![]() |
Zahaki Rashidi |
Ndugu msomaji,
Ili uweze kufaidikia na kisa cha Zahaki Rashid ni muhimu kwanza
usome mwanzo wa matatizo yake mwaka wa 1998 baada ya kutokea mauaji ya
Mwembechai yeye akiwa afisa wa polisi.
Tafadhali ingia hapa:
Zahaki, mtuhumiwa
wa Stakishari anayeamini anafanyiwa visasi
Zahaki Rashidi Ngai
si jina geni katika masikio ya Waislamu wengi hapa nchini. Yeye ni mmoja kati
ya wanaharakati wachache ambao wametajwa sana
na masheikh, vyombo vya habari na hata katika vitabu maarufu
vilivyoandikwa na waataaluma wa Kiislamu.
Umaarufu wa Zahaki umetokana
na kutajwa shuhuda muhimu wa tukio la
mauaji ya Mwembe Chai na dhuluma mbalimbali ambazo Serikali imewatendea
Waislamu.
Kwa mara ya kwanza,
Zahaki alitoa ushuhuda wake kwa mwanahistoria maarufu Muhammedi Saidi.
Alifanyiwa mahojiano maalum kuhusu ukweli wa mauaji ya Mwembe Chai. Hapo
aliyasema yote aliyoyaiona na aliyoyaamini.
Baada ya hapo,
ushuhuda huo ulichapishwa katika kitabu maarufu cha Prof. Hamza Njozi,
kilichoitwa, ‘Muslim and state in
Tanzania’ .
Zahaki atajwa katika ujambazi
Akizungumza na
gazeti la Imaan kabla ya kwenda polisi kuhoji kutajwa kwa jina lake katika
taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii akitajwa kama miongoni mwa
wahumiwa wa mauaji yaliyotokea kituo cha
polisi Stakishari.
Alisema baada ya
kupokea taarifa hizo za kuhusishwa na uhalifu huo, hatua ya kwanza aliyofanya
ni kutaka kukutana na waandishi wa habari ili Waislamu wenzake wajue ukweli juu
ya dhuluma ambayo jeshi la polisi linajaribu kumfanyia akiamini inatokana na historia
yake ya kusema kweli kuhusu tukio la mauaji ya Mwembe Chai.
Alisema kinachotokea
sasa ni matokeo ya chuki na kisasi cha muda mrefu kilichotokana na uamuzi wake
ya kusema kweli katika tukio lile la mwaka 1998 ambalo lilipelekea kufukuzwa
kazi ya polisi na kufedheheshwa baada ya kulikosoa jeshi hilo.
“Najua mtuhumiwa
akishafika katika mikono ya polisi ni vigumu kukutana na waandishi wa habari na
kuzungumza ukweli. Baada ya kuliona hilo nimeamua kukutana nanyi ili kuwaambia
ukweli Waislamu wenzangu kuwa katika tukio hili mimi sihusiki hata kidogo na
hata huyo anayetajwa kuwa kiongozi wa kundi simfahamu,” alisema Zahaki.
Alisema kutokana na
matukio ya Mwembe Chai, Jeshi la Polisi lilikasirishwa na limekuwa
likimfuatilia kila hatua ili ipatikane
nafasi ya kumpa kesi ili wampoteze
ulimwenguni.
“Ndugu waandishi wa
habari, mimi miaka yote nipo hapa nchini, nina wake wawili ambao naishi nao. Ajabu
ni kwamba Jeshi la Polisi linadai mimi nimerejea kutoka Ethiopia. Huo ni uzushi
ambao wanajaribu kuutumia ili nionekane muhalifu wakati ni uongo mtupu”, alisema Zahaki.
Zahaki aliongeza: “Jeshi
la polisi wawe wa kweli. Wafanye utafiti wao kwa makini badala ya kuvamia watu
kwa kuwa shuku kwani hatua hiyo itafanya kukamatwa kwa watu ambao hawana hatia
jambo ambalo halitamuathiri mtuhumiwa peke yake bali litaathiri maisha ya
watoto, wake na wazazi wake”.
