
Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi
kwa rais wa TANU, Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu
kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama kipya - African National Congress
(ANC). Chama cha Mtemvu kilikuja kujulikana kama “Congress” neno ambalo
kutokana na vyama vyote viwili jina hili lilikuja kunasibishwa na usaliti.
Mtemvu akimshutumu Nyerere kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na
wananchi; na Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kuacha mapambano na kujiunga na
upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai uhuru.
Msimamo wa Mtemvu ulikuwa “Afrika Kwa Waafrika” - hakuna mgeni atakayekubaliwa
kuitawala Tanganyika.
Mtemvu
alikuwa amelenga kwenye serikali ya Waafrika watupu ndani ya Tanganyika huru.
Ujumbe wa Mtemvu ulipokelewa katika ofisi ya TANU mjini Tabora na mara moja
tarishi alipanda baiskeli kupeleka ujumbe ule mkutanoni kule Parish Hall.
Nyerere aliwasomea wajumbe wa mkutano mkuu ile simu kwa sauti. Ilikuwa ni
habari za kustusha. Hatua hii ya Mtemvu ilikuwa ya pekee katika historia fupi
ya TANU. Hapakuwahi kutokea kiongozi wa chama kujiuzulu na kuanzisha chama cha
upinzani. Mtemvu alikuwa mpinzani wa kura tatu toka mwanzo na Nyerere
aliufahamu msimamo wake. Katika maandalizi ya mkutano wa Tabora ilikuwa Mtemvu
ndiye atakaeongoza hoja ya “kwa nini lazima TANU ikatae pendekezo la kura tatu”.
Lakini baadae Nyerere alimshawishi Mtemvu abaki nyuma Dar es Salaam kuendesha
makao makuu kwa kuwa haitakuwa busara kwa viongozi wote kuondoka na kuiacha
ofisi bila kiongozi wa juu ofisini. Nyerere alimshawishi Mtemvu akubaliane na
ushauri wake na kuhusu hoja ya upinzani wa kura tatu, Nyerere alishauri hoja
hiyo aachiwe Amos Kissenge aiwasilishe kwenye mkutano wa Tabora.
Vita
kati ya Mtemvu na Nyerere inasemekana ilikuwa imeanza siku nyingi na Nyerere
alijaribu kushinikiza atolewe Kamati Kuu ya TANU lakini hili lilipingwa vikali
na John Rupia, kwa hiyo Nyerere hakufanikiwa lengo lake. Miezi michache kabla
ya uhuru Rais wa Congress, Zuberi Mtemvu akiwahutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu
Cha Karl Marx mjini Leipzig, Ujerumani ya Mashariki, Mtemvu alibashiri kuwa
kutolewa kwa uhuru wa Tanganyika kwa uongozi wa TANU, hautabadili chochote kwa
kuwa wanaoingia madarakani wameamua kushirikiana na walewale wanyonyaji wa
zamani na hii itavunja nguvu za wazalendo na matumaini yao. Siku za mwisho za
Mzee Mtemvu alikuwa anakuja nyumbani kwa mwanae Abbas Mtemvu akitokea Morogoro
ambae tukiishi jirani. Nikitoka kazini njia ya kwenda kwangu ilikuwa inapita
mbele ya nyumba yake. Nyakati za jioni Mzee Mtemvu alikuwa akipenda kukaa nje
kupunga upepo. Nikifika pale nilikuwa nakwenda kumwamkia na hapo tutaanza
gumzo. Ilikuwa akinishinda kwa hoja basi mimi humchokoza kwa kumwambia, “Lakini
baba unajua kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika imekuweka wewe katika kundi la
wasaliti?” Hapo ninakuwa nimechokoza nyuki. Mzee Mtemvu atanijibu, “Msaliti
mimi au Nyerere aliyetoa nchi kwa walewale waliokuwa wakitutawala?” Hapo
atazungumza sana na mwisho huagana nikenda zangu. Mtemvu na Nyerere kuanzia
mwaka wa 1958 walinuniana hawakuzungumza hadi mwisho wa maisha yao na kisa cha
ugomvi wao kilikuwa ni kura tatu.

No comments:
Post a Comment