“Mimi nilikuwa
Sajenti katika kitengo cha ‘Crime Stoppers Unit’ -
Central Police. Tukio la Mwembe Chai lilivyotokea mimi nilikuwa ndio ‘in
charge’. Nilitoa maelezo yangu kuhusu taarifa za tukio hilo lakini jeshi
halikuridhika. Wamenifukuzwa kwa aibu na
sasa wananishughulikia nje ya Jeshi la Polisi”. Alilalamika Zahaki huku machozi
yakimlenga lenga.
Ujumbe kwa Waislamu
Zahaki amewataka
Waislamu wenzake kumuombea dua kwa mtihani huo ambao ameupata huku akiwahakikishia
kuwa hajahusika katika uhalifu huo uliotekelezwa katika kituo cha Stakishari.
“Wa Llaah wa Billaahi
sijahusika na uhalifu wa Stakishari, Mwenyezi Mungu anajua zaidi. Nitakwenda
kuwahoji kwa nini wametaja jina langu na kulihusisha na mauaji yale, na pia kwa nini wanadanganya umma wa Watanzania kuwa
mimi nimerejea kutoka Ethiopia wakati nipo hapa nchini? Wana ajenda gani ya
siri” alisema Zahaki.
Aidha, Zahaki alisema
anataka Waislamu wajue ukweli wote hata akiwa ameshikwa na Jeshi la Polisi ama
kuuliwa katika mazingira ya kutatanisha, wajue kilichomuua ni chuki kutokana na
kusema kweli katika kadhia ya Mwembe Chai.
Aibukia Jeshi la Polisi, akamatwa
Kama alivyoahidi
kwa waandishi wa habari kuwa angekwenda kuhoji Jeshi la Polisi juu ya jina lake
kuhusishwa na mauaji ya Stakishari, Zahaki
kweli alifanya hivyo . Lakini taarifa ambayo Jeshi la Polisi kanda
maalum ya Dar es Salaam ilIitoa kwa waandishi wa habari ilisema mtuhumiwa huyo alijisalimisha.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova alisema Mtuhumiwa Zahaki Ngai amejisalimisha kwa Jeshi la Polisi akiwa na
wake zake wawili na kusema kuwa wale ambao bado hawajapatikana msako bado
unaendelea.
Maneno hayo ya
Kamishna Kova ni kama mwiba kwa Zahaki ambaye alishatangaza kuwa anaenda kuhoji
kwa nini jina lake limetajwa na sio kujisalimisha. Kama alivyotabiri, inaonekana
kama polisi wameendelea kupotosha umma.
Akizungumza na
gazeti Imaan, Mwanasheria wa mtuhumiwa huyo alisema wanashangazwa na upotoshaji
wa Kamanda Kova kwa umma wa Tanzania kwani Zahaki hakwenda kujisalimisha bali
alikwenda kuuliza ukweli wa tetesi anazozisikia katika vyombo vya habari.
Kilindo alisema
upotoshaji huo unakera na unaudhi kwani matamshi ya Kamishna wa polisi ni sawa
na kuthibitisha kuwa ana uhakika Zahaki ni
mhalifu na hivyo kupewa kesi hiyo wakati yeye hakuhusika na kadhia hiyo.
Katika tukio ambalo
polisi wanadai Zahaki alihusika, majambazi kadhaa yalivamia kituo cha polisi
cha Stakshari na kuua watu saba majira ya saa 5 usiku, Julai 12, 2015. Mpaka
sasa tayari watuhumiwa tisa wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo.
(Makala kwa hisani ya gazeti la Imaan Agosti 31 - Septemba 6, 2015)
(Makala kwa hisani ya gazeti la Imaan Agosti 31 - Septemba 6, 2015)
No comments:
Post a Comment